Benjamin Netanyahu: Kiongozi wa Israel mwenye maisha ya kisiasa kama ya paka
Na Leonard Mubali
BBC Swahili,Dar es Salaam

Chanzo cha picha, Reuters
Israel inajipata katika hali ngumu wakati huu ambapo inahusika na vita katika eneo la Gaza na mzozo unaozidi kutokota na kundi la Hezbolla la nchini Lebanon.
Katikati ya maamuzi muhimu ya kijeshi na kisiasa ambayo Israel inalazimika kuyachukua wakati huu ni Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu.
Uongozi wake ulitikiswa kidogo alipoondolewa madarakani lakini Netanyahu amejipata akipambana na ajenda ya usalama wa Israel na kutuliza upinzani wa ndani ya nchi .
Hata hivyo Pamoja na kwamba sasa ana miaka 73 Netanyahu ni mmoja wa watu wanaotajwa kwamba walianza masuala ya uongozi akiwa bado na umri mdogo,kiasi ambacho baadhi ya wachambuzi wa siasa za Israel wanaona kwamba imempatia fursa kubwa ya kupata uzoefu.
Alipoteza nafasi yake mwaka 1999 baada ya kuitisha uchaguzi miezi 17 kabla ya muda,ambapo alishindwa na kiongozi wa chama Labour Ehud Barak.

Chanzo cha picha, Reuters
Kiongozi huyu anayetajwa kuwa imara katika siasa za Israel mwenye umri wa miaka 73 na mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha Likud na waziri mkuu aliyekaa muda mrefu zaidi wa Israel, anatarajiwa kuanza muhula wa tatu ambao haujawahi kushuhudiwa kama Waziri Mkuu baada ya kufanya mazungumzo ya muungano na washirika wake wa kidini na wa mrengo mkali wa kulia juu ya kuunda serikali.
Ushindi wake unaleta Imani kubwa kwa wafuasi wake na kuonekana kuwa ni mwanasiasa asiye tabirika,na anatarajiwa kuweka rekodi ya kushinda chaguzi mara tano na kuikalia ofisi hiyo mara sita zaidi ya Waziri mkuu yeyote katika historia ya miaka 74 ya uongozi wa taifa hilo.
Mafanikio haya ya Bwana Netanyahu ni kutokana na imani aliyoijenga kwa raia wa taifa hilo na wafuasi wake kwamba ana uwezo wa kutetea maslahi ya Israel.
Daima amekuwa ni mtu mwenye msimamo mkali dhidi ya Wapalestina, na kuleta hali ya wasi wasi katika mazungumzo yoyote ya usuluhishi wa mgogoro kati ya mataifa hayo. Wapinzani wake wanamuona Bwana Netanyahu kama mtu hatari kwa demokrasia ya Israel.
Netanyahu ni nani hasa?

Chanzo cha picha, GPO VIA GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Benjamin Netanyahu alizaliwa huko Tel Aviv mwaka 1949. Na mwaka 1963, familia yake ilihamia Marekani,pale baba yake Bwana Benzion, mwanahistoria maarufu na mwanaharakati wa kizayuni alipewa fursa ya masuala ya kitaaluma nchini humo.
Akiwa na umri wa miaka 18, alirejea Israel, ambako alikaa kwa miaka mitano akiwa ndani ya jeshi,akihudumu katika cheo cha Kapteni katika kambi ya kikomandoo ya Sayeret Matkal. Alijeruhiwa katika shambulio la anga katika uwanja wa Ubelgiji lililotekelezwa na wapiganaji wa Kipalestina lililotua Israel mwaka 1972, na pia alipigana vita mashariki ya kati mwaka 1973.
Katika Habari nyingine za kifamilia ni kwamba kaka yake bwana Netanyahu, bwana Jonathan, aliuawa wakati alipokuwa akiongoza kuwaokoa mateka wa Israel Entebbe, nchini Uganda. Kifo chake kilikuwa na matokeo makubwa katika familia ya Netanyahu na jina lake likawa Fahari ya Israel.
Katika kumuenzi kaka yake Netanyahu alianzisha taasisi maalumu ya kukabiliana na ugaidi kama kumbukumbu ya kaka yake na mwaka 1982 akawa naibu wa ujumbe maalum huko Washington.
Kuibuka kwake kisiasa
Bwana Netanyahu alianza kujihusisha katika siasa baada ya kurejea Israel mwaka 1988,akifanikiwa kushinda kiti cha chama cha Likud katika bunge la Knesset na kuwa naibu waziri wa mambo ya nje.
Baadaye alifanikiwa kuwa mwenyekiti wa chama,mwaka 1996,na kisha akawa Waziri mkuu wa Israel aliyechaguliwa moja kwa moja baada ya kuuawa kwa aliyekuwa Waziri mkuu wa taifa hilo Yitzhak Rabin.
Netanyahu alijiuzulu kama kiongozi wa chama cha Likud nafasi ya mtangulizi wake Ariel Sharon. Baada ya Sharon kuchaguliwa Waziri mkuu mwaka 2001, Netanyahu alirejea tena serikalini,kwanza kama Waziri wa mambo ya nje na baadaye kama Waziri wa fedha.Mwaka 2005, alijiuzulu kutokana na maandamano katika uwanja wa mdogo wa ndege wa Gaza.
Mafungamano ya kiuongozi

Chanzo cha picha, AFP
Kiongozi huyu wa Israel katika mafungamano yake na viongozi wa mataifa mengine inaelezwa kwamba alikuwa mtu wa karibu wa rais wa Marekani aliyemaliza muda wake Donald Trump.
Baada ya mwaka 2016 Netanyahu alikumbwa na mazingira magumu kisiasa baada ya kukumbwa na kashfa ya rushwa na udanganyifu na kuunganishwa na kesi nyingine tatu tofauti Novemba 2019.
Kwa hiyo kama wasemavyo waswahili kwamba usione vinaelea vimeundwa,ama kwa hakika katika masuala ya kiuongozi na siasa za ndani ya Israel,bwana Netanyahu mapito yake hayo yanaonyesha kwamba,kaona mengi na kajifunza mengi katika siasa za ndani ya Israel,ukanda wa mashariki ya kati na siasa za kimataifa pia,hivyo ushindi wake huenda ni matokeo ya mapito yake na kujijenga kwake kisiasa kwa miaka mingi ndani ya Israel.















