Mauaji ya Wayahudi yaliyosahaulika: 'Kwa nini walituua?

.

Chanzo cha picha, Delfin lakatosz

Maelezo ya picha, Hinta Gheorge na mkewe

"Kwanini walitaka kutuua? Kwanini walituua?" anauliza, ajuza mwenye umri wa miaka 83 manusura wa mauaji ya Holocaust ya Roma Hinta Gheorghe.

Alipelekwa kwenye kambi huko Transnistria, eneo kati ya mito ya Dniester na Bug, iliyosimamiwa na Ufalme wa Romania kati ya 1941 na 1944, akiwa na umri wa miaka miwili wakati wa Vita vya Pili vya dunia.

 "Sina kumbukumbu nyingi za safari yenyewe, kwani iliacha madoa katika maisha yangu yote," Gheorghe aliambia BBC kupitia kwa mjukuu wake Izabela Tiberiade.

 Takriban watu milioni 11 waliuawa kwa sababu ya sera ya mauaji ya kimbari ya Nazi. Milioni tano kati ya waliouawa hawakuwa Wayahudi.

Wanahistoria wanakadiria watu 250,000 hadi 500,000 Waroma na Wasinti waliuawa wakati wa Maangamizi Makuu. Lakini waathiriwa hawa wanabaki kusahaulika kwa kiasi kikubwa.

 Wanazi waliamini kuwa Wajerumani walikuwa Waarya na kwa hivyo "kuwa kabila kuu". Baadhi ya watu hawakutakiwa na viwango vya Nazi kwa sababu ya wao walikuwa nani, asili yao ya kijeni au kitamaduni, au hali za afya. Hawa ni pamoja na Wayahudi, Wagypsies, Poles na Waslavu wengine, na watu wenye ulemavu wa kimwili au kiakili.

 Waathiriwa wengine walikuwa Mashahidi wa Yehova, watu wa jinsia-moja, makasisi wasiokubalika, wakomyunisti, wanasoshalisti, ‘wanazi’ (neno lililotumiwa na Wanazi kuainisha kikundi cha watu ambao hawakupatana na kanuni zao za kijamii), na maadui wengine wa kisiasa

Kambi za mauaji

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Mama yangu alipoteza watoto wakati wa kusafiri katika treni hizo za ng'ombe, na nadhani sehemu yake ilibaki pale milele, hata baada ya miaka mingi, wakati yote yalikuwa kumbukumbu tu," Gheorghe anaongeza.

 "Tulielewa kilichokuwa kikitokea kambini hata kabla hatujafika huko. Wengi walikufa njiani. Watu wengi sana kwenye treni ndogo, iliyoundwa kwa ajili ya usafirishaji wa ng'ombe."

 Ofisi Kuu ya 'Mapambano dhidi ya Kero ya Gypsy' ilianzishwa mnamo Juni 1936 na Wanazi. Ofisi ya Munich ilipewa jukumu la "kutathmini matokeo ya utafiti wa kibaolojia wa rangi" kuhusu Sinti na Roma.

 Kufikia 1938, Sinti na Roma walikuwa wakipelekwa kwenye kambi za mateso.

Kama Wayahudi, walinyimwa haki zao za kiraia. Watoto wa Roma na Sinti walipigwa marufuku kutoka shule za umma na watu wazima walipata shida zaidi kudumisha au kupata ajira.

 Waroma, watu wahamaji wanaoaminika kuwa walitoka kaskazini-magharibi mwa India, walikuwa na makabila au mataifa kadhaa.

Wengi wa Waroma walioishi Ujerumani walikuwa wa taifa la Sinti. Walikuwa wameteswa kwa karne nyingi. Utawala wa Nazi uliendelea na mnyanyaso huo, ukiwaona Waromani kuwa watu wa jamii na watu wa hali ya chini kuliko Wajerumani.

 "Hakuna mtu aliyetujali lakini wakati huo huo, walituchukia sana," anakumbuka Gheorghe.

.Zaidi ya Waroma 21,000 waliuawa huko Auschwitz-Birkenau

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Zaidi ya Waroma 21,000 waliuawa huko Auschwitz-Birkenau

Kambi za Gypsy Auschwitz

.Izabela Tiberiade anasema mjomba-mjukuu wake ameumia sana hivi kwamba hawezi kusimulia hadithi zote za kutisha alizosikia.

Chanzo cha picha, Delfin lakatosz

Maelezo ya picha, Izabela Tiberiade anasema mjomba-mjukuu wake ameumia sana hivi kwamba hawezi kusimulia hadithi zote za kutisha alizosikia.

Kufikia 1943, eneo kubwa la kambi ya Auschwitz-Birkenau lilipewa mgawo wa kuwaweka Sinti na Roma waliofukuzwa.

 Idadi ya wafungwa inakadiriwa kuwa 23,000 hivi. Wengi wakawa wahathiriwa wa majaribio ya kitiba; wengine walikufa kwa uchovu au waliuawa katika vyumba vya gesi.

 Kambi hiyo ilivunjwa mnamo Agosti 1944. Wengi wa wafungwa wake waliuawa au kuhamishiwa kwenye kambi nyinginezo. Mwishowe angalau wanaume, wanawake na watoto 21,000 waliuawa.

 Wakati Hinta Gheorghe na washiriki walionusurika wa familia yake waliporudi kutoka kambi ya kifo baada ya miaka mitatu ya kuchosha, walipata nyumba zao huko Rumania ama zimeharibiwa au kuchukuliwa na mtu mwingine.

 "Walitudharau na vibaya zaidi ni kwamba bado wanatuondoa kwenye historia yetu, watoto wengi wa siku hizi hawana fununu ya kilichotokea, ila wanasikia nyimbo za bibi vikongwe wanaokumbuka na kulia huku wakiimba."

 "Nyimbo zetu hubeba mateso, hali zisizovumilika katika kambi ambazo zilikuwa mbaya sana. Uchafu, njaa, baridi, si makazi bora [...] msongamano unaosababisha magonjwa polepole na maumivu."

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ni kuanzia 2015 ndiposa mauaji ya halaiki ya Warumi yalianza kuadhimishwa rasmi huko Uropa

Ubaguzi uliokitwa

.Wengi waliuawa katika kambi za mateso ambako Waromani waliwekwa kando. Hii ni picha ya Roma iliyopigwa katika kambi ya Belzec mnamo 1940.

Chanzo cha picha, Holocausr Libary collection

Maelezo ya picha, Wengi waliuawa katika kambi za mateso ambako Waromani walitengwa. Hii ni picha ya Roma iliyopigwa katika kambi ya Belzec mnamo 1940.

Barbara Warnock, msimamizi mkuu wa Maktaba ya Holocaust ya Wiener iliyoko London anasema kuwa kutengwa kwa kijamii na ubaguzi uliohalalishwa ndani ya jamii ya Ujerumani kulifanya iwe rahisi zaidi kwa Wanazi kulenga jamii ya Waroma.

 "Mwanzoni ilianza kama aina ya mwendelezo wa hatua na mitazamo ya chuki iliyopo tayari. Wanazi walikuwa wakijenga sheria zilizopo. Warumi lilikuwa kundi lililotengwa sana nchini Ujerumani," anasema.

 Dkt Warnock pia anaonyesha ukosefu wa rekodi rasmi za watu wa Roma wakati wa Vita vya dunia vya pili.

 "Kuna mashaka mengi kuhusu idadi hiyo. Wengine waliuawa katika kambi za kifo, wengi walikufa kwa kupigwa risasi na watu wengi, hasa katika maeneo ya Sovieti. Jeshi la Ujerumani lilifuatiwa na Einsatzgruppen (vikosi vya mauaji ya kijeshi ya Ujerumani ya Nazi) na washirika wa ndani walihusika katika kupiga risasi nyingi."

Mara tu baada ya vita, Wanazi wengi wakuu walikamatwa na kuhukumiwa na mahakama za kijeshi na katika mahakama ya Nuremberg.

Katika kesi hizi, hakuna hata mmoja aliyeshtakiwa kwa mauaji ya Warumi. Wanazi mara nyingi walidai kwamba "watu wa Roma waliowakamata walikuwa wahalifu".

Hofu mpya

.

Chanzo cha picha, Delfin lakatosz

Maelezo ya picha, Kizazi cha vijana wa Roma kama Izabela Tiberiade wana nia ya kuweka kumbukumbu za mauaji ya Holocaust ili kubadilisha simulizi kuhusu jamii yao.

Kwa Gheorghe, ubaguzi ambao yeye na jamii yake walikabili nchini humo kama 'mgeni' haukuwa tu kwa utawala wa Nazi.

