Jinsi Venezuela inavyotumia 'meli za mapepo' kukwepa vikwazo vya mafuta

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Ángel Bermúdez
- Nafasi, BBC News Mundo
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipoweka vikwazo dhidi ya sekta ya mafuta ya Venezuela mwaka 2019 ili kuipa shinikizo serikali ya Nicolás Maduro, mauzo ya mafuta ghafi ya Venezuela yalishuka hadi takriban mapipa 495,000 kwa siku. Miaka sita baadaye, vikwazo bado vipo, lakini mauzo ya mafuta ya Venezuela yamepanda na kufikia karibu mapipa milioni moja kwa siku.
Ingawa kiasi hiki ni kidogo kwa nchi ambayo mwaka 1998 kabla ya Hugo Chávez kuingia madarakani ilikuwa ikizalisha mapipa milioni tatu kwa siku, kupanda huku kwa mauzo kunaifanya Venezuela kukaribia mauzo ya zaidi ya mapipa milioni 1.1 kwa siku ambayo ilikuwa ikisafirisha mwishoni mwa mwaka 2018, na ni dalili kwamba vikwazo dhidi ya Venezuela havifanyi kazi kama Marekani ilivyotarajia.
Serikali ya Maduro imekuwa ikitafuta njia za kufufua tena uzalishaji na kutengeneza njia mpya za kuuza mafuta ghafi ya Venezuela huku ikiepuka vikwazo.
Katika jukumu hili la masoko, kile kinachoitwa "ghost fleet" kinachukua nafasi muhimu: mfululizo wa meli za kubeba mafuta ambazo, kupitia mbinu mbalimbali, kubwa huficha utambulisho wao kama meli zinazobeba mafuta yaliyowekewa vikwazo na mamlaka za Marekani.
Moja ya meli hizi ilikamatwa Jumatano hii na jeshi la Marekani ikiwa karibu na pwani ya Venezuela.
"Tumekamata tu meli moja ya mafuta karibu na pwani ya Venezuela, meli kubwa sana; kwa kweli, kubwa zaidi kuwahi kukamatwa," Trump alisema, akitangaza operesheni hiyo kwa waandishi wa habari katika Ikulu ya White House.
Serikali ya Maduro ilijibu kwa kuiita kukamatwa huko "wizi wa wazi na kitendo cha uharamia", na kusema kuwa itakata rufaa kwa vyombo vya kimataifa vilivyopo kulalamikia kilichotokea.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatua hii ya Marekani inaongeza mvutano na Caracas ambao umekuwa ukiongezeka tangu Agosti mwaka huu, wakati serikali ya Trump ilipoanza kutuma jeshi kubwa katika pwani ya Caribbean kwa lengo rasmi la kupambana na biashara ya dawa za kulevya, lakini ambalo wachambuzi wengi wanaamini lina lengo la mwisho la kubadilisha utawala nchini Venezuela.
Zaidi ya malengo yake ya kisiasa, hatua hii ina athari ya kiuchumi kwani inaifanya Venezuela kuwa na ugumu zaidi katika kuuza mafuta yake kwa kuongeza shinikizo dhidi ya "meli za mapepo', kwa maana ya meli zinazofanya kazi kwa kificho kama mizuka.
Lakini tunajua nini kuhusu jinsi meli hizi zinavyofanya kazi?
Kushamiri kwa mutumizi ya meli za mafuta kwa kificho
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Matumizi ya zinazoitwa ghost fleets ni jambo linalokua na halitokei tu Venezuela, bali pia katika nchi zingine mbili zinazozalisha mafuta ambazo zimewekewa vikwazo na Marekani na mataifa ya Magharibi, nchi za Urusi na Iran.
Kampuni ya kijasusi ya kifedha S&P Global inakadiria kuwa meli moja kati ya tano duniani hutumika kusafirisha mafuta kinyemela kutoka nchi zilizowekewa vikwazo.
Kati ya hizi: 10% husafirisha mafuta ya Venezuela, 20% hufanya hivyo kwa mafuta ya Iran, 50% husafirisha mafuta ya Urusi, na 20% zilizobaki hubeba mafuta kutoka zaidi ya nchi moja kati ya hizo.
Kwa mujibu wa kampuni ya uchambuzi wa masuala ya baharini Windward, kuna takriban meli 1,300 kwenye biashara hii ya kimataifa ya siri.
Lengo la vikwazo vya mafuta ni kuzuia nchi au kampuni kuhusika katika ununuzi au shughuli zozote zinazohusu mafuta ghafi kutoka nchi zilizowekewa vikwazo.
Kwa kujibu, nchi zilizowekewa vikwazo huanza kutoa punguzo kubwa ili kuvutia waendeshaji au nchi zinazothubutu kununua mafuta, huku bila wasiwasi wakitumia mbinu za kuficha nini inabeba na kufanya

