Jinsi Hamas walivyofanya shambulio lisilofikirika

Chanzo cha picha, AFP
Waisraeli wengi huenda walikuwa wamelala ilipoanza.
Jumamosi ilikuwa Sabato ya Kiyahudi na pia sikukuu takatifu, kumaanisha kwamba familia zilikuwa zikipanga kutumia wakati nyumbani pamoja au katika sinagogi, na marafiki walikuwa wakikutana.
Lakini kutoka angani alfajiri, mvua ya mawe ya roketi iliashiria kuanza kwa shambulio ambalo halijawahi kutokea katika kiwango kile.
Kwa miaka mingi, Israel imeimarisha kizuizi kati yake na eneo dogo la Wapalestina la Gaza. Ndani ya saa chache, kutopitika kwake kulifichuliwa kuwa na kasoro.
BBC News imekuwa ikichambua picha zilizochukuliwa na wanamgambo na raia chini ili kuweka kubainisha Hamas walivyoratibu mashambulizi yao ya hali ya juu zaidi kuwahi kutokea Gaza.
Roketi ziliashiria kuanza kwa mashambulizi
Karibu 06:30 saa za ndani, roketi zilianza kuruka.
Kundi la wapiganaji wa Kiislamu, linalodhibiti Gaza na kuorodheshwa kuwa kundi la kigaidi nchini Uingereza na kwingineko duniani hutumia mbinu hii mara kwa mara.
Makombora hayo ya kizamani mara nyingi yanatatizika kukwepa mfumo wa hali ya juu wa ulinzi wa makombora wa Iron Dome wa Israeli, lakini maelfu yalirushwa katika muda mfupi ili kuushinda.
Kiwango kinaashiria kuwa kulikuwa na miezi ya kupanga hilo.
Hamas inasema ilifyatua 5,000 katika duru ya kwanza (Israel inasema ilikuwa nusu ya idadi hiyo).
Ving'ora vya mashambulizi ya anga vilianza kusikika hadi Tel Aviv - kilomita 60 kutoka Gaza na Yerusalemu ya magharibi na moshi ulionekana ukipanda juu ya miji ambayo kulikuwa na milio ya moja kwa moja.
Wakati roketi hizo zikiendelea kurushwa, wapiganaji walikuwa wakikusanyika ambapo walipanga kupenya kizuizi kikubwa cha Gaza.
Ingawa Israel iliondoa wanajeshi wake na walowezi kutoka Gaza mwaka 2005, bado inadhibiti anga yake, mpaka wa pamoja na ufuo.
Pamoja na doria za kawaida za kijeshi kuzunguka eneo hilo ambalo ni ukuta wa zege katika baadhi ya maeneo na uzio katika maeneo mengine, pia kuna mtandao wa kamera na vihisi ili kuzuia uvamizi.
Lakini ndani ya saa chache, kizuizi kilikuwa kimevunjwa tena na tena.
Maeneo ambayo Hamas walivuka hadi Israeli

Hamas waliingia vipi?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadhi ya wapiganaji wa Hamas walijaribu kukwepa kizuizi kabisa, ikiwa ni pamoja na kuruka juu yake kwenye paraglider (picha ambazo hazijathibitishwa zilionesha angalau saba zikipeperushwa juu ya Israeli) na kwa mashua.
Vikosi vya Ulinzi vya Israel vimesema vimezuia majaribio mawili ya Hamas ya kuvuka kuingia Israel kwa kuifikisha meli ufukweni.
Lakini kinachotenganisha shambulio hili ni mashambulizi kadhaa yaliyoratibiwa, ya moja kwa moja kwenye maeneo ya vizuizi.
Saa 05:50 kwa saa za huko, akaunti ya Telegram inayohusishwa na mrengo wenye silaha wa Hamas ilichapisha picha za kwanza kutoka ardhini, zilizopigwa Kerem Shalom, kusini zaidi mwa vivuko vya Gaza.
Walionesha wanamgambo wakivuka kizuizi na miili iliyojaa damu ya wanajeshi wawili wa Israel ikiwa chini.
Picha nyingine ilionesha pikipiki zisizopungua tano, kila moja ikiwa na wanamgambo wawili waliokuwa na bunduki, zikipita kwenye shimo lililokuwa limekatwa kwenye sehemu ya uzio wa waya wa kizuizi.

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA
Katika sehemu yenye ulinzi mdogo, tingatinga lilionekana likibomoa kipande cha uzio wa waya wenye miinuko.
Makumi ya watu walioonekana kutokuwa na silaha walikuwa wamekusanyika hapo, na wengine wakaanza kukimbia kupitia uwazi.

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA
Huko Erez, kaskazini zaidi ya vivuko vya Gaza, karibu kilomita 43.4 (maili 27) kutoka Kerem Shalom, Hamas walikuwa wakivuka kivuko kingine.
Picha za video ziliwekwa kwenye moja ya chaneli za propaganda za kikundi hicho. Inaonesha mlipuko kwenye kizuizi cha zege, ambacho kilikuwa kama ishara ya kuanza shambulio, na mwanamgambo alionekana akipunga kundi la wapiganaji kuelekea eneo la mlipuko.
Wanaume wanane waliovalia fulana zinazozuia risasi na kubeba bunduki walikimbia kuelekea kwenye kituo cha ukaguzi kilichoimarishwa sana na kuwafyatulia risasi wanajeshi wa Israel.
Baadaye kwenye video hiyo, miili ya wanajeshi wa Israel inaonekana ikiwa imelala sakafuni huku wanamgambo hao wakienda kutoka chumba hadi chumba kufagia boma, wakiwa wamejipanga vyema na kupewa mafunzo.
Gaza ina vivuko saba rasmi, sita vinadhibitiwa na Israel, kimoja kuelekea Misri kinadhibitiwa na Cairo.
Lakini ndani ya muda wa saa chache, Hamas ilikuwa imepata njia za kuingia katika eneo la Israel kwenye urefu wa kizuizi.
Mashambulizi yafika ndani kabisa ya eneo la Israeli
Wapiganaji wa Hamas walitoka Gaza katika pande zote. Sasa tunajua kutoka kwa mamlaka ya Israel kwamba walishambulia maeneo 27 tofauti, inaonekana kwa amri ya kuua mara moja.
Hamas ilipenya zaidi mji wa Ofakim, ambao uko kilomita 22.5 (maili 14) mashariki mwa Gaza. Ramani iliyo hapa chini inaonesha maeneo tofauti waliyofikia.

Huko Sderot, wanamgambo walionekana wakiwa wamesimama nyuma ya lori lililokuwa likiendeshwa katika mji huo, ambao uko karibu kilomita 3 (maili 1.8) mashariki mwa Gaza.
Takribani wapiganaji dazeni waliokuwa na silaha walionekana wakipepea kupitia mitaa mitupu ya Ashkeloni, kaskazini mwa kivuko cha Erez ambacho kilikuwa kimevamiwa.
Matukio kama hayo yalirudiwa kote kusini mwa Israeli na raia waliambiwa na wanajeshi kujificha ndani ya nyumba.
Katika tamasha la muziki karibu na Re'im, watu wenye silaha walifyatua risasi wapendavyo kundi kubwa la vijana waliokuwa wamekusanyika jangwani.
Mtu aliyeshuhudia aliiambia BBC jinsi wanamgambo hao walivyokuwa wakiendesha gari karibu na gari lililokuwa na silaha na kutumia saa tatu kutafuta eneo hilo ili kuwapata Waisraeli wengine.
Wanajeshi na raia waliochukuliwa mateka
Sasa tunajua kwamba mateka walichukuliwa kutoka kwenye tamasha na maeneo mengine na kusafirishwa kurudi Gaza. Israel inasema watu 100, wanajeshi na raia wametekwa nyara.
Picha zilizopigwa katika mji wa Be'ri na kuthibitishwa na BBC zinaonesha takribani raia wanne wakiongozwa kwa nguvu na wanamgambo.
Video kadhaa zimesambaa mtandaoni za Waisraeli, baadhi yao wakiwa wamejeruhiwa vibaya, wakioneshwa gwaride kwenye mitaa yenye watu wengi huko Gaza.
Ukatili mwingine ambao haujathibitishwa ambao hauwezekani kuchapishwa ulinaswa kwenye kamera, ikiwa ni pamoja na dereva kuburutwa kutoka kwenye gari lake na kukatwa koromeo, na miili ya raia waliokufa na wanajeshi kunajisiwa.

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA
Pamoja na kulenga jumuiya za Israeli, Hamas pia ilishambulia maeneo mawili ya kijeshi: kituo cha Zikim na kingine huko Re'im.
Picha zilizochukuliwa kutoka karibu na Re'im zinaonesha matokeo, huku magari kadhaa yaliyoteketea yakiwa yametawanyika kando ya barabara hadi chini. Haijulikani ni watu wangapi waliuawa wakati wa mapigano hayo.
Idhaa za mitandao ya kijamii za Hamas mara kadhaa zimesambaza picha za wanajeshi wa Israel waliouawa. BBC News haijathibitisha picha hizi.
Ndani ya saa chache tu ya kuanza kwa shambulio la roketi, mamia ya Waisraeli walikuwa wamekufa na ilitokea kwa njia ambayo hakuna mtu aliyefikiria inawezekana.
Usaidizi ulianza kufika katika eneo la kusini lililoathiriwa ndani ya saa chache lakini Hamas ilikuwa katika udhibiti mzuri wa vipande vya eneo nje ya Gaza.
Kasi na muda wa mwisho wa shambulio hilo la kushtukiza limeishangaza Israel. Maswali juu ya jinsi iliweza kutokea yataulizwa kwa miaka.
Kufikia katikati ya asubuhi, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alitangaza: "Tuko vitani."












