Israel na Hezbollah zakabiliana katika mapigano makali

Ndege ya kivita ya Jeshi la Wanahewa la Israeli ikiwasha moto kuzuia kombora lililorushwa kutoka mpaka wa Lebanon. Picha kutoka maktaba: 25 Agosti 2024

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Israel imesema ndege zake za kivita zimeshambulia maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon baada ya kubaini hatua za kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Israel.

Jeshi la Israel limesema takriban ndege 100 za kivita zimeharibu "maelfu" ya roketi zilizorushwa siku ya Jumapili asubuhi, katika kile ilichokitaja kama kitendo cha "kujilinda". Wizara ya afya ya Lebanon iliripoti kuwa watu watatu wameuawa.

Hezbollah baadaye ilisema kuwa ilirusha mamia ya makombora kuelekea kaskazini mwa Israel, na kuiita "awamu ya kwanza" ya mashambulizi ya hatua mbalimbali za kulipiza kisasi mauaji ya kamanda mkuu.

Makabiliano hayo yanaashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya Israel na kundi la Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaoungwa mkono na Iran.

Kumekuwa na matokeo ya kurushiana silaha karibu kila siku katika mpaka wa Israel na Lebanon tangu siku moja baada ya kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza tarehe 7 Oktoba.

Hezbollah imesema inachukua hatua hizo kuunga mkono kundi la Palestina ambalo pia linaungwa mkono na Iran. Hamas na Hezbollah zote zimepigwa marufuku kama mashirika ya kigaidi na Israel, Uingereza na nchi zingine.

Jeshi la Israeli linasema kuwa ndege zake za kivita zinashambulia maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon baada ya kubaini makombora na maroketi yakirushwa kuelekea Israeli.

"Katika kitendo cha kujilinda dhidi ya vitisho hivi, IDF (Jeshi la Ulinzi la Israeli) linafanya mashambulizi kulenga maeneo ya ugaidi," msemaji wa IDF Daniel Hagari alisema.

Israeli ilisema raia wa Lebanon wameonywa kuondoka mara moja katika maeneo ambayo Hezbollah, kundi la Kiislamu la Shia linaloungwa mkono na Iran, lilikuwa likiendesha shughuli zake.

Muda mfupi baadaye, Hezbollah ilisema kuwa imeanzisha mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Israeli kujibu mauaji ya kamanda mkuu wa kijeshi wa kundi hilo yaliyotokea mwezi uliopita.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika maeneo ya kaskazini mwa Israeli ving'ora vya kuonya kuhusu roketi zinazoingia vilisikika mapema Jumapili.

Hakukuwa na ripoti zilizotolewa haraka kuhusu majeraha yoyote.

Katika taarifa, IDF ilisema Hezbollah "imerusha makombora zaidi ya 150 kutoka upande wa Lebanon kuelekea eneo la Israeli".

Wakati huo huo, Hezbollah imesema tayari imerusha zaidi ya roketi 320 za Katyusha, ikisema kuwa ilikuwa ikishambulia kambi 11 za kijeshi za Israeli.

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alisema anaitisha mkutano wa dharura wa baraza lake la mawaziri la usalama.

Ofisi ya Bw Netanyahu ilisema waziri mkuu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant walikuwa ndio "wanaosimamia hali inayoendelea" kutoka kituo cha kijeshi cha IDF huko Tel Aviv.

Wakati huo huo, Hezbollah ilisema katika taarifa yake kwamba mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel hatua ya ni kujibu "uchokozi wa kikatili wa Wazayuni, ambao ulipelekea kuuawa kwa shahidi... Fuad Shukr".

Kamanda mkuu wa kijeshi wa kundi la Shia aliuawa katika shambulizi la anga la Israeli katika mji mkuu wa Lebanon Beirut mwezi Julai.

Israeli imekuwa ikirushiana risasi na kundi la wanamgambo lenye makao yake nchini Lebanon tangu kuanza kwa vita Oktoba mwaka jana na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Hamas, kama Hezbollah, inaungwa mkono na Iran.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (wa pili kushoto) na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant (wa tatu kushoto) "wanafuatilia matukio" kutoka kituo cha IDF huko Tel Aviv, ofisi ya Waziri Mkuu inasema.

Chanzo cha picha, EVN

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (wa pili kushoto) na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant (wa tatu kushoto) "wanafuatilia matukio" kutoka kituo cha IDF huko Tel Aviv, ofisi ya Waziri Mkuu inasema.

Marekani inasema inajitahidi kuepusha uhasama zaidi baada ya mgogoro wa miezi 10 ambayo yamezusha hofu ya kuzuka kwa vita vikali.

Kumekuwa na makabiliano ya risasi karibu kila siku katika mpaka wa Israel na Lebanon tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza tarehe 7 Oktoba.

Duru ya hivi punde ya mazungumzo ya amani ya Gaza yanayoungwa mkono na Marekani huko Cairo bado haijafua dafu.

Kabla ya kujiondoa kwenye kikao, Hamas ilisema inapinga masharti mapya ya Israel na kuishutumu Israel kwa kuvunja ahadi. Israel inakanusha kubadilisha matakwa yake tangu duru ya mwisho ya mazungumzo mapema Julai.

Hezbollah imesema inaunga mkono kundi la Palestina ambalo pia linaungwa mkono na Iran. Hamas na Hezbollah zimeorodheshwa kama mashirika ya kigaidi na Israel, Uingereza na nchi nyingine za magharibi.

Tangu Oktoba, zaidi ya watu 560 wameripotiwa kuuawa na wizara ya afya ya Lebanon, wengi wao wakiwa wapiganaji wa Hezbollah, huku raia 26 na wanajeshi 23 wakiuawa nchini Israel, kwa mujibu wa mamlaka.

Umoja wa Mataifa unasema karibu watu 200,000 pia wamekimbia makazi yao pande zote za mpaka.

xx

Chanzo cha picha, AFP

Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah alisema katika hotuba yake kwa njia ya televisheni Jumapili jioni kwamba kundi hilo lililenga kambi ya kijasusi ya kijeshi iliyo umbali wa kilomita 110 (maili 68) katika eneo la Israel, ambalo lilikuwa umbali wa kilomita 1.5 tu kutoka Tel Aviv.

Alisema Hezbollah imeweza kufanya mashambulizi yake kama ilivyopangwa, na ndege zote zisizo na rubani zimefikia malengo yake kwa mafanikio, kuingia anga za Israel, kulingana na tafsiri ya shirika la habari la Reuters.

Alionya kuwa kundi hilo litajibu tena endapo litahisi kushambuliwa tena.

Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati - ambaye serikali yake ina ushawishi mkubwa ya Hezbollah - alisema "anafanya msururu wa mawasiliano na marafiki wa Lebanon ili kukomesha uhasama".

Alitoa wito wa kusitishwa kwa "uchokozi wa Israel" na utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilimaliza vita vya 2006.

Bw Mikati pia alisisitiza uungwaji mkono wa Lebanon katika juhudi za kimataifa za kufanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuwaachilia mateka kati ya Israel na Hamas.

Mshauri wa usalama wa kitaifa wa White House, Jake Sullivan, alisema matumaini ni kwamba mapigano ya hivi karibuni hayatasababisha vita vya kikanda.

Marekani inachukulia makubaliano kuwa mpango wa kupunguza hali ya mvutano kwenye mpaka wa Israel na Lebanon kwa sababu Hezbollah imesema itasitisha vita mara tu mapigano ya Gaza yatakapomalizika.

Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi