Netanyahu ana chaguzi mbili: Maslahi yake ya kisiasa au maslahi ya taifa - Magazeti

Chanzo cha picha, Reuters
Gazeti la Yedioth Ahronoth kutoka Israel, kuna makala yenye kichwa “Chaguo la Netanyahu: Maslahi ya kisiasa au ya taifau.” Mwandishi ni Ben Dror-Yemini.
Mwandishi wa makala hiii anasema, Marekani haihitaji taifa la Palestina, lakini inahitaji kibali cha Israel kwa ajili ya kuanzishwa kwa taifa la Palestina.
Kuhusu kambi ya Uzayuni, inayounga mkono nchi moja kutoka Bahari ya Mediterania hadi Mto Yordani, mwandishi anasema haya ni maoni mabaya.
Mwandishi anaamini kuwa Netanyahu kupingana na serikali ya Marekani kuhusu suala la nchi mbili si busara, bali kutasababisha machafuko ya kisiasa.
Kuna wito katika Seneti ya Marekani kuunganisha misaada iliyotolewa kwa Israel na sharti la ulinzi wa haki za binadamu na suluhisho la mataifa mawili.
Kuna ripoti, kwa mujibu wa mwandishi kuwa, "hata marafiki wa Israel walishtushwa na kukataa kwa Netanyahu kuonyesha utayari juu taifa la Wapalestina.
Ben Dror-Yemini anatoa wito kwa Benjamin Netanyahu kuchukua msimamo wa kweli zaidi, sio kuanzisha taifa la Hamas, lakini kuruhusu serikali ya Marekani kuratibu uhusiano wa Israel na Saudi Arabia na Palestine.
Netanyahu kusisitiza juu ya "udhibiti kamili wa usalama katika Ukanda wa Gaza, hili linapingana na matakwa ya uhuru wa Palestina."
Je, Netanyahu atachukua hatua kwa mujibu wa maslahi ya kimkakati ya pamoja ya Israel na Marekani, au atafuata dira ya serikali moja inayoongozwa na Smotrich na Ben Gvir?
Sitarajii Netanyahu kutoa jibu la wazi.
Biden-Netanyahu na suluhisho la serikali mbili

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sasa tunaligeukia gazeti la Palestina la Al-Quds, ambapo Ziad Abu Ziad aliandika makala chini ya mada "Biden-Netanyahu, suluhisho la serikali mbili, na jinai katika Ukanda wa Gaza, haswa dhidi ya wanawake."
Mwandishi huyo anasema kauli ya Rais wa Marekani baada ya mazungumzo yake kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel ambapo alisema Netanyahu anakubaliana na suluhu ya serikali mbili na suluhu hilo linawezekana chini ya serikali yake ya sasa.
Kauli hiyo inauthibitishia ulimwengu kwamba Biden ametengwa na ukweli, au labda ni mjinga na ni rahisi kudanganyawa, au hasemi ukweli.
Mwandishi huyo anasema Netanyahu alizungumza zaidi ya mara moja kuhusu suluhu la mataifa mawili, lakini amekwamisha suluhu ya mataifa mawili na kuimarisha udhibiti wa Israel juu ya maeneo ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Jerusalem."
Mwandishi anaamini washirika wa karibu wa Waziri Mkuu wa Israel wanamtaja kuwa "husema uongo na kutoheshimu ahadi zake." Kwa hiyo, Biden anashirikiana na Netanyahu au anadanganywa naye? "
Lengo la Netanyahu "ni kutoa ushuru wa maneno kununua ukimya wa Biden, ambaye hawezi kufanya lolote dhidi yake, kwa sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa rais; anahitaji michango na kura za Wayahudi wa Marekani."
Mwandishi anasema wakati Biden anamtangaza Netanyahu kama mtu wa amani anayekubali suluhu ya serikali mbili, huku akikataa usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, na kuendelea kwa mauaji ya kila siku dhidi ya raia wasio na silaha, wanawake na watoto na wazee.
Makundi yanayoteseka zaidi ni akina mama hasa wajawazito kukosa chakula na huduma za afya, baadhi yao wanajifungulia majumbani, kwenye mahema au mitaani huku wakiteseka kwa kukosa maji kwa ajili ya usafi wa mwili au kufua nguo na wanakosa faragha zao.
Kwa kukataa usitishaji vita, Rais Biden anahesabiwa kuwa mshirika katika vita hivi pamoja na Israel na anabeba sehemu kubwa ya dhima ya ukiukaji wa haki za binadamu za Wapalestina, hasa wanawake katika Ukanda wa Gaza.
Kisha mwandishi anarejelea ukiukwaji mwingine wa haki za binaadamu na mazoea mabaya yanayofanywa na wanajeshi wa Israel, kama vile kupora na kuiba pesa na vitu vya thamani kutoka kwenye nyumba ambazo wakazi wake walilazimika kukimbia kutokana na mlipuko.
Mwandishi anamalizia makala yake kwa kusema: Yanayotokea katika Ukanda wa Gaza ni fedheha kwa Israel na wale wanaohalalisha au kunyamaza, na wakati umefika kila mtu kuvunja ukimya na kusimama ili kukomesha uhalifu huu.
Chaguo gumu la kimkakati

Chanzo cha picha, Reuters
Hatimaye, tunahamia gazeti la Marekani, The Washington Post, ambako tunasoma tahariri chini ya kichwa: “Huku mateka wakiteseka, Israel lazima ifanye maamuzi magumu ya kimkakati.”
Tahariri hiyo inaangazia mpasuko katika utawala wa Biden na Israel. Ingawa Washington iliweza kuishawishi Israel kuruhusu kuingia kwa misaada ya kibinadamu na kupunguza makali ya operesheni zake huko Gaza.
Bado kuna kutokubaliana kuhusu suala la msingi, ambalo linaamua mwisho wa vita hivyo. Rais Biden anahimiza kuanzishwa kwa taifa la Palestine. Lakini Waziri, Mkuu Benjamin Netanyahu amekataa kabisa hilo.
Tahariri inasema msimamo wa Biden juu ya suala hili ni sahihi, na msimamo wa Netanyahu, sio sawa. Inasema Waisraeli wamepoteza imani katika mchakato wa amani, kama mkuu wa nchi, Isaac Herzog, alivyosema kabla ya Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos wiki iliyopita.
Asilimia 65 wanapinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina, kulingana na kura ya maoni ya Gallup iliyofanywa huko Desemba.
Gazeti hilo linasema kuna “uhitaji wa uongozi mpya Israel, kwa sababu mizozo inayoibuka ndani ya baraza la mawaziri la vita la Israel, inaweza kuwa na athari.
Gazeti hilo lilimnukuu mjumbe wa Baraza la Mawaziri Gadi Eisenkot akisema, “Israel hadi sasa imeshindwa kufikia lengo lake kuu la vita, kuipindua Hamas - na lengo lake kuu lingine, ambalo ni kuachiliwa kwa mateka.”
Eisenkot anaamini kuna haja ya kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano kwa muda mrefu na wale wanaodai vinginevyo ni wale wanaojaribu kuuza udanganyifu kwa umma.
Tahariri inasema kwamba maneno ya Eisenkot yana maana kubwa kwa sababu ya jukumu lake la awali, kama mkuu wa jeshi la Israel, na kwa sababu mtoto wake na mpwa wake wameuwawa huko Gaza.
Gazeti hilo linasema kuwa idadi ya mateka ambao bado wako kizuizini 132, na idadi hii inajumuisha mabaki ya 27 wanaoaminika kufariki huko. Umri wa mateka huanzia miaka ya 80 hadi mwaka mmoja.
Wengi ni wagonjwa na kuna uwezekano wanashikiliwa katika maeneo ndani ya Gaza na katika mahandaki ya chini ya ardhi ya Hamas.
Tahariri inabainisha kukiri kwa Eisenkot kwamba "licha ya jitihada zisizo na kuchoka za IDF, lakini wazo la kuendelea na vita ili kuokoa mateka ni kujidanganya."
Watu hawa hawawezi kusahaulika, kama vile mateso ya raia wa Palestina hayawezi kusahaulika. Hii ina maana “kama jeshi la Israel haliwezi kuiangamiza Hamas hivi karibuni, njia pekee ya kuwatoa mateka hao ni kufikia makubaliano nao. Hata hivyo, Netanyahu haoni hivyo.
Gazeti hilo linahitimisha uhariri wake kwa kusema: Kadiri muda unavyosonga mbele kwa mateka, na maandamano ya Israel dhidi ya mtazamo wa Netanyahu kuhusiana na suala hili yakiongezeka, nchi hiyo inahitaji maafikiano mapya ya kisiasa ili kuiwezesha kufanya maamuzi magumu ya kimkakati.
Imetafsiriwa n Rashid Abdallah












