Jinsi mkakati mpya wa usalama wa Trump unavyobadili sera ya kigeni ya Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump, ameketi, katika suti ya bluu, shati, tai yenye mistari nyekundu na beji ya bendera ya Marekani.

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    • Author, James Lewis
    • Nafasi, BBC News World Service
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Mkakati wa Usalama wa Taifa wa serikali ya Trump umeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa washirika wa karibu wa Marekani na unaashiria mabadiliko makubwa kutoka misingi iliyounda sera ya mambo ya nje ya Marekani kwa miongo kadhaa.

Hati hiyo ya kurasa 33, iliyotolewa wiki iliyopita, inaichora dunia hasa kama uwanja wa ushindani wa kiuchumi. Inasisitiza mikataba ya moja kwa moja kati ya nchi na uzalendo wa kiuchumi, badala ya ushirikiano wa kimataifa, taasisi za pamoja na uendelezaji wa demokrasia.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC anayefuatilia Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tom Bateman, mkakati huu unaakisi misimamo mikali ya kiitikadi ndani ya serikali ya Trump.

Kinachojitokeza zaidi si tu yaliyomo, bali pia yale yaliyokosekana.

Hakuna ukosoaji mkubwa kwa mahasimu wa jadi wa Marekani kama Urusi au China. Badala yake, lugha kali zaidi imelenga Ulaya, hali iliyozua hofu katika miji mikuu ya Ulaya wiki hii.

Hoja ya "kufutwa kwa ustaarabu"

Tofauti na mikakati ya awali ya usalama wa taifa iliyokuwa ikisisitiza maadili na vipaumbele vya pamoja kati ya Marekani na Ulaya, mkakati huu umechukua mwelekeo mpya.

Hati hiyo inadai kuwa Ulaya itakuwa haitambuliki tena ndani ya miaka 20 au chini ya hapo, kutokana na kukumbatia taasisi za kimataifa na sera za uhamiaji, ambazo zinatajwa kuwa zinadhoofisha ''utambulisho wa Magharibi''.

Katika sehemu moja, mkakati huo unasema wazi kuwa Ulaya inakabiliwa na kile kinachoelezwa kama "kufutwa kwa ustaarabu".

Viongozi wa Ulaya wamepokea kauli hizi kwa mshangao mkubwa, angalau kwa mazungumzo ya faragha, mwandishi wetu anayefuatilia masuala ya jimbo anaiambia kitengo cha podcast.

''Ingawa hawakushangazwa na mwelekeo wa kiitikadi wa baadhi ya watu serikalini Marekani, kuuona msimamo huo ukiwekwa rasmi katika sera ya taifa kumezua hofu kubwa'', anaendelea kusema.

Mwanamume, JD Vance, aliyevaa suti nyeusi, shati jepesi na tai ya zambarau, anazungumza na hadhira, kutoka kwenye jukwaa lililokuwa kwenye jukwaa lililokuwa na maandishi makubwa ya samawati yanayosema: "MSC".

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alitoa mashambulizi makali dhidi ya demokrasia za Ulaya, katika Mkutano wa Usalama wa Munich.

Kwa miezi kadhaa sasa, dalili za kuzorota kwa uhusiano kati ya Marekani na Ulaya zimekuwa wazi.

Moja ya ishara za awali ilionekana mwezi Februari, wakati Makamu wa Rais JD Vance alipotoa hotuba kali katika Mkutano wa Usalama wa Munich, akiwakosoa viongozi wa Ulaya kwa kupuuza maoni ya wapiga kura kuhusu uhamiaji na uhuru wa kujieleza.

Mvutano huo umejitokeza kwa uwazi zaidi katika muktadha wa vita vya Ukraine.

Pia unaweza kusoma:

Hati hiyo inaashiria kuwa Ulaya haijaelewa kikamilifu mizani ya nguvu katika eneo hilo, na kwamba Marekani inalazimika kutumia juhudi za kidiplomasia kulirejesha eneo hilo katika hali ya utulivu.

Umoja wa Ulaya unatuhumiwa kuzuia jitihada za Marekani za kumaliza vita hivyo vya Ukraine.

Aidha, mkakati huo unapendekeza kuwa Marekani inapaswa kurejesha "utulivu wa kimkakati" na Urusi, hatua ambayo inadaiwa itasaidia ''kuimarisha uchumi wa Ulaya''.

Ujumbe wa msingi ni kwamba Ukraine inapaswa kuendelea kuwepo kama taifa, lakini hilo linahitaji kukubali nafasi kubwa ya Urusi katika usawa wa nguvu za kikanda.

Rais Donald Trump anaonesha dalili za kupoteza subira na Ulaya pamoja na Ukraine. ''Ni wazi....shinikizo linaelekezwa kwa Ulaya kukubali msimamo ambao Waukraine wengi wangeuona kama kujisalimisha,'' mwandishi huyu anaendelea kutoa maelezo kwa mahojiano yaliyofanywa na idhaa ya podcast.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky (Kulia), akiwa amevalia shati jeusi la mtindo wa kijeshi lililopambwa kwa roketi tatu za Kiukreni, ameketi katika Ofisi ya Oval ya White House, Washington DC, Marekani, pamoja na Rais wa Marekani, Donald Trump na Makamu wa Rais JD Vance (Kulia), wote wakiwa wamevalia suti za bluu iliyokolea, mashati mepesi, tai nyekundu na beji za bendera za Marekani. Wote wawili wanainua mikono yao ya kulia kuelekea Zelensky, kana kwamba wanamnyamazisha.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky (Kulia), aliitwa "asiye na heshima" na "asiye na shukrani", alipokutana na Rais wa Marekani Donald Trump na Makamu wa Rais JD Vance (Kulia)

Mvutano huo tayari umejitokeza hadharani, ikiwemo katika mkutano wa Februari katika Ikulu ya White House kati ya Trump, Makamu wa Rais Vance na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambapo Zelensky alikosolewa kwa kukosa heshima na kushindwa kuonyesha shukrani.

Kwa mtazamo huu, viongozi wa Ulaya sasa wanakabiliwa na uwezekano kwamba Marekani inaweza kushinikiza suluhu inayokaribia zaidi maslahi ya Moscow kuliko ya Kyiv.

Urusi, kwa upande wake, imeupokea mkakati huu kwa mtazamo chanya, ikiuelezea kuwa kwa kiasi kikubwa unaendana na msimamo wake.

Soma pia:

'Matokeo ya Trump'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Pamoja na ukosoaji wake kwa Ulaya, mkakati huu mpya unaipa kipaumbele kikubwa Wamarekani, wanaotajwa kama Ulimwengu wa Magharibi kama lengo kuu la sera ya kigeni ya Marekani.

Serikali ya Trump inalenga ''kuhakikisha,... eneo hilo linabaki thabiti na linaongozwa kwa ufanisi ili kuzuia au kupunguza uhamiaji mkubwa kuelekea Marekani'', hati hiyo yaeleza.

Hati hiyo pia inatambulisha kile kinachoelezwa kama "nyongeza ya Trump" katika Mafundisho ya Monroe, sera ya karne ya kumi na tisa iliyosisitiza ubora wa Marekani katika bara la Amerika na kupinga kuingiliwa na mataifa ya Ulaya.

Kwa mtazamo wa serikali, msisitizo huu mpya unaonekana kuwa muhimu katika kukabiliana na kuongezeka kwa ushawishi wa China katika Amerika ya Kusini, hata kama China haikutajwa moja kwa moja katika hati hiyo.

Trump anaamini kuwa China imejijengea nafasi kubwa ya kiuchumi katika eneo hilo, ingawa baadhi ya madai yake, ikiwemo kuhusu Mfereji wa Panama, hayana msingi wa moja kwa moja.

Ndege za kivita zimepakia sehemu tambarare ya kubeba ndege kubwa zaidi ya Jeshi la Wanamaji la Marekani, USS Gerald R Ford, pamoja na boti nne za kuvuta pumzi zikipita kwenye kina kifupi cha maji, zilizopigwa picha kutoka ufuo wa kisiwa cha Caribbean.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kuwepo kwa meli za kivita za Marekani katika Carribean kunasisitiza tishio la nguvu za kijeshi

Hata hivyo, juhudi za hivi karibuni za kidiplomasia za Marekani, ikiwemo ziara za Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio katika nchi za Amerika ya Kusini, zinaashiria dhamira ya Washington ya kurejesha ushawishi wake wa kiuchumi na kimkakati.

Ingawa mkakati huu haujadili kwa kina matumizi ya nguvu za kijeshi, mashambulizi ya anga dhidi ya magenge ya biashara haramu ya dawa za kulevya katika Carribean, pamoja na uwepo wa meli za kivita na wanajeshi wa Marekani karibu na pwani ya Venezuela, vinaonyesha uwezekano wa matumizi ya nguvu pale itakapoonekana kuwa lazima.

Kwa jumla, Mkakati huu mpya wa Usalama wa Taifa tayari umeathiri mijadala ya kisera nchini Marekani na barani Ulaya.

Athari zake kwa Ukraine, uhusiano wa Marekani na Ulaya, pamoja na mwelekeo wa mfumo wa kimataifa bado zinaendelea kujitokeza.

Hata hivyo, jambo moja liko wazi: serikali ya Trump inalenga kufafanua upya vipaumbele vya sera ya mambo ya nje ya Marekani, na inatarajia washirika wake wajipange kulingana na mabadiliko hayo.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na AMbia Hirsi