'Huwezi kuonyesha udhaifu' - kwa nini viongozi wa Afrika wanadumisha usiri kuhusu afya zao?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Danai Nesta Kupemba

BBC News

TH

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais wa Cameroon Paul Biya amekuwa madarakani tangu 1982

Uvumi wa afya mbaya umewakumba marais wawili wa Afrika katika wiki za hivi karibuni, na kuzua majibu tofauti na kufichua jinsi hali ya kiafya ya viongozi mara nyingi huchukuliwa kama siri ya serikali.

Ilianza na Rais wa Cameroon Paul Biya, 91, ambaye mawaziri wake walikanusha kuwa ni mgonjwa, wakisisitiza kuwa yuko katika "hali bora ya afya". Hata hivyo, vyombo vya habari nchini Cameroon vilipigwa marufuku kuripoti hali yake.

Kisha, ikulu ya Malawi ilipinga uvumi kwamba Rais Lazarus Chakwera alikuwa mgonjwa kwa kutuma video za kiongozi huyo akikimbia na kufanya mazoezi katika mji mkuu, Lilongwe.

"Unapaswa kuakisi aina fulani ya mtu kutawala katika siasa - huwezi kuonyesha udhaifu " anasema profesa mshiriki wa Chuo Kikuu cha Oxford katika siasa za Afrika, Miles Tendi, kuhusu mbwembwe na usiri unaowazunguka viongozi wa Afrika na afya zao.

Chakwera na Biya walitumia mbinu tofauti sana kukabiliana na uvumi kuhusu magonjwa, lakini walikuwa na nia sawa - kutayarisha, na kulinda, taswira ya nguvu na uanaume.

Lakini labda muhimu zaidi, kuwazuia wapinzani na wanaoweza kutumia vibaya fursa ya afya zao kudhoofika.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Prof Tendi anasema kuwa mchezo wa siasa ni "utendaji wa kiume" ambao unahitaji kufanywa ili kudumisha mamlaka.

Anaongeza kuwa tabia ya kiume ya siasa hufanya iwe vigumu sana kwa wanawake kufanikiwa. Hivi sasa kuna rais mmoja tu mwanamke wa nchi barani Afrika, Samia Suluhu Hassan nchini Tanzania , na alirithi madaraka kama naibu kiongozi wakati bosi wake wa kiume alipofariki.

Viongozi wa kisiasa, barani Afrika na kwingineko, wanatarajiwa kuwa alama za nguvu na uthabiti.

Kwa hivyo, hasa wakati kiongozi anapozeeka, afya yao inakuwa jambo nyeti sana la umuhimu mkubwa wa kitaifa, kama tulivyoona katika uchaguzi wa Marekani mwaka huu.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Johannesburg Adekeye Adebajo alisema viongozi katika bara "wanatoa hisia kwamba afya ya nchi zao inafungamana na afya zao binafsi", na kile kinachomsumbua kiongozi mara nyingi huchukuliwa kama siri ya serikali.

Ikiwa kitu kitawatokea, kinaweza kuathiri uchumi, masoko na kubadilisha hali ya kisiasa, mtaalam wa usalama kutoka Zimbabwe aliiambia BBC, na hii ndiyo sababu tahadhari za ziada zinachukuliwa.

Katika nchi ambazo taasisi za kisiasa ni dhaifu, taratibu za urithi wa kisiasa mara nyingi hazijawekwa vizuri, na hivyo kusababisha hofu kwamba ombwe lolote la uongozi linaweza kusababisha kugombania madaraka.

Zaidi ya miongo miwili iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Laurent-Désiré Kabila aliuawa na mmoja wa walinzi wake.

Mamlaka ilikataa kukiri kwamba aliuawa, na kuendelezadhana kwamba alipelekwa Zimbabwe kwa matibabu, huku wakipanga nini cha kufanya baadaye.

Kwa hakika, ilikuwa ni maiti yake ambayo ilisafirishwa kwa ndege kuvuka bara zima hadi upande wa pili kwa shangwe kubwa.

Mwanawe asiye na uzoefu, Joseph, hatimaye alichaguliwa kuwa kiongozi anayefuata wa nchi.

Nchini Malawi, serikali ilichelewesha kutangaza kifo cha Rais Bingu wa Mutharika mwaka 2012, na hivyo kuzua tetesi kwamba kulikuwa na jitihada za kumzuia k Makamu wake Joyce Banda kumrithi .

Lakini katika nchi jirani ya Zambia, ambako marais wawili wamefariki wakiwa madarakani, na nchini Ghana, ambako Rais wa wakati huo John Atta Mills alifariki mwaka 2012, mchakato wa katiba ulifanya kazi vizuri.

Kwa miaka mingi, viongozi mbalimbali wa Kiafrika wamekutana na maswali kuhusu afya zao mbaya kwa ukimya au hasira.

Mnamo mwaka wa 2010, kiongozi wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe alikashifu uvumi wa miaka mingi kama "uongo uliotungwa na vyombo vya habari vinavyotumiwa na nchi za Magharibi".

Miaka mitatu iliyopita, tangazo kwamba Rais wa Tanzania John Magufuli amefariki lilikuja baada ya wiki kadhaa za kukanusha kuwa alikuwa mgonjwa. Watu walikamatwa hata kwa kueneza habari za uwongo kuhusu afya yake, ili tu wao kuthibitishwa kuwa sahihi baadaye.

Unaweza Pia Kusoma
TH

Chanzo cha picha, Lazaro Chakwera/Facebook

Maelezo ya picha, Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, 69, alitoa picha zake akipiga mazoezi ya push-ups ili kuwahakikishia umma kuwa hakuwa mgonjwa.

Moja ya kesi kali zaidi za serikali kuficha afya ya kiongozi wake ilikuwa Nigeria, ambapo Rais Umaru Yar'Adua hakuonekana hadharani kwa miezi mitano.

Ofisi yake ilisema alikuwa akipokea matibabu Januari 2010 na kwamba alikuwa "anaendelea vizuri" hata hivyo, kulikuwa na ripoti nyingi zinazosema "ubongo wake ulikuwa umekufa".

Yar'Adua hakuonekana tena hadharani, na kifo chake kilitangazwa Mei mwaka huo.

"Baadhi ya watu hawa wanataka tu kung'ang'ania mamlaka," alisema Prof Tendi, hata hadi mwisho kabisa .

Viongozi wengi, nje ya Afrika pia, hawafikiri kwamba raia wao wana haki ya kujua kuhusu afya zao, ambayo inachukuliwa kuwa ya siri sana.

Lakini kumekuwa na tofauti.

Baada ya wiki saba za likizo rasmi ya matibabu mnamo 2017, Rais Buhari wa Nigeria alifichulia taifa lake kwamba hajawahi kuwa "mgonjwa" kiasi hicho maishani mwake, ingawa hakusema alikuwa akiugua nini.

Rais wa zamani wa Cameroon Ahmadou Ahidjo anaaminika kuwa kiongozi pekee wa Afrika kujiuzulu kutokana na afya mbaya, mwaka 1982, baada ya kutawala kwa miaka 22.

Aina hii ya uwazi na kuachia madaraka ni nadra. Zaidi ya viongozi 20 wa Afrika wamefariki wakiwa ofisini, baadhi yao bila kuiambia nchi yao kuwa walikuwa wagonjwa.

Mfano huo haujachukuliwa na mrithi wa Ahidjo, Paul Biya.

Viongozi wanaweza kuhofia kuwa kufichua masuala ya afya kunaweza kuwatia moyo wapinzani wao au hata mataifa ya kigeni yanayotaka kushawishi au kuyumbisha nchi.

Baadhi ya marais wamepinduliwa baada ya habari za afya zao kutangazwa.

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Zaire, sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Mobutu Sese Seko aliondolewa madarakani baada ya kulazwa hospitalini.

Mnamo 1996, ilijulikana kwa umma kwamba kiongozi wa kiimla wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo) Mobutu Sese Seko, alikuwa akipokea matibabu ya saratani ya kibofu.

Hili bila shaka lilifanya iwe rahisi zaidi kwa Laurent Kabila kuongoza kundi la waasi wanaoungwa mkono na Rwanda katika nchi nzima.

Mobutu alikuwa mgonjwa sana kutoweza kuratibu upinzani wowote, na alikimbilia uhamishoni Morocco, akimuacha Kabila kunyakua madaraka.

"Ikiwa unaonekana kuwa dhaifu, ni ishara kwa wapinzani wako wa ndani," Prof Tendi alisema.

Lakini mkulima na mwalimu wa Nigeria, Abeku Adams, 41, ambaye amepitia marais wawili kufariki wakiwa madarakani, alisema usiri huo unaweza pia kuwa "jambo la kitamaduni".

“Kuwa msiri kuhusu afya ya mtu ni jambo linalochukuliwa kuwa sehemu ya mchakato wa uponyaji katika tamaduni nyingi za Kiafrika. Hiki kinaweza kuwa chanzo cha kwa nini wanaficha au kusema uwongo kuhusu afya zao,” alisema.

Wakati raia wa kibinafsi wana haki ya kuweka rekodi zao za matibabu kuwa siri, inasemekana kuwa viongozi wa kisiasa hawana fursa hii kwa sababu afya zao zinaweza kuwa na athari kwa nchi nzima.

Wakati nchi nyingi za Kiafrika zikiweka taratibu thabiti za urithi, kuna wito wa kuwepo kwa uwazi zaidi linapokuja suala la afya ya viongozi wao, hasa kutoka kwa idadi ya vijana inayozidi kuongezeka barani humo.

"Serikali zina deni kwa raia wao kutoa habari kama hizo," alisema Bw Adams.

Anasisitiza kuwa kwa sababu wananchi wanalipa kodi, wanapaswa kujua afya za viongozi wao.

Huenda ikawa kwamba mfumo wa kisiasa wenye ushindani mkubwa wa Malawi, huku uchaguzi ukitarajiwa mwaka ujao, ndio uliomsukuma Chakwera kufanya mazoezi yake ya hadharani - kuonyesha yuko 'fiti' zaidi kuliko mpinzani wake mkuu, Peter Mutharika, anayemzidi umri kwa miaka 15 .

Kinyume chake, Biya anakabiliwa na tishio dogo kutokana na chaguzi - tayari ameshinda mara tano, licha ya malalamiko ya upinzani ya kuibiwa kwa kura.

Katika demokrasia ya kweli, afya ya kiongozi inapaswa kuwa wazi, mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa aliambia BBC.

Lakini hali ya siasa katika sehemu kubwa ya Afrika, ambako vyama tawala mara nyingi vinashutumiwa kwa wizi wa kura, mapinduzi ya kijeshi siku zote ni tishio na hata urais wa kuchaguliwa unaweza kuwa wa kurithi, uwazi si utaratibu ambao viongozi wengi wanaonekana kuwa tayari kuutekeleza hivi karibuni.

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Seif Abdalla