''Uso wa pili wa Dubai: Jinsi nyota wa Instagram wanafanya biashara ya ngono kufadhili maisha ya anasa"

Chanzo cha picha, Getty Images
Tunaanza ziara yetu katika vyombo vya habari vya Uingereza kutoka Sunday Times, ambayo ilichapisha ripoti chini ya kichwa: "Uchafu wa Dubai: Nyota wa Instagram ambao wanafanya biashara ya ngono kwa maisha ya anasa."
Gazeti hili linaanza ripoti hiyo ambayo ilitayarishwa na Louise Callaghan kwa kuzungumzia moja ya washawishi wa mtandao huo anayeishi Dubai, huku akionyesha picha za maisha ya anasa anayoishi.
Lakini kwa mfanyabiashara ambaye anajifafanua kama rafiki wa rafiki, biashara yake halisi ni tofauti. "Je! unalipa zawadi? Euro 4,000, ndiyo au hapana?", Alijibu haraka ujumbe wa faragha aliotuma kupitia Instagram.
Aliongeza, "Nilipata 10,000 jana, unadhani wewe ni maarufu au mzuri ili kukupa punguzo?
Mwandishi wa ripoti hiyo anasema kuwa mazungumzo haya yanaonyesha upande wa uchafu iliopo Dubai.
Maelfu ya washawishi wamewasili katika mji huo kipindi cha miaka michache iliyopita, wakijaza mitandao ya kijamii na machapisho kuhusu maisha ya kupendeza katika emirate.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa washawishi wanaonyesha maisha ya Dubai katika picha za sherehe za fukwe za bahari na mivinyo inayopatikana kila siku kwenye meza huku wakilala na matajiri duniani, ambao wamejiunga nao katika miezi ya hivi karibuni Pamoja na maelfu ya raia Warusi baada ya. kuzuka kwa vita vya Ukraine
Kulingana na ripoti hiyo, zaidi ya mahojiano 12 na washawishi, wanaotafuta ngono na watu walio karibu nao yalifichua kuwa baadhi ya washawishi hufadhili maisha yao kwa kufanya biashara ya ngono kwa maelfu ya pauni kwa usiku.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kadiri umaarufu unavyoongezeka kwenye mitandao ya kijamii, ndivyo mapato yanavyoongezeka, kulingana na mmoja wa washawishi, "kwa sababu wana wafuasi wengi, wanalipwa zaidi, na malipo yao yanaweza kuwa katika mfumo wa ndege, vito vya mapambo, na bila shaka pesa taslimu.”
Wanalipwa kima cha chini cha $5,000 na hupanda hadi $20,000 wikendi.
Jarida hilo linanukuu ushuhuda wa mwanamke mwingine ambaye anasema anaweza kuleta wateja kwenye nyumba aliyokuwa akimiliki katika hoteli moja, ambapo kodi inaweza kufikia hadi £5,000 kwa mwezi.
Callaghan anasema mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya jinsi Dubai inavyowasilishwa kimataifa. Serikali ya Imarati imewawekea zulia jekundu washawishi, ikiwalipa wengi wao kwa usaidizi wao, na baadhi ya watu maarufu wamepewa "visa za dhahabu," makazi ambayo yanaweza kuongezwa muda kila baada ya miaka kumi.
Kulingana na gazeti hilo, daima kumekuwa na ukahaba huko Dubai, sawa na mahali pengine popote ulimwenguni.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa biashara ya ngono ilishamiri mjini humo, licha ya ukweli kwamba imeharamishwa kisheria. Lakini katika baadhi ya maeneo, baadhi ya watu hupata kadi za matangazo kwenye magari yao kwa wasichana ambao hutoa huduma ya "massage".
Gazeti hilo linamnukuu mfanyabiashara mmoja kutoka UAE akisema: "Ukahaba bila shaka unaongezeka. Huwezi kujua siku hizi kama msichana unayemwona ni wa kawaida au kahaba."
Zawadi ya Qatar kabla ya kombe la dunia
Na tunageukia gazeti la Observer, ambalo lilichapisha ripoti kuhusu wajumbe wa Bunge la Uingereza kupokea zawadi za thamani kutoka Qatar kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia la 2022.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwandishi wa ripoti hiyo, Shanti Das, anasema kuwa Qatar ilitumia pesa nyingi zaidi kwa zawadi na safari za wabunge wa Uingereza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kuliko nchi nyingine yoyote, kulingana na uchambuzi wa Observer ambao unafichua baadhi ya juhudi za nchi hiyo ya Ghuba kabla ya Kombe la Dunia mwezi ujao.
Gazeti hilo lilisema kuwa serikali ya Qatar ilitoa zawadi kwa wabunge zenye thamani ya zaidi ya pauni 250,000 kwa mwaka hadi Oktoba hii, ikiwa ni pamoja na malazi ya hoteli za kifahari, safari za ndege za daraja la juu na tikiti za mbio za farasi.
Thamani ya zawadi za Qatar ilikuwa kubwa kuliko kiasi kilichotumiwa na nchi nyingine 15 ambazo serikali zake kwa pamoja zilitoa michango kwa wabunge wa Bunge la Uingereza.
Gazeti la The Observer lilibainisha kuwa zawadi za Qatar katika kipindi cha miezi 12 iliyopita zimezidi zile walizotoa katika mwaka mwingine wowote, na kufichua jinsi mamlaka ya Qatar ilivyoongeza juhudi zao za kuwavutia wabunge wa Uingereza kabla ya Kombe la Dunia.
Rekodi zinaonyesha Wabunge walitangaza zawadi za thamani ya £100,000 na ukarimu kutoka Qatar katika kipindi cha miaka mitano hadi Oktoba 2021, lakini zaidi ya mara mbili ya hiyo iliripotiwa katika kipindi cha miezi 12 pekee.
Transparency International ilionyesha wasiwasi wake mkubwa kwamba wabunge watakubali "maelfu ya pauni za ukarimu" kutoka kwa serikali za kigeni zenye rekodi za kutiliwa shaka za haki za binadamu, gazeti hilo liliripoti.
Gazeti hilo lilidokeza kuwa baadhi ya manaibu waliopokea zawadi hizi baadaye walionekana kuzungumza vyema kuhusu Qatar katika mijadala ya bunge.
The Observer ilieleza kuwa uhusiano kati ya Uingereza na Qatar umeimarika katika miaka ya hivi karibuni. Mwezi Mei, Waziri Mkuu wa wakati huo Boris Johnson alitangaza "ushirikiano wa kimkakati wa uwekezaji," ambao utaifanya Qatar kuwekeza katika sekta muhimu za uchumi wa Uingereza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.












