Haya ndiyo matarajio ya timu za Afrika katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rob Stevens
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mechi za Mataifa ya Afrika za kufuzu Kombe la Dunia la Fifa 2026 zinaendelea tena wiki hii baada ya kusimama kwa miezi tisa.
Baadhi ya mechi zilizoanza Alhamisi na Ijumaa zimeshuhudia DRC ikiifunga 1-0 Sudan Kusini, Rwanda ikalala nyumbani 0-2 dhdi ya Nigeria, Afrika Kusini ikaibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Lesotho, Kenya ikaenda sare na 3-3 ugenini na Gambia na Ghana ikiirarua 5-0 Chad.
Tanzania itakipiga na Morocco ugenini siku ya Jumatano.
Timu sita katika kila kundi, hucheza mechi 10, na mechi mbili zitachezwa mwezi huu na zitasaidia kuamua hatima ya timu nyingi. Washindi tisa katika makundi wanakata tiketi ya kucheza kombe hilo nchini Canada, Mexico na Marekani.
DR Congo
Mabadiliko ya usimamizi yametokea tangu duru iliyopita mwezi Juni, huku Nigeria, Senegal na Tunisia zikiwa miongoni mwa timu zilizo na makocha wapya.
Timu zenye makocha wapya
Miongoni mwa timu vigogo katika bara ni Nigeria ambao wana uhitaji mkubwa wa matokeo mazuri. Hawajashinda katika Kundi C, na wako nyuma ya viongozi wa kundi Rwanda kwa pointi nne.
Kocha wa Nigeria, Eric Chelle, kocha wa zamani wa Mali ni Mwafrika wa kwanza asiye Mnigeria kuchukua mikoba ya kuiongoza Super Eagles.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wenyeji hao wa Afrika Magharibi watasafiri hadi Kigali kabla ya kuwakaribisha Zimbabwe nchini Nigeria. Chelle kocha wa mabingwa hao mara tatu katika Afcon, anakubali kwamba ni lazima washinde mechi ili kusonga mbele.
Mshambulizi nyota Victor Osimhen wa Nigeria, anasema yeye na wachezaji wenzake "wanatamani" kushiriki kombe la dunia baada ya kukosa kushiriki katika michuano ya 2022 nchini Qatar.
Bosi mwingine mpya anayehitaji ushindi ni Tom Saintfiet, ambaye anatazamia kufufua kampeni zake akiwa na timu ya Mali katika Kundi I baada ya kumrithi Chelle.
Kuna pengo la pointi nne kutoka timu inayoongoza kundi, Comoro, pengo hilo linaweza kupunguzwa ikiwa Eagles wanaosafiri kukabiliana na wenyeji wa visiwani, watashinda.
Mali haijawahi kufika kucheza Kombe la Dunia. Baada ya kupita bila kufungwa katika mechi za awali za kundi katika Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2025), Saintfiet ana matumaini ya kwenda kombe la dunia.
"Baada ya mechi sita na ushindi wa mechi nne na sare mbili, nina matumaini," amesema Mbelgiji huyo.
Hapo hapo Kundi I, Ghana itapambana kusawazisha rekodi yao mbaya ya kutofuzu Afcon 2025, pale watakapo cheza dhidi ya Chad na Madagascar.
Kocha Corentin Martins sasa yuko dimbani akiinoa Madagascar, huku Rigobert Song akikabiliwa na mechi zake za kwanza kama kocha wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wababe wa Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika kundi B, Bosi wa Senegal Pape Thiaw ni mtu mwingine aliyechukua mikoba kuelekea mechi za Kombe la Dunia baada ya kumrithi kocha Aliou Cisse, ambaye alikuwa msaidizi wake, Oktoba mwaka jana.
Wenyeji hao wa Afrika Magharibi walimaliza mechi zao Afcon 2025 bila kupoteza na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo El Hadji Diouf amefurahishwa na mabadiliko ya timu hiyo.
"Senegal ni familia na tuna udugu mzuri. Tunapaswa kufanya kazi pamoja na kuwa na furaha wote pamoja."
Mabingwa hao wa zamani wa Afcon wako pointi mbili nyuma ya vinara wa Kundi B, Sudan na watacheza mchezo wao wa ugenini dhidi ya Sudan, utakaochezwa katika jiji la Benghazi nchini Libya.
Na mechi inayofuata ya nyumbani dhidi ya Togo, bila washambuliaji wa Ligi Kuu ya Uingereza Nicolas Jackson na Iliman Ndiaye waliojeruhiwa.
Mbabe mwingine wa Afrika ni Misri, inayoongoza katika kundi na kwakuwa na matokeo mazuri, inaongoza kundi kwa pointi nne katika Kundi A.
Nahodha wa Mafarao, Mohamed Salah alipumzishwa katika hatua za mwisho za mechi za kufuzu Afcon 2025, lakini fowadi huyo amerudi katika kiwango chake kizuri akiwa na Liverpool, na atacheza mechi dhidi ya Ethiopia na Sierra Leone.
Salah atapambana na vijana wa kocha mkuu mpya wa Sierra Leone, Mohammed Kallon, ambaye amemteua beki mpya kijana wa Manchester City, Juma Bah na Kei Kamara mwenye umri wa miaka 40 kwenye kikosi chake cha kwanza.
Wakati huo huo, Sami Trabelsi amerejea kwa awamu ya pili ya kuinoa Tunisia huku timu hiyo ikiwa kileleni mwa Kundi H kwa pointi mbili.
Mabingwa watetezi wa bara Ivory Coast wana faida ya pointi moja katika Kundi F. Naye kocha mpya wa timu ya Kenya, Benni McCarthy analenga kufuzu kwa mara ya kwanza kwenda Kombe la dunia huku akilenga kupunguza pengo la pointi tano.
Katika Kundi D, Cameroon inayosaka kushiriki mara ya nane katika kombe la dunia, wako pointi moja tu mbele ya Cape Verde na Libya, wiki iliyopita Libya ilimteua Aliou Cisse kama bosi wao mpya.
Kundi lisilotabirika na lililoparaganyika
Kwa jinsi mambo yalivyo, kundi lisilo tabirika ni Kundi G, ambapo timu tano za juu zimetenganishwa kwa pointi tatu pekee.
Kocha Vladimir Petkovic aliiongoza vyema Algeria kufuzu Afcon 2025, timu hiyo itamenyana na Msumbiji na Botswana.
Wenyeji wa Guinea na Afcon ya 2027 Uganda pia wako tayari kunufaika na mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea.
Timu inayoshika nafasi ya juu barani Afrika kwa viwango vya Fifa Morocco, ni timu iliyopo katika Kundi E lenye mparaganyiko wa mambo.
Eritrea ilijiondoa kabla ya mechi za mchujo kuanza na mwezi uliopita Congo-Brazzaville ilifungiwa kushiriki soka la kimataifa na shirikisho la soka duniani Fifa.
Mechi za timu hiyo mwezi Machi dhidi ya Tanzania na Zambia zimefutwa, na kuna nafasi ndogo ya kupanga upya michezo hiyo katika kalenda ya kimataifa, hata kama watafanikiwa kubatilisha marufuku yao.
Macho yote sasa yanaelekezwa Fifa na Shirikisho la Soka Afrika kwa uamuzi wa jinsi timu zitakazomaliza nafasi ya pili kwenye kundi hilo zitakavyopangwa.















