“Rais wa mpito wa Venezuela hawezi kuaminiwa” – asema Machado

Machado pia amemshukuru rais wa Marekani, Donald Trump kwa operesheni ya kumwondoa Nicolas Mduro madarakani na kuongeza kuwa anataka kurudi Venezuela "haraka iwezekanavyo," baada ya kuwa mafichoni kwa miezi kadhaa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Mariam Mjahid & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

  2. Waziri wa mambo ya nje wa Israel ameitembelea Somaliland

    Hh

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli Gideon Saar ameitembelea Somaliland, eneo lililojitenga la Somalia, siku ya Jumanne, vyanzo viwili viliiambia Reuters.

    Ni siku 10 baada ya Israeli kuitambua rasmi Jamhuri ya Somaliland iliyojitangaza kuwa nchi huru.

    Moja ya vyanzo hivyo, afisa mkuu wa Somaliland, alisema Saar alikutana na Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi kujadili njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

    Chanzo cha pili kilithibitisha uwepo wa waziri wa Israeli huko Somaliland.

    Wizara ya mambo ya nje ya Israel hakujibu ombi la kutoa maoni kuhusu kama alikuwa Somaliland.

    Israeli iliitambua rasmi Somaliland kama taifa huru Desemba 27, hatua ambayo ilikosolewa na Somalia, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipinga juhudi za Somaliland za kujitenga.

    Hakuna nchi nyingine ambayo imeitambua rasmi Somaliland.

    Wakati huo, Abdullahi amesema Somaliland itajiunga na Makubaliano ya Abraham , makubaliano yanasimamiwa na utawala wa Trump kutoka mwaka 2020 ambayo yalishuhudia mataifa ya Ghuba, Falme za Kiarabu — mshirika wa karibu wa Somaliland — na Bahrain yakianzisha uhusiano na Israeli.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Wahamiaji 22 wa Ethiopia wafariki katika ajali mbaya ya barabarani

    Jjj

    Chanzo cha picha, Facebook

    Mamlaka inasema wahamiaji wasiopungua 22 wameuawa na wengine 65 kujeruhiwa baada ya lori walilokuwa wakisafiria kupinduka katika eneo la kaskazini mashariki mwa Afar nchini Ethiopia

    Takriban wahamiaji 85 wa Ethiopia walikuwa wakisafiri mashariki wakati lori hilo lilipopinduka katika mji wa Semera Jumanne asubuhi, afisa mkuu wa Afar, Mohammed Ali Biedo amesema katika taarifa.

    Bado haijajuulikana walikuwa wanaelekea wapi, lakini njia hiyo kwa kawaida huanzia Ethiopia kupitia Djibouti, kuvuka Bahari ya Shamu hadi Yemen, na kuendelea hadi Saudi Arabia na nchi zingine za Mashariki ya Kati.

    Biedo alisema kwamba 30 kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.

    Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linaelezea safari kutoka Pembe ya Afrika - inayojumuisha Somalia, Djibouti, Ethiopia na Eritrea - hadi Yemen kama "mojawapo ya njia za uhamiaji zenye shughuli nyingi na hatari zaidi".

    Licha ya hatari hizo, zaidi ya wahamiaji 60,000 waliwasili Yemen mwaka wa 2024 pekee, wengi wao wakielekea Saudi Arabia, kulingana na IOM.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Operesheni ya Marekani nchini Venezuela 'yadhoofisha sheria za kimataifa' - UN

    ds

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ravina Shamdasani katika mkutano na waandishi wa habari Geneva.

    Operesheni ya Marekani nchini Venezuela "imedhoofisha kanuni ya msingi ya sheria ya kimataifa," imesema tume kuu ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR).

    Akihutubia waandishi wa habari mjini Geneva, Ravina Shamdasani, msemaji wa OHCHR amesema "nchi hazipaswi kutishia au kutumia nguvu dhidi ya eneo au uhuru wa kisiasa wa taifa lolote."

    Ukosoaji huo unafuatia mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana, ambapo baadhi ya washirika wa Marekani pia walichukua msimamo wa kukosoa operesheni ya kijeshi ya Trump.

    Miongoni mwao, Ufaransa, Naibu mwakilishi wa kudumu, Jay Dharmadhikari, amesema kukamatwa kwa Maduro na Marekani "kunapingana na kanuni ya utatuzi wa migogoro kwa amani na kunapingana na kanuni ya kutotumia nguvu."

    Asubuhi ya leo, China ilirudia ukosoaji wake kwa vitendo vya Trump.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning amesema China iko "tayari kufanya kazi na nchi katika eneo hilo ... ili kudumisha amani na utulivu kwa pamoja."

    Maduro kihistoria anaichukulia China kama mshirika.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Msaidizi wa Trump asema hakuna atakayepigana na Marekani kuhusu Greenland

    l

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Stephen Miller

    Mmoja wa wasaidizi wenye ushawishi mkubwa wa Donald Trump amesema Greenland inapaswa kuwa sehemu ya Marekani ili kuilinda Nato na Aktiki.

    Alipoulizwa katika mahojiano na CNN ikiwa Marekani haitatumia nguvu kulinyakua eneo hilo lenye uhuru wa ndani la mwanachama mwenzake wa Nato, Stephen Miller amesema, "hakuna mtu atakayepigana na Marekani kuhusu mustakabali wa Greenland."

    Siku ya Jumapili Trump alirudia msisitizo wake kwamba Marekani "inaihitaji" Greenland - jambo lililomshangaza Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen ambaye amesema uvamizi wa Marekani utakuwa mwisho wa Nato.

