'Walimwambia mama yangu nilikufa katika moto, kumbe nilitekwa nyara'

fc

Chanzo cha picha, Wag Entertainment

Maelezo ya picha, Walifikiri Delimar Vera alifariki katika moto wa nyumbani mwaka 1997.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Usiku wa Desemba 15, 1997, moto ulizuka katika nyumba ya wana ndoa kutoka Puerto Rico, Luz Cuevas na Pedro Vera, huko Philadelphia, Marekani, wakiwa na wana wao wawili wadogo wa kiume na binti yao mchanga wa siku kumi, Delimar.

Mama huyo alipanda ngazi baada ya kuona moto katika chumba cha binti yake aliyelala. Alitafuta katika kitanda alichomuweka lakini hakumuona.

Maafisa walihusisha moto huo na waya mbovu wa umeme. Mtoto huyo hakuonekana tena baada ya hapo, na ripoti ya mchunguzi wa matibabu ilihitimisha kuwa alifariki kwa moto na kuteketea kabisa.

Wazazi wake waliumizwa sana na tukio hilo, lakini huo ulikuwa mwanzo tu wa hadithi ya kutisha.

Mtoto kutoweka

fc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Luz Cuevas alimwona binti yake miaka michache baada ya kutangazwa "kifo" chake

Muda mfupi kabla ya moto huo, kuna mtu aligonga mlango. Luz alifungua mlango. Ni Caroline, mmoja wa binamu wa Pedro (mjomba wa Pedro alimuoa mama yake Caroline).

Caroline alimwambia Luz anataka kuzungumza na Pedro kwa sababu amemtafutia kazi. Pedro hakuwa na kazi wakati huo, kwa hiyo aliondoka nyumbani pamoja na Caroline kwenda kumtembelea mtu aliyefahamiana naye ili kuzungumza kuhusu kazi mpya.

Wawili hao wakiwa wametoka, Caroline alisema ameacha pochi yake nyumbani kwa Pedro na hivyo akarudi nyumbani kwa Pendro peke yake kuchukua pochi yake ambako Luz alikuwepo.

Caroline alipofika, aliomba kutumia choo. Baada ya dakika chache, Luz alipanda ghorofani kumwona binti yake, Delimar. Kwa mshangao, aligundua kichanga chake hakipo kitandani pake, bali yupo katika kitanda kidogo kilicho karibu na dirisha.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Caroline alipotoka bafuni, Luz alimuuliza kuhusu kumtoa mtoto katika kitanda kikubwa na kumuweka katika kitanda kidogo.

"Nilidhani ataanguka kitandani na sikutaka adhurike," Caroline alisema, kisha akaondoka nyumbani.

Muda mfupi baada ya kuondoka Luz alisikia kelele za ajabu kutoka ghorofani. Alipanda juu hadi chumbani na kuona chumba cha mtoto kinawaka moto. Wakati chumba kikiwa katikati ya moshi na moto, mtoto hakuwepo, ulikuwa ni usiku wa baridi na dirisha lilikuwa wazi.

Dakika chache baadaye, zima moto walifika na kuzima moto, na kuleta vipande vya godoro la mtoto. Walimpa Luzi godoro kama mabaki ya Delimar.

Ni wakati huo ndipo Pedro aliporudi nyumbani akiwa na hofu na kumwona Caroline akiwa amesimama kando ya barabara.

Wakati wa siku za tukio hilo Caroline pia alikuwa anatarajia kupata mtoto. Alionekana kuwa na furaha. Alizungumza na familia yake, marafiki, na wafanyakazi wenzake kuhusu ujauzito wake na kisha mtoto wake wa nne akazaliwa.

Mtoto wake alikuwa msichana aitwaye Alia, na alijifungua nyumbani kwa msaada wa rafiki yake.

Pia unaweza kusoma

Siku ya sherehe ya kuzaliwa

f

Chanzo cha picha, VERA

Maelezo ya picha, Alia alipogundua ukweli huu kwa mara ya kwanza, alijiona ana mama wawili.

Caroline aliishi karibu kilomita 20 kutoka nyumba ya Luz na Pedro. Hawakutembeleana mara kwa mara, na miaka michache baada ya tukio la moto, Luz na Pedro walitengana.

Januari 2004 Karamu ya sherehe ya kuzaliwa ilifanyika katika nyumba ya dada yake Pedro.

Ingawa Luz na Pedro hawakuwa pamoja tena, Luz bado alikuwa na uhusiano mzuri na familia ya mume wake wa zamani, na walimwalika pia.