Chanzo cha picha, Getty Images
Meli zinazodanganya
Moja ya mbinu kuu wanazotumia ni kubadilisha jina au bendera ya meli mara kwa mara.
Katika tukio la Jumatano, meli iliyokamatwa inajulikana kama The Skipper, kwa mujibu wa CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani.
CBS ilisema meli hiyo imewekewa vikwazo tangu 2022 kutokana na tuhuma za kuhusika kwenye mtandao wa magendo ya mafuta unaofadhili Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran na kundi la Hezbollah la Lebanon.
Wakati inakamatwa, iliwahi kuitwa Adisa, na kabla ya hapo The Tokyo. Ilihusishwa pia na tajiri wa mafuta wa Urusi Viktor Artemov, aliyewekewa vikwazo pia.
Meli hii pia ina umri wa miaka 20 jambo la kawaida kwa 'ghost fleet'. Kampuni kubwa za usafirishaji huwa zinaachana na kuitupa meli baada ya miaka 15, na baada ya miaka 25 hupelekwa kuteketezwa.
Mbinu nyingine ni kujifanya meli iliyokwisha kutelelekezwa (scrapped) kwa kutumia namba zao rasmi za IMO. Hizi ndizo zinaitwa "zombie ships" sawa na mtu kutumia kitambulisho cha mtu aliyekufa.
Mfano ni meli ya Varada, ambayo Aprili mwaka huu iliwasili Malaysia baada ya kuondoka Venezuela. Ingawa meli halisi ya Varada iliharibiwa Bangladesh mwaka 2017, hii ilibeba utambulisho wake feki.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbinu nyingine za kawaida
Mbinu nyingine za kawaida zinazotumika na meli hizi ni kubadilisha 'kufaulisha' mafuta kwenye bahari ya kimataifa (ship-to-ship transfer), kuwasha na kuzima mfumo wa ufuatiliaji wa AIS ili kuficha mahali meli ilipo, na kutumia bendera za nchi zisizo na ufuatiliaji mkali kama Panama, Comoros na Malta.
Uchunguzi wa Transparency Venezuela uliofanywa Oktoba 2025 uligundua kuwa kati ya meli 71 za kigeni zilizokuwa bandarini Pdvsa, 15 ziko chini ya vikwazo, 9 ziko kwenye mtandao wa meli za mapemo ama mazombi, na 6 zikitumika kurahisisha uhamisho wa mafuta baharini kutoka meli moja hadi nyingine.
Hali hii inakinzana na meli za Chevron, ambazo zinazoruhusiwa na Marekani na hukaa bandarini siku 6 tu. Transparency pia ilibaini kuwa meli 38 zilitumia zaidi ya siku 20 bila kugusa bandari, jambo linalotia shaka kuhusu aina ya shughuli zinazoendelea.
Hata hivyo, ukamataji wa hivi karibuni wa meli hii uliofanywa Jumatano na operesheni kutoka kwenye meli ya kubeba ndege Gerald Ford, kubwa zaidi duniani, ambayo sasa ni sehemu ya jeshi lililotumwa Carrebian, unaashiria uwezekano mkubwa kwamba uwezo wa serikali ya Maduro kutumia meli za kificho au mapepo' utapungua sana kuanzia sasa.

Chanzo cha picha, Getty Images












