Benjamin Netanyahu: Waziri Mkuu wa Israeli aliyeng'olewa madarakani alichoma nyaraka za siri

Chanzo cha picha, Getty Images
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alificha siri zake kuu zilizakuwemo kwenye ofisi ya Waziri mkuu kabla ya kuondoshwa madarakani, vimeripoti vyombo vya habari vya Israeli.
Makavazi ya Waziri Mkuu wa Israeli yaliharibiwa na mtu kufuatia amri yake ambapo Bw Netanyahu anaripotiwa kumuamrisha mtu kuzichoma nyaraka zote za ofisi yake kabla ya kuondoka mamlakani.
Vyombo vya habari nchini humo vinasema kwamba nyaraka hizo ziliteketezwa kwa moto katika siku ambayo muhula wa Bw Netanyahu ulikuwa unamalizika, na saa chache kabla ya kuingia madarakani kwa Waziri Mkuu mpya wa Israeli, Naftali Bennett, kuchukua Ofisi ya Waziri Mkuu.
Sheria ya Israeli inazuia uchomwaji au kuharibiwa kokote kwa nyaraka na badala yake zinaagiza kwamba nyarakahizo zinapaswa kutunzwa mahala salama kwenye kabati maalum zilizopo kwenye makavazi ya ofisi ya Waziri Mkuu. Kulingana na sheria kuhusu utunzwaji wa nyaraka, ni Waziri Mkuu pekee na wasaidizi wake wachache wa ngazi ya juu wa karibu wanaoruhusiwa kuziona.

Chanzo cha picha, Reuters
Jumatatu, Bw Netanyahu alimkabidhi waziri Mkuu mpya madaraka yake katika mkutano uliodumu kwa nusu saa tu, ambapo Waziri Mkuu anayeondoka madarakani alimfahamisha mrithi wake masuala yanayopaswa kushughulikiwa bila kutoa taarifa yoyote juu ya kikao au kuchapisha picha ya tukio hilo.
Awali vyombo vya habari vya Israeli vilisema kuwa Netanyahu hatashiriki katika hafla yoyote ya kukabidhi mamlaka, kwasababu hataki kumhalalisha bw Bennet kama waziri Mkuu.
Netanyahu alisema katika hotuba yake kwa manaibu wake katika vuguvugu la mrengo wa kulia na vyama vya kidini vya upinzani ''serikali mpya itapinduliwa mapema sana kwasababu ni "serikali hatari fisadi" na " watu wa Israeli wataokolewa.
Jinsi netanyahu alivyong'olewa madarakani
Bwana Netanyahu aliweka rekodi ya kuongoza taifa lake kwa mihula mitano , mara ya kwanza kuanzia mwaka 1996 hadi 1999, na baadaye kuendelea kutoka mwaka 2009 hadi 2021.
Allitisha uchaguzi 2019 lakini akashindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha ili kuunda serikali mpya ya muungano.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulifanyika chaguzi nyengine mbili baadaye ambazo zilikamilika bila kupata mshindi wa moja kwa moja.
Uchaguzi wa tatu ulipelekea kuundwa kwa serikali ya muungano ambapo bwana Netanyahu alikubali kugawa mamlaka na aliyekuwa kiongozi wa upinzani Benny Gantz.
Lakini mpango huo ulishindwa kufua dafu mwezi Disemba na kusababisha uchaguzi wa nne.
Ijapokuwa chama cha Likud kilijitokeza kama chama kikubwa katika bunge la Knesset lenye viti 120, bwana Netanyahu kwa mara nyengine alishindwa kuunda serikali ya muungano na jukumu hilo likapewa bwana Lipid, ambaye chama chake cha mrengo wa kati cha Yesh Atid kilikuwa cha pili kwa ukubwa.
Upinzani uliokuwa ukipinga utawala wa Netanyahu madarakani uliongezeka , sio tu miongoni mwa vyama vya mrengo wa kushoto na ule wa kati bali pia miongoni mwa walio katika mrengo wa kulia ambavyo vina mawazo sawa na chama cha mrengo wa kulia cha Likud ikiwemo Yamina.












