Waridi wa BBC: 'Mtoto ana mtoto na ujauzito mwingine''

Chanzo cha picha, Bahati Mgogwe
Na Martha Saranga
Alishuhudia ugumu wa maisha ya mama yake, ambaye aliendelea kuishi kwa kujitahidi kuwalea wadogo zake mapacha, aliowapata miaka michache tu baada ya kumzaa Bahati.
Kwa msaada wa mjomba wake, Bahati Mgogwe mkurugenzi wa taasisi ya Msichana Kwanza ya jijini Dar es Salaam alikamilisha elimu yake ya chuo kikuu mwaka 2018, jambo lililomfundisha umuhimu wa elimu kama nyenzo ya kubadilisha maisha.
"Nilijua kuwa elimu ingekuwa suluhisho la kubadilisha familia yangu, na hasa kumsaidia mama yangu ambaye alikulia katika familia maskini," anasema.
Mdogo wangu nae alipata ujauzito uliokatisha ndoto zake
'2020 wakati dunia inakumbwa na janga la Corona,nakumbuka shule zilifungwa hapa Tanzania kwa muda, baadae zilipofunguliwa iliripotiwa idadi kubwa ya wasichana wa shule nchini Tanzania walikutwa na ujauzito,niliguswa sana na kujiuliza sasa itakuwaje kwa wasichana hawa? Alieleza
Bahati anasema mdogo wake wa kike alipata ujauzito mara baada ya kumaliza kidato cha nne,aliwaza sana kwa namna gani angeweza kufufua tumaini lililopotea kwa wasichana kama mdogo wake.
Anasema taarifa za wasichana kupata ujauzito katika kipindi cha likizo ya Covid ilimfikirisha kwamba hawa wasichana wote wameingia katika njia kama ya mama na mdogo wake''
Hii ilikuwa changamoto kubwa kwa Bahati, lakini pia aliona fursa ya kufanya jambo la maana kwa wasichana ambao ndoto zao zimekatishwa na ujauzito, hasa katika jamii ya Afrika Mashariki.
'Nilipata wazo la kutengeneza tovuti ya Msichana Kwanza'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
'Mara nyingi elimu yetu ya msingi na sekondari haitufundishi kujitegemea kwamba ukimaliza unaweza kuanzisha biashara na kukimu Maisha yako'alisimulia Bahati
Bahati mwenye shahada ya kwanza ya Elimu kutoka chuo kikuu Mwenge anaamini kuwa, elimu ni nguzo, inayoweza kuwa suluhisho la kubadili maisha ya wasichana wengi.
Kutokana na ari hii, Bahati alianzisha taasisi ya kiraia iitwayo Msichana Kwanza, ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wasichana nchini Tanzania.
Nilianza kwa kuzungumza na wasichana walionizunguka,baadae niliwashirikisha rafiki zangu kuanzisha tovuti ambayo ilitoa elimu ya ujasiriamali,tuliweka machapisho ya jinsi ya kutengeneza wazo la biashara na muongozo wa kufanya biashara.
Tuliweka mafunzo mbalimbali katika tovuti ili kuwawezesha wasichana kutoka maeneo mbalimbali ambako wangeweza kupata mtandao na kujisomea.
Bahati anasema tovuti ilipata muitikio mzuri hasa kutoka kwa wasichana wa mikoa mbalimbali.
Wasichana wengi walikuwa na simu janja lakini hawakuwa na intaneti, tuliwawezesha na kuanza kuwafuatilia katika vikao vya mtandaoni.
Niligundua wasichana wengi wana wazo la biashara lakini hawana mitaji na jinsi ya kuanza utekelezaji wa biashara.
Niliwezesha baadhi ya wasichana na bado walipata ujauzito kwa mara nyingine wengi walisema ni kwa sababu ya kukosa elimu ya afya ya uzazi.
''Unakuta msichana ana umri wa miaka 15 ana mtoto na ujauzito mwingine''
Changamoto nyingine ni kwamba hawakopesheki kutokana na kutokuwa na dhamana.

Chanzo cha picha, Bahati Mgogwe
'Kutengeneza mazingira salama ya msichana kufanikiwa'
Bahati alitumia maono yake kupitia Taasisi ya Msichana Kwanza na kufanikiwa kugusa Maisha ya wasichana 1200 kote nchini Tanzania katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa,anasimulia Bahati.
Kwa ufadhili wa kimasomo, elimu ya ujasiriamali, na masuala ya afya ya uzazi, Bahati amegusa maisha ya wasichana akiwapa fursa ya kujiendeleza na kutimiza ndoto zao kupitia taasisi yake.
Utaratibu na vigezo katika kuwasaidia wasichana unazingatiwa,kwa kushirikiana na serikali ya mtaa au Kijiji na hata wazazi katika kuthibitisha taarifa za msichana muhitaji.
Ninaguswa hasa na wasichana kuanzia umri wa miaka 9-18, tumefanikiwa kufika mikoa mbalimbali Mara, Rukwa na Dar es Salaam.
'Program ya girls connect nilianzisha ili kuwawezesha wasichana wanaomaliza vyuo kujijengea uwezo ili kuweza kushindana katika soko la ajira.Imekuwa na mwitikio mzuri na tumepokea wasichana wengi kutoka vyuoni wakijitolea kufanya kazi na kupata mafunzo yanayowapatia uzoefu wa kazi'.

Chanzo cha picha, Getty Images
Namna jamii inavyonipokea na kuniamini inanipa moyo wa kuendelea na mapambano kuwakomboa wasichana zaidi.
Ukienda kwa mzazi ukamwambia tunatoa ufadhili,au serikali na ikakuamini ni mafanikio makubwa kwangu,alisisitiza
Kutambuliwa na shirika la kimataifa na UNDP ni hatua kubwa ambayo inanipa hamasa kufanya vizuri zaidi na kusababisha mabadiliko chanya kwenye jamii.
Changamoto zangu ninazikabili kwa mtazamo chanya sana,ukishakuwa mzungumzaji na muhamasishaji wa masuala ya wasichana kwenye jamii kuna namna jamii hukuchukulia kama mjuaji unayeshindana na wanaume''hiyo hainikatishi tamaa ninasali na kusonga mbele
Wasichoelewa ni kwamba harakati zozote za kumsaidia na kumuwezesha msichana zinamuhitaji mwanaume ili zifanikiwe na mimi ninashirikiana sana na wanaume kufanikisha hili.
Ana furaha kubwa kuona mafanikio ya wasichana hao na anaendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uwezeshaji wa wasichana kwa kuwapatia elimu, kwani anajua kuwa mabadiliko haya yataendelea kutoa matokeo chanya kwa jamii nzima.
"Elimu ni ufunguo wa mafanikio. Inahitaji kuungwa mkono na jamii nzima ili wasichana waweze kufanikiwa. Mimi niko hapa kuhamasisha jamii na kuwasaidia wasichana kufikia malengo yao," alisisitiza Bahati.















