Israel yasema kambi ya wakimbizi ya Jabalia imezingirwa huku Umoja wa Mataifa ukionya 'hakuna maeneo salama'

Israel inasema Jabalia - ambayo ilikuwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi huko Gaza - ilikuwa ikitumika kama kituo cha Hamas.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena hapo kesho majaaliwa.

  2. Kilichosababisha mafuriko na maporomoko ya matope Tanzania

    h

    Mamlaka nchini Tanzania zinasema mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Manyara Kaskazini mwa nchi hiyo zilisababisha maporomoko ya matope na kusababisha vifo vya watu 65 na kuwaacha wengine 117 wakijeruhiwa.

    Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi amethibitisha kuwa mmomonyoko wa udongo katika Mlima Hanang ndio chanzo kikuu cha maporomoko ya matope.

    Bw Matinyi amesema miamba iliyolegea juu ya mlima huo ilisomba maji ya mvua na kusababisha shinikizo ambalo lilisababisha kuporomoka.

    "Mlima Hanang unajumuisha mchanga wa volkano... eneo hilo lilishindwa kuhimili shinikizo hilo na hivyo sehemu ikaanguka, na matope yakaanza kutiririka chini ya mto Jorodom ukisomba miti, na kuathiri makazi kando ya kingo za mto," asema Bw Matinyi.

    Aliongeza kuwa uchunguzi uliofanywa tangu Septemba umeondoa uhusiano wowote na shughuli za volkano ndani ya eneo la mlima.

    Wengi wa majeruhi na waliokufa ni wanawake na watoto wakati maporomoko ya matope yalipoharibu makazi kando ya mto Jorodom.

    Kati ya vifo 65, 26 ni wanawake, 24 walikuwa watoto na 15 walikuwa wanaume. Wengine 117 wamejeruhiwa na wanaendelea kupata huduma za matibabu katika vituo vitatu katika wilaya ya Hanang.

    Shughuli za uokoaji zinaendelea katika maeneo ya mbali huku kukiwa na wasiwasi kwamba idadi ya watu waliofariki huenda ikaongezeka.

    Shirika la hali ya hewa nchini humo limetoa tahadhari ya mvua kubwa kwa mwezi wa Disemba. Mlima Hanang unasimama kama moja ya volkano kadhaa za Tanzania ndani ya eneo la Bonde la Ufa.

  3. Aliyekuwa Rais wa Mauritania Aziz afungwa miaka mitano jela kwa ufisadi

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Mohamed Ould Abdel Aziz, aliyeonekana hapa mwaka 2018, anadaiwa kujilimbikizia mali nyingi wakati wa utawala wake wa miaka 10.

    Mahakama nchini Mauritania imemfunga rais wa zamani Mohamed Ould Abdel Aziz kifungo cha miaka mitano kwa kosa la rushwa.

    Ilimpata Aziz na hatia ya utakatishaji fedha na kutumia nafasi yake vibaya ili kujitajirisha kinyume cha sheria, lakini ilimwachilia huru kwa mashtaka mengine.

    Mahakama pia iliamuru kutaifishwa kwa mali yake aliyoipata kinyume cha sheria.

    Aziz, mwenye umri wa miaka 66, alichaguliwa kuwa rais mwaka wa 2009 baada ya kumg’oa madarakani Rais Sidi Ould Cheikh Abdallahi katika mapinduzi, na akaendelea kuiongoza Mauritania hadi 2019.

    Alikuwa ameshtakiwa katika mji mkuu, Nouakchott, tangu Januari, pamoja na watu wengine 10 mashuhuri, wakiwemo mawaziri wakuu wawili wa zamani na mawaziri wa zamani waliohudumu katika utawala wake.

    Walikuwa wameshtakiwa kwa makosa kadhaa, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka, utakatishaji fedha, kujitajirisha haramu na kufanya biashara ya ushawishi.

    Mahakama hiyo ambayo ni mtaalamu wa masuala ya rushwa na uhalifu wa kiuchumi, pia iliwahukumu baadhi ya washtakiwa wenza siku ya Jumatatu, japo kwa adhabu nyepesi kuliko Aziz, huku mawaziri wakuu wa zamani na mawaziri wawili wa zamani wakiachiliwa huru.