    Washirika watano wa Ulaya wanaiunga mkono mkono Denmark na wametoa taarifa ya pamoja siku ya Jumanne.

    "Greenland ni ya wa-Greenland, na Denmark na Greenland ndizo zinazoweza kuamua masuala yanayohusu uhusiano wao," inasema taarifa hiyo kutoka kwa viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Uhispania, na Denmark.

    Katika mahojiano yake na CNN, Miller amesema "msimamo rasmi wa serikali ya Marekani ni kwamba Greenland inapaswa kuwa sehemu ya Marekani."

    "Denmark ina haki gani kuwa na udhibiti wa Greenland? Kwa msingi gani Greenland ni koloni la Denmark?" amehoji Miller.

    Msaidizi mkuu wa Trump pia amesema Marekani "ndiyo nguvu ya Nato. Ili Marekani ipate usalama katika eneo la Aktiki, kuilinda na kutetea maslahi ya Nato, ni wazi Greenland inapaswa kuwa sehemu ya Marekani."

    Nato ni kundi la kijeshi ambapo washirika husaidiana iwapo kutatokea mashambulizi ya nje.

    Suala la mustakabali wa Greenland limeibuka tena baada ya jeshi la Marekani kuingia nchini Venezuela, na kumkamata Rais wa nchi hiyo Nicolás Maduro na kumpeleka Marekani kukabiliana na mashtaka ya dawa za kulevya na silaha.

    Pia unaweza kusoma:

  6. “Rais wa mpito wa Venezuela hawezi kuaminiwa” – asema Machado

    k

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Maria Corina Machado

    Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Maria Corina Machado akizungumza na runinga ya Fox News ya Marekani amesema rais wa mpito wa Venezuela Delcy Rodríguez "hawezi kuaminiwa."

    Machado pia amemshukuru rais wa Marekani, Donald Trump kwa operesheni ya kumwondoa Nicolas Mduro madarakani na kuongeza kuwa anataka kurudi Venezuela "haraka iwezekanavyo," baada ya kuwa mafichoni kwa miezi kadhaa.

    Delcy Rodríguez ameapishwa kuwa kama rais wa mpito wa Venezuela na wakati wa sherehe hiyo, amesema amekula kula kiapo cha ofisi "kwa uchungu kutokana na mateso ambayo yamewapata watu wa Venezuela baada ya uvamizi haramu wa kijeshi dhidi ya nchi yetu."

    Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 56 ni mshirika wa Maduro na alihudumu kama makamu wa rais kuanzia mwaka 2018. Pia ameshikilia wadhifa wa waziri wa uchumi na fedha wa Venezuela.

    Kwa upande mwingine, chama cha upinzani cha Machado kinataka kuachiliwa kwa wafungwa wote wa kisiasa kupitia chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X.

    "Wale wafungwa wa kisiasa wa wanaoshikiliwa kijeshi isivyo haki wanapaswa kuachiliwa huru mara moja," inasema taarifa hiyo.

    María Corina Machado, mwenye umri wa miaka 58, anachukuliwa kuwa mmoja wa watu wanaoheshimika zaidi katika upinzani wa Venezuela na kwa muda mrefu amekuwa akiishutumu serikali ya Nicolás Maduro kwa "uhalifu."

    Alizuiwa kugombea katika uchaguzi wa 2024 lakini aliendelea kumpigia kampeni mgombea aliyechukua nafasi yake, Edmundo González.

    Maduro alitangazwa mshindi, ingawa hesabu za vituo vya kupigia kura zilionyesha kuwa González alishinda kwa kishindo.

    Ametishiwa kukamatwa mara nyingi, na kwa sababu hii, mama huyo wa watoto watatu alitumia muda mwingi mwaka jana akiishi mafichoni. Aliwapeleka watoto wake ng'ambo kwa ajili ya usalama wao, na hakuwaona kwa takriban miaka miwili.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Makundi ya haki za binadamu yasema watu wasiopungua 25 wamefariki katika maandamano Iran

    x

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takribani watu 25 wameuawa nchini Iran wakati wa siku tisa za kwanza za maandamano yaliyoanza katika soko la Tehran kuhusu kushuka kwa thamani ya sarafu na mfumuko wa bei, kulingana na makundi ya haki za binadamu.

    Kwa mujibu wa Reuters, maandamano hayo yameenea katika baadhi ya miji magharibi na kusini mwa Iran lakini hayafikii ukubwa wa machafuko yaliyolikumba taifa hilo mwaka 2022-23 kutokana na kifo cha Mahsa Amini, aliyefariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa maadili wa Iran kwa madai ya kukiuka kanuni kali za mavazi za Jamhuri ya Kiislamu.

    Ingawa ni madogo lakini yamepanuka haraka, huku baadhi ya waandamanaji wakiimba nyimbo za kuukosoa watawala wa kidini wa nchi hiyo.

    Iran bado iko chini ya shinikizo la kimataifa, siku ya Ijumaa Rais wa Marekani Donald Trump alitishia kuwasaidia waandamanaji nchini Iran ikiwa vikosi vya usalama vitawafyatulia risasi.

    Hengaw, kundi la haki za binadamu la Kikurdi la Iran, linasema idadi ya vifo ni 25, wakiwemo watu wanne walio chini ya umri wa miaka 18. Linasema zaidi ya watu 1,000 wamekamatwa.

    HRANA, mtandao wa wanaharakati wa haki za binadamu, umesema takribani watu 29 wameuawa, wakiwemo maafisa wawili wa polisi, pamoja na kukamatwa watu 1,203, kufikia Januari 5.

    BBC haijaweza kuthibitisha idadi hiyo kwa uhuru.

    Serikali ya Iran haijatoa idadi ya vifo kwa waandamanaji, lakini imesema maafisa wawili wa usalama wamefariki na zaidi ya kumi na wamejeruhiwa katika machafuko hayo.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Chelsea yapata kocha mpya

    sdxz

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Liam Rosenior amewahi kuwa kocha wa timu za Derby County na Hull City katika ligi ya Championship.

    Kocha wa timu ya Strasbourg, Liam Rosenior ndiye kocha mpya wa klabu ya Ligi Kuu Uningereza, Chelsea.

    Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 41 anatarajiwa kuchukua nafasi ya Enzo Maresca, ambaye aliondoka siku ya Mwaka Mpya.

    Mapema Jumanne, katika mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari kama meneja wa Strasbourg, Rosenior alithibitisha kwamba "amekubali kwa maneno" kuwa kocha wa Chelsea.

    "Siwezi kukataa fursa hii ya kujiunga na klabu kubwa, kikosi kikubwa ambacho ni mabingwa wa Kombe la Dunia la Klabu," Rosenior alisema.

    "Sijasaini bado. Lakini tumeshakubaliana kwa kila kitu na huenda nikasaini saa chache zijazo," Rosenior alisema.

    "Kukabidhiwa jukumu hili kunamaanisha jambo kubwa kwangu na nataka kuwashukuru wote waliohusika kwa fursa hii. Nitafanya kila kitu ili kuleta mafanikio ambayo klabu hii inastahili."

    Rosenior amesema kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza cha Strasbourg Kalifa Cisse, kocha mwingine msaidizi Justin Walker na mkuu wa uchambuzi Ben Warner watajiunga naye Chelsea.

    Ronseior aliteuliwa na Strasbourg Julai 2024 na kuiongoza klabu hiyo ya Ufaransa hadi nafasi ya saba katika Ligue 1 msimu uliopita.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Machado mpinzani wa Maduro aapa kuwa atarudi Venezuela

    l

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Picha inayomuonyesha kiongozi wa upinzani wa Venezuela Maria Corina Machado, huku watu wakisherehekea baada ya Marekani kuishambulia Venezuela na kumkamata Rais wake Nicolas Maduro na mkewe Cilia Flores, huko Santiago, Chile Januari 3, 2026.

    Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Venezuela Maria Corina Machado ameapa kuwa atarudi nyumbani haraka, huku akimsifu Rais wa Marekani Donald Trump kwa kumpindua adui yake Nicolas Maduro na kutangaza kuwa yuko tayari kwa uchaguzi huru.

    "Napanga kurudi Venezuela haraka iwezekanavyo," amesema Machado, 58, wakili na mama wa watoto watatu ambaye alitoroka Venezuela akiwa mafichoni Oktoba kwenda kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel.

    Katika mahojiano na Fox News siku ya Jumatatu alisema, "tulishinda uchaguzi (mwaka 2024) kwa kishindo chini ya hali ngumu. Katika uchaguzi huru na wa haki, tutashinda zaidi ya 90% ya kura."

    Machado amesema hajazungumza na Trump tangu Oktoba 10, wakati alipopokea tuzo ya Nobel. Amesema Marekani inapaswa kusaidia kushughulikia matatizo ya Venezuela kabla ya uchaguzi wowote mpya.

    Ni mahojiano yake ya kwanza ya Machado tangu Maduro alipokamatwa na Marekani mwishoni mwa wiki.

    Machado anatafutwa na serikali ya Chama cha Kisoshalisti kilichopo madarakani.

    Utawala wa Marekani hadi sasa unaonekana huenda ukafanya kazi na Rais wa mpito Delcy Rodriguez, mshirika wa muda mrefu Maduro ambaye amekosoa "utekaji nyara" wa Maduro huku pia akitaka ushirikiano na uhusiano wa heshima na Washington.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mwanamke aliyebakwa na genge la watu India atoka hospitalini

    k

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kumekuwa na ufuatiliaji mkubwa juu ya matukio ya ubaki nchini India tangu ubakaji wa kwenye basi mwaka 2012.

    Mwanamke aliyebakwa na genge la watu katika jimbo la Haryana kaskazini mwa India ameruhusiwa kutoka hospitalini wiki moja baada ya shambulio hilo la kutisha, afisa wa polisi ameiambia BBC.

    Mama huyo wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 26 alipelekwa hospitalini katika jiji la Faridabad asubuhi ya tarehe 30 Desemba akiwa na majeraha makubwa ya kichwa na usoni na kuvunjika mifupa kadhaa.

    Dada yake alisema alitoka kwenda kumtembelea rafiki yake na alikuwa akisubiri usafiri majira ya saa sita usiku pale wanaume wawili waliokuwa kwenye gari la wagonjwa walipompa lifti.

    Walimpeleka katika eneo lililohamwa ambapo walimbaka kisha wakamtupa nje ya gari lililokuwa likiendeshwa kwa kasi.

    Msemaji wa polisi amesema wamechukua hatua haraka na kuwakamata wanaume hao wawili na kukamata gari hilo.

    Mwanamke huyo aliruhusiwa kutoka hospitalini Jumatatu usiku baada ya matibabu na upasuaji.

    Afisa mkuu wa polisi Mukesh Kumar ameiambia BBC wamewasiliana na mahakama ili kumruhusu mwanamke huyo kulitembelea gereza kwa ajili ya kuwatambua watuhumiwa.

    Polisi walisema uhalifu huo ulitokea usiku wa tarehe 29 kuamkia 30 Desemba.

