Kutekwa kwa Uvira na mustakabali wa utawala wa Évariste Ndayishimiye Burundi - Uchambuzi

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Hatua ya kundi la waasi la AFC/M23 kuuteka mji wa Uvira katika jimbo la mashariki la Kivu Kusini "itakuwa na athari kubwa kwa Burundi kwa njia tofauti", na kwa mustakabali wa utawala wa Rais Évariste Ndayishimiye, anasema mchambuzi wa kisiasa wa Marekani akiangazia mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Profesa Jason Stearns amabaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Simon Fraser nchini Canada, anasema kwamba Burundi tayari ilikuwa imetuma zaidi ya wanajeshi 10,000 - japo serikali ya haikufichua idadi hiyo - katika majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini, kwa makubaliano na serikali ya DRC, ambao walikuwa wakipigana upande wa serikali ya nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Édouard Bizimana alikuwa ameiambia redio ya Ufaransa RFI kabla ya Uvira kuangukia mikononi mwa waasi kwamba wanajeshi wangeondoka tu ikiwa serikali ya Kinshasa itawataka kufanya hivyo, kwani walikuwa wametia saini makubaliano nayo. Hata hivyo, kutekwa kwake siku ya Jumatano kuliwaacha wanajeshi hao bila chaguo jingine ila kuondoka.
Siku ya Ijumaa, kufuatia milipuko ya mabomu huko Cibitoke, Balozi Zéphyrin Maniratanga, mwakilishi wa Burundi katika Umoja wa Mataifa (UN), aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ikiwa hakuna kitakachofanyika, kuna hatari ya kuibuka kwa "makabiliano ya moja kwa moja" kati ya nchi yake na Rwanda.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Mike Waltz aliishutumu Rwanda katika mkutano huo kwa "kutishia kulitumbukiza eneo hilo vitani" kwa kuwasaidia na kuwaongoza M23.
Serikali ya Rwanda imekanusha mara kwa mara kwamba inaunga mkono M23, ikisema tu kwamba imeweka "hatua za usalama." Balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa Martin Ngoga amesema nchi hiyo haina mpango wa kuivamia Burundi. Hapo awali, M23 pia ilisema haikuwa na mipango kama hiyo.
Siku ya Jumamosi, Marekani ililaani vitendo vya Rwanda mashariki mwa Congo, na kuahidi kuchukua hatua kuhakikisha kuwa makubaliano ya amani ya Washington yanaheshimiwa.
Katika mahojiano ya simu na Mtandao wa Habari wa BBC siku ya Ijumaa, Profesa Stearns alisema kukamatwa kwa Uvira kulikuwa na "athari kubwa" kwa Burundi, akisema ni moja ya washirika muhimu wa DRC.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anasema kwamba wanajeshi wake walipigana pamoja na vikosi vya serikali (FARDC) "vita vya Rwanda na M23". Alisema: "Sasa Burundi imeondolewa kwenye uwanja wa vita kwa sababu Uvira ndiko walikopita hadi kufika Kongo.
"Kwa hiyo kama Burundi itasalia [katika vita] au la, hilo ni swali [la kuulizwa]. Sasa, usalama wa Burundi pia unaweza kuwa suala."
Anasema kutekwa kwa Uvira ni "faida kubwa ya kwanza ya eneo" M23 imepata tangu ilipouteka mji wa Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Februari (2) mwaka huu, ambayo iliongezwa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, ambayo M23 iliuteka mwishoni mwa Januari (1) mwaka huu.
Profesa Stearns anasema kwamba Burundi ilikuwa imepenya ndani zaidi ya Congo kuliko Kivu Kusini, ambako waasi wa Burundi pengine walikuwa wamekwenda kupigana, na kwamba ilikuwa na wanajeshi huko Kivu Kaskazini. Rwanda inashutumiwa kwa kuwasaidia waasi wa RED-Tabara, madai ambayo inakanusha.
Uhusiano kati ya Burundi na Rwanda umedorora tangu 2015 wakati Gitega alipoishutumu Kigali kwa kushiriki katika jaribio la mapinduzi lililofeli nchini Burundi na kuwahifadhi baadhi ya viongozi, tuhuma ambayo Rwanda imekuwa ikikanusha.
Gitega aliendelea kuitaka Kigali kuwarudisha wale anaowatuhumu kwa kujaribu kufanya mapinduzi ili kujibu mashtaka, jambo ambalo Kigali haijafanya hadi sasa.
"Kwa kuteka jiji la Uvira na Bonde la Ruzizi, huo ndio mpaka wa ardhi yote [Congo inashiriki] na Burundi ambayo sasa inadhibitiwa na Rwanda na M23," Profesa Stearns alisema.

Chanzo cha picha, SIMON FRASER UNIVERSITY
Mchambuzi huyu anasema Uvira ni kitovu cha kibiashara cha Brundi na mauzo yake mengi kwenda Congo yanapitia mji huo kwamba kiasi kikubwa cha fedha za kigeni na dhahabu zinaingia Burundi kupitia Uvira.
"Kwa kudhibiti uvira M23 imepata uwezo mkubwa dhidi ya serikali ya Burundi, nguvu ya kiuchumi, katika nchi ambayo tayari inakabiliwa na migogoro ya kijamii na kiuchumi," alisema.
"Ni wazi kwamba Rwanda sasa inadhibiti mipaka ya kaskazini na magharibi na hili bilashaka ni suala la usalama ambalo linazua tumbo joto kwa serikali ya Burundi."
"Lakini nadhani jambo muhimu zaidi, pamoja na hilo, ni usalama wa ndani [nchini Burundi]."
Profesa Stearns anasema kuwa wanajeshi waliotumwa na Burundi nchini DR- Congo, idadi ya waliouawa na kujeruhiwa inaweza kufikia maelfu. Jeshi la Burundi halijawahi kutoa takwimu ya wanajeshi wake waliouawa au kujeruhiwa.
"Hii imesababisha matatizo kwa serikali ya Burundi, ndani kati yake na jeshi lake, pamoja na majenerali wakuu na wananchi kwa ujumla, ambao hawaelewi kikamilifu kwa nini Burundi inafanya haya yote," alisema.
"Kwa hiyo suala hilo linakwenda zaidi ya mgogoro wa kijamii na kiuchumi ambao wanakabiliana nao kwa sasa [kama Burundi]. Mgogoro huu wa ndani [kati ya utawala] na makamanda wenye nguvu, nadhani hilo pia litakuwa tatizo kwa Rais Ndayishimiye."
Serikali ya Burundi haijawahi kutoa kauli yoyote ya kuibuka kwa mvutano kati yake baadhi ya maafisa wake wa kijeshi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Ndayishimiye alikuwa miongoni mwa maafisa waliohudhuria utiaji saini wa makubaliano ya amani kati ya Rwanda na DR Congo mjini Washington DC Desemba 4, ambayo yalitiwa saini na Rais Paul Kagame na Rais Félix Tshisekedi, chini ya uangalizi wa Rais wa Marekani Donald Trump.
Ni makubaliano yenye lengo la kumaliza vita mashariki mwa DRC ambayo yalizuka tena tena mwishoni mwa 2021, baada ya karibu miaka 30 ya kudorora kwa usalama. Rais Trump aliusifia akiutaja kuwa "muujiza" ambao umetokea.
Baada ya M23 kuuteka mji wa Uvira, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Édouard Bizimana alisema hatua hiyo ni "kofi usoni... [akionyesha] kidole cha ukuu [ishara ya dharau]" kwamba hatua za Marekani zilizosababisha makubaliano ya amani.
"Kutia saini makubaliano na kisha kutotekeleza ni dharau kwa kila mtu, haswa Rais Trump," aliambia AFP.
Profesa Stearns anaunga mkona hoja hii. Anasema: "[Rais] Donald Trump amekuwa akihimiza utiaji saini wa amani Desemba 4, [akisema] kwamba sasa [Kagame na Tshisekedi] wataishi pamoja kwa amani, na kutangaza kwamba haya ni makubaliano mengine ya amaya kihistoria, japo mchakato huo ulipokuwa ukiendelea, majeshi ya Rwanda yalikuwa yakisonga mbele kuelekea Uvira."
Profesa Stearns aidha anasema kuwa kutekwa kwa mjimwa Uvira kumeikasirisha mamlaka ya Marekani na kwamba huenda Rwanda ikakabiliwa na vikwazo zaidi katika siku zijazo.
Lakini, kwa sasa, mpango wa amani wa Congo unaosimamiwa na Washington unakabiliwa na utata.
"Ingekuwa bora kama mkataba huo haungetelekezwa kabisa," alisema.
Waziri wa mambo nje ya Marekani Marco Rubio alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba hatua ya Rwanda mashariki mwa DRC ni "ukiukaji wa wazi" wa makubaliano ya Washington yaliyoongozwa na Rais Trump na kuongeza kwamba Marekani itachukua hatua kuhakikisha kuwa ahadi za Rais zinazingatiwa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) iliripoti kuwa zaidi ya watu 500,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano katika muda wa wiki moja, wakikimbia ndani ya nchi hiyo na kuelekea nchi zinazopakana na Congo.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