    Aziz alidumisha kutokuwa na hatia katika kipindi chote cha kesi hiyo na alielezea mashtaka yake kama yalichochewa kisiasa.

    Inasemekana kuwa alitofautiana na mrithi wake na Rais wa sasa Mohamed Ould Ghazouani, ambaye wakati mmoja alikuwa mshirika wake wa karibu wa kisiasa, shirika la habari la AFP linaripoti.

  4. Mpango wa uhamiaji wa Uingereza Rwanda: Hakuna pesa zaidi zilizotolewa kwa Rwanda kwa ajili ya mkataba - Cleverly

    h

    James Cleverly anasema haoni sababu ya kuaminika kwa nini Uingereza isingeweza kupeleka watu Rwanda chini ya mkataba huo.

    "Natumai sasa tunaweza kusonga mbele haraka," anasema. "Tumeshughulikia masuala ambayo yaliibuliwa na majaji (katika Mahakama ya Juu) katika mkataba huu na ambayo yataonyeshwa katika sheria za ndani hivi karibuni," Cleverly alisema na kuongeza kuwa Uingereza imejitolea kabisa kuvunja mtindo wa biashara wa watu wanaosafirishwa kimagendo.

    g
    Maelezo ya picha, Mkataba umesainiwa baina ya Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza James Cleverly na Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Birura mjini Kigali

    Alipoulizwa ni kiasi gani cha fedha za ziada Uingereza imekubali kuilipa Rwanda kama sehemu ya mkataba huu, anasema hakuna ufadhili unaohusishwa na kusainiwa kwa waraka huo.

    “Ufadhili wa mkataba wa kimataifa unaakisi gharama zinazoweza kuwekewa Rwanda kupitia mabadiliko ambayo ushirikiano huu umeanzisha katika mifumo yao, katika mifumo na taasisi zao za kisheria,” anasema.

    Wanyarwanda hawakuomba pesa kwa ajili ya mkataba huu, wala hawakupewa, Cleverly anaongeza.

    Alipoulizwa kama Rwanda itaendelea kujitolea hata kama inakabiliwa na vikwazo zaidi waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta amesema Rwanda imejitolea sana kwa ushirikiano huo, na haina mpango wa kujiondoa.

    Unaweza pia kusoma:

    • Uhamiaji: Kwanini Uingereza inawapeleka waomba hifadhi Rwanda?
    • 'Mpango wa Uingereza wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda 'ni kinyume cha Mungu' - Welby
  5. Habari za hivi punde, Uingereza: Mkataba wa uhamiaji wa Rwanda unahakikisha wanaotafuta hifadhi hawatarejeshwa katika nchi zao

    Tumepokea taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa serikali ya Uingereza, ikieleza baadhi ya maelezo ya mkataba mpya uliotiwa saini na Rwanda:

    ·Mkataba huo "unahakikisha kwamba watu waliohamishwa hadi Rwanda... hawako katika hatari ya kurejeshwa katika nchi ambayo maisha au uhuru wao utatishiwa - kitendo kinachojulikana kama efoulement (au kurejeshwa kwa nguvu aulikotoka)"

    ·Pia unahimarisha kazi za kamati huru ya ufuatiliaji "kuhakikisha utiifu wa majukumu katika mkataba kama vile masharti ya mapokezi, usindikaji wa madai ya hifadhi, na matibabu na usaidizi kwa watu binafsi ikiwa ni pamoja na hadi miaka mitano baada ya kupokea uamuzi wa mwisho"

    ·Pia, ili "kuimarisha zaidi uhakikisho kwamba watu waliohamishwa hawatarejeshwa walikotoka, chini ya mkataba huo, mfumo wa hifadhi wa Rwanda utaimarishwa kupitia chombo kipya cha rufaa"

    Unaweza pia kusoma:

    • Uhamiaji: Kwanini Uingereza inawapeleka waomba hifadhi Rwanda?
    • 'Mpango wa Uingereza wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda 'ni kinyume cha Mungu' - Welby
  6. Mpango wa Uingereza wa wahamiaji Rwanda: Sheria mpya itawasilishwa bungeni karibuni

    Reuter

    Chanzo cha picha, Reuter

    Maelezo ya picha, Katibu wa Mambo ya Ndani wa Uingereza akiwasili mjini Kigali Jumatatu

    Serikali ya Uingereza imesema itazindua hivi karibuni sheria "thabiti " ya dharura iliyoundwa ili kuondokana na pingamizi la Mahakama ya Juu dhidi ya sera ya wahamiaji ya Rwanda, waziri wa uhamiaji amesema.

