‘Majirani tu ndio wanaonitambua na si serikali’

- Author, Paula Odek
- Nafasi, BBC Swahili
Katika eneo la Kinondo, Mswambweni katika pwani ya Kenya wapo mamia ya watu walioishi Kenya hata kabla ya Uhuru lakini hawatambuliwi kama wakenya.
Kwa kuwatazama tu ni vigumu kufahamu madhila wanayoyapitia hadi pale wanapofunguka na kukuelezea dhiki wanayopitia kwa kukosa uraia.
Baadhi yao waliingia Kenya na wazazi wao kutoka sehemu mbalimbali nchini Burundi wakati wa serikali ya ukoloni wakivutiwa na fursa za kazi kama vile ukulima wa wakonge na miwa.
Kulingana na mzee anayeiwakilisha jamii Bwana Kiza Shadrack Barnaba ameeleza shida ambazo wanakumbana nazo kila uchao.
''Sisi tunaishi kama vile serikali haitutambui kwani huwa hatupokei huduma yoyote,'' Kiza amesema.
''Hata kwa neti za kukinga dhidi ya mbu tu zinazotolewa kama msaada lazima uwe na kitambulisho ndio upewe,' Bwana Kiza ameongeza.

Kulingana na Kiza anajivunia kwani anatambuliwa na majirani akisema yeye binafsi ameishi nao vyema lakini serikali haiwatambui kamwe.
Kwa kuwa hawana vitambulisho Warundi hawa wamekuwa wakikimu maisha yao kupitia ukulima na changamoto kubwa imekuwa njia ya kuzihifadhi pesa zao.
Hawawezi kufungua akaunti za benki bila vitambulisho.
''Kipindi hiki sina nguvu ya kulima lakini mbeleni nilikuwa nikilima na kupata pesa lakini nilipotaka kwenda kuweka pesa kwenye akaunti haikuwezekana.''
''Nilikuwa natengeneza pembe ya ng'ombe ndiyo iliyokuwa benki yangu,'' Kiza ameeleza.
Wanaume kutoka jamii ya Warundi waliamua kuoa wanawake waliokuwa wakiishi nao ili mradi tu watoto wao watambulike na waweze kufaidika na misaada inayotolewa na serikali. Lakini hawakujua kinachowasubiri katika siku zijazo.
Madhila ya kuoa kwa ajali ya utambulisho.
Wanaume wa jamii ya Warundi waliamua kuoa wake wa makabila tofauti ambao ni raia wa Kenya ili mradi tu wajihisi wako nyumbani na pia waweze kutambuliwa na hata kulinda rasimali zao walizokuwa wamezirithi kutoka kwa mababu zao lakini mambo yakawa tofauti.
Mzee Simon, alioa mke na wakajaliwa watoto wawili lakini sasa mke wake amebadilisha majina ya watoto wake na kuwapatia jina la mume wa zamani wa mke wake aliyefariki miaka 20 iliyopita. Simon anadai kuwa angekuwa na kitambulisho basi angeenda kuwatafutia vyeti vya kuzaliwa watoto wake mwenyewe.
''Sasa hata sijui kwanini hakuniandika kama baba ya watoto wangu na kuandika jina la mtu aliyekufa miaka mingi iliyopita.''
Lakini Simon anasema mama ya watoto wake alimueleza baada ya muda kuwa alitaka watoto wake wasijulikane kama ni Warundi.
''Kwa vile sina kitambulisho sina njia yoyote ile ya kutafuta haki.''
Naye Mzee Yusuf alimuoa mwanamke raia wa Kenya na kwa kiasi fulani alibahatika kwani aliweza kupata angalau kipande kidogo cha shamba.
Lakini baadaye alipokonywa.
Lakini uchungu ni kwamba hana uwezo wa kufuatilia kesi hiyo ya shamba kwa sababu anadai hali yake kiafya si njema na hana fedha wala kitambulisho cha kuwasilisha kesi yake katika mahakama nchini Kenya.
''Nikitembea karibu na hilo shamba ambalo nilikuwa nimepanda minazi, maembe huniuma sana,'' amesema Yusuf.

Cha kusikitisha zaidi namba yangu ya simu ya kuhifadhi pesa iko chini ya jina la mke wangu.Nikienda kutoa pesa muhudumu huniuliza mbona wewe ni mwanamume na jina hapa ni la mwanamke?
Wanawake ambao wazazi wao wa kiume ni Warundi pia wanapitia changamoto tofauti.
Bi Mwanakombo Yohannes licha ya yeye kuwa Mrundi ameamua kujifunza zaidi lugha ya mama yake ya Kidigo angalau aweze kujihisi mmoja wao.
Mwanakombo anasema amesoma lakini kupata kazi imekuwa changamoto kubwa katika maisha yake.
''Hata kufagia nyumba ya mtu lazima uwe na kitambulisho.''
Mtu anawezaje kupata uraia Kenya?
Mtu anaweza kupata uraia iwapo mmoja ya wazazi wake ni raia wa Kenya.
Mfano watoto wanaozaliwa kutokana na ndoa kati ya watu wa asili ya Burundi na Wakenya wanapata uraia kutoka kwa mzazi huyo wa Kenya.
Njia nyingine ni kwa njia ya kujiandikisha, ambapo mtu akiingia kihalali nchini Kenya na kuishi kwa zaidi ya miaka saba bila kuwa na hatia yoyote basi anaweza kuomba uraia.
Njia hiyo pia inaweza kutumika na raia wa kigeni ambao wameolewa au kuoa raia wa Kenya na wamekaa pamoja kwa miaka saba.
Kulingana na afisa wa shirika la kibinafsi linaloshugulikia haki za kibinadamu la Haki Centre Amos Mwatata, changamoto ambayo watu waliotoka mataifa mengine wanakumbana nayo ni ukosefu wa vyeti vya kuonyesha waliingia Kenya kihalali. Kwa hivyo hawawezi kupata cheti za maadili mema kuonyesha wameishi Kenya bila kufanya makosa.












