Trump: Nilikuwa na 'udhibiti kamili' wa mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Donald Trump
Muda wa kusoma: Dakika 2

Rais wa Marekani Donald Trump amewaambia waandishi wa habari katika mkutano na waandishi wa habari wa Ikulu ya White House siku ya Alhamisi kwamba "aliwajibika na alisimamia" mashambulio ya Israel ya Juni 13 dhidi ya Iran. Aidha amesema katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na viongozi wa nchi za Asia ya Kati katika Ikulu ya White House kwamba Iran imetaka kuondolewa vikwazo vizito vya Marekani na kwamba yuko tayari kulizungumzia suala hilo.

Bw. Trump alisisitiza kwamba yuko "wazi kwa mazungumzo."

Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval ya Ikulu ya White House jana kwamba alikuwa "katika udhibiti kamili" wakati Israeli ilipoishambulia Iran.

Alielezea shambulio la Israel kuwa "kubwa na lenye nguvu " na kusema uharibifu uliotokea katika shambulio la kwanza ni "zaidi ya mashambulizi yote yaliyofuata."

Kauli za Bw Trump zinatofautiana kwa kiasi fulani na msimamo wa awali wa serikali ya Marekani kuhusu jukumu la nchi hiyo katika vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran.

Iran imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yalikuwa na uratibu kamili na maafisa wa Marekani.

Katika siku ya kwanza ya shambulio la kushtukiza la Israel, makamanda wengi, pamoja na wanasayansi na wataalamu wa mpango wa nyuklia wa Iran, waliuawa.

Trump: Iran inataka vikwazo vya Marekani viondolewe, tuko tayari kwa mazungumzo

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Trump akutana na viongozi wa nchi za Asia ya Kati katika Ikulu ya White House

"Kusema ukweli, Iran imeomba vikwazo viondolewe. Iran inakabiliwa na vikwazo vizito sana kutoka kwa Marekani, na hilo limefanya mambo kuwa magumu sana kwao," Bw. Trump alisema katika karamu ya White House iliyohudhuriwa na viongozi wa nchi za Asia ya Kati.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Iran inakabiliwa na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani katika miaka ya hivi karibuni hasa baada ya Marekani kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 (JCPOA). Lakini sasa, kwa hatua ya serikali za Ulaya, vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, ambavyo vilikuwa vimesitishwa kwa takriban miaka 10, vimerudishwa.

Bw. Trump aliendelea na karamu ya jana usiku kwamba Iran wakati mmoja ilikuwa "mnyanyasaji wa Mashariki ya Kati" lakini "haina uwezo tena wa kupata silaha ya nyuklia."

Rais wa Marekani amekuwa akisema mara kwa mara kwamba mashambulizi ya hivi karibuni ya kijeshi yameharibu mpango wa nyuklia wa Iran. Hata hivyo, Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki bado hawajatoa makadirio sahihi ya uharibifu huo.

Nchi za Ulaya zinatoa wito kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kufuatilia mpango wa nyuklia wa Iran haraka iwezekanavyo na mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yaanze.

Rais wa Marekani hapo awali alisema katika mahojiano na mtandao wa Marekani wa CBS kwamba Iran inatafuta kufikia makubaliano na Marekani.

Matamshi ya Bwana Trump yanakuja wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alisema jana katika kipindi cha maswali na majibu na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Bu Ali Sina kwamba Iran iko tayari kwa "mazungumzo sawa na ya heshima" na Marekani, lakini haina "uzoefu mzuri" katika mazungumzo na nchi hii.

Katika siku za hivi karibuni, ripoti zimechapishwa kuhusu uwezekano wa kuanza tena mazungumzo kati ya Iran na Marekani.

Oman ambayo imekuwa mwenyeji wa duru kadhaa za mazungumzo kati ya Iran na Marekani, imetoa wito kwa pande zote mbili kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Lengo la mazungumzo haya lilikuwa kufikia makubaliano mapya ya kupunguza shughuli za nyuklia za Iran kwa kubadilishana na kuondolewa kwa vikwazo.