Matumaini kwa Timu za Afrika katika Kombe la Dunia

Chanzo cha picha, BBC Sport
- Author, Na Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
Michuano ya Kombe la Dunia ya FIFA ya 2022 itakuwa inafanyika kwa mara ya 22, kuangazia ubingwa wa kandanda wa kimataifa wa miaka minne unaoshindaniwa na timu kuu za kitaifa za vyama vya wanachama wa FIFA.
Michuano hiyo ya Kombe la Dunia ambayo huwa na hamasa kubwa katika kandanda inaanza kufanyika kuanzia tarehe 20 Novemba hadi 18 Desemba 2022 huko Qatar.
Na kama bara jingine lolote lile, Afrika inawakilishwa na Cameroon, Ghana, Morocco, Senegal na Tunisia.
Na ili kuangazia matumaini ya timu za Afrika kwa mashindano ya Kombe la Dunia nimezungumza na Daniel Mlimuka mchambuzi wa masuala ya michezo ambaye ameanza kwa kuangazia changamoto zinazokumba timu za Afrika katika michuano hiyo.
“Mara nyingi timu za Afrika zinakumbana na changamoto ambayo imekuwepo kwa muda mrefu, hazipati faida sawa katika mashindano haya ikilinganishwa na timu za mataifa ya Ulaya na Amerika Kusini.”
Bw.Mlimuka anasema pengine hilo limetokana na kutokuwa na wachezaji wenye vipaji vya juu zaidi ikilinganishwa na wachezaji wengine wa maeneo tofauti.
Kuna baadhi ya timu zina wachezaji wazuri, kwa mfano, Senegal, ina wachezaji wengi barani Ulaya lakini ukija Afrika kuna changamoto ya kuunganisha wachezaji hao wenye vipaji na kupata matokeo bora.
Na hii imekuwa changamoto ya Afrika nzima, kuunganisha wachezaji wanaocheza katika vilabu vya Ulaya, kuwaleta wote pamoja na kupata timu imara. Daniel Mlimuka ameongeza kuwa:
“Kuna timu kama Cameroon ambayo ilikuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa wa masindano ya kombe la Dunia. Tatizo ni kwamba wachezaji nyota haswa sio wengi ikilinganishwa na kipindi kile cha kina Roger Milla waliokuwa na uwezo mkubwa wa kutoa matokeo bora, kwa Misri ukiangalia nguvu yao kubwa bado iko kwa Mohamed Salah tofauti na timu ya taifa ya Misri ya miaka iliyopita.”
Ushawishi wa timu za Afrika katika Kombe la Dunia ukoje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mchambuzi wetu anasema kuwa kwa yeye, timu yenye ushawishi katika zile za Afrika zilizofuzu ya kwanza ni Morocco.
“Kwanza kikosi chao kimejipambanua, na pia taifa hili limeweza kuwatumia nyota ambao wapo katika ngazi ya kimataifa kama vile akina Achraf Hakimi, Hakim Ziyech na Noussair Mazraoui ikilinganishwa na timu zingine za Afrika.”
Kulingana na Mlimuka timu ya Morocco ndio yenye kuonyesha matumaini kwa Afrika ikifuatiwa na Senegal, na zingine zilizosalia hata kufika nusu fainali, anaona ni jambo ambalo litakaloshangaza wengi.’’
Ikumbukwe kwamba timu ya Morocco ipo pamoja na Ubelgiji, Canada na Croatia.
Barani Afrika timu ya Senegal iliyoishinda Misri katika fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), imeonyesha kuwa imara latizo ni kwamba bado haijathibitisha na kujiweka kama tishio kwa timu za kimataifa. Mchambuzi wetu anasema Daniel Mlimuka:
“Muktadha wa mashindano ya kombe la Afrika (AFCON) ni tofauti kabisa na Kombe la Dunia. Je vipaji vilivyopo sasa hivi vinashawishi kutoa matumaini kwamba tutafaulu, hiyo ndio hofu yangu mimi ukianza kuliangazia suala hili kwa mtazamo huo”.
Timu nyingine inayoingia kuiwakilisha Afrika ni ya Ghana, Black Stars ambayo nayo ina mengi ya kujifunza katika kombe la Dunia. Kwanza kabisa wanakutana na Uruguay.
Wawili hao walipokutana mara ya mwisho, Ghana ilibanduliwa kupitia penalti ya 4-2 baada ya kutoka sare ya 1-1 katika robo fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mnamo mwaka 2010.
Bila shaka kila mmoja wao atakuwa makini na mwenzake na kutaka kupima kama pengine mbinu ya mchezo imebadilika.
Lakini usisahau kuwa pia kikosi cha Ghana kilichoshiriki mwaka 2010, kimebadilika kabisa. Wachezaj maarufu kama Asamoah Gyan na Andre 'Dede' Ayew hawapo.
Hatua hii itakuwa inaonesha maendeleo katika soka nchini Ghana lakini mchambuzi wetu anaona kikosi kilichotangulia kilikuwa na uzoefu mzuri zaidi kuliko cha sasa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mpangilio wa timu kwenye makundi
Mtazamo wa mchambuzi Daniel Mlimuka ni kuwa hakuna makundi mepesi wala magumu. Kuna mengi ambayo yametokea katika soka siku za nyuma.
Pengine mashabiki waliona ni kama timu yao ipo kwenye kundi rahisi lakini mwisho wa siku zile timu zinazoonekana kuwa miamba zilitolewa na zile zilizoonekana rahisi zikasalia.
