Gaza inahitaji msaada gani?

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Familia nyingi huko Gaza zinategemea misaada kama vile unga. Picha ya maktaba iliyopigwa katika kambi ya wakimbizi ya Al-Shati tarehe 31 Julai 2023

Chakula, mafuta na maji ya kunywa yanapungua vibaya huko Gaza, Umoja wa Mataifa (UN) umeonya, huku maelfu ya tani za msaada zikikaribia kuingia kupitia mpaka wa kusini wa Ukanda huo na Misri.

Viongozi wa dunia na mashirika ya kibinadamu yanatoa wito kwa misaada muhimu kuruhusiwa, huku mzozo kati ya Israel na Hamas ukizidi kuwa mbaya.

Takriban lori 20 zilizobeba chakula, maji na vifaa vya matibabu huenda zikaruhusiwa kuingia siku zijazo. Hata hivyo, mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutoa misaada Martin Griffiths anasema lori 100 za msaada kwa siku, zinahitajika kusaidia wakazi milioni 2.1 wa Gaza.

Kwa nini misaada haiwezi kufika Gaza na nini kinahitajika?

tt

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Lori la misaada ya kibinadamu lililokusudiwa kwenda Ukanda wa Gaza limeegeshwa kwenye mpaka na Misri tarehe 18 Oktoba.

Israel na nchi jirani ya Misri zimezuia usafirishaji wa bidhaa na watu kuingia na kutoka Gaza tangu Hamas ilipochukua udhibiti wa eneo hilo mwaka 2007. Nchi hizo mbili zinasema kuwa kizuizi hicho kinahitajika kwa sababu za kiusalama.

Gaza imezungukwa na vizuizi vinavyodhibiti watu kuingia na kutoka katika Ukanda huo. Kuna vivuko vitatu vilivyodhibitiwa vikali, ambavyo vilifungwa baada ya Hamas kufanya shambulio dhidi ya Israel na kuua zaidi ya watu 1,400.

Kujibu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant aliamuru "kuzingirwa kabisa" kwa Gaza na kuongeza: "Hakutakuwa na umeme, hakuna chakula, wala mafuta na kila kitu kimefungwa."

Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti takriban watu 3,785 wameuawa katika Ukanda huo tangu kuanza kwa mzozo huu wa hivi karibuni, na wengine 12,500 kujeruhiwa.

Vivuko viwili - Erez kaskazini mwa Gaza, na Kerem Shalom kusini - ambavyo vinaenda Israeli vimefungwa kwa muda usiojulikana.

Njia ya tatu, Rafah kuvuka kuelekea Misri, sasa ndiyo njia pekee inayoweza kutumika kwa misaada ya kibinadamu. Hata hivyo mashambulizi ya mabomu ya Israel yameharibu njia na mashimo yanarekebishwa ili kuruhusu malori kupita kwa usalama.

Je Israel imesema nini kuhusu misaada kwa Gaza?

 Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Israel imesema haitaruhusu msaada wowote kupita katika eneo lake hadi mateka wanaoshikiliwa na Hamas waachiliwe huru.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema takriban watu 203, wakiwemo watoto 16, wanaaminika walitekwa katika shambulio hilo la tarehe 7 Oktoba.

Kufuatia mazungumzo na Rais wa Marekani Joe Biden, Israel ilikubali kuruhusu baadhi ya misaada kuingia Gaza kutoka Misri, kupitia kivuko cha mpaka wa Rafah.

Hata hivyo, mamlaka ya Israel imesema ikiwa kuna dalili zozote Hamas inajaribu kutumia misaada iliyoruhusiwa kuingia Gaza basi wataingilia kati.

Kivuko cha mpaka cha Rafah kiko wapi?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kivuko cha Rafah ni muhimu linapokuja suala la kupata misaada Gaza, huku mzozo wa Israel na Hamas ukiongezeka.

Ni njia ya kutoka kusini mwa Gaza na kivuko pekee ambacho hakiendi moja kwa moja ndani ya Israeli. Badala yake, inatoa njia kuelekea rasi ya Sinai ya Misri.

Misri inaonekana kuwa tayari kufungua tena kivuko chake cha mpaka na Gaza huko Rafah ili kuruhusu wenye pasipoti za kigeni kutoka na kusaidia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry, aliambia kipindi cha Newshour cha BBC kwamba kwa mtazamo wa Misri, "kivuko cha Rafah upande wetu kiko wazi", lakini alilaumu "milipuko ya mabomu" kwa kufanya kivuko "kisifikike" na kutokuwa salama kwa lori za misaada kuingia ndani ya Gaza.

Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi aliongeza: "Kinachotokea sasa huko Gaza ni jaribio la kuwalazimisha wakazi wa kiraia kupata hifadhi na kuhamia Misri, jambo ambalo halipaswi kuruhusiwa."

Aliongeza kuwa ni muhimu Wapalestina "kusalia imara na kuwepo kwenye ardhi yao" huku kukiwa na hofu ya wengi kuhama makazi yao nchini Palestina.

Zaidi ya hayo, Misri pia ina wasiwasi kuhusu uwezekano wa wanamgambo wa Kiislamu kuingia nchini humo, baada ya kukabiliwa na waasi wa kijihadi huko Sinai kwa takriban muongo mmoja.

Nani anapeleka msaada Gaza?

tt

Chanzo cha picha, EPA

Umoja wa Mataifa umepeleka takriban tani 3,000 za misaada katika kivuko cha Rafah. Chini ya kilomita 1 kutoka mpakani, gunia za chakula, mafuta, maji na dawa zinangoja kuruhusiwa kuingia Gaza.

Phillippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Kazi (UNRWA) alionya "janga la kibinadamu ambalo halijawahi kutokea linawakodolea macho" na bila njia salama ya kufikisha misaada, vifaa vya msingi vitaisha.

Kufuatia ombi la dharura la msaada kutoka kwa mashirika ya World Food Bank, Shirika la Afya Duniani na UNICEF, Shirika la Kimataifa la Misaada ya Kibinadamu, lenye makao yake Dubai, lilizindua mpango wa kupeleka vifaa muhimu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa El-Arish kaskazini mwa Misri.

Kufuatia hatua hiyo uwanja wa ndege umepokea msaada kutoka kwa chakula kilicho tayari kuliwa hadi glovu za mpira. Hizi zilipakiwa kwenye malori na kuendeshwa kilomita 45 (maili 28) hadi kwenye kivuko cha Rafah ambako wamekuwa wakingoja njia salama ya kuingia Gaza.

Juhudi za kidiplomasia zimekuwa zikiendelea kuomba njia ya misaada, ambapo Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak wote wamefanya ziara nchini Israel na kukutana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Makubaliano ya kuruhusu takriban lori 20 zinazobeba chakula, maji na vifaa vya matibabu yamefikiwa na huenda zikaruhusiwa kuingia Gaza wakati wowote.

Yatahitaji kukaguliwa na kuongozwa na Umoja wa Mataifa kwa usaidizi wa Shirika la Red Crescent la Misri, shirika lingine la kutoa misaada kibinadamu, ili kuhakikisha hakuna chochote zaidi ya misaada kinachoingia Ukanda huo.

Wafanyakazi wa misaada walisema walikuwa wakisubiri upande wa Misri wa kivuko kwa siku kadhaa kupewa ruhusa ya kusambaza vifaa vya dharura.

Mohsen Sarhan kutoka Shirika la World Food Bank Chakula la Misri aliambia kipindi cha Radio 4 cha BBC kwamba kulikuwa na lori 120 za misaada zilizoegeshwa mpakani na "ndege saba au nane za mizigo zilizopakia vifaa kutoka Uturuki".

Alielezea kufadhaika kwake kwa kutoweza kusaidia na kuongeza: "Tuna hasira sana kwa sababu tunajua watu huko wameishiwa na maji, hata wameishiwa na mifuko ya kuhifadhi miili."