    Robert Jenrick amesema sheria mpya itawasilishwa Bungeni "muda si mrefu" baada ya James Cleverly, Waziri wa mambo ya ndani, kutia saini mkataba na Rwanda leo.

    Robert Jenrick
    Maelezo ya picha, Robert Jenrick

    Kauli hiyo ya Bw Jenrick imetolewa huku Waziri wa Mambo ya Ndani James Cleverly, akiwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa sasa kutia saini mkataba huo.

    Jenrick amekiambia kipindi cha BBC Breakfast: "Tunataka kuanzisha mpango wa Rwanda haraka iwezekanavyo.

    "Kwa bahati mbaya umekwamishwa na mahakamani hadi sasa lakini mkataba ambao tunakaribia kutia saini utaunda uhusiano wenye nguvu zaidi na Rwanda ambao unajibu wasiwasi wa Mahakama ya Juu kuhusu mpango huo.

    "Hilo ni pamoja na kipengele cha sheria kali ya dharura ambayo tutaileta mbele ya Bunge hivi karibuni, natumai, itaboresha mpango huo."

    Unaweza pia kusoma:

    • Uhamiaji: Kwanini Uingereza inawapeleka waomba hifadhi Rwanda?
    • 'Mpango wa Uingereza wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda 'ni kinyume cha Mungu' - Welby
  7. Vikwazo vipya vyalenga mali za kiongozi wa Hamas

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ufaransa imetangaza kushikilia mali ya kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar kama sehemu ya wimbi jipya la vikwazo.

    Kulingana na amri iliyochapishwa katika Jarida Rasmi, fedha na rasilimali za kiuchumi za Sinwar zitashikiliwa kwa miezi sita kuanzia tarehe 5 Desemba.

    Haijulikani ni kiasi gani cha mali za Sinwar zilizopo nchini Ufaransa ni za thamani gani.

    Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Bwana Cameron alichukua hatua hiyo dhidi ya viongozi wakuu wa kundi la wanamgambo wa Palestina na wafadhili wa Hamas kufuata mfano sawa na wa Marekani ambayo imewachukulia pia hatua sawa wakuu wa Hamas.

    Unaweza kusoma:

    • Jinsi Hamas walivyounda jeshi la kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba
    • 'Waarabu na Waislamu wote wako wapi? Mumewaacha watu wa Palestina wateseke'
  8. Hatua ya pili ya vita itakuwa 'ngumu' - msemaji wa serikali ya Israeli

    j

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Msemaji wa serikali Eylon Levy wakati wa mkutano na waandishi wa habari

    Huku Israel ikisema imechukua udhibiti wa baadhi ya vituo vya kijeshi vya Hamas kaskazini mwa Gaza, msemaji mkuu wa serikali ametoa mawazo yake kuhusu jinsi vita hivyo vinaendelea.

    Mapema leo asubuhi, Eylon Levy amewaambia waandishi wa habari katika mkutano fupi uliopita kwamba: "Tunasonga mbele na hatua ya pili sasa. Hatua ya pili ambayo itakuwa ngumu kijeshi."

    Israel inatarajia mapigano magumu katika awamu mpya ya vita vyake mjini Gaza lakini iko wazi kwa "maoni ya kujenga" juu ya kupunguza madhara kwa raia mradi tu ushauri huo unaendana na lengo lake la kuiharibu Hamas, Levy aliongeza.

    Unaweza kusoma:

    • Jinsi Hamas walivyounda jeshi la kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba
    • 'Waarabu na Waislamu wote wako wapi? Mumewaacha watu wa Palestina wateseke'
  9. Shambulizi la anga la Nigeria lililotekelezwa 'kimakosa' lawaua waumini katika tamasha la kidini

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Jeshi linapambana na kile linachokiita "magaidi" na "majambazi" kote kaskazini mwa Nigeria

    Takriban raia 85 waliuawa katika jimbo la Kaduna, kaskazini-magharibi mwa Nigeria, katika shambulio la anga wakati wa sherehe za kidini za Waislamu zilizofanyika siku ya Jumapili, afisa wa usimamizi wa dharura wa eneo hilo amesema.