Alipoingia kwenye sherehe, alimwona Caroline akiwa na msichana mdogo, na kuna kitu kilimvutia: mashavu ya msichana huyo yana dimpo.

Muda huo huo, Luz alimwambia dada yake kwamba msichana huyo ni Delimar.

Baada ya msichana huyo kupanda juu kwenda kucheza na watoto wengine, Luz naye alikwenda na kusema, "kuna kipande ubani kimekwama kwenye nywele zako.”

Luz alivuta nywele za mtoto huyo kwa nguvu na nywele chache zilibaki mkononi mwake.

Alia alishuka na Caroline akamwambia waondoke kwenye sherehe. Alia alipouliza kwa nini, Caroline alisema, "kuna mwanamke mbaya hapa anataka kukuchukua. Usimruhusu akuchukue.”

Kipimo cha DNA

FC

Chanzo cha picha, VERA

Maelezo ya picha, Delimar bado hajui ni nani aliyeshirikiana na Caroline katika kutekeleza utekaji nyara.

Wiki chache baadaye, Caroline alimpeleka Alia na binti yake mwingine, Angelica kwa daktari. Wakiwa wanasubiri katika chumba cha daktari, Caroline aliwapeleka bafuni.

Alimtaka Angelica kulinda mlangoni na akatoa kichupa kidogo kilichojaa kimiminika. Caroline alimtaka Alia afumbue mdomo wake na yeye akamimina maji hayo kwenye ulimi wake.

Akamwamuru, "usiyameze.”

Alifanya hivyo mara kadhaa, kisha Alia akaenda katika ofisi ya daktari na kuchukuliwa sampuli kutoka katika ulimi wake.

Majimaji hayo yalikuwa ni mate ya Caroline, na walichokifanya ni kipimo cha DNA. Lengo ni Caroline kuweka ushahidi wake.

Hata hivyo, akiwa na nywele za Alia, Luz aliweza kuripoti polisi na wao kufanya uchunguzi wa kujitegemea wa DNA.

Pia aliweza kupata kituo cha kisheria ambacho kilikuwa tayari kumsikiliza na kumpa msaada, na aliweza kupata mpelelezi wa kufuatilia kesi hiyo.

Februari 2004, kipimo kilithibitisha kile ambacho Luz alikiamini. Alia Hernandez mwenye umri wa miaka sita alikuwa ni Delimar Vera. Caroline alidanganya kuhusu ujauzito wake na kumteka nyara mtoto huyo.

Muda mfupi baadaye, Caroline alikiri na akahukumiwa kifungo kwa kosa la kuiba watoto.

Mama wawili

X

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Delimar na mama yake Luz mwaka 2007

Nilitaka kumuuliza Luz, "kwa nini unataka kunitenganisha na mama yangu?" Lakini kadiri muda ulivyosonga na kutazama mkasa huo, nilitambua kwamba Caroline ndiye mkosaji,” anasema.

Alilazimika kuishi na mama yake na ndugu zake ambao walikuwa wageni kwake.

“Awali nilidhani nina mama wawili. Mama yangu, Caroline, na sasa nina mama yangu, Luz,” anasema baada ya miaka 30.

Delimar akiwa bado na hasira. Alimtembelea Caroline gerezani na kumuuliza: 'Kwa nini uliniteka? Ulikuwa na watoto wengine watatu. Kwa nini umenifanyia hivi?

“Kwa nini umeniweka katika hali ya kuchanganyikiwa na na mabadiliko haya yote ya ajabu katika maisha yangu?" Nina hasira naye, lakini hajawahi kuomba msamaha, anasema tutaonana tena.

Delimar hajamtembelea tena.

Mtekaji ni nani?

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Luz Cuevas alihuzunishwa sana na kifo cha bintiye wa siku kumi, Delimar.

Lakini maswali mengi bado yanabaki akilini mwake. Ikiwa Caroline alikuwa kando ya barabara na baba yake mara tu baada ya moto, angewezaje kumteka nyara?

Kulikuwa na mshirika ambaye alimwiba kutoka kwenye chumba chake kupitia dirisha. Mtu huyu ni nani? Je, baba yake pia alihusika katika utekaji nyara huu?

Pedro anakanusha kuhusika katika tukio hili, na Delimar anamuamini.

"Tunajua kuwa Caroline alikuwa na mshirika na huyu ni mtu ambaye alimsaidia katika utekaji," anasema Delimar.

"Mtu aliyeniteka nyara, alinitoa kupitia dirishani, na kisha akakimbia nami kwenye giza la usiku. Kwa bahati mbaya, bado hatujui ni nani."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi