Traoré 'chupuchupu' kupinduliwa Burkina Faso

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imesema imezuia "njama kubwa" ya kumpindua kiongozi wa utawala wa kijeshi, Kapteni Ibrahim Traoré, ambapo inadai kuwa wapanga njama hao walikuwa wakifanya kazi kutoka nchi jirani ya Ivory Coast.
Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana, alisema kuwa jaribio hilo la mapinduzi liliongozwa na wanajeshi wa sasa na wa zamani waliokuwa wakishirikiana na viongozi wa makundi ya kigaidi. Alisema kuwa mpango wao ulikuwa kushambulia Ikulu ya rais wiki iliyopita.
Lengo kuu, alisema, lilikuwa "kusababisha vurugu kubwa na kuiweka nchi chini ya usimamizi wa shirika la kimataifa." Alitoa kauli hiyo kupitia televisheni ya taifa Jumatatu.
Kapteni Traoré: Kiongozi Kijana anayeungwa mkono na Umma

Chanzo cha picha, Getty Images
Kapteni Ibrahim Traoré aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwezi Septemba 2022, akimuondoa Kanali Paul-Henri Damiba, aliyekuwa ameahidi kurejesha usalama lakini akashindwa kudhibiti mashambulizi ya makundi ya wanamgambo. Traoré, akiwa na umri wa miaka 34 wakati huo, alikua kiongozi mdogo zaidi barani Afrika.
Tofauti na watangulizi wake, Traoré alipokelewa kwa hamasa kubwa na sehemu kubwa ya wananchi, hasa vijana, waliomwona kama mzalendo na mkombozi. Aliahidi kuweka mbele maslahi ya taifa, kupambana na rushwa, na kuongeza juhudi za kijeshi kukabiliana na ugaidi uliokuwa umekithiri.
Tangu alipochukua madaraka, amejitahidi kuimarisha jeshi, kubadilisha mikakati ya kiusalama, na kuanzisha ushirikiano mpya wa kijeshi na Urusi, huku akikata uhusiano wa karibu na Ufaransa hatua imepokelewa kwa hisia mseto kimataifa lakini kwa kuungwa mkono na sehemu kubwa ya wananchi wa Burkina Faso.
Lakini pia katika maendeleo ya kawaida ndani ya nchi kuanzia miundombinu mpaka huduma mbalimbali kwa miaka mwili kuna tofauti kubwa, akijitahidia pia kuinua sekta za kiuchumi ikiwemo Kilimo, iliyokuwa imedorora kwa miaka kadhaa.
Umaarufu wake na namna anavyovaa kijeshi, kutembea na silaha kiuoni na kusalimiana kwa kukunja ngumi (tano), kunamuweka kuwa kiongozi wa kipekee Afrika.
Historia ya mapinduzi na changamoto za Usalama kwa utawala wa Traoré Burkina Faso

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Burkina Faso imepitia misukosuko mingi ya kisiasa tangu uhuru wake mwaka 1960, ikiwa ni pamoja na mapinduzi ya mara kwa mara. Moja ya mapinduzi yanayokumbukwa zaidi ni yale ya 1983, yaliyomuweka madarakani Thomas Sankara, ambaye aliuawa miaka minne baadaye na rafiki yake wa karibu Blaise Compaoré, aliyeitawala nchi hadi alipoondolewa mwaka 2014 kupitia maandamano makubwa ya wananchi.
Kwa sasa, nchi iko katika hali ngumu ya kiusalama, ikiwa ni mojawapo ya mataifa yanayokumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya kijihadi. Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 40 ya eneo la nchi limo nje ya udhibiti wa serikali.
Katika njama ya hivi karibuni ya kumpindua Traoré , ambayo ilipangwa kufanyika tarehe 16 Aprili 2025, Waziri Sana alisema kuwa wapanga njama walijaribu kutumia viongozi wa dini na wa mila kushawishi maafisa wa jeshi kuunga mkono mapinduzi hayo. Alieleza kuwa "viongozi wa mpango huo walikuwa nje ya nchi, viko Ivory Coast", akiwasema maafisa wawili wa zamani wa jeshi kuwa ndio waliokuwa wakiongoza njama hiyo.
Waziri huyo pia alidai kuwa taarifa nyeti zilifichuliwa kwa magaidi ili kusaidia mashambulizi dhidi ya raia na wanajeshi, na hivyo kuchochea ghasia dhidi ya serikali ya kijeshi.
Wiki iliyopita, wanajeshi kadhaa, akiwemo maafisa wawili, walikamatwa kwa tuhuma za kupanga njama ya "kuvuruga utawala."
Ivory Coast bado haijatoa kauli kuhusu madai haya, lakini serikali ya Burkina Faso imekuwa ikilaumu mara kwa mara nchi hiyo jirani kwa kuwahifadhi wapinzani wake walioko uhamishoni.
Madai haya mapya yanakuja miezi michache tu baada ya serikali kusema ilizima jaribio lingine la "kuvuruga utawala" mwezi Novemba mwaka jana.
Burkina Faso, pamoja na Mali na Niger, ambazo zote zinatawaliwa na serikali za kijeshi, zimeng'atuka kutoka jumuiya ya kikanda ya ECOWAS na kuanzisha ushirikiano mpya wa kikanda.
Vilevile, zimekata mahusiano na Ufaransa, na kuanzisha ushirikiano wa karibu na Urusi. Pamoja na mengine zimekuwa zikikumbwa na changamoto za kiusalama mara kadhaa na majaribio ya mapinduzi.













