Hiki ndicho kilichovunja ndoa ya Maresca na Chelsea, nani kurithi mikoba yake?

Enzo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chelsea chini ya Enzo Maresca imeshinda mechi moja tu ya ligi kuu mwezi Disemba.
Muda wa kusoma: Dakika 3

Enzo Maresca ameondoka rasmi katika wadhifa wake kama kocha mkuu wa Chelsea, chini ya miezi sita tangu alipoiwezesha klabu hiyo kutwaa Kombe la dunia kwa vilabu, mafanikio yaliyokuwa yameongeza matumaini makubwa miongoni mwa mashabiki wa The Blues.

Kuondoka kwake kunakuja katika kipindi ambacho Chelsea imeporomoka kwenye msimamo wa Ligi kuu ya England, ikishinda mechi moja pekee kati ya saba za mwisho, na sasa ipo nafasi ya tano, alama 15 nyuma ya vinara Arsenal.

Ingawa matokeo uwanjani yalionekana kuwa sababu ya wazi, taarifa zinaonyesha kuwa kulikuwa na mgongano mkubwa wa ndani kati ya Maresca na uongozi wa klabu, hali iliyohusisha maamuzi ya kiufundi, matumizi ya wachezaji na aina ya mawasiliano na umma.

Makala hii inaangazia kilichosababisha kuvunjika kwa uhusiano kati ya Chelsea na Maresca, rekodi yake ndani ya klabu hiyo, na hatimaye majina yanayoongoza katika mbio za kurithi mikoba yake Stamford Bridge.

Kipi kimeenda kombo kati ya Maresca na Chelsea?

Mwanzoni mwa msimu, Chelsea ilionekana kuwa katika hali ya utulivu. Timu ilikuwa nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu, ikicheza soka lililovutia, na hata kuifunga Barcelona katika ligi ya mabingwa Ulaya.

Maresca alitajwa kuwa kocha bora wa mwezi wa Novemba, jambo lililodhihirisha imani kubwa kutoka kwa uongozi wa klabu. Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla mwezi Disemba baada ya Chelsea kushinda mechi moja tu ya ligi.

Kauli ya Maresca baada ya ushindi dhidi ya Everton alipodai kuwa amepitia "saa 48 mbaya zaidi" tangu ajiunge na klabu hiyo, kauli iliyowashangaza viongozi wa Chelsea, waliotafsiri maneno hayo kama lawama kwa uongozi.

Chanzo cha mvutano kilikuwa ni kile Maresca alichokiona kama kuingiliwa katika kazi yake, hususan kwenye upangaji wa kikosi, mabadiliko wakati wa mechi na ushauri wa kitabibu kuhusu wachezaji waliokuwa wakirejea kutoka majeraha. Hilo likawa sababu ya kilichotokea.

Rekodi zake Chelsea, na je klabu hiyo kurudi kileleni?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa upande wa mafanikio, Maresca aliacha alama chanya. Aliiongoza Chelsea kufuzu Ligi ya mabingwa Ulaya, kutwaa kombe la Conference League, na kushinda Kombe la dunia kwa vilabu baada ya kuifunga Paris St-Germain.

Hata hivyo, mafanikio hayo hayakuweza kuficha matatizo ya timu hiyo kwenye ligi kuu, ambako Chelsea ilishindwa kasi ya kukaa kileleni na kujikuta ikipoteza alama muhimu katika kipindi kifupi.

Swali linalobaki ni kama Chelsea iko katika mwelekeo sahihi wa kurejea kileleni kupitia mradi wa muda mrefu unaolenga wachezaji vijana, au kama mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha yataendelea kuikwamisha klabu hiyo.

Kwa sasa, nafasi ya tano inaweza kuwa ya kutosha kuirudisha Chelsea ligi ya mabingwa msimu ujao, lakini presha ya mashabiki na ratiba ngumu hasa ya mwezi Februari na Machi inaendelea kuipima klabu hiyo.

Kuna hofu pengine tatizo la Chelsea ni zaidi ya kocha. Imekuwa na makocha wengi wazuri kuanzia Carlo Ancelotti, Avran Grant, Luiz Scolari, Raphael Benitez, Guus Hiddink mpaka Jose Mourinho, hakuna aliyekaa zaidi ya miaka minne. Tangu mwaka 2000 ni Claudio Ranieri pekee aliyekaa miaka minne, wengine wengi ni msimu mmoja, au miwili na wachache mitatu, haishangazi Maresca amekaa chini misimu miwili.

Nani kurithi mikoba ya Maresca?

Jina linaloongoza kwa sasa ni Liam Rosenior, kocha wa Strasbourg, ambaye anaheshimiwa ndani ya mtandao wa umiliki wa BlueCo kwa uwezo wake wa kukuza vipaji na mtindo wa soka unaoendana na falsafa ya Chelsea.

Majina mengine yanayotajwa ni pamoja na Roberto De Zerbi wa Marseille, Kieran McKenna wa Ipswich, Francesco Farioli wa Porto, pamoja na Frank Lampard, ambaye kurejea kwake kunaweza kuwagusa mashabiki kutokana na historia yake Stamford Bridge.

Kwa muda, kocha wa timu ya vijana ya Chelsea Calum McFarlane ataiongoza timu, huku klabu ikikabili ratiba ngumu inayojumuisha mechi dhidi ya Manchester City, Arsenal na Napoli.

Uamuzi wa kocha ajaye utakuwa muhimu sana kwa mustakabali wa Chelsea, huku klabu ikitafuta mwendelezo, utulivu na mafanikio ya kudumu.