Gaza: Mama akata tamaa ya kupata kitu cha kumlisha mwanawe

Abdulaziz al-Hourani mwenye umri wa miezi mitano amelazwa katika hospitali ya al-Ahli kaskazini mwa Gaza, mwili wake mdogo ukionyesha dalili za utapiamlo.
Akiwa na uzani wa kilo 3 tu, Abdulaziz ametoka tu chumba cha wagonjwa mahututi ambapo alitibiwa kwa utapiamlo mkali.
Mamake anasema hawezi kupata chakula anachohitaji huko Gaza. “Huyu ndiye mtoto wangu wa pekee. Anatakiwa kuwa na uzito wa angalau kilo 5 na nina wasiwasi sana kuhusu afya yake,” anasema. "Siwezi kumpeleka nje ya nchi kwa sababu mipaka imefungwa."
Simulizi ya Abdulaziz si ya kipekee. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watoto 8,000 walio chini ya umri wa miaka mitano wamegunduliwa na kutibiwa kutokana na utapiamlo uliokithiri tangu vita hivyo kuanza - kati ya hao 1,600 walikuwa na utapiamlo mkali.
Wiki iliyopita, mkurugenzi mkuu wa WHO Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema "tayari kumekuwa na vifo 32 vinavyotokana na utapiamlo, vikiwemo 28 kati ya watoto chini ya miaka mitano".
Mwanzoni mwa Juni, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef, liliripoti kuwa watoto tisa kati ya 10 huko Gaza wanakumbwa na ukosefu mkubwa wa chakula, wakiishi kwa kupata mlo mara mbili au hata chini ya hapo kwa siku.
Lilisema kwamba "miezi ya uhasama na vikwazo vya kupatikana kwa misaada ya kibinadamu vimeporomosha mifumo ya chakula na afya, na kusababisha matokeo mabaya" na kwamba watoto "wako katika hatari ya utapiamlo unaotishia maisha".

Masoko yasio na cha kuuza
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nilizaliwa Gaza na kuishi huko na familia yangu – nikaendesha shughuli zangu kutoka huko hadi Februari.
Kabla ya vita, nilijua wilaya ya kaskazini ya Gaza ya al-Tufah kuwa mahali penye watu wengi na maelfu ya wanunuzi. Lakini ninapowapigia simu watu ambao bado wapo huko kuulizia hali ilivyo, wananitumia picha zinazoonyesha kuwa sasa inakaribia kuwa eneo lisilo na watu.
"Hakuna nyanya, matango, matunda wala mkate," anasema Salim Shabaka, mzee wa eneo la sokoni. Ananiambia baadhi tu ya nguo zilizotumika na vyakula kidogo vya makopo ndivyo vinavyopatikana.
"Hatujawahi kuishi maisha kama haya - hakuna cha kununua wala kuuza," anaongeza mchuuzi mwingine wa mitaani.
"Nina watoto saba na sijapata msaada wowote."
Kila siku, kunakuwa na foleni ndefu mbele ya "Tikkeyas" - maduka madogo ya chakula yanayotoa milo ya bure. Mengi yamefadhiliwa na watu wanaojiweza kaskazini mwa Gaza, lakini uhaba wa vifaa unamaanisha mustakabali wao haujulikani.
Kwa sasa, hapa ndipo watoto wengine huenda kujaribu kupata mlo wa moto moto uliotoka kupikwa, huku wengine wakitembea umbali mrefu kuchota maji.
Njaa na magonjwa

