Wafahamu marais waliobadili sera za watangulizi wao Afrika

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
Mwezi Machi mwaka huu Bi Samia Suluhu Hassan ameandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Tanzania.
Mama Samia ambaye alikuwa Makamu wa Rais toka 2015, pia ameandika historia ya kuingia madarakani baada ya kufariki kwa rais aliyekuwepo madarakani, John Pombe Magufuli.
Mara baada ya kushika hatamu, Rais Samia amekuwa akijipambanua kwa staili ya uongozi tofauti na ya mtangulizi wake Hayati Magufuli. Utofauti huo si kwenye sera tu bali hata katika mambo masuala kama uzungumzaji, namna ya kufikisha ujumbe, uungwana na katika mambo mengine madogo madogo wakiwamo wasaidizi wake wanaoonekana naye kila siku.
Katika sera, ameanza na kutaka mabadiliko ya hali ya mahusiano na nchi za nje akitaka yaboreshwe zaidi na kuvutia wawekezaji, kupanua uhuru wa habari na kutaka ubabe usitumike katika ukusanyaji wa kodi. Pia amekemea watu kubambikiwa kesi za uhujumu uchumi na kuitaka malaka ya kupambana na rushwa kuachana na kesi ambazo hazina ushahidi wa kutosha.
Yawezekana kubwa kuliko yote ni nia yake ya kulipatia ufumbuzi suala la janga la corona nchi humo. Utawala wa Rais Magufuli ulishutumiwa vikali kwa kutochukua hatua stahiki kupambana na janga hilo, lakini sasa Mama Samia amesema ataunda kamati ya wataalamu kushauri serikali yake nini cha kufanya juu ya janga hilo.
Hatua hizo zimezua mjadala mkubwa ndani na nje ya Tanzania. Lakini Tanzania si nchi ya kwanza kuona hali kama hiyo, mwaka jana rais wa Burundi Pierre Nkurunziza alifariki miezi michache kabla ya kutoka madarakani, na nafasi yake ikachukuliwa na Evariste Ndayishimiye ambaye alishinda uchaguzi kabla ya kifo cha Nkurunziza.
Nkurunziza pia pia alituhumiwa kwa kutozingatia tahadhari dhidi ya corona, mara baada ya mrithi wake kuingia amadarakani alichukua hatua kadhaa kubadili hali ya mambo. Pia alianzisha mazungumzo ya kuboresha mahusiano na taifa jirani na hasimu la Rwanda. Na hivi karibuni utawala wake umeonekana kuonesha dalili za kutanua wigo wa uhuru wa vyombo vya habari kwa kuvifungulia vyombo vya ndani vilivyofungiwa kwenye utawala uliopita.
Japo mifano ya Tanzania na Burundi mabadiliko hayo yametokea wakati watangulizi wakiwa wamefariki dunia zipo nchi za Afrika ambazo mabadiliko ya uongozi yalifanyika kwa bashasha huku watangulizi wakiamini warithi wao wataendeleza pale walipoachia ama hata kuwalindia maslahi yao watakapoingia madarakani. Hata hivyo hali ya mambo ikabadilika na warithi wakabadili sera za watangulizi bila kificho. Katika baadhi ya nchi hali hiyo ikazaa na mizozo mikubwa ya kisiasa.
Angola - Jose Eduardo dos Santos na João Lourenço
Baada ya kuiongoza Angola kwa miaka 38 kuanzia mwaka wa 1979 hadi mwaka wa 2017, Rais wa zamani wa nchi hiyo Jose Eduardo dos Santos alitarajia kustaafu kwa amani na kumkabidhi mshirika wake João Lourenço madaraka kuchukua usukani kama rais .
Alikuwa mtu wa ndani na mwanajeshi aliyepokea mafunzo yake huko Urusi na majenerali wote jeshini pamoja na rais anayeondoka walikuwa wameridhika kwamba hapatakuwa na tatizo.

Alipochukua madaraka ya urais wa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta mnamo 2017 - na mara tu baada ya kuwa kiongozi wa MPLA inayotawala - matarajio yalikuwa kwamba atatikisa mambo kidogo, aanzishe mageuzi ya kiuchumi kwa tahadhari, azime ufisadi kwa njia ambayo haingewaogopesha majenerali wengi matajiri, kufufua sifa ya chama chake na kumwacha mtangulizi wake, Jose Eduardo dos Santos na familia yake, wafurahie milki zao za biashara kwa amani.
Kilichofuatia hakikuwashangaza tu wanaofuatilia siasa za nchi hiyo lakini pia kiliwashtua wote waliokuwa washirika wa rais huyo mpya kwani alianza msako mkali dhidi ya watu mashuhuri na wenye ushawishi waliodaiwa kupora mali ya umma . Hakumsaza yeyote na mtangulizi wake na familia yake walijipata katika upande mbaya wa sheria .
Wengi walijawa matumaini lakini kwa wale walioonekana kulengwa na kampeni hiyo ya rais mpya hofu iliwajaa na wengine wakatoroka Angola .
Lengo la kwanza, na maarufu zaidi la la kampeni hiyolilikuwa familia ya Dos Santos.
Iliwashangaza na kuwafurahisha Waangola wengi, ambao walikuwa wamechoka kutazama familia ya rais huyo wa zamani ikitajirika sana, angalau kwa sehemu kutoka kwa mikataba ya serikali, na ambao kwa muda mrefu walikuwa wameogopa uongozi wa kifamilia ambao rais huyo wa zamani alionekana kuutengeza kupitia mali na ushawishi wake .
Rais Lourenço - au JLo, kama anavyojulikana kwa Waangola wote - alifanya kwa kasi na kwa fujo mengi kuidhibiti mali na mikataba iliyokuwa ikiinufaisha "familia ya kwanza" ya mtangulizi wake .
Isabel dos Santos aliondolewa kutoka kwa kazi yake ya kuendesha kampuni kubwa ya mafuta ya serikali, Sonangol. Ndugu yake wa kambo alijipata katika hatma kama hiyo kwa kuondolewa kama mkuu wa mfuko mkuu wa utajiri wa serikali, na mara baadaye alijikuta kizuizini na sasa anakabiliwa na kesi ya kujaribu kusafirisha $ 500m (£ 380m) nje ya nchi.
Kisha baadaye ukafuata msururu wa hatua kali Zaidi dhidi ya familia ya Dos Santos ambapo mali ya bintiye Dos Santos na biashara zake zikaanza kuchukuliwa na serikali . badaye hata waranti ya kukamatwa kwake ilitolewa na mahakama .
Bi Dos Santos ameendelea kukana madai ya ufujaji au ufisadi na ametaja kampeini ya serikali iliyochukua utawala baada ya babake kama hila na yanayochochewa kisiasa .
Kwa hatua hizo ambazo hakuna aliyeweza kuzitabiri miaka ya hapo nyuma , Familia ya Dos Santos ilisambaratishwa na mpango wake wa kuendelea kuwa na ushawishi atika uongozi wa Angola ukafika mwisho .
DRC - Joseph Kabila na Felix Tshisekedi
Felix Tshisekedi alichukua usukani wa DR Congo katika kile ambacho wengi walihofia ulikuwa mundelezo wa utawala wa mtangulizi wake Joseph Kabila . Chama chake Kabila kilifanya ushirikiano wa kisiasa na chama cha rais huyo mpya na kumsaidia kushinda uchaguzi uliomleta madarakani .

