'Hiki ndicho anachotaka Netanyahu' - Gazeti la Maariv

Chanzo cha picha, Getty Images
Tunaanza ziara yetu na gazeti la Israel, Maariv, lilichapisha makala ya Uri Silberscheid, profesa wa falsafa ya siasa na sheria katika Chuo Kikuu cha Haifa, anaona dalili zote zinaonyesha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu hana nia ya kumaliza vita huko Gaza.
Silberscheid anasema, Netanyahu hakatai hilo, akielezea kile ambacho waangalizi wengi wakiwemo majenerali wastaafu wa Israel, wanakieleza; nacho ni kukataa kwake kuandaa mpango wa kupata mbadala wa Hamas huko Gaza.
Silberscheid anasema Netanyahu anataka kuiweka Israel kwenye mtego wa serikali ya mrengo wa kulia kwa muda mrefu zaidi, ili kuhakikisha yeye mwenyewe anaendelea kuwa madarakani.
Ili Netanyahu afanikishe hilo, ni lazima kuwa na maadui wa nje. Atafanya kila kitu ili vuguvugu la Wapalestina, Hamas libaki kama lilivyo, ili libakie kama adui wake wa milele.
Netanyahu pia amefanya kazi ya kudhoofisha Mamlaka ya Palestina kwa nia ya kuimarisha Hamas, hata katika Ukingo wa Magharibi, kwa lengo la kudhoofisha nguvu yoyote kubwa ambayo inaweza kuwa mbadala wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Silberscheid anasema Israel chini ya uongozi wa Netanyahu, haitafuti kuchukua fursa ya ushindi wake katika eneo la Gaza ili kuiweka serikali mbadala wa Hamas, na kurekebisha uhusiano na Saudi Arabia, au kuunda uhusiano na mataifa ya ki-Sunni yenye msimamo wa wastani dhidi ya Iran.
Silberscheid anasisitiza: Hivi ndivyo hasa Netanyahu anavyotaka, na vita vya upande wa kaskazini vitaleta lengo hilohilo.
Kwa kuwa kufikia makubaliano ya kuwaachilia huru watu waliotekwa nyara kungekomesha vita, jambo ambalo Israeli inalihitaji, Netanyahu anasimama kuwa kizuizi cha kufikia mapatano hayo.
"Kadhia ya Gaza haihusu kundi moja tu la watu”

Chanzo cha picha, LORNE CAMPBELL/GUZELIAN
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tunageukia gazeti la Uingereza la The Guardian, limechapisha makala ya mwandishi wa Sudan, Nisreen Malik, anasema athari ya vita vya Gaza inaonekana duniani kote.
Nisreen anapinga wazo kwamba ni Waislamu pekee ndio wanaojali kile kinachotokea Gaza. Hakubaliana na wazo kwamba ni Waislamu pekee katika nchi mbalimbali za dunia ndio wanaoihurumia Gaza.
Mwandishi alifuatilia wagombea binafsi ambao walishinda uchaguzi wa hivi karibunui nchini Uingereza, kwa sababu tu walielekeza kampeni zao za uchaguzi kwenye vita vya Gaza.
Ingawa kura za maoni zinaonyesha wengi wa Waingereza wanaunga mkono kusitishwa mapigano Gaza, wanasiasa - haswa katika uongozi wa Chama cha Labour - wanasisitiza kupuuza matokeo ya kura hizi.
Mwandishi anaendelea, wagombea binafsi walioshinda uchaguzi wa Uingereza hawakupata viti vyao vya ubunge kwa sababu tu kuna Waislamu wengi katika majimbo yao ya uchaguzi, bali pia kwa sababu wapiga kura wasio Waislamu nao waliwapigia kura.
Ikiwa kura ya maoni itapigwa kuhusu Gaza kote Uingereza, pamoja na maandamano yote makubwa, itakuwa wazi kuwa ni vigumu kusema suala la Gaza linahusu kundi la aina moja tu la watu.
"Palestina ndogo”

Chanzo cha picha, REUTERS
Tunahitimisha ziara yetu na gazeti la London, Asharq Al-Awsat, limechapisha makala ya mwandishi wa Lebano,n Samir Atallah chini ya anuani "Palestina Ndogo.”
Mwandishi anasema, ushindi wa Wapalestina huko Gaza unaweza usiwe mkubwa, lakini nchini Chile unaweza kuwa mkubwa, akiashiria mafanikio ya timu ya soka ya Palestina katika Amerika ya Kusini.
Mwandishi anasema, takribani wahamiaji nusu milioni wa Kipalestina wanaishi Chile tangu mwanzoni mwa karne iliyopita, wamefanikiwa katika biashara, wanafanya vyema katika siasa, na hawasahau kadhia ya Palestina.
Atallah anasema uwepo wa Wapalestina nchini Chile katika nyanja zote, kumefanya maoni ya umma nchini Chile kusimama na suala la Gaza bila kusita.
Vita havikuacha mtu yeyote asiyeegemea upande wowote, wakati ulimwengu ukishuhudia vita vya maangamizi vilivyodumu kwa muda mrefu na vinavyoendelea.
Atallah anadokeza baadhi ya watu wanaiita Chile ni “Palestina Ndogo,” akibainisha kuwa jumuiya ya Wapalestina nchini Chile inajumuisha wanasiasa, waandishi, wasanii, na maprofesa wa vyuo vikuu.
Mwandishi anarejelea methali moja maarufu nchini Chile inayosema: “Katika kila kijiji kuna polisi, kasisi, na Mpalestina.”
Jumuiya za Wapalestina zimeanza kujitokeza katika nyanja za kisiasa katika nchi nyingine kadhaa, mfano El Salvador, ambako rais huyo ana asili ya Palestina.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuharirirwa na Ambia Hirsi