    Raia hao "waliuawa kimakosa" na ndege isiyo na rubani ya kijeshi wakati ilipokuwa "ikiwalenga magaidi na majambazi", kulingana na Gavana wa jimbo Uba Sani, ambaye hakutoa idadi ya waliouawa.

    Wizara ya ulinzi iliitaja operesheni hiyo kama "janga lisilo la lazima".

    Makumi wamejeruhiwa wakati wa shambulio hilo.

    Afisa wa serikali, Samuel Aruwa, alisema afisa wa jeshi "Maj VU Okoro, amesema kuwa jeshi la Nigeria lilikuwa kwenye harakati zake za kijeshi za kawaida dhidi ya magaidi lakini zimewaathiri wanajamii bila kukusudia".

    Katika taarifa yake siku ya Jumanne, Msemaji wa wizara ya ulinzi Meja Jenerali Edward Buba alisema shambulio hilo la anga lilitokana na taarifa za kijasusi kuhusu kuwepo kwa "magaidi" katika eneo hilo.

    Gavana Sani ameagiza uchunguzi ufanywe kuhusu "tukio la kusikitisha" lililotokea wakati wanakijiji kutoka Tundun Biri walipokusanyika kwa tamasha la kidini la Jumapili jioni.

    "Ofisi ya Kanda ya Kaskazini-Magharibi imepokea taarifa kutoka mamlaka za mitaa kwamba miili 85 hadi sasa imezikwa huku msako ukiwa bado unaendelea," taarifa kutoka kwa Wakala wa Kitaifa wa Usimamizi matukio ya dharura katika mji mkuu wa shirikisho, Abuja, ilisema.

    "Inastahili kuzingatiwa kuwa waliojeruhiwa ni watoto, wanawake na wazee."

    Mtu mmoja, ambaye alishuhudia kilichotokea, aliambia BBC, kwamba kulikuwa na mashambulizi mawili.

  10. Nyota wa YouTube afungwa jela kwa kuulaghai umma juu ya ajali ya ndege ili kupata ‘views’

    h

    Chanzo cha picha, TREVOR JACOB

    Maelezo ya picha, Trevor Jacob alionekana akiruka kutoka kwenye ndege kwenye milima ya Los Padres California mnamo 2021.

    Nyota wa YouTube amefungwa jela miezi sita kwa kuangusha ndege yake kimakusudi ili kupata idadi kubwa ya watazamaji , na kisha kuwadanganya wachunguzi wa Marekani.

    Trevor Jacob, 30, alichapisha video ya ajali ya ndege ndege iliyoonekana kuanguka mnamo Desemba 2021, akimaanisha kuwa ilikuwa ajali.

    Alijiondoa kwenye ndege – akiwa anajipiga picha ya selfie kwa kutumia kamera ya selfie ya fimbo - na kuruka kwa parachuti kutoka kwenye ndege hadi akutua.

    Klipu hiyo ilitazamwa mara milioni.

    Katika makubaliano ya kuomba msamaha , Jacob alisema alirekodi video hiyo kama sehemu ya mpango wa udhamini wa bidhaa.

    Mwanariadha huyo wa zamani wa Olimpiki alikiri hatia ya ulaghai huo mapema mwaka huu kwa kosa moja la uharibifu na kuficha kwa nia ya kuzuia uchunguzi wa shirikisho.

    Jacob "uwezekano mkubwa alitenda kosa hili ili kutengeneza mitandao ya kijamii na matangazo ya habari kwa ajili yake mwenyewe na kupata faida ya kifedha," waendesha mashtaka wa serikali ya California walisema Jumatatu.

    "Hata hivyo, aina hii ya tabia haiwezi kuvumiliwa," waliongeza.

    Katika taarifa, Jacob alisema kuwa "uzoefu huu umekuwa wa kufedhehesha" na akaielezea hukumu dhidi yake kama "uamuzi sahihi".

