Elon Musk: Bilionea anayeishi kimasikini

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Elon Musk, Bilionea wa kwanza kuwa na utajiri wa zaidi ya dola bilioni 500 mwezi Oktoba 2025.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Elon Musk, Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla, amekuwa mmoja wa watu matajiri zaidi duniani katika miaka ya hivi karibuni, na utajiri wake umefikia kiwango cha juu sana hivi karibuni, na kufikia dola nusu trilioni.

Licha ya utajiri huo mkubwa, Musk anadai kuwa anaishi maisha rahisi na yasiyo na anasa. Mwaka 2021, alisema anaishi katika nyumba huko Texas yenye thamani ya takribani dola 50,000.

Grimes, mwenzi wake wa zamani, ambaye ana watoto wawili na Musk, alisema katika mahojiano na jarida la Vanity Fair mnamo 2022 kwamba Musk haishi maisha ya kifahari kama watu wengi wanavyofikiri.

"Haishi kama bilionea," aliambia jarida hilo. "Wakati mwingine anaishi chini ya kiwango cha umaskini." Grimes pia alisema kwamba Musk aliwahi kukataa kununua godoro jipya, ingawa lile alilokuwa nalo lilikuwa limetoboka.

Ingawa makazi ya Elon Musk yanaweza yasiwe ya kifahari kama wengine wanavyotarajia, anajulikana kwa kupenda kwake magari ya kifahari, ikiwa ni pamoja na moja ambalo hubadilika kuwa manowari.

Pia anamiliki ndege binafsi kadhaa zenye thamani ya mamilioni ya dola.

Nyumba za kifahari alizowahi kumiliki na baadaye kuziuza

Musk aliwahi kumiliki na nyumba nyingi za kuvutia ambazo zilitumika kama makazi.

Jarida la The Wall Street Journal liliripoti mwaka 2019 kwamba aliwahi kununua nyumba saba kwa takribani dola milioni 100 ndani ya kipindi cha takribani miaka saba.

Aidha nyumba nyingi kati ya hizo zilikuwa katika eneo la kifahari la Bel Air, California, na zilikuwa karibu karibu.

Katika nyumba hio kila moja ilikuwa na bwawa la kuogelea, uwanja wa tenisi, chumba cha kupata mvinyo, maktaba binafsi, na hata ukumbi wa dansi.

Moja kati ya nyumba hizo ilijengwa kwa kuuzngukwa na shamba kubwa ambalo hapo awali lilimilikiwa na muigizaji maarufu wa filamu ya Willy Wonka, Gene Wilder.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini mwaka wa 2020, Musk alibadilisha mawazo yake, akiandika kwenye Twitter kwamba "angeuza karibu mali yake yote" na kutobaki na nyumba yoyote."

"Sihitaji pesa," aliandika. ''Umiliki wa vitu vingi humfanya mtu kubeba mizigo mizito zaidi."

Pia alitoa sharti moja: kwamba nyumba ya Gene Wilder "haipaswi kuharibiwa au kupoteza uzuri wake kwa namna yoyote."

Aliuza nyumba hiyo ya vyumba vitatu vya kulala kwa Jordan Walker-Perlman, mpwa wa Wilder, na akampa mkopo wa mamilioni ya dola ili kumsaidia kuinunua.

Hata hivyo Juni 2025, aliichukua tena nyumba hiyo baada ya kuripotiwa kwamba Bw. Walker-Perlman alikuwa ameshindwa kulipa mkopo wake.

Mwaka wa 2021, Musk aliandika ujumbe kwenye Twitter kwamba "nyumba yake kuu" ilikuwa nyumba ya kawaida ya kubebeka yenye thamani ya takriban $50,000 iliyoko Texas Kusini, karibu na makao makuu ya kampuni yake ya anga, SpaceX, katika eneo ambalo sasa limepata hadhi ya kuwa jiji la Starbase.

Mwaka uliofuata, Musk alisema kwamba hana nyumba kabisa, akitumia hali hiyo kama mfano wa maisha yake ya matumizi madogo, licha ya utajiri wake mkubwa.

"Kwa kweli mimi hukaa katika nyumba za marafiki," alimwambia Chris Anderson, rais wa TED Media. "Ninapoenda katika Eneo la Bay, ambapo kazi nyingi za uhandisi za Tesla hufanyika, hupendelea kukaa katika vyumba vya wageni vya marafiki zangu."

Hili si jambo jipya. Larry Page, Mkurugenzi Mtendaji wa Google wakati huo, alimwambia mwandishi Ashley Vance mnamo 2015 kwamba Musk hakuwa na makazi."

"Anatuma barua pepe na kusema, 'Sijui nilale wapi usiku wa leo. Je, ninaweza kuja kwako?'" alisema.