    Mmoja alisimama nje ya gari na kufuatilia huku mwingine akimbaka mwanamke aliye ndani ya gari," anasema Yashpal Yadav, afisa wa uhusiano wa umma wa polisi wa Faridabad.

    Polisi wamewahoji washukiwa hao, ambao baadaye walifikishwa mahakamani na kupelekwa gerezani, aliongeza.

    Daktari katika hospitali ambayo manusura alitibiwa alisema mwanamke huyo aliletwa "Desemba 30 ... akiwa na majeraha mengi."

    Kesi hiyo imesababisha hasira na ghadhabu nchini India na kulinganishwa na ubakaji wa kutisha wa mwanamke mwenye umri wa miaka 23 kwenye basi huko Delhi Desemba 2012.

    Uhalifu huo uligonga vichwa vya habari duniani, ulisababisha maandamano makubwa Delhi na miji mingine kadhaa na kuilazimisha serikali kuanzisha sheria mpya kali za kupinga ubakaji zilizojumuisha adhabu ya kifo kwa mashambulizi ya kutisha.

    Wanaume wanne waliohukumiwa kwa ubakaji na mauaji katika kesi hiyo walinyongwa mwaka wa 2020. Mmoja wa wabakaji alifariki gerezani huku mmoja mwenye umri wa chini ya miaka 18 akiachiliwa huru baada ya kukaa katika kituo cha kurekebisha tabia.

    Licha ya sheria kali bado maelfu ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono yanaendelea kuripotiwa kila mwaka.

    Kulingana na rekodi za hivi karibuni za polisi, matukio 29,670 ya ubakaji na majaribio 2,796 ya ubakaji yaliripotiwa mwaka 2023. Zaidi ya hayo, polisi pia walirekodi visa 849 vya ubakaji wa watoto na visa 94 vya majaribio ya ubakaji wa watoto.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ashinda muhula wa tatu kwa kishindo

    p

    Chanzo cha picha, Reuter

    Maelezo ya picha, Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Faustin-Archange Touadéra amepata asilimia 76 ya kura zote.

    Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Faustin-Archange Touadéra, ameshinda muhula wa tatu baada ya kupata wingi wa kura katika uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita.

    Profesa huyo wa hisabati mwenye umri wa miaka 68 alitarajiwa kushinda baada ya muungano mkuu wa upinzani kususia uchaguzi, ukieleza wasiwasi kuhusu haki kutotendeka katika uchaguzi.

    Touadéra alifanya kampeni katika taifa hilo lisilo na utulivu baada ya waasi kunyakua madaraka mwaka 2013, mgogoro uliosababisha serikali kuomba msaada kutoka kwa mamluki wa Urusi na wanajeshi wa Rwanda.

    Amekabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya katiba ya 2023 kuondoa mipaka ya mihula, na kumruhusu kuendelea kugombea wadhifa huo.

    Zaidi ya watu milioni 2.4 walijiandikisha katika uchaguzi mkuu wa Desemba 28, ambao waangalizi waliuelezea kuwa wa amani kwa kiasi kikubwa licha ya ucheleweshaji uliosababishwa na kuchelewa kufika kwa vifaa vya kupigia kura na matatizo katika daftari la wapiga kura.

    Touadéra alipata asilimia 76 ya kura, kulingana na matokeo ya awali yaliyotangazwa Jumatatu jioni na tume ya uchaguzi.

    Wapinzani wake wa karibu, Anicet-Georges Dologuélé na Henri-Marie Dondra, wote mawaziri wakuu wa zamani, walipata 15% na 3% ya kura.

    Wote wawili wametaka matokeo na kutaka yafutwe, wakidai kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na udanganyifu.

    Muungano mkuu wa upinzani, unaojulikana kwa kifupi kama BRDC, ulisusia uchaguzi huo, ukisema hautowezekana kuwa wa haki.

    Serikali imekanusha madai hayo.

    Mahakama ya Katiba ina hadi Januari 20 kutoa uamuzi kuhusu changamoto zozote kabla ya kutangaza matokeo ya mwisho.

    CAR ni mojawapo ya nchi maskini zaidi na isiyo na utulivu barani Afrika, ingawa ina utajiri wa rasilimali kama vile almasi na uraniamu. Umoja wa Mataifa unakadiria karibu nusu ya idadi ya watu wanategemea misaada ya kibinadamu.

    Tangu mwaka 2013, nchi hiyo isiyo na bahari imekuwa ikikumbwa na migogoro baada ya waasi kunyakua madaraka, na kumng'oa madarakani Rais wa wakati huo François Bozizé.

    Mkataba wa amani wa 2019 kati ya serikali na makundi 14 yenye silaha ulisaidia kupunguza mvutano, ingawa makundi sita kati ya hayo baadaye yalijiondoa kwenye makubaliano hayo.

    CAR ilikuwa mojawapo ya nchi za kwanza za Kiafrika ambapo Wagner, kundi la mamluki la Urusi, lilianza kufanya kazi, likitoa ulinzi kwa Touadéra.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Washirika wa Ukraine kukutana Paris kujadili dhamana za usalama dhidi ya Urusi

    Zelensky alisema pointi 20 zilizokubaliwa na Wamarekani zilitoa dhamana ya usalama ya Ukraine ambayo inaakisi uanachama wa Nato

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Zelensky alisema pointi 20 zilizokubaliwa na Wamarekani zilitoa dhamana ya usalama ya Ukraine ambayo inaakisi uanachama wa Nato

    Wakuu wa majeshi wa washirika wa Ukraine wanakutana mjini Paris leo Jumanne kwa lengo la kukamilisha kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo michango yao katika dhamana za usalama za baadaye, ili kuipa Kyiv uhakika endapo kutafikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano na Urusi, kwa mujibu wa wanadiplomasia na maafisa wa serikali.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, anatarajiwa kuungana na zaidi ya viongozi 27 katika mji mkuu wa Ufaransa, sambamba na wajumbe wakuu wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner.

    Mkutano huo ni sehemu ya juhudi pana za kuunda msimamo wa pamoja wa Ukraine, Ulaya na Marekani, ambao baadaye unaweza kuwasilishwa kwa Urusi.

    Juhudi za kumaliza mzozo huo unaokaribia kutimiza miaka minne zimeongeza kasi tangu Novemba.

    Hata hivyo, bado kuna dalili chache kwamba Urusi iko tayari kukubali mapendekezo ya sasa yaliyo mezani, huku suala la mipaka ya eneo likibaki kuwa kikwazo kikuu cha mazungumzo.

    Wakati huo huo, mapigano kati ya pande hizo mbili yanaendelea bila dalili ya kupungua.

    Kabla ya mkutano huo, wanadiplomasia walisema maafisa wa kijeshi, wakiwemo mkuu wa majeshi ya Ukraine, tayari walikuwa Paris kwa ajili ya kuweka kwa maandishi ahadi mahususi za kijeshi, ili viongozi waweze kutoa uungwaji mkono wa kisiasa.

    Hadi sasa, ahadi nyingi zimekuwa za jumla na zisizo na maelezo ya kina.

    Kwa mujibu wa kumbukumbu iliyotumwa kwa wajumbe 35 walioalikwa na kukaguliwa na Reuters, mkutano huo unalenga kupata michango kwa ajili ya kikosi cha kimataifa kitakachowekwa Ukraine endapo sitisho la mapigano litafikiwa, kwa uratibu wa karibu na Ukraine na kwa msaada wa Marekani.

    Waandalizi wa mkutano huo pia wanakusudia kukubaliana juu ya mchango wa dhamana pana za usalama kwa Ukraine, zikiwemo ahadi za kisheria iwapo itashambuliwa tena.

    Aidha, juhudi zinafanywa kuhakikisha kuwa mipango ya kile kinachoitwa Muungano wa Wenye Nia inaratibiwa na misimamo ya mazungumzo ya Ukraine, Marekani na Ulaya.

    Afisa mmoja mwandamizi wa Ulaya alisema matumaini ni kwamba kuimarishwa kwa dhamana za muungano huo kutasaidia pia kuthibitisha ahadi za Marekani, ambazo kwa kiasi kikubwa zimeainishwa katika mazungumzo ya pande mbili kati ya Washington na Kyiv.

    Katika hotuba yake kwa taifa Jumapili jioni, Rais Zelensky alisema mikutano hiyo ya Ulaya inapaswa kuwa mchango muhimu katika ulinzi wa Ukraine na kuharakisha juhudi za kumaliza vita.

    “Ukraine itajiandaa kwa hali zote mbili: diplomasia, ambayo tunaendelea nayo, au ulinzi zaidi wa vitendo endapo shinikizo la washirika kwa Urusi litathibitika kuwa halitoshi. Ukraine inataka amani,” alisema.

    Unaweza kusoma pia:

  13. Machado wa Venezuela asema hajazungumza na Trump tangu Oktoba

    Machado ni mshindi wa Tuzo za Noble

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kiongozi wa upinzani wa Venezuela na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Maria Corina Machado, amesema Jumatatu kwamba hajazungumza na Rais wa Marekani, Donald Trump, tangu Oktoba 2025, kwa mujibu wa Shirika la habari la Reuters.

    “Kwa kweli, nilizungumza na Rais Trump Oktoba 10, siku ile ile tuzo ya Nobel ya Amani ilipotangazwa, lakini si tangu wakati huo,” alisema Machado katika kipindi cha Hannity kilichoonyeshwa na Fox News.

    Machado alipewa tuzo hiyo kutokana na mapambano yake dhidi ya kile Kamati ya Nobel ya Norway ilichokiita udikteta.

    Machado, anayechukuliwa kama mpinzani mwenye kuaminika zaidi wa rais wa sasa aliyekamatwa na Marekani, Nicolas Maduro, aliondoka Venezuela mwezi uliopita kwenda Norway kupokea tuzo hiyo na hajarudi tangu wakati huo.

    “Ninapanga kurudi nyumbani haraka iwezekanavyo,” aliwaambia waandishi wa Fox News alipoulizwa kuhusu mipango yake ya kurudi Venezuela.

    Mahojiano hayo yalikuwa ya kwanza kwa Machado tangu Marekani ilipozindua mashambulizi dhidi ya Venezuela Jumamosi na kushika rais wake.

    Soma pia:

  14. Angola yawasilisha mapendekezo ya kumaliza mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

    Lourenco ndiye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Lourenco ndiye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.

    Rais wa Angola, Joao Lourenco, ameyawasilisha “mapendekezo kadhaa” ya kumaliza mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imesema Ikulu ya Congo jana, akieleza kuwa “yanavutia sana,” bila kutoa maelezo zaidi.

    Ofisi ya Lourenco ilisema kuwa alikutana na mwenyekiti mwenzake wa Congo, Felix Tshisekedi, mjini Luanda kwa saa chache jana kujadili mgogoro huo na jitihada za kuumaliza.

    Tshisekedi alisema kuwa Lourenco alitoa mapendekezo kadhaa “yanayovutia sana” ambayo yanaweza “kuchangia kwa kiasi kikubwa” katika jitihada za kutafuta amani.

    Lourenco ndiye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.

    Mkutano huo ulifanyika siku chache kabla ya mkutano wa siku tatu nchini Zambia wa mawaziri wa ulinzi kutoka nchi za Kati na Mashariki mwa Afrika, ili kujadili hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Hali ya mapigano mapya ilitokea Januari 3 kati ya kundi la silaha la M23 linaloungwa mkono Rwanda na majeshi yanayounga mkono serikali ya Congo mashariki, licha ya mkataba mbalimbali wa amani uliosainiwa mwaka jana.

    Pia Unaweza Kusoma:

  15. Maandamano ya kupinga bei za juu nchini Iran yaendelea siku 10 mfululizo

    GG

    Chanzo cha picha, EPA

    Maandamano ya kupinga ongezeko la bei yameendelea kwa siku ya kumi mfululizo katika miji mbalimbali nchini Iran.

    Ripoti zinaonyesha kuwa waandamanaji wameshuka mitaani hata katika miji mipya, ikiwemo Lahija.

    Vikosi vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi katika hali ya kutawanya waandamanaji na vurugu zinazotokea kinyume na haki za binadamu nje ya Iran imevutia malalamiko kutoka kwa serikali za kigeni, hasa Ikulu ya Marekani.

    Rais Donald Trump alionya kuwa: “Ikiwa Iran itaanza kuuawa watu kama ilivyokuwa zamani, Marekani itaishambulia vikali”.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeelezea onyo la Donald Trump kama “vita vya kisaikolojia.”

    Wakati huo huo, Masoud Pezzekian ametoa amri ya kuchunguza shambulio lililotokea katika Hospitali ya Imam Khomeini mjini Ilam. Shambulio hilo, ambalo picha zake zilitolewa Jumapili, limekosoolewa vikali, huku Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani ikilitaja kama “kosa la wazi dhidi ya binadamu.”

    Baada ya matukio haya, Wizara ya Afya ya Iran ilitoa taarifa Jumatatu, Januari 5, ikisema: “Baada ya tukio lililotokea katika hospitali ya Ilam, kwa amri ya wazi ya Waziri wa Afya, mgongano katika kituo hiki cha matibabu unafanyiwa uchunguzi makini na wa kina, na matokeo yake yatafuatiliwa kwa mujibu wa sheria.”

    Wizara hiyo ilisisitiza:

    “Kuzingatia usalama wa vituo vya matibabu, haki za wagonjwa, na kuunga mkono wafanyakazi wa afya ni ahadi thabiti ya Wizara ya Afya. Ukiukaji wowote wa haki hii ya binadamu utashughulikiwa kisheria. Hospitali, mabasi ya wagonjwa, na vifaa vya matibabu ni mali za umma na sehemu salama zinazomilikiwa na wananchi wote, na lazima zibaki salama dhidi ya uvamizi, mvutano, na migongano katika hali zote.”

    Shirika la habari la Fars, linalohusiana na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi, limethibitisha operesheni ya maafisa wa usalama na shambulio lao katika hospitali, likiandika kuwa waandamanaji walitumia hospitali hiyo kama kizuizi.

    Ripoti ya Fars inasema: “Usiku uliopita, wakati wa operesheni ya maafisa wa usalama, waandamanaji kadhaa walikamatwa ndani ya hospitali na maeneo yake jirani.

    Maafisa wa usalama na wa sheria kwa sasa wanajitahidi kurejesha amani kamili katika kituo hiki cha matibabu na maeneo yanayozunguka.”

    Jumapili, Januari 4, Mtandao wa Haki za Binadamu wa Kurdistan ulitangaza kuuawa kwa Rasoul Kadivorian na kujeruhiwa kwa raia wengine angalau 10 wakati wa maandamano katika mtaa wa Jafarabad, Kermanshah, siku chache zilizopita.

    Maandamano haya yalianza Jumapili, Januari 27, baada ya wafanyabiashara kadhaa mjini Tehran kupinga ongezeko la bei ya dola na kushuka kwa thamani ya rial, na yakasambaa haraka katika miji mingine.

    Uchumi wa Iran uko katika matatizo makubwa, huku kukiwa na matarajio madogo ya kukua mwaka huu au ujao.

    Mfumuko wa bei rasmi wa kila mwaka unasimama karibu 42%, mfumuko wa bei ya vyakula unazidi 70%, na baadhi ya bidhaa za kimsingi zimeripotiwa kupanda kwa bei kwa zaidi ya 110%.

    Soma pia:

  16. Chrystia Freeland wa Canada kujiuzulu kama mbunge na kuwa mshauri wa Zelensky

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Makamu wa zamani wa Waziri Mkuu wa Canada, Chrystia Freeland, amethibitisha kuwa atajiuzulu bungeni ili kukubali nafasi ya mshauri wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

    Freeland alisema kuwa jukumu lake kama mshauri wa maendeleo ya kiuchumi kwa Ukraine litakuwa bila malipo.

    Aidha, mwezi Julai atachukua wadhifa wa kuongoza Rhodes Trust, shirika la hisani linalojihusisha na elimu lililoko Uingereza.

    Alichaguliwa bungeni mwaka 2013 na amehudumu katika nyadhifa muhimu ikiwemo Waziri wa Fedha, Waziri wa Mambo ya Nje, na Waziri wa Biashara ya Kimataifa chini ya Waziri Mkuu wa zamani, Justin Trudeau.

    Mwisho mwa 2024, Freeland alitofautiana na Trudeau, akimlaumu katika barua yake ya kustaafu hadharani kwa kushindwa kuchukulia kwa umakini tishio la ushuru wa Marekani, jambo lililoisaidia kuharakisha kuondoka kwake kisiasa.

    Alichapisha katika mtandao wa X Jumatatu: “Ukraine iko mstari wa mbele katika mapambano ya kidemokrasia duniani. Ninakumbatia fursa hii ya kuchangia bila malipo kama mshauri wa kiuchumi kwa Rais Zelensky.

    “Katika wiki zijazo pia nitaondoka bungeni. Ninashukuru wapigakura wangu kwa imani yao katika miaka yote. Nimejisikia heshima kubwa kuwa mwakilishi wenu.”

    Mbali na kujiuzulu kama Mbunge wa kiti cha University-Rosedale cha Toronto, kilicho kisiwa salama kwa Wabunge wa Liberal, Freeland pia atajiuzulu wadhifa wake wa ziada kama Mwakilishi Maalum wa Canada kwa ajili ya ukarabati wa Ukraine.

    Mapema Jumatatu, Zelensky alitangaza kuwa Freeland atachukua nafasi ya mshauri, akibainisha kuwa ana “uzoefu mkubwa katika kuvutia uwekezaji na kutekeleza mabadiliko ya kiuchumi.”

    Tangazo la Zelensky liliibua wito kutoka kwa wanasiasa wa upinzani kwa Freeland kujiuzulu.

    Mkosoaji wa mambo ya nje wa chama cha Conservative, Michael Chong, alisema: “Hawezi kuwa Mbunge wa Canada na mshauri wa serikali ya kigeni. Lazima achague moja kati ya hiyo miwili.”

    Mnamo Novemba ilitangazwa kuwa msimu huu wa joto, Freeland atakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Rhodes Trust, shirika linalosimamia ufadhili wa masomo ya Rhodes kwa Chuo Kikuu cha Oxford.

    Mnamo Septemba, aliijiuzulu kama Waziri wa Usafirishaji na Biashara ya Ndani wa Carney kuchukua nafasi mpya kama Mwakilishi Maalum wa Canada kwa Ukraine, na alitangaza kuwa hatagombea katika uchaguzi mkuu ujao.

    Kama mwandishi wa habari wa zamani mwenye asili ya Kiyukraine, Freeland amekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono Kyiv katika vita vyake na Urusi.

    Mnamo 2014, aliwekwa kwenye orodha ya Kremlin ya Wamagharibi waliokatazwa kuingia Urusi kama kisasi kwa vikwazo dhidi ya Moscow.

    Mnamo 2020, Freeland alikua mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Waziri wa Fedha nchini Canada, akisimamia majibu ya kifedha ya serikali kwa janga la Covid-19.

    Pia anatambulika kwa kusaidia upya makubaliano ya sasa ya biashara huru kati ya Canada, Marekani, na Mexico wakati wa muhula wa kwanza wa Rais Donald Trump mwaka 2018.

    Makubaliano ya USMCA (au CUSMA nchini Canada) yamechangia kuepuka kiwango kikali cha ushuru cha asilimia 35 kilichowekwa na Trump, aliyeipa Canada msamaha kwa bidhaa zilizo chini ya makubaliano hayo.

    Makubaliano hayo sasa yamepangwa kwa mzunguko mwingine wa mazungumzo mwaka huu.

    Soma pia:

  17. Mahakama Kuu ya Guinea yathibitisha ushindi wa Mamady Doumbouya

    Mamady alikuwa ametangaza kutoshiriki uchaguzi za urais lakini baadaye akabadilisha maamuzi na kuwania.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mamady alikuwa ametangaza kutoshiriki uchaguzi za urais lakini baadaye akabadilisha maamuzi na kuwania.

    Mahakama Kuu ya Guinea imethibitisha ushindi mkubwa wa uchaguzi kwa kiongozi wa junta, Mamady Doumbouya.

    Uamuzi huu sasa unafungua njia kwa aliyekuwa kamanda wa vikosi maalum kuhudumu kwa muhula wa miaka saba kama rais wa nchi yenye rasilimali nyingi za madini.

    Uamuzi huo ulitangazwa mwishoni mwa Jumapili, ukithibitisha matokeo ya muda wa uchaguzi wa Desemba 28 yaliyoonyesha Koloneli Doumbouya akipata asilimia 86.72 ya kura zote zilizopigwa.

    Uchaguzi huo uliripotiwa kupuuzwa na baadhi ya makundi ya upinzani na ukakosolewa na wagombea wa upinzani.

    Mahakama pia ilitangaza kuwa mshindi wa pili, Abdoulaye Yero Baldé, ameondoa changamoto yake ya kisheria dhidi ya matokeo.

    Baldé, kiongozi wa Democratic Front of Guinea, awali aliwaomba majaji kufutilia mbali matokeo ya kura, akidai kutokuwepo uwazi na kuondolewa kwa wajumbe wa chama chake katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

    Baldé alimaliza nafasi ya pili akipata asilimia 6.59 ya kura, katika mchuano wa wagombea nane.

    Wanasiasa kadhaa wa upinzani tayari walikataa mchakato huo, wakisema ulikuwa na mapungufu.

    Rais wa zamani, Alpha Condé, ambaye bado yuko uhamishoni, alielezea uchaguzi huo kama “tamasha la utani” katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, akirudia wasiwasi ulioibuliwa na wafuasi wa upinzani mitandaoni.

    Kiongozi wa junta ya Guinea, anayesemekana kuwa na umri wa miaka 40 hivi, alikuwa mkuu wa walinzi maalum wa rais Alpha Condé. Alimshusha madarakani aliyekuwa kiongozi wake, ambaye alikuwa madarakani kwa zaidi ya muongo mmoja, kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo Septemba 2021.

    Kutwaa madaraka kuliweka Guinea miongoni mwa idadi inayoongezeka ya nchi za Afrika Magharibi – ikiwa ni pamoja na Mali, Burkina Faso, na Niger, ambapo jeshi limeingilia siasa katika miaka ya karibuni.

    Baada ya uamuzi wa mahakama, Koloneli Doumbouya ametoa wito wa umoja na kuhamasisha Waguinea nyumbani na walioko ughaibuni kuungana ili kujenga Guinea mpya.

    Uchaguzi huu ulifanyika kama sehemu ya mchakato wa mpito uliotangazwa na junta, baada ya shinikizo kubwa kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na washirika wa kimataifa kurejesha utawala wa kiraia.

    Hata hivyo, wakosoaji wanasema kura hiyo haikuwa na uwazi, wakionyesha vikwazo vilivyowekwa kwenye shughuli za kisiasa, kutokuwepo kwa waangalizi wa kimataifa, na utawala wa kijeshi uliodhibiti mchakato.

    Guinea ni nchi yenye rasilimali nyingi za asili, ikiwa ni pamoja na bauxite na chuma, na imekabiliwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa kwa miongo licha ya utajiri wake wa madini.

    Uthibitisho wa ushindi wa Koloneli Doumbouya unaonekana kuendeleza mjadala kuhusu iwapo nchi hiyo kwa kweli imejiridhisha na kurudi kwenye utaratibu wa katiba au ikiwa ni kurasimisha utawala wa kijeshi unaoendelea.

    Soma pia:

  18. AFCON 2025: Nigeria yaivaa Msumbiji kwa ushindi mnono wa 4-0

    Mabao mawili ya Victor Osimhen yalimfanya afikishe mabao matatu kwenye fainali za Afcon 2025

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mabao mawili ya Victor Osimhen yalimfanya afikishe mabao matatu kwenye fainali za Afcon 2025

    Nigeria ilijihakikishia tiketi ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Msumbiji katika dimba la Fes.

    Super Eagles walitawala mchezo kuanzia mwanzo, huku mshambuliaji wao nyota Victor Osimhen akifunga bao lililofutwa kwa kosa la kuotea ndani ya dakika mbili za mwanzo.

    Mashambulizi ya Nigeria yaliendelea kuisumbua Msumbiji hadi dakika ya 20, ambapo Ademola Lookman alipachika bao la kwanza kwa mkwaju wa kiufundi, akimalizia pasi ya kurudishwa nyuma kutoka kwa Akor Adams.

    Dakika tano baadaye, Osimhen aliongeza bao la pili baada ya Alex Iwobi kuonyesha ubora wake katikati ya uwanja, kumuunga na pasi Lookman ambaye pasi yake ilimgonga Adams kabla ya Osimhen kuutumbukiza mpira wavuni.

    Msumbiji, iliyokuwa ikishiriki hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza, ililemewa na kasi na ubora wa Nigeria, ikishindwa kuleta upinzani wa maana mbele ya lango.

    Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ileile, Osimhen akifunga bao lake la pili na la tatu kwa Nigeria, akimalizia pasi safi ya Lookman kwenye nguzo ya pili kutoka upande wa kushoto.

    Akor Adams alikamilisha karamu ya mabao dakika ya 75, akifunga bao la nne baada ya kazi nzuri tena kutoka kwa Lookman, aliyekuwa mhimili wa ushindi huo.

    Nigeria, ambayo ingeweza kuongeza mabao zaidi, sasa inasubiri mshindi kati ya Algeria au DR Congo katika robo fainali itakayochezwa Jumamosi mjini Marrakech saa 16:00 GMT.

    Soma zaidi:

  19. Rais wa mpito aapishwa Venezuela, Maduro akikana mashitaka Marekani

    Delcy Rodríguez

    Chanzo cha picha, Reuters/Getty Images

    Delcy Rodríguez ameapishwa kuwa rais wa mpito wa Venezuela katika kikao cha bunge kilichoanza kwa wito wa kuachiliwa kwa rais aliyeondolewa na kuzuiliwa nchini Marekani Nicolás Maduro.

    Rodríguez, 56, makamu wa rais tangu 2018, alisema aliumizwa na kile alichokiita "kutekwa nyara" kwa Maduro na mkewe Cilia Flores ambao walikamatwa na vikosi vya Amerika katika uvamizi wa usiku wa Jumamosi.

    Katika matukio ya kushangaza ndani ya chumba cha mahakama jijini New York saa kadhaa hapo awali, Maduro alisisitiza kuwa bado ni rais wa Venezuela huku akikana mashtaka manne ya ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi.

    Marekani imekosolewa vikali mkali Umojnaa wa Mataifa, lakini balozi wa Marekani alisema hifadhi kubwa zaidi ya nishati duniani haiwezi kuachwa mikononi mwa kiongozi haramu, " mkwepaji haki".

    Kabla ya Maduro kufikishwa mahakamani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura kujadili hali ya Venezuela.

    Balozi wa Venezuela, Samuel Moncada, alisema nchi yake imekuwa ikilengwa na "shambulio haramu la silaha lisilo na uhalali wowote wa kisheria".

    Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, alihalalisha shambulio hilo kwa kumtaja Maduro kama "rais haramu".

    Soma zaidi:

  20. Hujambo na Karibu