  11. Mtoto mchanga wa Marekani auawa na mbwa mbwa mwitu Alabama

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mbwa mwitu wamepigwa marufuku kama mnyama wa kufuhgwa nyumbani katika baadhi ya majimbo ya Marekani, lakini ni halali katika jimbo la Alabama

    Mtoto mchanga wa miezi mitatu aameuawa na mbwa mwitu ambaye amekuwa akifugwa na familia yake katika jimbo la Alabama nchini Marekani, polisi wamesema.

    Mtoto huyo alifariki siku ya Alhamisi katika eneo la Chelsea, takriban maili 20 (32km) kusini-magharibi mwa Birmingham, Alabama, kutokana na majeraha ambayo yanashukiwa kusababishwa na mnyama huyo.

    Mbwa huyo aliuawa katika eneo la tukio na daktari wa mifugo, ofisi ya Sheriff ya kaunti ya Shelby ilisema.

    Meya wa jiji hilo alikiita kifo hicho kama "cha bahati mbaya na cha kusikitisha".

    "Imethibitishwa kwamba mmoja wa watoto wetu hapa Chelsea aliuawa mbwa mwitu ambaye alikuwa kipenzi cha familia na kufariki kutokana na majeraha jana alasiri baada ya kupelekwa hospitalini," alisema Meya Tony Picklesimer katika taarifa.

    Polisi walisema waliitwa nyumbani kwa mtoto huyo siku ya Alhamisi mchana mwendo wa saa saba za eneo (19:00 GMT) baada ya simu ya dharura, 911 kupigwa kuhusu shambulio la wanyama.

    Kisha mtoto huyo alipelekwa hospitali, ambapo alitangazwa kufariki kutokana na majeraha aliyokuwa nayo katika meneo mbali mbali ya mwili kutokana na shambulio hilo.

    Polisi walisema kuwa wanaendelea kuchunguza mazingira yaliyopelekea kifo cha mtoto huyo.

  12. Huenda makubaliano yalivunjika kwa sababu ya kukataa kuwaachilia mateka wanawake - Marekani

    Maandamano

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelewano ya wiki moja kati ya Israel na Hamas huenda yakasambaratika kwa sababu Hamas ilikataa kuwaachilia mateka wanawake, kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller.

    "Inaonekana moja ya sababu hawataki kuwageuza wanawake kuwa wamekuwa wakiwashikilia mateka na sababu ya makubaliano haya kuvunjika ni kutotaka wanawake hao waweze kuzungumza juu ya kile kilichowapata wakati wao. muda gerezani."

    Miller aliwaambia waandishi wa habari kwamba kundi hilo halikutaka wanawake hao kuzungumza hadharani kuhusu unyanyasaji wa kingono na kwamba serikali ya Marekani "haina sababu ya kutilia shaka" ripoti za ubakaji.

    Matamshi hayo yametolewa baada ya mamia ya watu kuandamana nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu wakikosoa shirika hilo kwa kutochukua hatua kutokana na unyanyasaji, utekaji nyara na ubakaji wa wanawake wa Israel.

    Hii ilitokea wakati mkutano katika Umoja wa Mataifa ukisikiliza ushuhuda kutoka kwa mamlaka ya Israeli na wengine ambao waliweka ushahidi kwamba Hamas ilifanya unyanyasaji wa kijinsia katika shambulio lake la 7 Oktoba.

  13. Tazama Video: Bomu la Vita vya Pili vya Dunia lalipuliwa pwani ya Denmark

    Maelezo ya video, Tazama Video: Bomu la Vita vya Pili vya Dunia lalipuliwa pwani ya Denmark

    Bomu la Vita vya Pili vya Dunia limelipuliwa kwenye maji karibu na eneo la Langeland, kisiwa cha Denmark kilichopo kusini mwa nchi hiyo.

    Mvuvi aliarifu mamlaka mara moja baada ya silaha hiyo ya kilo 130 kunaswa kwenye wavu wake.

    Sappers kutoka jeshi la wanamaji la Denmark walirudisha bomu ndani ya maji na kuambatanisha na kilipuzi cha kilo 10, na kuruhusu mlipuko unaodhibitiwa.

    Mlipuko huo ulitokea mita 15 (futi 49) chini ya sakafu ya bahari kulingana na idara ya ulinzi.

  14. Hamas ilipanga unyanyasaji wa kijinsia kama silaha ya vita - mwanaharakati wa Israeli

    Wanajeshi wa Israel wakikumbatiana wakitazama picha za wahanga wa tamasha hilo kutokana na mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba

    Chanzo cha picha, EPA

    Hamas walikuwa na mpango uliopangwa wa kutumia unyanyasaji wa kingono kama silaha ya vita, mwanaharakati wa haki za wanawake wa Israel na mwanasheria amesema.

    Prof Ruth Halperin-Kaddari alisema aliona picha za wanawake katika maeneo kadhaa ambao hali zao zilionesha "bila shaka" kwamba walibakwa.

    Kumekuwa na hasira juu ya kuchelewa kwa baadhi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa kukiri madai ya unyanyasaji wa kijinsia wa Hamas tarehe 7 Oktoba.

    Israel imekuwa ikichunguza ushahidi wa uhalifu wa kingono wakati wa mashambulizi hayo.

    Polisi wa Israel wanasema hadi sasa wamekusanya ushahidi zaidi ya 1,500 kutoka kwa mashahidi na matabibu.

    Hamas imekanusha kundi hilo kutekeleza unyanyasaji wa kingono wakati wa mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba.

    Picha na video za moja kwa moja zilizotiririshwa na wanamgambo hao ziliashiria hali ya kutisha ya mashambulizi katika tamasha la Supernova. Vurugu mbalimbali kuanzia ubakaji wa magenge hadi ukeketaji wa waathiriwa waliouawa zinachunguzwa na polisi.

    "Niliona mashuhuda kadhaa, kwa mfano wa mtu mmoja aliyenusurika ambaye alijificha vichakani na kumwona mwanamke karibu naye akibakwa na wanaume kadhaa," Prof Halperin-Kaddari aliambia kipindi cha Leo cha BBC Radio 4.

    Alisema pia alizungumza na mhudumu wa afya ambaye alimtibu mwanamke aliyepoteza kiasi cha damu kilichotishia maisha yake baada ya kuripoti kubakwa na wanaume wanne.

    "Niliona picha kutoka sehemu nyingi za miili ambayo hali zote zilikuwa zikionesha mtindo sawa wa ukeketaji na bila kuacha shaka kuwa ubakaji ulifanywa kwa wanawake hao kabla ya kunyongwa," alisema.

    Prof Halperin-Kaddari aliongeza kuwa wingi wa kesi, zote kwa siku moja lakini katika maeneo kadhaa ulimwacha "bila shaka" kwamba kulikuwa na "matayarisho ya kutumia unyanyasaji wa kingono kama silaha ya vita."

  15. Hillary Clinton ataka ‘ukatili wa kingono unaotumika kama silaha’ ‘ulaaniwe kikamilifu’

    Waandamanaji walikusanyika nje ya majengo ya Umoja wa Mataifa mjini New York, wakitaka uangalizi zaidi kulipwa kwa akaunti za unyanyasaji wa kingono wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Balozi wa Israel katika Umoja wa mmataifa, Gilad Erdan amekuwa na hafla iliyolenga “kufichua matendo ya kusikitisha ya ukatili wa kingono uliofanywa na magaidi wa Hamas dhidi ya wanawake wa Israel” mnamo Oktoba 7.

    Hillary Clinton alirekodi picha ya video yenye ujumbe kwa washiriki, akisema “inasikitisha kwamba baadhi ya watu wanaodai kutetea haki wanafumba macho yao na mioyo yao juu ya waathirika wa matendo ya Hamas”.

    Hillary Clinton amesema jumuiya ya kimataifa lazima ishughulikie ukatili wa kingono unaotumika kama silaha, popote unapotokea, kwa “kuulaani kikamilifu" .

    “Ubakaji kama silaha ya kivita ni uhalifu dhidi ya ubinadamu,” aliongeza.

    Yael Richert, ambaye ni mrakibu mkuu wa Polisi nchini Israel, alihudhuria hafla hiyo na kuonesha video yenye kauli za kusikitisha zilizotolewa na wazungumzaji wa mwanzo waliokuwa kwenye tamasha la muziki la Nova liliposhambuliwa.

    Seneta wa New York, Kirsten Gillibrand pia alizungumza wakati wa hafla hiyo dhidi ya alichosema ni jumuiya ya kimataifa “kuchelea” kulaani matendo ya Hamas ya ukatili dhidi ya wanawake hapo Oktoba 7.

  16. Israel yakana madai ya WHO kuhusu jeshi lake kutaka kundolewa vifaa tiba katika bohari

    Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Israel imekanusha madai ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa limeamriwa na jeshi la Israeli kuondoa vifaa tiba katika bohari mbili za vifaa tiba Kusini mwa Gaza, kutokana na kile kilichotajwa kuwa “operesheni za ardhini zitasababisha visifae kwa matumizi''.

    Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkuu wa WHO, alichapisha ujumbe kwenye mtandano wa X kuitaka Israel “kuondoa amri hiyo”.

    Tangu wakati huo, idara ya kuratibu shughuli za serikali ya Israel imesema taarifa hizo si sahihi. Katika ujumbe wake idara hiyo imesema:

    ‘’Ukweli ni kwamba hatukukuelelekeza kuondoa vifaa tiba katika bohari na pia tuliweka bayana (na kwa maandishi ) kwa wawakilishi husika wa Umoja wa Mataifa.’’

    ‘’Kutoka kwa afisa wa Umoja wa Mataifa tulitarajia walau atoe taarifa sahihi."

    Unaweza kusoma;

  17. Ndege ndogo yatua kwa dharura na kugonga jengo katika kitongoji cha Paris

    Ndege hiyo ilianza kutua kwa dharura kwenye barabara kabla ya kugonga ukuta wa jengo la ghorofa

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ndege ndogo ya injini mbili imelazimika kutua kwa dharura katika kitongoji cha kusini mwa Paris.

    Watu watatu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walipelekwa hospitalini kuhitaji uangalizi wa haraka, lakini majeraha yao hayakuchukuliwa kuwa ya kutishia maisha, maafisa walisema.

    Hakuna mtu mwingine aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Ndege hiyo ilitua katika eneo la makazi huko Villejuif baada ya injini kuharibika, kulingana na Waziri wa Uchukuzi wa Ufaransa, Clément Beaune.

    Watu watatu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walikuwa mwalimu wa safari za ndege mwenye umri wa miaka 80 na abiria wawili walio na umri wa miaka 20 hivi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.

    Ndege hiyo ilianza kutua kwa dharura kwenye barabara kabla ya kugonga ukuta wa jengo la ghorofa.

    Hatimaye ilisimama kwenye bustani iliyokuwa nyuma ya jengo la ghorofa, huku sehemu za ndege zikiwa zimetapakaa juu ya paa la karakana iliyokuwa karibu.

    Mkia wa ndege ulitenganishwa na sehemu nyingine ya ndege na mabawa yalivunjika kwa kiasi kikubwa.

  18. Pande zote za mashariki na magharibi za Khan Younis zashambuliwa kwa mabomu

    Moto unawaka kwenye eneo la nyumba iliyoharibiwa na shambulio la anga la Israeli huko Khan Younis - 4 Desemba

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mashuhuda na waandishi wa habari wa ndani katika eneo karibu na mji wa kusini wa Khan Younis wanazungumza kuhusu mizinga inayotoka katika maeneo ya Khuzaa na Abasan, nje kidogo ya mji huo.

    Khan Younis ina sehemu mbili, moja ambayo iko mashariki mwa barabara ya Salah al-Din, na sehemu nyingine magharibi.

    Zote mbili zimeshambuliwa kwa mabomu mengi, lakini sehemu ya mashariki inaundwa na vijiji vinne vikuu.

    Waisraeli wanaomba watu wengi katika vijiji hivi kuondoka.

    Kumekuwa na mashambulizi ya risasi na angani katika maeneo hayo. Kati ya mashambulio ya anga 200 kote Gaza jana usiku, 60% ya hayo yalilenga Khan Younis, kulingana na mamlaka za mitaa zinazoendeshwa na Hamas.

    Ndani na karibu na jiji la kusini, karibu maeneo 15-20 yalilengwa.

    Mji wa kati wa Deir al-Balah pia ulilipuliwa kwa bomu kubwa.

    Timu ya BBC katika hospitali nilikokaa kwa takribani wiki nne, ilisema makumi ya majeruhi walifika usiku kutoka maeneo tofauti.

    Wengi wao walikuwa wameuawa na wengine kujeruhiwa vibaya.

    Wanawake na watoto walikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa.

  19. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja