Tofauti yazuka kati ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa Ulinzi - Kunani?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Na, Mahmoud Adama

BBC Jerusalem

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Galant akiwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya wizara ya ulinzi mjini Tel Aviv mwezi Oktoba mwaka jana.

Ukosoaji wa waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Galant dhidi ya waziri mkuu na kiongozi wa chama tawala cha Likud ambacho wawili hao wote ni wanachama, imeonyesha mwelekeo mpya unaoonyesha namna viongozi hao wanavyoendelea kutofautiana zaidi kuhusu makubaliano ya kusitisha vita na kubadilishana mateka.

Galant alimkosoa vikali Netanyahu mbele ya Kamati ya Mambo ya Nje na Usalama ya Bunge la Israeli (Knesset), akisema kuwa makubaliano hayo yalicheleweshwa "kwa sababu ya Israeli," kwa kuzingatia kuwa Netanyahu "haonyeshi ujasiri anapozungumza hadharani, nyuma ya milango iliyofungwa."

Galant anawakilisha mtazamo wa jeshi na taasisi ya usalama, ambayo imekuwa ikijaribu kwa miezi kadhaa kuzungumzia hofu yake kwamba Israel itapoteza matokeo ya mafanikio yake ya kijeshi kutokana na masuala ya ndani ya kisiasa.

Mara moja Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ilitoa taarifa ikisema kuwa Waziri wa Ulinzi Yoav Galant anaidhinisha ilichokiita "mawazo ya chuki dhidi ya Israeli na inaathiri uwezekano wa kufikia makubaliano ya kubadilishana wafungwa," ikibainisha kuwa Galant alipaswa kumshambulia mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, Yahya Sinwar, ambaye ilimtuhumu kwa "kukataa kutuma ujumbe kwenye mazungumzo" na " kuendelea kuwa kikwazo kwa kukamilika kwa mazungumzo hayo."

Hata hivyo huku taarifa za malumbano kati yao zikizidi kuongezeka , kituo cha televisheni cha Israel Channel 12 kiliripoti, kikiwanukuu watu walio karibu na Netanyahu, wanaosema waziri huyo mkuu na muungano wa Likud haufikirii kumfukuza Galant ," licha ya tofauti zao.

Wakati huo huo gazeti la Yedioth Ahronoth lilithibitisha kwamba Netanyahu anatambua kwamba Galant hawezi kufukuzwa "katikati ya vita."

Ni nini kilichosababisha tofauti hizi kati yao

"Tofauti kati ya Galant na Netanyahu zilianza kuibuka mwezi Machi/Aprili 2023 wakati wa marekebisho ya sheria," Tal Shalev, mwandishi mkuu wa kisiasa wa Walla, aliiambia BBC.

Mchambuzi wa masuala ya Israel Mazal Moalem ameiambia BBC kwamba mzozo kati ya viongozi hao kimsingi ni suala la kisiasa na kwamba bila shaka wako katika ushindani, akiamini kwamba Galant "anapanga kuchukua nafasi ya Netanyahu katika jaribio la kumfedhehesha na kumfanya kuwa dhaifu mbele ya ulimwengu."

Moalem alichukulia kuwa Galant alianza kumshambulia Netanyahu, hivyo ofisi ya Netanyahu ilitoa taarifa inayoelezea kwamba Galant ameidhinisha kile ilichokiita "taarifa ya chuki dhidi ya Israel" na ofisi ya serikali ilimtuhumu kwa mashtaka ambayo iliyaelezea kuwa "makubwa na mazito."

"Karibu na usaliti"

Moalem anaamini kwamba kauli za Galant "zinakaribia uhaini" na kwamba anaharibu sifa ya Israeli ulimwenguni.

Aliiambia BBC kwamba hali hii haitaathiri vita hivi karibuni, akibainisha kuwa "Netanyahu ana muungano imara wa serikali, na hali yake katika chama tawala cha Likud ni nzuri na kura za maoni za hivi karibuni zinathibitisha hilo."

Kura ya maoni ya hivi karibuni ya gazeti la Maariv ilionyesha kuwa chama cha Likud, kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu, kiko mbele kwa umaarufu, na kwamba vyama vya upinzani vinaendelea kuondoka kutoka kwa wingi wa wabunge 61 katika bunge la Israeli, isipokuwa vyama vya Kiarabu.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Galant akiwa katika ofisi za wizara ya ulinzi ya Israel kabla ya kuhudhuria mkutano wa baraza la mawaziri

Usiku wa Allant" Tena

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Galant ndiye waziri pekee aliyejitokeza kupinga marekebisho ya sheria na kutangaza kwa ulimwengu kwamba marekebisho hayo ni hatari kwa Taifa la Israeli.

Saa ishirini na nne baada ya kauli yake wakati huo, Netanyahu alimfuta kazi na Waisraeli waliandamana kote nchini humo kwa idadi isiyo ya kawaida, ambapo karibu waandamanaji milioni moja walishiriki, na maandamano hayo yaliitwa "Usiku wa Galant," kulingana na maelezo ya Shalev kwa BBC.

Wakati huo, Muungano wa Wafanyakazi wa Israeli ulitangaza mgomo wa jumla, na Netanyahu aliunga mkono uamuzi wake wa kumfukuza Galant. Tangu wakati huo, uhusiano kati ya Galant na Netanyahu umeelezewa kama "mbaya," akibainisha kuwa Galant ana maamuzi na maoni ambayo "yanampinga waziri mkuu wake."

Tal Shalev anaamini kuwa taasisi ya usalama ya Israel inaunga mkono makubaliano yoyote yaliyofikiwa kwa njia ya amani na inataka usitishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Anaamini kwamba duru ya mazungumzo iliyopangwa kufanyika Alhamisi kuhusu makubaliano ya kubadilishana wafungwa na Hamas itasaidia Israel kupata "uhalali wa kimataifa," hata kama mazungumzo hayo yataanzisha vita kaskazini dhidi ya Hezbollah, kama alivyoelezea.

Shalev ameiambia BBC kwamba Netanyahu ameweka masharti ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa jambo ambalo anasema linafanya makubaliano hayo yawe magumu kufikiwa.

Alitarajia kwamba Galant ataondolewa katika nafasi yake na kwamba Netanyahu anajaribu kutafuta njia mbadala ya kuchukua nafasi yake, lakini hajapata mbadala kama huo hadi sasa, akiashiria kuwa ana uwezo wa kufanya hivyo.

Netanyahu anahofia majibu ya Israel iwapo waziri wa ulinzi atafukuzwa, maandamano dhidi ya uamuzi huo yatafanywa upya, na "Usiku wa Galant" utarudiwa tena. Shalev alisema kwamba maandamano makubwa nchini Israeli katikati ya vita yanaweza "kusababisha uhasama katika jeshi."

Netanyahu anafikiria kumfukuza kazi mkuu wa jeshi la Israel Herzi Halevi na mkuu wa Shin Bet Ronen Bar na kuwabadilisha maafisa wote wa ngazi ya juu wa usalama na watu watiifu zaidi kwa Netanyahu.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maandamano ya Waisrael ya kupinga kutimuliwa kwa ghafla kwa Waziri wa Ulinzi Yoav Galant Machi mwaka jana/Aprili

"Galant haamini nia ya Netanyahu"

Mchambuzi wa masuala ya kijeshi Eyal Alima amesema katika mahojiano na BBC Idhaa ya Kiarabu kwamba kumfukuza Galant kwa wakati huu kutasababisha kuvunjika kwa kazi ya pamoja kati ya jeshi na ngazi za kisiasa na kwamba itakuwa ni ishara kwamba mambo yamefika njia panda kuhusu hali ya ndani ya Israel.

Alimaa ameiambia BBC kwamba iwapo katikati ya vita na kuendelea kwa operesheni za kijeshi katika Ukanda wa Gaza kutaendelea kuwa na hali ya kutofikiwa kwa makubaliano ya kuwarejesha mateka "inaweza kusababisha mlipuko wa hali ya ndani ya Israel."

Alima anasisitiza kuwa ujumbe wa msingi wa taasisi ya usalama ya Israeli ni kurejeshwa kwa mateka, na hii inalazimisha Israeli kusitisha vita, akibainisha kuwa Mkuu wa Majeshi ya Israeli alizungumza juu ya hili hadharani na kwamba haitofautiani na kile alichosema Galant.

Alima anaamini kuwa Galant haamini nia ya Netanyahu na hili ni jambo hatari, na kwamba kwa kuzingatia kuwa wale wanaompinga waziri mkuu kama "uhaini" na adui wa taifa la Israeli, kunaibua wasiwasi miongoni mwa taasisi za kijeshi.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Israel Eli Nissan anaamini kuwa "Netanyahu hapendi mmoja wa mawaziri wake wa muungano kujitokeza katika eneo la tukio na anapendelea kuwa mdhibiti mkuu."

Nissan imeiambia BBC kwamba kuna wito kutoka kwa watu kurejesha mambo katika hali ya kawaida kutokana na mvutano uliopo kaskazini mwa Lebanon , vitisho vya Iran na vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza.

Anatarajia kwamba ikiwa mambo yatatulia katika pande zote, Netanyahu atamfuta kazi waziri Galant .

Nissan anaamini kwamba Galant alifanya makosa alipozungumza siku chache zilizopita na kumkosoa Netanyahu, jambo ambalo lilimkasirisha kiongozi huyo, akibainisha kuwa kauli zake zilionyesha malumbano ya hali ya juu yaliopo kati ya viongozi hao.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla