Mamia ya wagonjwa wamekwama katika hospitali za Gaza-UN

Alisema watu wengi wa kaskazini - sio wagonjwa pekee - pia "hawawezi kusonga kwa sababu hawana usafiri, hawana njia".

Moja kwa moja

Yusuf Jumah and Ambia Hirsi

  1. Familia ya mtanzania aliyetekwa Gaza: Tunatumaini atarejea salama, japo wasiwasi upo,

    Dada wa Clemence, Neema Christina Mtenga

    Familia ya mmoja wa watanzania wawili wanaoshikiliwa mateka na kundi la Hamas huko Gaza, Clemence Felix Mtenga imesema wana matumaini juu ya ndugu yao kurejea salama japo pia bado kuna wasiwasi na mashaka juu ya mustakabali wake

    Mtanzania mwingine anayeshikiliwa mateka ni Joshua Loitu Mollel. Wawili hao ni wanafunzi wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo. Walitekwa Oktoba 7 wakati wa mashambulio ya Hamas kwa Israel kisha Israel kuanzisha mashambulizi ya kulipa kisasi.

    Dada wa Clemence, Neema Christina Mtenga, ameiambia BBC taarifa mpya za kutajwa kwa majina ya waliotekwa akiwemo ndugu yao zimewapata matumaini mapya kuliko awali lakini hiyo haimaanishi wasiwasi umeondoka kabisa.

    “Kiukweli kwa sasa siwezi siwezi kusema kwamba tuna ahueni sana lakini kidogo baada ya kuzungumza na ubalozi kuna taarifa tulipewa ambazo zilitutia matumaini kulinganishana hapo awali. Balozi wa Tanzania aliyepo Israel aliwasiliana na baba na alichotuambia ni kwamba Clemence ni mmoja wa watu ambao hawaonekani na kuna namna ambavyo anafanya ili kumpata”

    Maelezo ya video, Familia ya mtanzania aliyetekwa Gaza: Tunatumaini atarejea salama, japo wasiwasi upo

    Neema, ameongeza kuwa: “Kwa kweli, kila mtu ana mashaka, ana huzuni, ukizingatia kuwa ni mdogo wetu na ni juzi tu amekwenda na hali ukiangalia katika vyombo vya habari inatia mashaka, hakuna mtu ambaye anaweza kulala vizuri. Kwa kweli sijui nielezeje lakini ni hivyo”.

    Hata hivyo, amesema “Tunaamini kwamba kwa uwezo wa Mungu watarejea kulingana na taarifa tunazopata kuopitia machapisho mbalimbali kw ani miongoni mwa waliotekwa na Hamas, kwa hiyo tunaamini kwamba kwa huruma ya Mungu ndugu yetu atarejea salama”.

    Akimzungumzia Clemence kitabia na mwennedo amesema ni mtu mtulivu, anayefanya mamabo yake kwa umakini pia mtaratibu na kwa sababu ya utulivu huo ndiyo maana wanapata mashaka juu ya hali yake huko aliko kwa sasa na kwamba wangependa apate ujumbe kuwa wanampenda na wanamuombea usiku na mchana.

    Unaweza kusoma;

  2. Luis Rubiales: Aliyekuwa mkuu wa shirikisho la soka nchini Uhispania apigwa marufuku ya miaka mitatu na Fifa

    Luis Rubiales

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa zamani wa shirikisho la soka nchini Uhispania Luis Rubiales amepigwa marufuku na Fifa kujihusisha na soka kwa miaka mitatu.

    Rubiales alimbusu mshambuliaji Jenni Hermoso kwenye midomo kufuatia ushindi wa fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake wa Uhispania dhidi ya England.

    Busu hilo, ambalo mshambuliaji Hermoso anasema halikuwa la maafikiano, lilizua kelele, na hatimaye Rubiales alijiondoa kwenye jukumu lake mnamo Septemba.

    Hermoso baadaye aliwasilisha malalamiko ya kisheria dhidi ya Rubiales.

    Siku ya Jumatatu, shirikisho la soka duniani Fifa lilitangaza marufuku ya miaka mitatu kwa kukiuka kifungu cha 13 cha kanuni zake za nidhamu.

    Rubiales anasema ananuia kukata rufaa dhidi ya marufuku hiyo.

    “Nitakwenda hatua ya mwisho kuona haki inatendeka na ukweli unadhihirika,” alisema kwenye mitandao ya kijamii.

    Fifa ilithibitisha kesi dhidi yake ilihusu "matukio yaliyotokea wakati wa fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake la Fifa mnamo tarehe 20 Agosti 2023, ambapo Bw Rubiales alikuwa amesimamishwa kwa muda wa siku 90".

    "Fifa inasisitiza dhamira yake kamili ya kuheshimu na kulinda uadilifu wa watu wote na kuhakikisha kuwa kanuni za msingi za maadili zinafuatwa," ilisema taarifa hiyo.

  3. Luis Diaz: Wanajeshi wamsaka baba wa mchezaji wa Liverpool

    Luis Diaz

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Msako mkubwa wa jeshi na polisi unaendelea nchini Colombia kumtafuta baba yake mshambuliaji wa Liverpool Luis Diaz, huku mamlaka ikitenga zawadi ya pauni 40,000 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za kumuwezesha kumuokoa.

    Zaidi ya wanajeshi 120, pamoja na polisi, walimtafuta Luis Manuel Diaz kaskazini mwa Colombia siku ya Jumapili, huku kukiwa na ripoti kuwa watu waliokuwa na silaha walikuwa wamemchukua yeye na mke wake.

    Mama yake mchezaji huyo, Cilenis Marulanda, alipatikana mjini Barrancas siku ya Jumamosi. Diaz hakuwepo katika kikosi cha Liverpool ambacho kiliishinda Nottingham Forest siku ya Jumapili.

    Jeshi hilo limesema limeweka vizuizi barabarani na kupeleka vikosi viwili vya magari, ndege zisizo na rubani, helikopta na ndege yenye rada katika kumsaka baba yake.

    Mamlaka ya Colombia haijatoa maelezo zaidi kuhusu utekaji nyara huo ulioripotiwa, lakini vyombo vya habari vya ndani vilisema mama na baba yake Diaz walichukuliwa na watu wenye silaha wakiwa kwenye pikipiki katika kituo cha mafuta cha Barrancas, mji wa nyumbani kwao, ulioko La Guajira, eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.

    Rais wa Colombia Gustavo Petro alisema "majeshi yote ya umma yametumwa" kumtafuta babake Diaz.

  4. Tazama Video: Kifaru cha jeshi la Israel chashambulia gari moja huko Gaza

    Maelezo ya video, Kifaru cha Israel chashambulia karibu na gari moja kaskazini-kusini mwa Gaza

    Video iliyothibitishwa inaonyesha kifaru cha kijeshi kikilishambulia gari moja kwenye barabara ya kusini mwa Gaza City.

    BBC imethibitisha kanda hii ya kifaru kwenye barabara ya Salah-al-Din, kusini mwa Gaza City mapema. Inaonekana kushambulia gari moja hali iliosababisha mlipuko

    Ripota wetu huko Gaza, Rushdi Abualouf, anasema barabara sasa iko wazi na haijazibwa tena.

  5. Nilitazama nyuma na kuona mizinga ya Israeli, anasema mpiga picha kwenye njia ya Gaza

    Haya ni maendeleo makubwa sana. Watu wamekuwa wakituma video na picha za mizinga na tingatinga za Israel zikifunga barabara ya Salah-al-Din.

    Inaonekana kuingia na kutoka kwa Jiji la Gaza na kaskazini mwa Gaza kwenye barabara hiyo kumekatwa.

    Nimezungumza na mpiga picha ambaye alikuwa eneo hilo akirekodi shambulio la anga na akasema "ghafla nilitazama nyuma na nikaona vifaru vya Israeli". Alichukua picha kadhaa kisha akakimbia.

    Tunaelewa kuwa mizinga ilikuwa ikirusha makombora katika eneo hilo.

    Gari moja lililokuwa likirudi Gaza City kutoka Khan Younis lililengwa na kulikuwa na majeruhi, kulingana na mamlaka ya eneo hilo.

  6. Vurugu za DR Congo zasababisha watu milioni 7 kuyakimbia makazi yao - UN

    Katika picha hii ya mwaka jana watu wanaonekana wakikimbia ghasia huko Kivu Kaskazini

    Chanzo cha picha, Reuters

    Umoja wa Mataifa unasema rekodi ya watu milioni 6.9 sasa ni wakimbizi wa ndani ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na kuongezeka kwa ghasia.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji limekusanya data za ufuatiliaji kutoka majimbo yote 26 ya nchi hiyo.

    Inasema idadi kubwa ya waliokimbia makazi yao wanaishi mashariki ambako migogoro inatajwa kuwa sababu kuu.

    Huko Kivu Kaskazini pekee, hadi watu milioni moja wamekimbia makazi yao mwaka huu kutokana na mapigano yanayoendelea na waasi wa M23.

    Imeonya kuwa DR Congo inakabiliwa na mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao na ya kibinadamu.

    Unaweza kusoma;

  7. Mfalme Charles akabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu unyanyasaji wa enzi ya ukoloni nchini Kenya

    Mfalme Charles III na mkewe Malkia Camilla wanatarajiwa nchini Kenya siku ya Jumanne, katika ziara ya siku nne

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mfalme Charles III na mkewe Malkia Camilla wanatarajiwa nchini Kenya siku ya Jumanne, kwa ziara ya siku nne

    Tume ya Haki za Kibinadamu nchini Kenya, ambayo ni shirika lisilo la kiserikali, imesema Mfalme Charles III anapaswa kuomba msamaha kwa unyanyasaji uliofanywa na Uingereza wakati wa ukoloni.

    Zaidi ya 10,000 waliuawa wakati mamlaka ya Uingereza ilipokandamiza vuguvugu la kupigania uhuru katika miaka ya 1950 - 1,000 walinyongwa baada ya kudaiwa kupatikana na makosa.

    Kundi la haki za binadamu siku ya Jumapili lilisema linatarajia " ombi la msamaha wa umma usio na shaka" kutoka kwa mfalme.

    Miaka kumi iliyopita, serikali ya Uingereza ilitambua rasmi kwamba watawala wa kikoloni walifanya ukatili.

    Ilionyesha masikitiko yake ya dhati na kukubali kulipa fidia kwa maelfu ya maveterani wa uasi huo.

    Baadhi ya jamii za Wakenya, ikiwa ni pamoja na Nandi, Kipsigis na Pokot pia wanadai kuombwa msamaha na fidia ya kifedha kutoka kwa serikali ya Uingereza kwa dhuluma za kihistoria zilizofanywa dhidi yao wakati wa utawala wa kikoloni.

    Baadhi ya jumuiya hizo pia zinaitaka Uingereza kurudisha mali zao za kitamaduni na ardhi za mababu zao, ambazo zilinyakuliwa na utawala wa kikoloni na bado zinashikiliwa na vyombo vya Uingereza.

  8. Kusafiri ni sehemu ya kazi yangu - rais wa Kenya

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Kenya William Ruto ametetea ziara zake nyingi nje ya nchi akisema zimenufaisha taifa hilo kiuchumi.

    Bw Ruto amelaumiwa kwa kufanya idadi kubwa zaidi ya safari za nje kwa mwaka mmoja ikilinganishwa na watangulizi wake.Vyombo vya habari vya ndani vinasema amekuwa katika nchi 38 tangu aingie madarakani Septemba 2022.

    Lakini katika hotuba yake Jumapili, Bw Ruto alisema kupitia safari hizo, ameweza kupata ajira kwa Wakenya na kupata mikataba kadhaa ya nchi mbili iliyolenga kufungua soko la mazao ya Kenya

    "Kuna watu wanaohoji kwa nini ninafanya safari za nje.Hayo ni majukumu yangu kama rais.Mimi ndiye ajenti mkuu wa Kenya na balozi ambaye nitapanga jinsi nchi itasonga mbele,” Bw Ruto alisema akiwhudhuria misa moja kanisani.

    Rais alisema alipata kazi 350,000 na fursa za uwekezaji kwa Wakenya wakati wa ziara za hivi majuzi nchini Saudi Arabia na Uchina.

  9. Mamia ya wagonjwa wamekwama katika hospitali za Gaza, UN yasema

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mamia ya wagonjwa wamekwama katika hospitali kaskazini mwa Gaza na hawawezi kuhamia kusini, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina katika eneo hilo amesema.

    Tom White kutoka UNRWA aliunga mkono kile madaktari na mashirika mengine ya misaada yamesema - kwamba haiwezekani kuhamisha wagonjwa kutoka hospitali kama Al-Quds kaskazini mwa Gaza.Shirika la Red Cresent la Palestina linasema Israel iliwaambia wahame hospitali siku ya Jumapili huku mashambulizi yakiendelea karibu na jengo la hospitali.

    "Watu wengi wa kaskazini wanatafuta makazi katika shule za UNRWA, wanatafuta hifadhi katika hospitali," alisema White."Nilikuwa katika moja ya hospitali wiki hii na kuna mamia na mamia ya wagonjwa ambao hawawezi kuhamishwa."

    Alisema watu wengi wa kaskazini - sio wagonjwa pekee - pia "hawawezi kusonga kwa sababu hawana usafiri, hawana njia".

    Watu "wana njaa sana, wana kiu sana na wanaogopa sana", na wengi wanaishi kwa kutumia vipande vya mkate na "tunapoweza [tuna] kupata chakula cha makopo".

    • Jeshi la Sudan lawazuia watoto 'waliolazimishwa' na RSF kupigana

      xx

      Chanzo cha picha, X/Reuters

      Jeshi la Sudan linasema kuwa limewazuilia watoto ambao "walilazimishwa" kupigana pamoja na Kikosi cha Waasi (RSF) katika mzozo unaoendelea.

      Televisheni ya Sudan inayomilikiwa na serikali inasema idadi isiyojulikana ya watoto wanashikiliwa Wadi Saidna, kaskazini mwa Khartoum.

      Tarehe 15 Septemba, SAF ilikabidhi watoto 30 waliokuwa wameshikiliwa kama wafungwa wa vita kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).

      RSF imekuwa ikishutumiwa mara kwa mara kwa kukiuka sheria za kimataifa kwa kuwaajiri watoto wadogo katika mzozo unaoendelea nchini Sudan.

      Wakati huo huo, RSF ilisema Jumamosi kwamba wanajeshi 260 wa jeshi la Sudan walijiunga nao mjini Khartoum.

      Mapigano yanaendelea kati ya jeshi na RSF katika mikoa ya Khartoum, Darfur na Kordofan huku kukiwa na ripoti kwamba mazungumzo mapya nchini Saudi Arabia yanalenga kufikia usitishaji mapigano na usaidizi wa kibinadamu.

      Maelezo zaidi:

    • Umoja wa Mataifa unasema watoto wanakunywa maji ya chumvi huko Gaza

      TH

      Chanzo cha picha, EPA

      Watoto wanakabiliwa na hali ya "janga" huko Gaza, huku wazazi wakibaki bila chaguo jingine ila kuwapa maji ya chumvi, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa watoto Unicef.

      Toby Fricker, msemaji wa shirika hilo , aliambia BBC kwamba uhaba uliokuwepo Gaza hata kabla ya mzozo wa sasa "umezidishwa kwa kiwango kingine".

      "Mmoja wa wafanyikazi wetu, ana mtoto wa miaka minne, wa miaka saba, na anajaribu tu kuwaweka wasichana salama, kuwaweka hai kila siku," alisema.

      "Alizungumza kuhusu jinsi wanavyokunywa maji ya chumvi, na binti yake akisema, 'Mama, kwa nini nisipate maji ya kawaida tuliyokuwa tukiyapata siku za kawaida?'

      Alipoulizwa kuhusu vifaa vya msaada ambavyo sasa vimeweza kuingia Gaza, Fricker alisema: "Kumekuwa na vifaa, lakini ni kidogo sana.

      "Unapoona mahitaji makubwa katika ardhi tuliyo nayo, kunahitajika kuwa mengi, mengi, mengi zaidi."

      Fricker alitoa wito wa "kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu" na kuongezwa kwa misaada katika Gaza .

      "Tunachokiona sasa kila siku ni kwamba watoto wanauawa, watoto wanajeruhiwa, wanalemazwa," alisema.

      "Na hilo ndilo jambo la kwanza - kulinda maisha ya watoto na kuwaweka hai watoto."

      Daktari wa Al Shifa asema zaidi ya watu 55,000 waliokimbia makazi yao wamepiga kambi hospitalini

      th

      Chanzo cha picha, Reuters

      Tumekuwa tukikuletea ripoti za mashambulizi makali ya risasi katika hospitali ya Al-Quds katika Jiji la Gaza.Jeshi la Israeli lilitoa agizo la kuondolewa kwa watu siku ya Jumapili lakini wafanyikazi wa matibabu wanasema kuhamisha mamia ya wagonjwa wanaotibiwa huko haiwezekani.

      Pia kuna wasiwasi kwa wagonjwa na wafanyakazi katika hospitali nyingine katika mji wa Gaza - Al Shifa -ambapo hali imeelezwa kuwa "janga" na mkuu wake wa upasuaji.

      Baadhi ya wakimbizi wa ndani 55,000 (IDPs) sasa "wanaishi katika kila mita ya mraba" ya hospitali ya Al Shifa, Dk Marwan Abusada alisema katika ujumbe wa sauti kwa BBC, uliorekodiwa Jumapili alasiri.

      Abusada alisema hospitali hiyo "imezidiwa" na wagonjwa "wanavamia" korido zake huku wengine wakifika.Takriban wagonjwa 100 walihamishiwa katika hospitali nyingine mwishoni mwa juma, alisema."Lakini bado tunapokea kesi nyingi, nyingi, nyingi. Kila nusu saa, tunapokea idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa."

      Uhaba wa kila kitu kuanzia dawa za ganzi hadi dawa za kutuliza maumivu na antibiotiki unafanya hali kuwa "ngumu sana", aliongeza."Hatuwezi kufanya zaidi."

      Jeshi la Israel limesema kituo kikuu cha harakati za Hamas kiko chini ya Al Shifa.Hamas inakataa madai hayo na baadhi ya madaktari wanaofanya kazi hapo wametaka hospitali hiyo ilindwe.

      Siku ya Jumapili, shirika la habari la Associated Press liliripoti kuwa ndege za kivita za Israel zilifanya mashambulizi usiku kucha karibu na hospitali hiyo, likiwanukuu wakazi wa mji wa Gaza.Siku ya Jumamosi,watu katika eneo hilo walimweleza mwandishi wa BBC Rushdi Abualouf huko Gaza kwamba barabara za karibu zilishambuliwa.

      Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

    • Daktari bandia wa TikTok akamatwa katika hospitali ya Afrika Kusini

      Matthew Lani anashutumiwa kwa kuiba kitambulisho cha mhudumu wa matibabu

      Chanzo cha picha, Matthew Lani/TikTok

      Mshawishi maarufu wa TikTok nchini Afrika Kusini ambaye alidai kuwa daktari amekamatwa, karibu wiki tatu baada ya mamlaka kumtuhumu kwa ulaghai.

      Matthew Lani alikamatwa na usalama wa Hospitali ya Helen Joseph ya Johannesburg alipokuwa akijaribu kuingia katika kituo hicho Jumapili usiku.

      Idara ya Afya ya Gauteng ilisema kuwa timu ya usalama ya hospitali ilimsalimisha kwa polisi.

      "Lani alinaswa kabla ya saa nane usiku akiwa amejifunika kofia na kuvaa barakoa ya upasuaji na stethoscope shingoni," idara hiyo ilisema katika taarifa.

      Iliongeza kuwa Lani "hapo awali alikuwa ameingia katika kituo hicho ili kudhibiti maudhui ya kupotosha kwa kisingizio kwamba alikuwa daktari aliyehitimu".

      Lani alikuwa amejikusanyia mashabiki wengi kwenye TikTok, ambapo alichapisha maudhui ya matibabu na kuuza aina yake ya vidonge.

      Alidai kuwa alihitimu udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Witwatersrand, jambo ambalo chuo hicho kilikanusha.

      Pia alidai kuwa jina lake halisi ni Dkt Sanele Zingelwa, lakini alifichuliwa kuwa alijifanya kuwa daktari katika kituo kingine.

      Baraza la Taaluma za Afya la Afrika Kusini lilisema kuwa Lani hakuwa daktari aliyesajiliwa.

    • Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili mzozo wa kibinadamu huko Gaza

      Wapalestina walikimbia makazi yao kwa kuhofia mashambulizi ya Israeli, wanajificha kwenye hema katika kituo kinachosimamiwa na Umoja wa Mataifa huko Khan Younis, Gaza.

      Chanzo cha picha, Reuters

      Maelezo ya picha, Wapalestina walikimbia makazi yao kwa kuhofia mashambulizi ya Israeli, wanajificha kwenye kambi ya mahema na kituo kinachosimamiwa na Umoja wa Mataifa huko Khan Younis, Gaza.

      Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya mkutano wa dharura baadaye leo kuhusu mzozo wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, baada ya Israel kupanua operesheni yake ya ardhini katika eneo la Palestina mwishoni mwa juma.

      Wakati wa mkutano huo ulioombwa na Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Usalama litaongozwa na UNRWA, shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa Wapalestina.

      Siku ya Jumamosi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alielezea masikitiko yake kwamba Israel imeimarisha operesheni za kijeshi badala ya kuruhusu usitishaji wa kibinadamu unaohitajika sana kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.

      Baraza la Usalama hadi sasa limeshindwa katika majaribio manne ya kupata azimio la kusitisha mapigano, kwa sababu ya Urusi au Marekani kutumia kura yao ya turufu.

      Umoja wa Mataifa unasema kwamba, kulingana na ushahidi wa kihistoria, kaskazini mwa Gaza, mashambulizi ya anga yanaonekana kuharibu maeneo ya makazi.

      Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

    • Malalamishi yaibuka kuhusu oparesheni ya kikatili ya kijeshi nchini Ghana

      th

      Chanzo cha picha, AFP

      Wabunge nchini Ghana wanadai uchunguzi ufanyike juu ya madai ya ukatili wa kijeshi dhidi ya vijana wa Garu kaskazini-mashariki mwa Ghana na wahusika kufikishwa mahakamani.

      Wanajeshi wanadaiwa kuvamia jamii siku ya Jumapili katika kile kinachoonekana kuwa ni shambulio la kulipiza kisasi kufuatia shambulio dhidi ya maafisa wa ujasusi wa usalama wa taifa waliotumwa huko kupambana na ugaidi.

      Wabunge wa maeneo bunge ya Garu na Tempane, ambao wanashinikiza uchunguzi huo ufanyike, wamelaani mashambulizi hayo na wanatoa wito wa kuondolewa mara moja kwa wanajeshi katika eneo hilo.

      Wabunge hao pia wanataka vijana waliokamatwa waachiwe huru na waliojeruhiwa katika mchakato huo walipwe fidia na serikali.

      Picha zilizosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha baadhi ya vijana wakiwa na majeraha mbalimbali, yakiwemo majeraha kwenye miili yao na nyuso zilizovimba.Wale waliojeruhiwa kwa sasa wanapokea matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Garu, ambayo ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa imejaa watu waliojeruhiwa.

      Baadhi ya vijana hao pia wanasemekana kutoroka eneo hilo kwa kuhofia kukamatwa na kunyanyaswa na wanajeshi.

      Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamelaani operesheni hiyo ya kikatili ya usalama.

      Hata hivyo, Wizara ya Usalama wa Taifa ya Ghana imekanusha madai hayo, ikisema operesheni ya usalama ilianzishwa ili kunasa silaha zilizotumiwa na kundi la magenge kuwashambulia maafisa wake wiki iliyopita.

    • Hezbollah yasema iliidungua ndege isiyo na rubani ya Israel

      th

      Chanzo cha picha, Getty Images

      Kundi la Hezbollah lenye makao yake makuu kusini mwa Lebanon, limetangaza kuwa liliidungua ndege isiyo na rubani ya Israel - mara ya kwanza kutoa madai hayo wakati wa mapigano ya hivi majuzi.

      Ilitokea siku ya Jumapili juu ya Khiam, kama kilomita 5 (maili 3) kutoka mpaka na Israeli.Ndege hiyo isiyo na rubani ilionekana ikianguka katika eneo la Israel, Hezbollah ilisema.

      Kwa mujibu wa shirika hilo, ambalo limetajwa kama kundi la kigaidi na Uingereza na Marekani, wapiganaji wake 46 wameuawa katika mapigano na Israel tangu shambulio la Oktoba 7 la Hamas, pamoja na 43 kujeruhiwa.

      Hezbollah pia inasema imeanzisha mashambulizi 84 katika maeneo 42 mpakani katika mapigano ya kila siku na wanajeshi wa Israel.

      Israel inasema kuwa takriban wanajeshi wake saba wameuawa kufikia sasa.

      Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

    • Andhra Pradesh: Ajali mbaya ya treni yaua watu 13 nchini India

      TH

      Chanzo cha picha, ANI

      Takriban watu 13 wamefariki na wengine 50 kujeruhiwa baada ya treni mbili za abiria kugongana katika jimbo la Andhra Pradesh kusini mwa India siku ya Jumapili.

      Shughuli ya uokoaji ilizinduliwa na mamia ya wafanyikazi wa dharura walikuwa kwenye eneo la ajali kuondoa mabaki.

      Maafisa walisema uchunguzi wa awali umegundua kuwa "kosa la kibinadamu" lilisababisha ajali hiyo.

      Waziri Mkuu Narendra Modi alitoa rambirambi zake na kusema alikuwa akiwasiliana na waziri wa reli.

      Ajali hiyo ilitokea katika wilaya ya Vizianagaram Jumapili jioni.

      Maafisa walisema mabehewa matatu ya treni ya abiria, inayosafiri kati ya Visakhapatnam na Palasa, yaliacha njia mwendo wa 19:00 (13:30 GMT), baada ya kugongwa na treni nyingine.

      Treni hiyo ilikuwa imesimama kwenye reli "kutokana na kukatika kwa kebo ya juu", wakati treni ya pili ya abiria iliyokuwa ikiingia iliyokuwa ikisafiri kati ya Visakhapatnam na Rayagada ilipoigonga kwa nyuma, afisa wa reli aliliambia shirika la habari la Reuters.

      Mamia ya magari ya kubebea wagonjwa, madaktari, wauguzi na waokoaji walitumwa kwenye eneo la tukio kuokoa abiria na kutoa miili.

    • Video:Waandamanaji wanaopinga Israel wavamia uwanja wa ndege nchini Urusi na kuulazimisha kufungwa

      Maelezo ya video, Waandamanaji wanaopinga Israel wavamia uwanja wa ndege nchini Urusi na kuulazimisha kufungwa

      Picha za video zinaonyesha kundi la watu wanaoipinga Israel wakivamia uwanja wa ndege nchini Urusi, wakiripotiwa kujaribu kuwatafuta watu waliokuwa wakiwasili kutoka Tel Aviv.

      Uwanja wa ndege katika mji wa Russia wa Makhachkala huko Dagestan ulifungwa baada ya waandamanaji kumiminika kwenye njia ya kurukia ndege, mamlaka ya usafiri wa anga ya Urusi Rosaviatsia ilisema.

      Baadhi ya waandamanaji walipiga kelele za chuki dhidi ya Wayahudi na kupeperusha bendera za Palestina.

      Rosaviatsia alisema hali sasa imedhibitiwa, baada ya mamlaka kufika eneo la tukio.

      Israel ilisema Urusi lazima ichukue hatua madhubuti dhidi ya uchochezi wa ghasia dhidi ya Wayahudi na Waisraeli.

      Kulingana na mashirika kadhaa ya habari ya Urusi, watu 60 wamekamatwa baada ya ghasia kwenye Uwanja wa Ndege wa Makhachkala.

      Maafisa tisa wa polisi walijeruhiwa katika ghasia hizo, huku jumla ya waandamanaji 150 wakitambuliwa.

      Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

    • Magic Johnson atangazwa kuwa bilionea na Forbes

      th

      Chanzo cha picha, Reuters

      Nyota wa zamani wa mpira wa vikapu, Magic Johnson ametangazwa na Forbes kuwa bilionea na hivyo kumfanya kuwa mwanamichezo wa nne pekee kujiunga na klabu hiyo ya kipekee.

      Jarida hilo la biashara linakadiria utajiri wa Johnson kuwa takriban $1.2bn (£990m).

      Wanamichezo wengine mabilionea ni wachezaji wa NBA Michael Jordan na Lebron James, na mchezaji wa gofu Tiger Woods.

      Johnson ana uwekezaji katika makampuni mengi ikiwa ni pamoja na hisa za umiliki katika timu mbalimbali za michezo.

      Lakini Forbes inasema hisa zake katika kampuni ya bima ya maisha inashikilia sehemu kubwa ya utajiri wake.

      Mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 64 alikuwa na moja ya kazi nzuri zaidi katika historia ya NBA kabla ya kustaafu mnamo 1996, lakini ilikuwa nje ya mchezo ambapo aliingiza pesa nyingi.

      Forbes inasema kuwa Johnson alitengeneza $40m kutokana na kazi yake ya NBA.

      Johnson ana hisa za umiliki katika timu tatu za michezo za Los Angeles, pamoja na MLB's Los Angeles Dodgers.

      Nje ya michezo ana uwekezaji katika Starbucks, Burger King, 24 Hour Fitness na kampuni ya bima ya maisha EquiTrust.

      Johnson anasema angeweza kuwa bilionea mapema kama hangekataa hisa za Nike alipokuwa akiingia NBA miaka ya 1970.Alichukua mkataba na Converse, ambao ulimpa $100,000 kwa mwaka, badala yake.

    • Je, nchi ulimwenguni zina msimamo upi kuhusu mzozo wa Israel na Gaza?

      th

      Chanzo cha picha, UN

      Maelezo ya picha, Orodha kamili ya nchi na jinsi walivyopigia kura azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Gaza siku ya Ijumaa

      Njia nzuri ya kuona nchi zina msimamo upi ni kupitia kura zao katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Ijumaa kuhusu azimio linalotaka 'suluhu ya kibinadamu .' huko Gaza: Nchi 120 zilipiga kura ya ndio, 45 hazikupiga kura na 14 zilipinga.

      Mataifa mengi ya Magharibi yanaiunga mkono Israel hadharani.Marekani ilipiga kura kupinga azimio hilo la Ijumaa, huku Canada na Uingereza zikikosa kura.EU (ambayo haiwezi kupiga kura kama muungano) ilionyesha kuunga mkono Israel, lakini wanachama wake wamegawanyika.Ujerumani na Italia, ambazo zinaunga mkono haki ya Israel ya kujilinda, zilijizuia.Wengine kama Uhispania wamewahimiza viongozi wa Uropa "wasitufanye kushiriki katika mauaji ya kimbari.

      Urusi, ambayo ilikuwa mwenyeji wa Hamas hivi karibuni lakini pia inasaka uhusiano mzuri na Israeli, ilipiga kura kwa ajili ya suluhu.

      Mataifa mengi ya Mashariki ya Kati yalipiga kura ya kuunga mkono, na mengi yamelaani vikali operesheni ya kijeshi ya Israel.Iraq na Tunisia ndizo zilizojiepusha na kura hiyo

      Nchi nyingi za Amerika Kusinipia zilipiga kura kuunga mkono azimio hilo.Colombia imetishia kuvunja uhusiano na Israel, huku Brazili imetoa kauli kali dhidi ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza.Paraguay ndiyo nchi pekee ya Amerika Kusini iliyopiga kura kupinga azimio hilo la Ijumaa.

      Karibu Asia yote- ikiwa ni pamoja na China, ambayo inajaribu kujiweka kama mpatanishi wa amani katika Mashariki ya Kati - ilipiga kura kwa ajili ya kusitisha mapigano.India ilijizuia, huku kukiwa na uvumi kwamba serikali ya nchi ilikuwa ikiimarisha uhusiano na Israel.

      Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

    • 'Kuzuia utoaji wa misaada kunaweza kuwa uhalifu' - ICC

      th

      Chanzo cha picha, EPA

      Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu amekuwa akizungumza kuhusu hali ya Gaza.

      Amerejea kutoka ziara yake ya kivuko cha Rafah na Gaza na Misri.

      Karim Khan alisema kuwa kuzuia usambazaji wa misaada kwa Gaza kunaweza kujumuisha uhalifu wa kivita na kwamba lazima kuwe na juhudi za Israeli kuhakikisha vifaa muhimu vinaruhusiwa kuingia.

      "Raia lazima wapokee chakula na maji," alisema. "Niliona malori yaliyojaa bidhaa, yakiwa yamejaa misaada ya kibinadamu, yakiwa yamekwama Misri ambako hakuna anayehitaji. Imekwama nchini Misri, mbali na midomo yenye njaa na majeraha yanayotoka damu. Vifaa hivi lazima vifike kwa raia huko Gaza bila kuchelewa."

      Alisema kuwa Israel ilikuwa na “majukumu ya wazi katika vita vyake na Hamas. Sio tu majukumu ya kimaadili lakini majukumu ya kisheria ya kuzingatia sheria za migogoro ya silaha."

      Khan aliongeza kuwa "kanuni hii inatumika kwa Hamas, katika kurusha makombora ya kiholela nchini Israel".

      Alisema pia ana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa idadi ya matukio yaliyoripotiwa ya mashambulizi ya walowezi dhidi ya raia wa Palestina kwenye Ukingo wa Magharibi.

      Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza