Nini kitatokea ikiwa nchi za Kiarabu zitaacha kusambaza mafuta kwa nchi za Magharibi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Miaka hamsini iliyopita Waarabu walishambulia Israeli. Vita hivi vinajulikana katika historia kama 'Vita vya Yom Kippur'. Kama matokeo ya vita hivyo, Marekani iliunga mkono serikali mpya ya Kiyahudi iliyoanzishwa ya Israeli.
Ili kulipiza kisasi kwa Marekani, nchi za Kiarabu zilisimamisha usambazaji wa mafuta ya madini kwa nchi za magharibi. Uamuzi huo ulikuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia, sera ya nishati na usawa wa nguvu katika Asia Magharibi.
Miaka 50 kamili baada ya tukio hili, vita vinaendelea tena kati ya Israeli na Hamas.
Wakati Israel ikiendelea na mashambulizi yake dhidi ya Gaza, Marekani inasimama kidete na Israel.
Hatua za Israel zimezikasirisha nchi za Kiarabu. Katika hali hiyo, swali limeibuka iwapo nchi za Kiarabu zitashinikiza nchi za Magharibi kwa kupiga marufuku usambazaji wa mafuta ili kukomesha vita.
Je, mataifa ya Kiarabu yatachukua uamuzi mkali wa kukata usambazaji wa mafuta dhidi ya nchi za Magharibi?
Nchi za Kiarabu zilipokata usambazaji wa mafuta mapema, iliathiri uchumi wa dunia kwa kiasi gani? Tutaangazia hili kwa kina.
Je, usambazaji wa mafuta utavurugwa?
Uchumi wa dunia bado unakabiliwa na matokeo ya mzozo wa Corona, vita vya kibiashara na China, mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine na sera ya gesi dhidi ya Ulaya.
Iwapo nchi zenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi huko Asia Magharibi na Afrika Kaskazini zitakubali kupunguza uzalishaji wa mafuta na kukata usambazaji kwa 'nchi zisizo rafiki', inaweza kusababisha mgogoro mkubwa katika uchumi wa dunia.
"Kuna baadhi ya kufanana kati ya hali wakati wa Vita vya Yom Kippur na hali ya Asia Magharibi leo," anasema Fatih Birol, mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA).
Anasema, "Soko la nishati duniani limebadilika sana tangu miaka ya sabini. Nchi za Magharibi ziliunda Shirika la Kimataifa la Nishati baada ya nchi za Kiarabu kuamua kukata usambazaji wa mafuta."

Chanzo cha picha, Getty Images
Fatih Birol anaongeza, "Ulimwengu umejiandaa vizuri zaidi kukabiliana na hali kama hiyo kuliko ilivyokuwa miaka hamsini iliyopita. Je, tunajua nini cha kufanya na wapi pa kwenda?"
Hata hivyo, wapinzani wa Israel na wafuasi wa Palestina bado hawajasema lolote kuhusu kukata usambazaji wa mafuta kwa nchi za Magharibi.
Lakini wakati wa mkutano wa Novemba 7, waziri wa Saudi Arabia, Khalid al-Falih, aliulizwa ikiwa nchi yake iko tayari kutumia mafuta kama silaha kumaliza vita.
Khalid al-Falih alijibu kwa tabasamu, "Hatufikirii chaguo hili leo. Saudi Arabia inataka uwepo wa amani kupitia mazungumzo."
Uungaji mkono wa Iran kwa vikwazo vya mafuta
Kongamano la dharura la nchi za Kiarabu na Kiislamu lilifanyika mjini Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia tarehe 11 Novemba kuhusiana na kuongezeka kwa vita vya Israel na Hamas na hakukuwa na mjadala mwingi juu ya kukata usambazaji wa mafuta.
Baadhi ya nchi zilikuja na mawazo kadhaa ya kuongeza shinikizo kwa Marekani na Israeli. Lakini hakukuwa na chochote kilichogusia kupiga marufuku uuzaji wa mafuta nje ya nchi.
Lakini kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, adui wa Marekani na Israel, amependekeza kukatwa kwa usambazaji wa mafuta kwa Israel. Hata hivyo, hakupata kuungwa mkono na mataifa mengine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Israel inanunua mapipa 3,00,000 ya mafuta kwa siku. Wasambazaji wengine wa mafuta kwa Israeli ni pamoja na Kazakhstan na Azerbaijan.
Baada ya rufaa ya Iran, nchi za Kiarabu na Kiislamu zilitoa taarifa na kufafanua kuwa hazitaki kuingiza siasa katika suala la usambazaji wa mafuta.
Migogoro ya kijeshi na ya kibinadamu imezuka katika maeneo yanayozozaniwa ya Wapalestina tangu miaka ya 1950. Nchi za Kiarabu na Iran zimejadili kutumia mafuta kama silaha dhidi ya Magharibi.
Je, vikwazo vya mafuta vilinufaisha nchi za Kiarabu?
Nchi za Kiarabu zimekata usambazaji wa mafuta kwa nchi za Magharibi mara mbili. Mara ya kwanza usambazaji ulikatwa mnamo 1967 wakati wa Vita vya Siku Sita.
Baadaye mnamo 1973, wakati wa Vita vya Yom Kippur, usambazaji wa mafuta ulikatwa. Marufuku ya kwanza haikufanya kazi, lakini marufuku ya pili ilikuwa na athari mbaya.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nchi za Magharibi na Kiarabu zilijifunza kitu kutokana na matukio haya. Kwa hivyo, hakuna anayezungumza juu ya kusitisha usambazaji wa mafuta sasa. Hakuna mtu anataka kufanya hivyo tena.
Miaka hamsini iliyopita, Israeli walifikiri kwamba hakuna mtu ambaye angewashambulia. Vile vile, Marekani ilichukulia kuwa nchi za Kiarabu hazitasitisha usambazaji wa mafuta. Lakini imani hizi zote mbili zimevunjwa.
Siku kumi baada ya Israeli kushambuliwa katika Vita vya Yom Kippur, nchi za Kiarabu zilikata usambazaji wa mafuta kwa Marekani, Uholanzi na nchi nyingi za Magharibi. Si hayo tu, viongozi wa Ghuba ya Uajemi na Iran walikubali kuongeza bei ya mafuta kwa asilimia 70.
Kwa upande mmoja, usambazaji wa mafuta ulitatizika, kwa upande mwingine, bei ya mafuta iliongezeka mara tano kutokana na kupunguzwa kwa uzalishaji wa mafuta na nchi za Kiarabu.
Wakati huo, mafuta yalikuwa chanzo kikuu cha nishati ulimwenguni. Uchumi wa dunia uliathirika pakubwa na kupanda kwa bei ya mafuta ghafi.
Kati ya 1973 na 1975, uchumi wa Marekani ulipungua kwa asilimia sita. Kiwango cha ukosefu wa ajira kilifikia asilimia tisa. Vile vile, Pato la Taifa la Japan lilishuka kwa mara ya kwanza tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchi zinazoendelea zikiwemo India na China pia ziliathiriwa na tatizo hili.
Nchi za Magharibi zilikabiliwa na mfumuko wa bei kwa miaka mingi. Hii haikutokana tu na vikwazo vya mafuta, bali pia kushuka kwa uchumi na mfumuko wa bei ulioanza kabla ya vita. Hata hivyo, mgogoro huo uliongezeka kutokana na kuvurugwa kwa usambazaji wa mafuta.
Miezi mitano baadaye, tarehe 18 Machi 1974, marufuku hiyo iliondolewa kwa sababu kuu mbili.
Sababu ya kwanza ni kwamba nchi za Kiarabu hazikutaka mgogoro huo umalize mahitaji yao ya mafuta. Marekani na Ulaya zilianza kuzoea uhaba wa mafuta huko Asia Magharibi. Nchi zinazozalisha mafuta za OPEC zilikuwa zimeweka ukuu wao juu ya soko la mafuta la kampuni za mafuta za Magharibi.
Sababu nyingine ni kwamba hawawezi kamwe kufikia lengo kuu la vikwazo vya mafuta.
Marekani na washirika wake waliendelea kuiunga mkono Israel. Chini ya shinikizo kutoka kwa tishio la kukata usambazaji wa mafuta, Wamarekani hawakupenda kufanya kazi kama mpatanishi wa amani kati ya Israeli, Misri na Syria.
Baada ya kuondolewa kwa vizuizi vya usambazaji wa mafuta, amani ilirejeshwa polepole katika eneo lote.
Je, marufuku ya mafuta ilitoa mafunzo gani kwa nchi za Magharibi?
Kabla ya usambazaji wa mafuta kwa nchi za Magharibi kukatika, uchumi mzima wa ulimwengu ulitegemea mafuta pekee.
Lakini baada ya haya hali ilibadilika na sasa makaa ya mawe, gesi na nishati ya nyuklia vimepata umuhimu sawa. Nchi za Magharibi zenyewe zilianza kuzalisha mafuta.
Baadhi ya nchi za Ulaya mara moja ziliongeza uzalishaji wa mafuta katika Bahari ya Kaskazini. Marekani ilijenga bomba huko Alaska.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pamoja na hili, makampuni ya Magharibi yalianza kuwekeza katika maeneo yenye mafuta mengi zaidi ya Asia Magharibi. Marekani ilifahamu athari za kupunguzwa kwa mafuta.
Daniel Yergins, mwanahistoria mashuhuri na mwandishi wa kitabu cha 'Uchimbaji: anasema, "Mwaka 1973 Marekani ilikuwa muagizaji mkubwa wa mafuta duniani, lakini sasa Marekani ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta duniani na pia kubwa katika uuzaji wa nje ya nchi."
Aliongeza, "Funzo jingine ambalo nchi za Magharibi zimejifunza kutokana na hili ni kwamba ili kuishi duniani, sote tunapaswa kuishi pamoja.
"Nchi za Kiarabu hazikukata usambazaji wa mafuta kwa nchi zote. Kwa mfano, Uingereza ilikuwa kwenye orodha yake ya 'nchi rafiki'.
Lakini mzozo wa kisiasa wa ndani ulilazimisha Uingereza kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje."
Anaongeza, “Wakati nchi za OPEC zilipunguza mauzo ya mafuta, nchi za Magharibi zilikubaliana na kampuni zao za mafuta kusambaza mafuta kwa nchi zilizoendelea.
Imetafsiriwa na Asha Juma