‘’Lengo la timu yoyote ni kushinda mechi zao.” Hii ni sawa na kusema kuwa hakuna timu iliyo kwenye kundi rahisi kushinda kwasababu kila mmoja anapigania kuibuka na ushindi.
Na pengine kwa makundi ambayo timu za Afrika zipo, huenda timu wenzao zikachukulia kuwa hizo ndizo ambazo wataweza kuzitoa kwa urahisi.
Lakini sasa je, ni kibarua gani kigumu zaidi kilichopo kwa timu za Afrika?
‘’Kigumu zaidi ni kuainisha mkakati na mbinu za wachezaji,’’ amesema Mlimuka na kuongeza, “aidha mpira wa Uhispania unajulikana, wa Brazil unajulikana, wa Uingereza unajulikana… Lakini hakuna falsafa ya mpira wa Afrika inayoeleweka.”
Pengine hili linatokana na ukweli wa kwamba wenye vipaji kutoka Afrika wakianza tu kuchipuka, wanakimbilia Ulaya na wengine wanasalia huko huko.
Kwa hiyo, bado suala la kuwaleta pamoja wachezaji bora linajitokeza tena.
Lakini siri pengine iko wapi angalau ifike siku, timu moja ya Afrika iwe imeshinda michuano yake ya awali na kuingia kwenye fainali.
‘’Pengine tuanzie chini kukuza vipaji vyetu. Labda kuanza kuwekeza kwenye soka. Kwasababu Ulaya na baadhi ya timu zinasajili mtu wa miaka tisa. Lakini kwa Afrika haijaona hatua kama hii inaweza kufanyika.
‘’Pia kingine kinachoweza kufanyika ni kuelekeza nguvu nyingi kwa vijana kuanzia wakiwa wadogo kabisa ili wasipate tamaa ya kwenda Ulaya, na kuwakuza ili tupate falsafa yetu ya soka. Hili litakuwa jambo la msingi.”
Sio kuwazuia wasiende Ulaya, hapana, bali ni kukusanya vipaji vyetu ambavyo tunavyo Afrika na kuvikuza kwa misingi inayoeleweka.
Ukiangalia timu za Under-17 ambao unatarajia kuwaona kwa timu za wakubwa siku zijazo, wengi wao wanapotea hapa katikati.
Ifike wakati tuwe na kiunganishi kati ya soka ya Under-17 na ile ya watu wakubwa kama ilivyo kwa Ulaya na mifumo mizuri ya kukuza vipaji.
Mfano, Nigeria wachezaji wengi wa timu ya taifa aidha walikwenda Ufaransa wakiwa na umri mdogo au walizaliwa Ufaransa. Sasa je hivi vipaji vya ndani vinaendelezwa vipi?
Kuna wakati timu ya Afrika inaweza kushinda Kombe la Dunia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Inabaki kuwa matumaini kwasababu historia inaonesha kuwa timu zinazoshinda Kombe la Dunia ni zenye mchezo wa hali ya juu.
‘’Sio lazima ziwe timu ambazo zimewekeza hela nyingi sana. Kuna timu kutoka Amerika ya Kusini kama Argentina, Uruguay na Brazil ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika Kombe la Dunia, bila kuwa na wachezaji wa fedha nyingi sana lakini ni kwasababu tu mataifa hayo yanazalisha wachezaji wenye vipaji.
‘'Kwa hiyo, siku ambayo tutaona wachezaji wa Afrika wanakwenda kutawala soka ya Dunia, ndio itakayokuwa ishara kubwa kwamba huenda ipo siku Afrika itashinda Kombe la Dunia, lakini kwa hivi sioni kama hilo linaweza kutokea.” Bwana Mlimuka amesema.
Hata ukifuatilia kwa karibu, kumekuwa na tukio moja moja ya timu za Afrika kufika hatua ya juu kwenye mashindano hayo.
‘’Kulikuwa na Ghana walifika karibu lakini pia nao hakikuwa kitu cha kutegemewa.’’
Lakini kama inavyojulikana katika mpira wa migu, lolote linaweza kutokea.
Na pia ieleweke kwamba sio kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka kimataifa, hapana, bali ni kiwango cha mchezo kinachochezwa na wachezaji.
Ukiangalia timu nyingi ambazo zimewahi kushinda Kombe la Dunia, ‘’zimekuwa na miongoni mwa wachezaji bora. Ufaransa, Aurgentina, Brazil, Ujerumani, zimekuwa zikitayarisha wachezaji ambao wanatoa ushindani mkubwa kwenye soka kwa viwango vya juu. Na kama Afrika kuna siku tutafika huko, ndio siku ambayo Afrika itakuwa na nafasi ya kutwaa Kombe la Dunia,” amesema Mlimuka.
Mfano wakati timu ya taifa ya Uhispania ilishinda Kombe la Dunia 2010, ilikuwa na wachezaji nyota karibu kikosi kizima.
Ujerumani ilipochukua Kombe la Dunia 2014, timu hiyo ilikuwa na wachezaji wenye viwango bora vya uchezaji Duniani. Hii ni tofauti na Afrika ambapo utakuta mchezaji anacheza kwenye viwango vya dunia ni mmoja au wawili.
Mfano ukienda Senegal unaweza kumpata Sadio mane, Misri ukampata Mo Salah wala sio kikosi kizima.
Hii ina maana kwamba kufikia sasa, katika hili, Afrika bado ina mwendo mrefu kutimiza ndoto ambayo imekuwa matamanio ya wapenda soka wengi barani humo.















