Je, kweli maandamano nchini Iran yanaweza kusababisha mabadiliko ya serikali?
Na Lyse Doucet and Behrang Tajdin
BBC Persian

Katika kipindi cha wiki nne tangu kifo cha Mahsa Amini, Iran imekumbwa na maandamano makubwa zaidi dhidi ya serikali katika miaka ya hivi karibuni.
Maandamano hayo yanaonekana kuwa tishio kubwa kwa serikali ya kidini, ambayo imejibu kwa nguvu kwani yameenea kuliko wakati mwingine wowote kati ya kizazi kipya cha wanawake na wasichana wa Iran, ambao baba na babu walijaribu bila mafanikio kubadili mfumo kutoka ndani.
Mitandao ya kijamii imejaa video zinazoonyesha wanawake wakirarua na kuchoma picha ya Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei.
“Tusipoungana mmoja baada ya mwingine tutakuwa Mahsa Amini anayefuata,” ni mojawapo ya kauli mbiu zake zinazomtaja mwanadada aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kudaiwa kuvaa “isivyofaa” sitara.
Kama sehemu ya siku ya matangazo maalum, ripota wa BBC Kiajemi Behrang Tajdin na mwandishi mkuu wa kimataifa mkongwe Lyse Doucet walijibu maswali kutoka kwa watazamaji kuhusu kile kinachotokea nchini Iran na kwa nini.
Nani anaongoza maandamano?

Chanzo cha picha, EPA
Behrang Tajdin: Jibu fupi ni kwamba hakuna mwanasiasa hata mmoja au kundi linaloongoza maandamano.
Yanaendeshwa na wanawake wa Iran ambao wamechoshwa na serikali kujaribu kudhibiti kila nyanja ya maisha yao, pamoja na mavazi yao.
Nyimbo zinazosikika zaidi zina maneno: ‘’Mwanamke, maisha, uhuru’’ na ‘’Kifo kwa dikteta’’, akimaanisha kiongozi mkuu, Ayatollah Ali Khamenei.
Kinachoyaunganisha makundi yote hayo ni kutaka kuwepo mabadiliko ya kimsingi katika Jamhuri ya Kiislamu, hali yake isiyo ya kidemokrasia na sera zake zinazoongozwa na itikadi.

Chanzo cha picha, AFP
Behrang Tajdin: Maandamano haya kwa kweli hayakuanza miongoni mwa wanafunzi au katika mji mkuu wa Tehran.
Yalianza katika mji wa Saqqez, mkoa wa Kurdistan, na kuenea kama moto wa nyika.
Tumeona maandamano kati ya wanafunzi, watu katika miji mikubwa na hata miji midogo, ambayo kwa ujumla ni ya kihafidhina.
Katika maeneo yenye ustawi zaidi wa miji, na pia katika jamii maskini zaidi.
Ni vigumu sana kupima ni idadi gani hasa ya watu wanaounga mkono maandamano hayo.
Hata hivyo, ushahidi unaonyesha kwamba ni maandamano ya kuunga mkono zaidi ambayo yameshuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni nchini Iran na kwamba uungwaji mkono unatoka kwa watu wengi sana nchini kote na jamii.
Kwa nini hayaangaziwi zaidi na vyombo vya habari na hata kimataifa?

Chanzo cha picha, WANA NEWS AGENCY
Lyse Doucet: Serikali nyingi za Magharibi zimetoa taarifa kali za kulaani ukandamizaji wa maandamano.
Pia wameweka vikwazo vipya.
Uingereza, kwa mfano, imeidhinisha vikwazo dhidi ya polisi wa maadili wa Iran pamoja na maafisa watano wakuu wa kisiasa na usalama.
Hata hivyo, kuna vyombo vya habari vichache vya kigeni vilivyoko nchini Iran.
Wao, kama waandishi wa habari wa Iran, wanafanya kazi chini ya vikwazo lakini wanaendelea kuripoti.
Vyombo vingi, ikiwa ni pamoja na BBC, vinataka kupeleka wanahabari kuripoti habari hii, lakini hawawezi kupata visa.
Kwa hivyo tunategemea video na akaunti ambazo Wairani wanaweza kutuma kupitia huduma ya mtandao iliyowekewa vikwazo.
Je, maandamano ni dalili za kutengwa zaidi na dini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Behrang Tajdin: Katika miongo miwili iliyopita, Iran imekuwa jamii ndogo ya kidini, kwa kiasi fulani kama pingamizi kwa tafsiri kali ya Uislamu wa Kishia unaotetewa na serikali na utekelezaji wake kwa nguvu kwa watu.
Kukataa kuendeleza maadili ya Kiislamu ilikuwa moja ya sababu polisi wa maadili waliundwa hapo awali.
Kwa ujumla, kadri Jamhuri ya Kiislamu inavyojaribu kutekeleza maadili ya kidini na kuwekeza pesa za umma katika mashirika na sherehe za kidini, ndivyo Wairani wanavyozidi kukatishwa tamaa na kujitenga na maadili hayo.
Inafaa pia kuzingatia kwamba, chini ya sheria, kuuacha Uislamu na kuelekea kwenye ukafiri au hata dini nyinginezo ni marufuku kabisa na kunaweza kuadhibiwa kwa kifo.
Kwa hivyo, ni vigumu sana kuona mtu yeyote akitoa maoni kama hayo hadharani.
Je, polisi au jeshi wanaweza kushiriki maandamano?

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lyse Doucet na Behrang Tajdin: Iran ni taifa la karibu watu milioni 90 ambao wana maoni tofauti, kama nchi zingine.
Hii ni pamoja na vikosi vya usalama.
Ni vigumu kujua wanachofikiria sasa, katikati ya maandamano haya.
Wengine wataendelea kuwa waaminifu kwa sababu mustakabali wao unafungamana na mustakabali wa Jamhuri ya Kiislamu.
Wengine wanaweza kuhoji ukandamizaji ambao lazima ufanyike.
Hadi sasa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lenye wasomi waaminifu zaidi halijatumwa.
Lakini wengi wanashangaa ni nini kitatokea ikiwa uzito kamili wa vikosi vya usalama vya Iran utatolewa: Je, kweli wangetaka kulenga umati wa wanawake vijana na wazee, wanaume kutoka tabaka mbalimbali za maisha?
Wanaweza hata kuwa na wanafamilia ambao wanaunga mkono baadhi ya matakwa ya waandamanaji.
Kuna uwezekano wa kuwepo watu ndani ya polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanaoyaunga mkono maandamano hayo, lakini hakuna uwezekano wa kuweza kuonyesha hilo, kwani adhabu inaweza kuwa kali.
Ili kujiunga na polisi au huduma za usalama, lazima wathibitishe kwamba wao ni wa kidini, watiifu kwa Jamhuri ya Kiislamu na wanaamini katika ‘’maadili yake ya kimapinduzi’’.
Baadhi ya wajumbe wa ngazi za juu serikalini wameibua wasiwasi kuhusu utumiaji nguvu, huku kukiwa na vizuizi kama vile hijabu ya lazima au kujifunika kichwa kwa wanawake.
Lakini hatujui ukosoaji huu ulivyo wa kina.
Je, kwa sasa kuna makundi ya haki za binadamu nchini Iran?

Chanzo cha picha, TWITTER
Behrang Tajdin: Hapana, wanafuatilia hali kutoka nje ya nchi.
Iran inashuku mashirika yasiyo ya kiserikali, yakiwemo yale ya ndani.
Mara nyingi inawashutumu kwa ujasusi, kudhoofisha usalama wa taifa na kupanga njama za kupindua serikali.
Hiyo inafanya kuwa karibu kutowezekana kwa kundi la haki za binadamu kufanya kazi nchini Iran kwa uhuru na usalama.
Je, jumuiya ya kimataifa inaweza kuwasaidia vipi Wairani?

Chanzo cha picha, Reuters
Lyse Doucet: Kama waandishi wa habari wa BBC, hatungetoa mapendekezo ya kuunga mkono harakati za kisiasa.
Lakini mashirika mengi ya haki za binadamu na mashirika mengine ya kiraia yanatoa mapendekezo, naweza kutaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na serikali au makampuni.
Njia moja ambayo serikali ya Marekani inajaribu kusaidia ni kwa kurahisishia Wairani, ambao sasa wametengwa na mtandao, kufikia majukwaa na huduma za mtandaoni.
Hazina ya Marekani imetoa leseni mpya ya Jumla D-2, ambayo inaruhusu misamaha katika vikwazo dhidi ya Iran ili kuhakikisha kuwa makampuni ya teknolojia ya kimataifa hayakiuki vikwazo hivyo.
Elon Musk amewasha mtandao wake wa satelaiti, Starlink, nchini Iran ili kutoa ufikiaji wa mtandao bila kukaguliwa, ingawa Wairani wanahitaji kupata vituo maalum ambavyo vina hatari nyingine.
Kampuni zingine, kama vile Google na Signal, sasa zinatoa VPN (Mitandao ya Kibinafsi ya Kawaida) ili kukwepa mtandao wa Iran.
Je, maandamano hayo yangeweza kweli kuleta mabadiliko ya utawala?

Chanzo cha picha, Reuters
Lyse Doucet: Baadhi ya viongozi wakuu wameelezea wasiwasi wao kuhusu ukandamizaji huo, lakini muhimu zaidi kwao ni kunusurika kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Kumekuwa na maandamano mengi nchini Iran hapo awali, kuhusu masuala kuanzia uhaba wa maji, kupanda kwa bei, kuvaa hijabu kwa lazima.
Maandamano ya hali ya uchumi mnamo 2019 yalikuwa makubwa zaidi, lakini wimbi hili limevutia sekta nyingi za jamii.
Wenye mamlaka wanaweza kuamini kwamba wanaweza kukabiliana na hali hii, kama walivyofanya huko nyuma.
Kiongozi mkuu amesema kuwa baadhi ya waandamanaji wanaweza kutibiwa kwa ‘’njia za kitamaduni’’ au kuelimishwa upya.
Wengine wangeadhibiwa kwa hatua za mahakama au usalama.
Lakini wengi wa waandamanaji wako chini ya miaka 25, ishara ya mabadiliko makubwa ya kijamii inayotokea nchini Iran.
Kama mchambuzi Vali Nasr alivyosema: ‘Kunaweza kuwa na mabadiliko ya utawala,’’ ikiwa watakubali kwamba chanzo cha maandamano haya ni ndani ya Iran na sio nje, katika nchi za Magharibi sasa wanalaumu.
Siku za nyuma, maandamano nchini Iran hatimaye yameisha baada ya msako mkali wa vikosi vya usalama.
Tumeona, katika mawimbi mengine kama vile uasi katika nchi nyingi za Mashariki ya Kati ambazo zilikuja kujulikana kama Vuguvugu la katika nchi za Kiarabu maarafu kama Arab Spring, kwamba maandamano yasiyo na viongozi ya kizazi kipya yanaweza kutekwa nyara na watu waliojipanga zaidi, ikiwa ni pamoja na kijeshi na harakati za Kiislamu.
Mustakabali wa wimbi hili la maandamano bado haujulikani sana.















