Wajue marais watano wa Afrika waliouawa baada ya kupinduliwa

df

Chanzo cha picha, AFP

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kama yalivyo maeneo mengine ya dunia, bara la Afrika halijasalimika na mapinduzi ya kiraia na kijeshi. Lakini wakati mwingine mapinduzi haya, hupelekea mauaji ya wanaopinduliwa.

Miongoni mwao wapo marais ambao walipinduliwa lakini roho zao zikasalimika, wapo ambao waliponea katika tundu la sindano, na wengine bahati hazikuwa za kwao, wakaishi kuuawa.

Makala hii inaangazia orodha ya marais watano waliouawa barani Afrika, baada ya serikali zao kuzindiwa nguvu na kuondolewa madarakani, tangu mataifa ya Afrika yapate uhuru:

Pia unaweza kusoma

Sylvanus Olympio, Togo

rtf

Chanzo cha picha, SIPA

Maelezo ya picha, Sylvanus Olympio wa Togo mwezi Machi 1962.

Sylvanus Épiphanio Olympio, alizaliwa tarehe 6 Septemba 1902. Familia ya Olympio ilikuwa moja wapo ya familia tajiri nchini Togo mwanzoni mwa miaka ya 1900.

Alisoma na kuhitimu London School of Economics. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Olympio alipata umaarufu mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru wa Togo na chama chake kilishinda uchaguzi wa 1958, na kumfanya kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.

Nguvu yake iliimarika zaidi pale Togo ilipopata uhuru na akashinda uchaguzi wa 1961, na kumfanya kuwa rais wa kwanza wa Togo.

Tarehe 13 Januari 1963, Olympio na mke wake waliamshwa na wanajeshi waliokuwa wakivunja nyumba yao. Aliuawa 1963, miaka mitatu tu baada ya kuchukua madaraka.

Mwili wa Olympio ulipatikana na Balozi wa Marekani Leon B. Poullada futi tatu kutoka mlango wa Ubalozi wa Marekani. Akawa Rais wa kwanza kuuawa baada ya mapinduzi barani Afrika.

William Tolbert, Liberia

fd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, William Tolbert Jr, akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1976.

William Richard Tolbert alizaliwa 13 Mei 1913, alikuwa mwanasiasa wa Liberia na rais wa 20 wa Liberia kuanzia 1971 hadi mwaka 1980.

Tolbert aliingia katika Baraza la Wawakilishi mwaka 1943 kupitia chama cha True Whig, kikiwa chama pekee kilichoanzishwa nchini Liberia wakati huo. Tolbert alichaguliwa kuwa makamu wa rais wa 23 wa Liberia chini ya rais William Tubman mwaka 1952 na alihudumu katika nafasi hiyo hadi alipokuwa rais kufuatia kifo cha Tubman mwaka 1971.

Mapema tarehe 12 Aprili 1980, maofisa 17 wa Jeshi la Liberia wakiongozwa na Sajenti Samuel Doe walianzisha mapinduzi. Kundi hilo liliingia katika Ikulu ya Rais na kumuua Tolbert, na mwili wake ulitupwa kwenye kaburi la pamoja na wahanga wengine 27 wa mapinduzi hayo. Mwili wa Tolbert baadaye ulitolewa na kupelekwa Monrovia kwa mazishi rasmi.

Thomas Sankara, Burkina Faso

df

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Thomas Sankara kwa mkutano mmoja wa kilele mwaka 1983.

Thomas Isidore Noël Sankara, alizaliwa tarehe 21 Desemba 1949 , alikuwa afisa wa kijeshi wa Burkinabè, mwanamapinduzi wa Ki-Marxist na mwanamajumui wa Kiafrika ambaye aliwahi kuwa Rais wa Burkina Faso.

Baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1983, mizozo na serikali iliyo madarakani ilisababisha Sankara kufungwa. Akiwa katika kifungo cha nyumbani, kikundi cha wanamapinduzi kilichukua mamlaka kwa niaba yake katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na watu wengi.

Katika umri wa miaka 33, Sankara alikua Rais na kuzindua mageuzi ya kijamii, mazingira na kiuchumi. Sera zake za kigeni zilijikita katika kupinga ubeberu na alikataa mikopo kutoka kwa mashirika kama vile IMF. Hata hivyo alikaribisha baadhi ya misaada kutoka nje katika jitihada za kukuza uchumi wa ndani.

Tarehe 15 Oktoba 1987, Sankara na maafisa wengine kumi na wawili waliuawa katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoandaliwa na Blaise Compaoré.

Samuel Doe, Liberia

edfc

Chanzo cha picha, Samuel Foundation

Samuel Kanyon Doe alizaliwa 6 Mei 1951, alikuwa mwanasiasa na afisa wa kijeshi wa Liberia na Rais wa Liberia kuanzia 1986 hadi 1990.

Utawala wa Doe ulikuwa na sifa ya ubabe, ufisadi, na upendeleo kwa kabila la Krahns, jambo ambalo lilisababisha upinzani mkubwa dhidi ya utawala wake kutoka kwa wa -Liberia waliohamia kutokea Marekani.

Vita vya Kwanza vya wenyewe kwa wenyewe vya Liberia vilianza Desemba 1989 wakati chama cha National Patriotic Front of Liberia (NPFL) kinachoongozwa na Charles Taylor kilipoivamia Liberia kutoka Ivory Coast na kumpindua. Doe alitekwa na kuuawa tarehe 9 Septemba 1990.

Muammar Gaddafi, Libya

dfxc

Chanzo cha picha, EPA

Muammar Muhammad Abu Minyar al-Gaddafi alizaliwa 1942, alikuwa mwanamapinduzi na mwanasiasa wa Libya aliyetawala Libya kuanzia 1969 hadi kuuawa kwake na vikosi vya waasi mwaka 2011.

Alikuwa kiongozi wa Libya kwa zaidi ya miaka 40, alikamatwa na kuuawa na vikosi vya waasi Oktoba 20, 2011, baada ya kuondolewa madarakani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Libya. Uingiliaji kati wa NATO, kupitia mashambulizi ya anga, ulichangia pakubwa katika kudhoofisha utawala wake, na kusababisha kifo chake.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Seif Abdalla