Wajue marais wa Afrika walioshinda kwa zaidi ya asilimia 90

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ushindi wa kishindo ni matokeo ya uchaguzi ambapo mgombea au chama kinachoshinda kinapata wingi wa kura au viti vingi, na kuwaacha wapinzani wakiwa na sehemu ndogo sana ya kura.
Rais Samia Suluhu Hassan, miongoni mwa marais walioshinda kwa kishindo katika historia ya bara la Afrika. Wafuasi wake wanasema hiyo ni ishara ya kukubalika kwakwe miongoni mwa watanzania, ingawa halionekana kwa jicho la namna hiyo na wapinzani wake wa ndani na nje ya nchi.
Ni mara chache sana wanasiasa hupata ushindi wa kishindo wa asilimia 90 ya kura. Lakini katika nchi za Afrika, wapo viongozi hasa marais ambao ushindi wao umefika asilimia 90 au kuzidi katika uchaguzi mkuu.
Wakati tukijadli viongozi waliopata ushindi wa zadi ya asilimia 90, swali linaloibuka: Je, ushindi wa viongozi hawa huakisi kukubalika kwao, au kuminywa kwa demokrasia nyuma ya pazia yanayosukuma ushindi huu?
Brice Oligui Nguema - Gabon

Chanzo cha picha, FRANCE24
Katika uchaguzi wa mwezi April mwaka huu, Brice Oligui Nguema, ambaye aliongoza mapinduzi nchini Gabon Agosti 2023, alishinda uchaguzi wa rais kwa 90.35% ya kura zilizopigwa, kulingana na matokeo katika nchi hiyo Afrika ya Kati.
Matokeo hayo yanaimarisha nguvu ya Nguema baada ya mapinduzi ya kumaliza zaidi ya nusu karne ya utawala wa familia ya Bongo nchini Gabon, nchi ambayo ni mzalishaji wa mafuta yenye wakazi wapatao milioni 2.5.
Mpinzani mkubwa wa Nguema katika kinyang'anyiro cha wagombea wanane alikuwa Alain Claude Bilie By Nze, ambaye alikuwa waziri mkuu chini ya Rais Ali Bongo wakati wa mapinduzi. Nze, 57, alimaliza kwa 3.02% ya jumla.
Teodoro Mbasogo- Equatorial Guinea

Novemba 2022, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo alichaguliwa tena kuwa Rais wa Equatorial Guinea kwa 94.9% ya kura, ikiwa ni muhula wake wa sita madarakani.. Matokeo haya yalitangazwa na tume ya uchaguzi baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 20, 2022.
Ingawa baadhi ya wagombea wa upinzani walishiriki, uungwaji mkono wao ulikuwa mdogo, na chama tawala pia kilishinda viti vyote katika Bunge la Kitaifa na Seneti. Katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta, Obiang yuko madarakani tangu mapinduzi ya kijeshi ya 1979.
Matokeo ya uchaguzi yalikabiliwa na "mashaka makubwa" kutoka Marekani na waangalizi wengine wa kimataifa, ambao walitaja madai ya ukiukwaji mkubwa wa taratibu, vitisho, na udanganyifu.
Paul Kagame - Rwanda

Chanzo cha picha, Kigali Today
Julai 2024 Rais wa Rwanda Paul Kagame alishinda uchaguzi wa Rwanda kwa kishindo. Kagame alipata 99.1% ya kura, hilo liliongeza utawala wake wa miaka 24 kwa miaka mingine mitano zaidi.
Rais alikuwa akishindana na wagombea wachache ambao waligawana 1% ya kura kati yao. Kagame ameshinda zaidi ya 90% ya kura mwaka 2003, 2010 na 2017.
Kagame amesifiwa kwa kuleta umoja, amani na utulivu. Wakosoaji wake ingawa wanamshutumu kwa udikteta. Serikali ya Rwanda imekana kufanya udikteta wowote.
Alassane Ouattara - Ivory Coast

Chanzo cha picha, britannica
Oktoba mwaka huu Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara alishinda muhula wa nne kwa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa marudio, matokeo ambayo yalitarajiwa kwa kiasi kikubwa.
Mchumi huyo wa zamani wa benki ya kimataifa mwenye umri wa miaka 83 alipata 89.77% ya kura, ukiwa ni ushindi wake wa tatu mfululizo baada kuingia madarakani mwaka 2011.
Waziri wa zamani wa Biashara Jean-Louis Billon, ambaye alikubali kushindwa na Ouattara alipata 3.09% ya kura, huku mke wa rais wa zamani Simone Gbagbo akipata 2.42%, kulingana na matokeo.
Samia Suluhu Hassan - Tanzania

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitangazwa wiki iliyopita kuwa mshindi wa kishindo katika uchaguzi ambao ulizua maandamano makubwa .
Tume ya uchaguzi ya taifa hilo la Afrika Mashariki ilisema Hassan, ambaye alichukua madaraka mwaka 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, alipata zaidi ya kura milioni 31.9, sawa na asilimia 97.66 ya kura zote, na kumpa muhula wa miaka mitano.
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA - ambacho kilizuiwa kushiriki uchaguzi kwa kukataa kutia saini kanuni za maadili na kiongozi wake kukamatwa kwa tuhuma za uhaini mwezi Aprili. CCM, chama tawala na mamlaka za uchaguzi zinasema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki, licha ya malalamiko na vurugu zilizotokea kuanzia siku ya uchaguzi.
Hii ina maana gani?
Mchanganyiko wa mambo – kama vile uongozi wenye mvuto , kuridhika kwa umma au uungwaji mkono wa mwanasiasa , kampeni za kimkakati na taswira chanya ya vyombo vya habari – haya yote yanaweza kuchangia ushindi wa kishindo.
Kwa upande mwingine, ushindi wa kishindo unaweza kuja kutokana wizi wa kura, na mambo mengine ambayo yanaweza kuufanya uchaguzi huo utafsiriwe na waangalizi kuwa haukuwa huru wala wa haki.
Bilashaka kila uchaguzi unahitaji tathmini yake, hatuwezi kuwaingiza viongozi hawa katika tathmini moja. Lakini jambo moja linaloweza kukupa picha kuhusu ukweli juu ya ushindi wa asilimia 90, ni kutazama ripoti za waangalizi huru wa chaguzi hizo na pia kutazama hali ya vyama vya upinzania katika nchi hizo.















