'Huonekani, hupo' - maisha bila cheti cha kuzaliwa

Chanzo cha picha, Christian Parkinson / BBC
- Author, Mayeni Jones
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Watu wengi wana vyeti vya kuzaliwa, au karatasi rasmi za kuwatambulisha - lakini kwa wale wasio nazo, hilo linaweza kusababisha kuwa na maisha ya kutoonekana au maisha yasiyo na uhakika.
Kukosa cheti kunawaathiri mamilioni ya watu kote ulimwenguni, huitwa watu ‘wasio na utaifa’, na Arnold Ncube, Mu-Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 25, ni mmoja wa hao.
Kwa sababu hana hati zilizotolewa na serikali, hivyo kuosha magari katika mitaa ya mji wa Thembisa karibu na Johannesburg ni mojawapo ya njia chache anazoweza kuzitumia kujipatia riziki.
Alizaliwa Johannesburg na baba yake ni Mwafrika Kusini, jambo linalomfanya astahili kupata uraia. Lakini alipojaribu kujiandikisha shule ya upili, aligundua kuwa hana cheti cha kuzaliwa.
Baba yake alifariki kabla hajazaliwa na mama yake alifariki alipokuwa na umri wa miaka 14 – hivyo hakuweza kuthibitisha kuzaliwa kwake.
"Ni jambo gumu," anasema. "Kimsingi huonekani. Hupo. Ni kama unaishi gizani. Huna akaunti ya benki, huwezi kuomba kazi nzuri ambayo unaweza kujipatia riziki."
"Ninapowaona wenzangu, wamemaliza shule. Mimi sikuweza kuendelea kusoma. Msongo wa mawazo ulikuwa rafiki yangu hapo awali."
Tatizo ni kubwa kiasi gani?

Chanzo cha picha, Ed Habershon / BBC
Arnold ni mmoja wa watu wasiopungua 10,000 wasio na uraia wanaoishi Afrika Kusini, licha ya kuzaliwa hapa, wanahangaika kuthibitisha uraia wao ili kupata huduma za umma.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hakuna takwimu rasmi zinazopatikana kuhusu watu wasio na uraia. Kwa hivyo takwimu hizo zinatokana na makadirio ya mashirika kama vile shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR na mashirika ya haki za kiraia.
Kwa kutokuwa na uraia, watu wasio na uraia hawawezi kupata hati na wanahangaika kupata mahitaji ya msingi ikiwa ni pamoja na elimu na huduma ya afya.
Ukosefu wa uraia husababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya utawala na utunzaji duni wa kumbukumbu. Idadi halisi ya watu wasio na uraia ni ngumu kuipata katika sehemu nyingi za dunia.
Wakili wa haki za binadamu Christy Chitengu naye pia alikuwa hana utaifa.
Alipata uraia wa Afrika Kusini miaka mitatu iliyopita kwa msaada wa shirika la Mawakili wa Haki za Binadamu ambalo lilishughulikia kesi yake bila malipo.
"Niligundua sina uraia nikiwa na umri wa miaka 17. Mkuu wa shule yangu ya upili aliniita ofisini na kuniambia hana hati zozote za kwangu na haelewi jinsi nilivyoingia shuleni," anaambia BBC karibu na nyumbani kwake kaskazini mwa Johannesburg.
"Nilizaliwa Johannesburg na wazazi wawili wa kigeni [wote kutoka Zimbabwe] na nilipozaliwa nilipewa cheti cha kuzaliwa cha Afrika Kusini kilichoandikwa kwa mkono."
Lakini maafisa nchini Afrika Kusini wanahitaji cheti kilichochapishwa.
Christy anasema alipogundua hana uraia alifikiria kuchukua uraia wa wazazi wake lakini alikuwa amechelewa.
"Sikuweza kudai uraia wa Zimbabwe kwa sababu kufikia wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 16 na hawakuniruhusu kufanya usajili wa kuzaliwa. Pia ningelazimika kuondoka Afrika Kusini ili kupata pasipoti ya Zimbabwe na bila hati yoyote ya kuondoka nchini, nisingeruhusiwa kurudi."
Afrika Kusini ina idadi kubwa ya wahamiaji wasio na vibali huku serikali na makundi ya ulinzi wa ndani yanajaribu kukabiliana na wahamiaji kwa miaka mingi.
Alipoulizwa kama kuwapa uraia watoto wasio na uraia kunaweza kuonekana kama zawadi kwa wahamiaji wasio na vibali wanaojifungua Afrika Kusini, Christy anakataa hilo.
"Nadhani uraia si zawadi. Ni haki kwa mtu kuishi maisha yenye heshima na kuonekana kuwa ni mwanadamu. Nadhani tukiliangalia kupitia lenzi hiyo, tutatambua kwamba hakuna kitu tunachopoteza kwa kumtambua mtoto ambaye vinginevyo atashindwa kwenda shule ya msingi au kupata huduma ya afya."
Tatizo kimataifa

Chanzo cha picha, Getty Images
BBC iliwasiliana na wizara ya mambo ya ndani, ambayo hushughulikia masuala ya uhamiaji nchini Afrika Kusini, ili kujua jinsi inavyoshughulikia suala la ukosefu wa utaifa lakini haikupata jibu.
Ukosefu wa uraia si tatizo hapa tu, ni tatizo kubwa la kimataifa.
Kuna takriban watu milioni 4.5 wasio na uraia kote ulimwenguni. Baadhi wanasema idadi hiyo inaweza kufikia hata milioni 15.
Wataalamu wanaamini kukabiliana na tatizo hilo kunahitaji mabadiliko ya sera, ikiwa ni pamoja na kuruhusu wakimbizi kusajili watoto wao mahali walipozaliwa, na kuwapa akina mama haki ya kuwapa watoto wao uraia wao.
"Kwetu sisi kutokuwa na utaifa si suala la kisheria tu, ni suala linalohusisha haki ya maendeleo," anasema Jesus Perez Sanchez anayefanya kazi UNHCR.
"Mtu ambaye hata utaifa hataweza kuchangia kikamilifu katika nchi anayoishi. Kwa hivyo tunafikiri ni muhimu masuala yote ya ukosefu wa utaifa yashughulikiwe ili watu wote walio pembezoni mwa jamii waweze kuchangia kikamilifu katika jamii na uchumi."
Baada ya miaka mingi ya mapambano, sasa Arnold ana wakili anayemsaidia kupata hati rasmi. Anataka kurudi shuleni kusoma sayansi ya kompyuta. Anatumai kuwa na hati zitampa mustakabali mzuri zaidi za maisha.