Karibu kila siku, mimi huzungumza na jamaa na marafiki huko Gaza. Katika picha wanazonitumia naona wamepungua uzito na wana mabadiliko katika sura zao.
Naye Dk Tedros wa shirika la WHO ameonya kwamba "licha ya ripoti za kuongezeka kwa utoaji wa chakula, kwa sasa hakuna ushahidi kwamba wale wanaohitaji zaidi wanapokea kiasi cha kutosha na chakula bora".
Aliongeza kuwa kutokana na ukosefu wa usalama, ni vituo viwili tu vya kukabiliana na wagonjwa wa utapiamlo mkali ambavyo vinaweza kufanya kazi kwa sasa. Alionya kwamba ukosefu wa huduma za afya, maji safi na usafi wa mazingira "unaongeza kwa kiasi kikubwa hatari kwa watoto wenye utapiamlo".
Hali hiyo inamaanisha kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza na pia kuna uwezekano mkubwa wa magonjwa kama vile hepatitis. Hospitali nyingi na zahanati zimefungwa, na zile ambazo bado zinafanya kazi zimeharibika kwa sababu ya vita na kuzidiwa na watu.
"Tumeishiwa na nguvu," anasema Umm Fouad Jaber, mwanamke mzee kutoka Jabalia, kaskazini mwa Gaza. "Tumehamishwa mara kadhaa, na watu wanauawa kila siku."
"Tumekula chakula cha wanyama, watoto na wanawake wanapoteza fahamu kwa sababu ya utapiamlo. Magonjwa yametumaliza.”
Daktari wa Kipalestina Moatasem Saed Salah, mjumbe wa kamati ya dharura katika wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, anathibitisha kwamba makumi ya wenye utapiamlo wanaripotiwa kila siku, haswa miongoni mwa watoto, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.
Anasema watu wengi, ambao tayari wanaugua magonjwa sugu, sasa wanapambana na hali zingine za kiafya pia.
Changamoto za misaada ya kibinadamu
Vita hivyo vilianza baada ya Hamas kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba, na kuua takriban watu 1,200 na kuwarudisha wengine 251 huko Gaza kama mateka.
Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema zaidi ya Wapalestina 37,000 wameuawa tangu kuanza kwa vita hivyo, na mamia ya maelfu ya wengine wamejeruhiwa au kukimbia makazi yao.
Wananchi wa Gaza wametazamia misaada ya kibinadamu kuishi, lakini hakuna vyakula vya kutosha vinavyopatikana.

Wakati fulani, kivuko cha Rafah kwenye mpaka wa Misri kusini mwa Gaza kilikuwa sehemu kuu ya kuingilia kwa ajili ya kuwasilisha misaada. Lakini kwa kuwa Israel sasa inadhibiti upande wa Gaza wa kivuko, eneo hilo limefungwa.
Pia upande wa kusini kuna lango la Kerem Shalom kutoka Israel. Liko wazi, lakini mapigano yamezuia kuwasilishwa kwa misaada kupitia njia hii.
Baadhi ya chakula pia kinasafirishwa kuelekea kaskazini kupitia maeneo mapya ya vivuko, lakini kiasi cha misaada kimepungua kwa thuluthi mbili tangu Mei 7, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, na usambazaji unapungua upande wa kusini, kulingana na Mpango wa Chakula Duniani.
Gati ya kuelea iliyojengwa na Marekani kwa ajili ya usafirishaji wa misaada ilikuwa haifanyi kazi kwa siku kadhaa baada ya kuharibiwa na hali mbaya ya hewa, na tangu wakati huo imehamishwa kwa muda kutokana na maji makuu.
Wiki iliyopita, serikali ya Gaza inayoongozwa na Hamas iliripoti kwamba si zaidi ya malori 35 yanawasili Gaza kila siku, na kusema haya ndiyo chanzo pekee cha chakula na dawa kwa watu 700,000 kaskazini mwa Gaza.
Lakini katika ujumbe kwenye mtandao wa X mnamo Juni 13, bodi ya Israel inayohusika na uratibu wa kibinadamu, Cogat, ilisema: "Zaidi ya pauni bilioni moja za chakula zilihamishiwa Gaza tangu kuanza kwa vita.
"Hakuna kikomo kwa [msaada] wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kila aina ya dawa zinazoweza kuingia Gaza."
Katika ujumbe mwingine siku hiyo hiyo Cogat alisema lori 220 za misaada ziliingia Gaza siku hiyo. Inalaumu mashirika ya misaada kwa kushindwa katika kusambaza chakula na vifaa vingine.
Umoja wa Mataifa unasema usambazaji wa kile kinachopatikana unatatizwa sana na mapigano, uvunjaji wa sheria, ukosefu wa utulivu, na vikwazo vingine vya Israel.
Siku ya Jumapili, jeshi la Israel lilitangaza kila siku "kusimamishwa kimkakati kwa shughuli za kijeshi" kando ya barabara kusini mwa Gaza ili kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kuingia. Lakini ilisisitiza kuwa hakuna usitishaji vita na kwamba mapigano yataendelea huko Rafah. Israel inasema operesheni yake huko Rafah ni muhimu ili kuwaondoa Hamas kutoka kile inachokiita "ngome kuu ya mwisho ya kundi hilo".
Usitishaji ambao unasemekana kuwa ulianza Jumamosi, utaanza saa 08:00 hadi 19:00 saa za eneo na kwamba itakuwa tu ni kwa njia inayoelekea kaskazini kutoka kivuko cha Kerem Shalom.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa alikaribisha tangazo hilo lakini Jumapili alibainisha kuwa bado halijasababisha kuongezeka kwa misaada.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yalionya hapo awali kwamba iwapo vita vitaendelea, zaidi ya Wapalestina milioni moja huko Gaza huenda wakakabiliwa na njaa kali ifikapo katikati ya mwezi wa Julai.
Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Yusuf Jumah