Ilionekana kuwa haiwezekani kwa Tshisekedi kujitoa kutoka kivuli cha Kabila wakati aliposhika usukani wa nchi hiyo Januari 2019 - mwezi mmoja baada ya kushinda katika uchaguzi wa urais wakati palipokuwa na mashaka kutoka kwa waangalizi wa uchaguzi kwamba alikuwa amemshinda kwa kura nyingi mpinzani mkuu wa Kabila Martin Fayulu.
Tshisekedi alikuwa na nafasi ndogo ya kufanya ujanja: Kabila alikuwa madarakani tangu 2001, na alikuwa ameimarisha udhibiti wa taasisi kuu za DR Congo: jeshi, huduma za ujasusi, mahakama ya kikatiba na tume ya uchaguzi. Chama cha Kabila cha Common Front for Congo (FCC) kilidhibiti theluthi mbili ya viti vya bunge, na kumlazimisha Tshisekedi kuunda serikali ya muungano na chama chake cha walio wachache.
Lakini miaka mitatu baadaye Tshisekedi amefaulu kuwafursha kutoka nafasi kubwa na muhimu waliokuwa washirika wa mtangulizi wake na wabunge wengi wa FCC wamejiunga na chama kipya cha rais mpya ili kumpa uthabiti katika bunge
Wabunge hao walimtimua waziri mkuu aliyekuwa akiungwa mkono na Kabila Sylvestre Ilunga Ilunkamba kwa kura ya kutokuwa na Imani naye na kutoa ishara kwamba rais mpya sasa alikuwa huru kutoka kwa ushawishi wa mtanguli wake Kabila
Kabila amekaa kimya katika mchakato huu wote. Tangu kufutwa kazi kwa mshirika wake wa karibu Jeannine Mabunda kama mkuu wa Bunge, amekuwa akiishi katika shamba lake katika mkoa wa Katanga karibu na mpaka wa Zambia.
Kabila bado ni mtu mashuhuri nchini DR Congo. Yeye na familia yake wanadhibiti umiliki wa kampuni zaidi ya 80 zinazofanya kazi karibu katika kila sekta ya uchumi. Gécamines - kampuni kubwa zaidi ya madini nchini na inayotoa mchango mkubwa katika bajeti ya serikali - inaongozwa na mmoja wa luteni wa waaminifu wa rais wa zamani, Albert Yuma.
Botswana - Ian Khama Mokgweetsi Masisi
Katika hatua isiyokuwa ya kawaida katika demokrasia ya Botswana, rais wa zamani Ian Khama alipeleka vita kati yake na mrithi wake Mokgweetsi Masisi katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2019 .
Khama alikiunga mkono chama kipya kilichozinduliwa mwishoni mwa Mei kinachoitwa Botswana Patriotic Front (BPF), ambacho kilipunguza ufuasi wa chama tawala cha Masisi.

Baba ya Khama Seretse Khama alianzisha chama cha Botswana Democratic Party (BDP) mwanzoni mwa miaka ya 1960 na kimekuwa madarakani tangu 1966. Ian Khama alighadhabishwa na Masisi, ambaye Khama alimuunga mkono kuchukua nafasi yake kama kiongozi wa BDP, alichukua hatua za kupunguza ushawishi wake kama rais wa zamani na kumtimua mshirika wake muhimu, bosi wa zamani wa ujasusi Isaac Kgosi, ambaye alifunguliwa mashtaka mbali mbali .
Uhasama huo wa kisiasa kati ya kiongozi wa zamani na mrithi wake uliitia Botswana katika hali ya wasi wasi hadi uchaguzi ulipofanywa na Rais Masisi akashinda muhula mwingine ndiposa mambo yalipotulia lakini kwa muda tu .
Khama anadaiwa kuendelea kuwaongoza pembeni viongozi wengine wa vyama vya upinzani wanaoinga utawala wa Masisi uhasama wao utazidi kudhihirika katika mapambano yajayo ya kisiasa nchini humo