 Baada ya kuanguka kwa Ukomyunisti wa Soviet, Gheorghe aliondoka Rumania kwenda Ujerumani.

Lakini miezi michache baada ya kufika, alipata shambulio la kikatili la chuki dhidi ya wageni mwaka wa 1992, lililojulikana kama ghasia za Rostock-Lichtenhagen mnamo Agosti 1992.

 Ilikuwa ni vurugu mbaya zaidi za mrengo wa kulia nchini Ujerumani tangu Vita vya Pili vya Dunia. Watu wenye itikadi kali waliwalenga wahamiaji wakati wa ghasia hizo kwa kurusha mawe, mabomu ya petroli kwenye jengo la ghorofa ambalo waomba hifadhi waliishi.

 "Inasikitisha sana kwamba mrithi wa watu walioleta mateso mengi, alitekeleza urithi huo. Watoto wetu wanastahili bora kuliko chuki na hasira," anasema Hinta Gheorghe.

Kizazi kipya

.

Chanzo cha picha, Delfin lakatosz

Maelezo ya picha, Izabela Tiberiade anasema alifikiri ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wa Roma ulikuwa jambo la zamani hadi alipokabiliana na chuki mwenyewe.

Wahasiriwa waliosahaulika wa Maangamizi ya Holocaust pia walipendezwa na mateso ya mababu zao.

Mjukuu wa Hinta Gheorghe Izabela Tiberiade hata hakuzaliwa wakati familia yake ilipokabiliwa na mashambulizi mapya yaliyochochewa na itikadi ya Nazi mamboleo.

 Shuleni alisoma kuhusu Vita vya dunia vya pili na mauaji ya kimbari, lakini mateso ya Waromani yalipuuzwa, anasema. Ilikuwa nyumbani huko Rumania, ambapo aligundua zaidi. Akiwa ameazimia kutafuta haki, aliamua kusomea Haki za Kibinadamu na Sheria za Kimataifa.

 "Walikuwa wakisimulia hadithi ambazo vizazi vyetu vipya havikuweza kuelewa," Tiberiade aliiambia BBC.

 "Niligundua kwamba babu na nyanya yangu, wajomba na wengine wengi walishiriki uzoefu kama huo. Walihamishwa hadi kwenye kambi za kifo, kwa sababu tu walikuwa Waroma."

 "Vizazi vipya havina fursa ya kupata habari, kuna ukosefu wa uwakilishi na vijana mara chache huunganishwa na maisha yao ya nyuma na mizizi. Wengine hata wanaona kuwa Roma ni makosa," anasema.

 Tiberiade anataka vijana wa Roma pamoja na wengine kujifunza zaidi kuhusu Mauaji ya Wayahudi ambayo "anatumai yangewafanya wengine waitazame jamii yake kwa huruma zaidi."

 Kuna juhudi za kimataifa pia.

 Mnamo mwaka wa 2015, ripoti ya Umoja wa Mataifa ilitoa wito wa kujitolea kwa nguvu na dhahiri kisiasa kupigana na upendeleo na ubaguzi unaoendelea kukiuka haki za watu wa Roma.

 Bunge la Ulaya pia liliidhinisha kuzingatia, Siku ya Ukumbusho ya Holocaust ya Uropa ya Roma katika 2015. Iliwekwa alama tarehe 2 Agosti. Watu wa Roma pia wanakumbukwa pamoja na wahasiriwa wengine wakati wa Siku ya Ukumbusho wa Holocaust.

 "Hatuwezi kubadilika mara moja. Inachukua muda, uamuzi, na juhudi nyingi. Tunahitaji kukubalika na kuvumiliana," Tiberiade alisema.

 "Tunahitaji kusherehekea utamaduni wetu na historia na lugha kwa pamoja. Tunatakiwa kuacha kuzungumza kuhusu sisi kwa sisi, lakini badala ya kuzungumza sisi kwa sisi." 

Mjukuu wa mjomba wa Tiberiade aliyenusurika kwenye mauaji ya Holocaust Hinta Gheorghe sasa anaishi Craiova nchini Rumania. Ana hamu kwa jamii yake:

"Nataka vijana wote wa Kiromani kuhudhuria shule na kujifunza na kutimiza yote ambayo hatungeweza kamwe."