Waafrika waliokwama Lebanon: 'Nataka kuondoka lakini siwezi'

Ethiopian domestic workers gathered outside the embassy

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafanyakazi wengi wa nyumbani wa Ethiopia walipoteza kazi zao wakati wa msukosuko wa kifedha wa Lebanon
Muda wa kusoma: Dakika 5

Eulita Jerop, mfanyakazi wa ndani kutoka Kenya amekuwa akiishi katika viunga vya Beirut, mji mkuu wa Lebanon kwa miezi 14 sasa. Katika wiki chache zilizopita amekuwa akipata hofu kutokana na sauti za angani ambazo hajawahi kuzisikia hapo awali.

“Inatisha sana. Tuliambiwa hayakuwa mabomu, ni ndeg,” anasema. "Lakini sauti zilikuwa kali sana."

Sauti kubwa angani ni kutoka ndege za kivita.

Israel na Hezbollah zinashambuliana kila siku katika mpaka tangu shambulio la Oktoba 7 dhidi ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina. Shambulio hilo lilipelekea uvamizi wa Israel huko Gaza, kwa lengo la kuwaondoa Hamas.

Hezbollah, vuguvugu la kisiasa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran walioko Lebanon, wanasema wanaishambulia Israel kuunga mkono watu wa Palestina.

Katika wiki za hivi karibuni, hofu juu ya vita vya kikanda imeongezeka huku Hezbollah ikithibitisha kuwa mmoja wa makamanda wake wakuu wa kijeshi aliuawa katika shambulio la anga la Israel huko Beirut mnamo Julai 31.

Israel pia imelaumiwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) kwa kifo cha mkuu wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh. Iran imeapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel.

Pia unaweza kusoma

Raia wa kigeni watakiwa kuondoka

An Israeli artillery unit fires across the border towards Lebanon in January in Northern Israel

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kifaru cha Israel kikifyatua kombora kuelekea Lebanon

Kutokana na hali hiyo, nchi nyingi zikiwemo Marekani, Uingereza, Australia, Ufaransa na Canada zilitoa onyo rasmi kupitia balozi zao kwa raia wao kuondoka Lebanon haraka iwezekanavyo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini si rahisi kwa kila mtu kuondoka.

Eulita, mwenye umri wa miaka 35, anasema ni jambo la kawaida kwa waajiri wengi kuchukua pasi za wafanyakazi wa nyumbani pindi wanapofika.

Hata wakiwa na pasipoti, bado wanahitaji visa ya kuondoka ili kuondoka Lebanon - makaratasi ambayo lazima yaidhinishwe na bosi wao.

Ni kutokana na mfumo wa nchi hiyo uitwao 'kafala' kwa wafanyakazi wa kigeni - mfumo unaoajiri takribani watu 250,000.

Mfumo wa sasa wa 'kafala' (ufadhili) unawapa watu binafsi au makampuni vibali vya kuajiri wafanyakazi wa kigeni.

Licha ya wito wa mageuzi makubwa, bado mfumo huo unaendelea katika nchi kadhaa ya Ghuba. Kupitia mfumo huo baadhi wanafanya kazi kupita kiasi, wanalipwa ujira mdogo na wengine wananyanyaswa kimwili.

Daniela Rovina, afisa wa mawasiliano katika Shirika la Kimataifa la Uhamiaji aliiambia BBC News, chini ya sheria za kimataifa mojawapo ya kanuni za msingi zinazolinda raia ni "haki ya kuondoka katika nchi yoyote, ikiwa ni pamoja na yake" na haki ya kurejea nchi ya nyumbani.

Kama mzozo utatokea katika nchi unayoishi chini ya Mkataba wa Geneva wa Haki za Kibinadamu, sheria ya kimataifa ya kibinadamu pia itatumika - akimaanisha raia lazima waruhusiwe kuondoka mwanzoni au wakati wa vita.

Mvutano umekuwepo kati ya Israel na Hezbollah kwa muda wa miaka 40 iliyopita. Israel iliwahi kukalia kwa mabavu eneo la kusini mwa Lebanon. Vita vya mwisho kuzuka kati ya pande hizo ni mwaka 2006, wakati Hezbollah ilipofanya uvamizi wa kuvuka mpaka.

Katika kesi ya Eulita, waajiri wake wanamtaka aendelee kufanya kazi Lebanon.

"Wanasema hali imekuwa hivyo nchini Lebanon kwa miaka mingi, na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi" anasema. “Lakini kwetu sisi mvutano ni mkubwa. Hatujazoea aina hii ya sauti."

"Nataka kwenda nyumbani," anasema.

Safari ni ya gharama

Smoke billows following an Israeli airstrike in the southern Lebanese border village of Chihine on July 28,

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Shambulio la anga la Israel katika kijiji cha mpakani cha kusini mwa Lebanon cha Chihine mwezi Julai

Lakini hata wakiwa na makaratasi yote, Eulita na vijakazi wenzake na wafanyikazi wa nyumbani wanakabiliwa na changamoto nyingine.

“Kuna safari chache za ndege na ni ghali sana," anasema.

Tiketi za kwenda Kenya zinagharimu hadi dola za kimarekani 1000, ambayo ni ghali sana kwa walio wengi.

Banchi Yimer, aliyeanzisha shirika linalounga mkono haki za wafanyakazi wa nyumbani wa Ethiopia, anasema wastani wa mshahara wa kila mwezi ni dola 150, lakini kutokana na gharama ya maisha huko Lebanon "wengi wao hawalipwi kabisa."

Chiku, mfanyakazi mwingine wa ndani kutoka Kenya, ambaye jina lake tumelibadilisha ili kulinda usalama wake, hawezi kumudu gharama za ndege pia.

Ameishi Baabda, magharibi mwa nchi, kwa karibu mwaka mmoja.

“Binafsi ningependa kurudi nyumbani. Lakini tiketi ni ghali sana, "anasema. "Na mama yangu na baba pia hawawezi kumudu pesa hizo."

Amekuwa akiishi kwa hofu, lakini sawa na Eulita, ameambiwa abaki na mwajiri wake.

"Wanasema siwezi kuondoka kwa sababu sijamaliza mkataba wangu," Chiku anasema. "Lakini mkataba huu ni muhimu zaidi kuliko maisha yangu?"

BBC iliwasiliana na Wizara ya wafanyakazi nchini Lebanon ili kujibu madai haya lakini bado haijatoa

Serikali za Afrika kuwahamisha raia wao

Roseline Kathure Njogu, Katibu Mkuu wa Idara ya Kitaifa ya Kenya anayeshughulikia Masuala ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora, aliiambia BBC, idara hiyo inaweza kutoa hati za dharura za kusafiri kwa wale wasio na pasipoti zao.

Aliongeza kuwa mipango ya kuwahamisha watu iko tayari na serikali ya Kenya inaweza kutoa safari za dharura za ndege.

"Kuna takribani Wakenya 26,000 nchini Lebanon, na 1,500 wamejiandikisha kwa ajili ya kuhamishwa kufikia sasa," anasema.

Bi Ngoju anasema kuna marufuku ya wafanyakazi kwenda Lebanon tangu Septemba 2023, kutokana na malalamiko kutoka kwa raia juu ya mfumo wa 'kafala.'

Msemaji wa serikali ya Ethiopia, Nebiyu Tedla, aliiambia BBC "wanatayarisha mipango ya dharura ya kuwahamisha wanadiplomasia na raia kutoka Lebanon ikiwa itabidi."

Lakini Banchi Yimer anasema hata kabla ya mzozo wa Israel na Gaza tayari kulikuwa na wanawake wengi wa Ethiopia waliokuwa wamekwama nchini Lebanon waliokuwa na hamu ya kuondoka.

Kuporomoka kwa uchumi wa Lebanon mnamo 2020 kuliwaacha wafanyakazi wengi wa nyumbani wa Ethiopia bila kazi.

"Uchumi wa Lebanon bado unakabiliwa na shida za kifedha kutokana na uviko-19 na mlipuko bandarini. Yameacha wafanyikazi wengi wa nyumbani bila kazi. Wengi hawawezi kumudu hata kodi au matibabu, achilia mbali ndege ya kwenda nyumbani,” anasema.

Wakati balozi za nchi za nje zikiendelea na mipango ya kuwahamisha watu, wengi wao wanahisi wametelekezwa na serikali zao.

Mfanyakazi wa ndani wa Kenya, Chiku, tayari ameanza kuhifadhi pesa ili aweze kumudu usafiri wa ndege kurudi nyumbani.

"Lakini vipi kuhusu wengine ambao hawawezi kurudi?" Anauliza.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla