Mzozo wa Palestina na Israel: Kipi kinaendelea Israel na Gaza?

WE

Chanzo cha picha, EPA

Wanamgambo wenye silaha wa Hamas walifanya shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel kutoka Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba, na kuua zaidi ya watu 1,400 na kuwachukua mateka wasiopungua 239.

Tangu wakati huo, Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya kulipiza kisasi Gaza, ambapo zaidi ya watu 8,000 wameuawa, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas. Israel pia imetuma wanajeshi na vifaru katika eneo hilo.

Israel imeingia Gaza

E

Chanzo cha picha, IDF

Maelezo ya picha, Vifaru vya Israel

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema vikosi vya ardhini vimeingia Gaza "kusambaratisha" Hamas na kuwarudisha mateka nyumbani.

Siku ya Jumatatu Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema wanajeshi wake "wameua makumi ya magaidi ambao walijifungia katika majengo na mahandaki, walipojaribu kuwashambulia wanajeshi."

IDF ilisema imeendelea kushambulia mamia ya majengo ya Hamas kutoka angani. Magari ya kivita ya Israel yameonekana karibu na Mji wa Gaza, kwenye barabara kuu.

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema jeshi la Israel lilitoa amri ya kuhamwa hospitali ya Al-Quds kaskazini mwa Gaza, lakini haiwezekani kuwahamisha mamia ya wagonjwa wanaotibiwa humo.

Mashuhuda wanasema kuna mashambulizi makubwa ya makombora karibu na hospitali hiyo, ambapo watu 14,000 wanadhaniwa kuwa wamejihifadhi.

Jeshi la Israel limepeleka maelfu ya wanajeshi kwenye eneo la uzio wa Gaza, pamoja na vifaru na mizinga. Imeita askari wa akiba wapatao 300,000 pamoja na kikosi chake cha kudumu cha 160,000.

Hamas inadhaniwa kuwa na takriban wapiganaji 25,000. Pia ina mtandao wa mahandaki ya chini ya ardhi kote Gaza, yenye urefu wa kilimoita 500 (maili 310), yanayounganisha vituo vyake vya kamandi.

Siku ya Jumatatu, Hamas ilitoa video inayoonyesha watu watatu mateka huko Gaza. Wanawake hao watatu wanaonekana wakiwa na afya nzuri bila dalili zozote za kuumia.

Hali ya kibinadamu ikoje Gaza?

FDCV

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Njiwa akiruka juu ya vifusi vya nyumba huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, Unrwa, linasema maelfu ya wakaazi wa Gaza wamevamia vituo vyake vya maghala "na kuchukua unga wa ngano na vitu vingine muhimu vya kujikimu kama vile vifaa vya usafi."

Umoja wa Mataifa pia umesema watoto wengi wanatumia maji ya chumvi kunywa.

Shirika la Afya Duniani limesema hospitali za Gaza zinafanya kazi kwa shida kutokana na uhaba wa umeme na vifaa.

Mwishoni mwa wiki, makumi ya malori yaliyobeba misaada yaliingia Gaza kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah kutoka Misri. Hata hivyo, Gaza kwa kawaida hupokea malori 500 kwa siku.

Rais wa Marekani Joe Biden ameiambia Israel upelekaji wa misaada Gaza unahitaji kuongezwa kwa kiasi.

Israel imekataa kuruhusu usafirishaji wa mafuta kwa sababu inasema yanaweza kutumiwa na Hamas. Vilevile inasema Hamas inahifadhi maelfu ya lita za mafuta ambayo inakataa kuyakabidhi kwa mashirika ya misaada.

Jeshi la Israel limeamuru watu kuondoka katika maeneo ya kaskazini kwa usalama wao wenyewe, hadi sasa watu milioni 1.4 wamehamia kusini.

Mji wa kusini wa Khan Younis, ambao kawaida ni makazi ya watu 400,000, idadi ya watu imeongezeka hadi kufikia milioni 1.2. Familia nyingi hulala kwenye mahema. Takriban 600,000 wanahudumiwa na Unrwa.

Hamas ni nani na wanataka nini?

FD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mpiganaji wa Hamas katika handaki Gaza

Hamas ni kundi la Wapalestina ambalo limetawala Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2007. Kundi hilo limeapa kuiangamiza Israel ili kuunda taifa la Kiislamu.

Hamas imepigana vita kadhaa na Israel tangu ilipochukua mamlaka. Imerusha - au kuruhusu vikundi vingine kurusha - maelfu ya makombora kwenda Israel, na imefanya mashambulizi mengine mabaya.

Israel hujibu kwa kushambulia maeneo ya Hamas kutoka angani. 2008 na 2014, pia ilituma wanajeshi Gaza. Kwa pamoja na Misri, Israel imeufunga Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2007 kwa kile inachoelezwa kuwa ni sababu za kiusalama.

Hamas - au kwa jina jingine Brigedi za Izzedine al-Qassam - linatajwa kuwa kundi la kigaidi na Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na Uingereza, pamoja na mataifa mengine yenye nguvu.

Iran inaliunga mkono kundi hilo kwa kulipatia ufadhili, silaha na mafunzo.

Kwanini Hamas ilifanya shambulizi?

ED

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Mwaka huu umekuwa mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa kwa Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, jambo ambalo linaweza kuwa chanzo cha Hamas kuishambulia Israel.

Hamas pia inaweza kuwa inataka kupata ushindi muhimu wa propaganda ili kuongeza umaarufu wake miongoni mwa Wapalestina wa kawaida.

Kukamatwa kwa mateka wa Israel kunakisiwa kulenga kuishinikiza Israel kuwaachilia huru baadhi ya Wapalestina 4,500 wanaoshikiliwa katika jela za Israel.

Jeshi la Israel linasema watu 229 bado wanazuiliwa huko Gaza. Wakiwemo watoto 20 na watu 10 wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na wanajeshi pia walichukuliwa mateka.

Hamas hadi sasa imewarudisha mateka wanne, Qatar ikiwa ndio mpatanishi wa kuachiliwa kwao.

Gaza ni eneo la aina gani?

3W
Maelezo ya picha, Ukanda wa Gaza ni eneo la urefu wa kilomita 41 (maili 25) na upana wa kilomita 10

Ukanda wa Gaza ni eneo la urefu wa kilomita 41 (maili 25) na upana wa kilomita 10 – ukanda huo uko kati ya Israel, Misri na Bahari ya Mediterania.

Hapo awali ulikuwa chini ya Misri, kisha ulitekwa na Israel wakati wa vita vya Siku Sita vya 1967. Israel iliondoa wanajeshi wake na walowezi karibu 7,000 katika eneo hilo 2005.

Ni nyumbani kwa watu milioni 2.23. Ni eneo lenye msongamano mkubwa zaidi wa watu ulimwenguni. Zaidi ya 75% ya wakazi wa Gaza - watu milioni 1.7 - ni wakimbizi waliosajiliwa au vizazi vya wakimbizi, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya 500,000 kati yao wanaishi katika kambi nane zilizojaa watu kwenye Ukanda huo.

Israel inadhibiti anga ya Gaza na ufuo wake, na inadhibiti usafirishaji wa bidhaa kuingia na kutoka na inadhibiti safari za watu pia.

Ijue Palestina

EW
Maelezo ya picha, Israel ilitangazwa kuwa taifa mwaka 1948, ingawa ardhi hiyo bado inajulikana kama Palestina na nchi ambazo hazitambui taifa la Israel

Ukingo wa Magharibi na Gaza, yanajuulikana kama maeneo ya Palestina, pamoja na Jerusalem Mashariki na Israeli ya leo – hiyo yote ikijuulikana kama Palestina kutoka nyakati za Warumi hadi katikati ya Karne ya 20.

Pia zilikuwa ardhi za falme za Kiyahudi katika Biblia, na inaonekana na Wayahudi wengi kama nchi yao ya kale.

Israel ilitangazwa kuwa taifa mwaka 1948, ingawa ardhi hiyo bado inajulikana kama Palestina na nchi ambazo hazitambui taifa la Israel.

Wapalestina pia hutumia jina la Palestina kumaanisha Ukingo wa Magharibi, Gaza na Jerusalem Mashariki.

Rais wa Palestina ni Mahmoud Abbas, pia anajulikana kama Abu Mazen. Anaishi katika Ukingo wa Magharibi, ambao uko chini ya utawala wa Israel.

Amekuwa kiongozi wa Mamlaka ya Palestina (PA) tangu 2005, na anawakilisha chama cha kisiasa cha Fatah, mpinzani mkali wa Hamas