Kwa miaka mingi, kumekuwa na uvumi kwamba Musk ananunua mali kote Marekani. Hata hivyo, nyumba ya Texas inaonekana kuwa nyumba pekee rasmi anayomiliki yeye binafsi kwa sasa.

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bel Air imekuwa nyumbani kwa watu wengi maarufu wa Hollywood, kuanzia Beyoncé na Jay-Z hadi Alfred Hitchcock.

Ingawa Musk hatumii pesa nyingi kwenye mali isiyohamishika, ni suala la tofauti linapokuja suala la magari.

Kwa kuzingatia kwamba anamiliki Tesla, haishangazi kwamba ana idadi kubwa ya magari ya kipekee na, nyakati nyingine, ya ajabu.

Miongoni mwa magari hayo ni Ford Model T, gari la karne ya 20 ambalo linachukuliwa kuwa gari la kwanza la bei nafuu lililobadilisha kabisa sekta ya magari duniani.

s

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

Maelezo ya picha, Ford Model T, lililojulikana kwa jina la utani "Tiny Lizzie," lilikuwa gari lililofanya magari kuwa nafuu kwa mfanyakazi wa kawaida mwanzoni mwa miaka ya 1900.

Magari mengine ni pamoja na Jaguar E-Type Roadster ya 1967, ambayo Musk anasemekana kuihusudu tangu utotoni; McLaren F1 ya 1997, ambayo aliigonga, akatumia pesa nyingi kuitengeneza, na baadaye kuiuza; na Tesla Roadster, modeli ya kwanza ya Tesla kuingia sokoni, ambayo ilizinduliwa mwaka wa 2018.

Lakini gari maalum zaidi lilikuwa Lotus Spirit ya 1976, ambayo James Bond alitumia katika filamu ya 1977 ya The Spy Who Loved Me.

Katika filamu hiyo, gari hilo, lililopewa jina la utani "Wet Nellie," lilibadilishwa kuwa manowari.

Musk alinunua gari hilo katika mnada mwaka wa 2013 kwa takriban dola milioni 1 ili kulitumia tena kuwa manowari.

s

Chanzo cha picha, Screen Archives/Getty Images

Maelezo ya picha, Musk alinunua Wet Nelly kwa lengo la kuimarisha uwezo wake wa kimanowari

Kuruka kwa ndege kwenda kazini

Musk amekiri kwamba kitu kingine anachokifurahia kutumia ni ndege, lakini anasisitiza kwamba hii inahusiana na kujitolea kwake kwa kazi yake.

"Nisipotumia ndege, saa ninazoweza kufanya kazi zitakuwa fupi," alisema katika mahojiano ya TED ya 2022.

Miongoni mwa ndege zake za kibinafsi kuna aina kadhaa za Gulfstream, kila moja ikigharimu mamilioni ya dola.

Anazitumia kusafiri kati ya vituo vya SpaceX na Tesla nchini Marekani, na pia katika safari zake za kimataifa.

Mfadhili wa kipekee?

Musk ametoa mabilioni ya dola katika hisa kwa mashirika ya misaada na kuahidi mamilioni zaidi kwa mashirika mbalimbali, kulingana na nyaraka za kisheria za Marekani.

Hata hivyo aina ya hisani imekosolewa.

The New York Times iliielezea katika ripoti mwaka jana kama "isiyo ya kawaida na kwa kiasi kikubwa inajihudumia, kwa njia inayomstahili kupata punguzo kubwa la kodi linalomnufaisha kibiashara."

Shirika lake la hisani, Musk Foundation, linasema kwenye tovuti yake kwamba "limejitolea kuendeleza utu kupitia utafiti wa kisayansi, uvumbuzi wa kiteknolojia, na juhudi mahususi zinazopanua mipaka ya kile kinachowezekana."

Lakini New York Times iliripoti kwamba wakfu huo umelipa chini ya kiasi kinachohitajika kwa michango ya hisani kwa miaka mitatu mfululizo.

Gazeti hilo, ambalo lilipata marejesho ya kodi ya wakfu huo, pia liligundua kuwa michango mingi ilitolewa kwa mashirika yanayohusiana na Musk.

Elon Musk na Wakfu wa Musk wameombwa kutolea majibu suala hili.

Walipoulizwa kuhusu mashirika ya hisani, Musk alitilia shaka kuhusu utoaji wa hisani wa kawaida.

"Ukijali kuhusu ukweli wa wema, si mwonekano wake, hisani ni ngumu sana," alimwambia Chris Anderson mnamo 2022.

Kwa Musk, uwepo wa biashara zake ni hisani kiasili: "Tukisema hisani inamaanisha upendo kwa utu, basi ni hisani."

Alisema Tesla "inaharakisha kasi ya nishati endelevu," wakati SpaceX "ikijaribu kuhakikisha uhai wa muda mrefu wa ubinadamu" na Neuralink "inajaribu kusaidia kutibu ulemavu wa ubongo na hatari zinazotokana na AI."