Mapinduzi Mali: Je mapinduzi ya kijeshi yanaongezeka Afrika?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapinduzi ya kijeshi yamekuwa yakitokea mara kwa mara barani Afrika katika miongo kadhaa tangu uhuru.
Matukio ya hivi karibuni nchini Mali ni mfano tu wa hivi karibuni wa jeshi linalotoa ushawishi wake kwenye matukio haya- uingiliaji wa jeshi kwa mara ya pili nchini humo kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja.
Katika nchi jirani ya Niger, mapinduzi yalikwamishwa mnamo Machi siku chache kabla ya kuapishwa kwa rais.
Je! Hatua za kijeshi zinajitokeza mara nyingi zaidi katika bara hili?
Mapinduzi hufanyika namna gani?
Ufafanuzi mmoja uliotumika ni ule wa jaribio lisilo halali na la waziwazi la wanajeshi (au maafisa wengine wa raia) kuwatoa kwenye viongozi katika nafasi zao.
Utafiti uliofanywa na watafiti wawili wa Marekani Jonathan Powell na Clayton Thyne, umebainisha zaidi ya majaribio 200 huko Afrika tangu mwishoni mwa miaka ya 1950.
Karibu nusu ya majaribio haya yalifanikiwa - na kudumu zaidi ya siku saba.
Burkina Faso, Afrika Magharibi, imekuwa na mafanikio zaidi, mapinduzi saba na moja tu lilishindwa.
Wakati mwingine, wale wanaoshiriki katika matukio ya mapinduzi hukana kuwa si mapinduzi.
Mnamo mwaka wa 2017 huko Zimbabwe, Jeshi lilimaliza utawala wa Robert Mugabe uliodumu kwa miaka 37.
Mmoja wa viongozi wa hao Meja Jenerali Sibusiso Moyo, alionekana kwenye runinga wakati huo akikanusha wazi jeshi kuchukua udhibiti.
Mwezi Aprili mwaka huu, baada ya kifo cha kiongozi wa Chad Idriss Deby, jeshi lilimweka mtoto wake kama rais wa mpito akiongoza baraza la kijeshi la mpito. Wapinzani wake waliuita "mapinduzi ya nasaba".
"Viongozi wa mapinduzi karibu kila wakati wanakanusha kuwa yalikuwa mapinduzi katika juhudi za kuyapa uhalali," anasema Jonathan Powell.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je kuna matukio machache ya mapinduzi Afrika hivi sasa?
Katika miongo minne kati ya 1960 na 2000, idadi ya jumla ya majaribio ya mapinduzi barani Afrika imebaki kuwa sawa sawa kwa wastani wa karibu miaka minne.
Tangu wakati huo, hii imeshuka - hadi karibu mara mbili kila mwaka katika miongo miwili hadi 2019.
Jonathan Powell anasema hii haishangazi kutokana na kuyumba kwa nchi za Kiafrika miaka kadhaa baada ya uhuru.
"Nchi za Kiafrika zimekuwa na mazingira ya kufanana ya kusababisha mapinduzi, kama umasikini na utendaji, uchumi duni. Wakati nchi inapoingia mara moja katika mapinduzi, ni ishara ya kutokea mapinduzi zaidi."
Ndubuisi Christian Ani kutoka Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal anasema maandamano ya watu wengi dhidi ya madikteta waliohudumu kwa muda mrefu yametoa nafasi ya kurudishwa kwa mapinduzi barani Afrika.

Chanzo cha picha, Reuters
Nchi gani za kiafrika zimepitia matukio mengi ya mapinduzi?
Sudan imekuwa na zaidi yaani mapinduzi 15 - matano kati yao yalifanikiwa. Ya hivi karibuni ilikuwa mwaka 2019 na kuondolewa kwa Omar al-Bashir kufuatia miezi kadhaa ya maandamano.
Bashir alikuwa amechukua madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi mnamo 1989.

Tangu 2015, kati ya mapinduzi tisa yaliyoripotiwa ulimwenguni kote, yote isipokuwa mawili yalifanyika Afrika - Uturuki (2016) na Myanmar (2021).
Kwa ujumla, Afrika imepata mapinduzi mengi kuliko bara jingine lolote.
Inafuatwa na Amerika Kusini, na majaribio 95 ya mapinduzi, 40 kati yao yalifanikiwa.
Hata hivyo kwa miongo miwili iliyopita majaribio ya jeshi kuipindua serikali yamepunguua sana Amerika ya Kusini. Mapinduzi ya mwisho yalikuwa Venezuela mwaka 2002 ambapo walitaka kumtoa madarakani Hugo Chaves, lakini jaribio hilo lilishindwa.
Powell amebainisha kuwa kumalizika kwa Vita Baridi ambayo ililazimisha Marekani na Umoja wa Usovieti kuingilia mambo ya ndani ya nchi za Amerika ya Kusini na utayari wa Jumuiya ya Kimataifa kuziwekea vikwazo nchi zinazofanya mapinduzi, kama ilivyofanyika kwa Haiti mwaka 1994, kumepelekea kupungua kwa mapinduzi ya kijeshi.
Bara la Asia pia limeshuhudia kupungua kwa majaribio ya mapinduzi ya kijeshi.














