Mambo matano yaliyomuondoa Rigathi Gachagua madarakani

Chanzo cha picha, LIVE EVENT
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Maseneta wa Kenya walipiga kura ya kumuondoa Naibu Rais Rigathi Gachagua afisini licha ya yeye kutokuwepo katika bunge hilo.
Gachagua aliugua ghafla na kupelekwa hospitalini jijini Nairobi ambapo anaendelea kupata matibabu.
Gachagua alikuwa amekana mashtaka 11 ya "ukiukaji mkubwa" wa katiba siku iliyotangulia.
Kwa mujibu wa bunge la seneti kiongozi huyo alipatikana na hatia kwa tuhuma za "ukiukaji mkubwa" wa katiba, ikiwa ni pamoja na kutishia majaji na kufanya siasa za migawanyiko ya kikabila, lakini akafutiwa mashtaka mengine yakiwemo ufisadi na utakatishaji fedha.
Saa chache baadaye siku ya Ijumaa, Rais William Ruto alimteua Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki kuchukua nafasi yake.
Yafuatayo ni mambo matano yaliomuondoa madarakani aliyekuwa naibu wa Rais Rigathi Gachagua:
Shutuma dhidi ya huduma ya kitaifa ya Ujasusi NIS
Akihutubia kikao na wanahabari mjini Mombasa Naibu Rais Rigathi Gachagua alimshutumu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), Noordin Haji, kwa kukosa kumshauri ipasavyo rais kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ulisababisha machafuko na kupotea kwa maisha jijini Nairobi na maeneo mengine ya nchi.
"Lazima awajibike kwa taifa la Kenya kwa kutofanya kazi yake na kushauri ipasavyo," Gachagua alisema. "Lazima afanye jambo la heshima na ajiuzulu kutoka ofisi hiyo."
Alisema kuwa maisha na mali zingeokolewa ikiwa NIS ingemfahamisha rais miezi miwili iliyopita kuhusu jinsi Wakenya walivyohisi kuhusu Mswada tata wa Fedha wa 2024.
Naibu huyo wa rais alimtaja Haji kama asiye na uwezo na mdhaifu, huku akimshutumu kwa kujaribu kuelekeza lawama.
"Noordin Haji alikuwa akijaribu kuunda timu ya kubuni uwongo na propaganda, akihusisha machafuko kwangu na Rais wa zamani Uhuru Kenyatta," alisema 'Riggy G'.
Kuhujumu Idara ya Mahakama
Mashambulizi ya hadharani ya aliyekuwa naibu wa Rais Rigathi Gachagua dhidi ya jaji wa Mahakama ya Juu Esther Maina yaliibua msukosuko mpya wa mashambulio yanayofanywa na viongozi wa serikali katika idara ya mahakama.
Mahakama ya Juu hatimaye ilitoa uamuzi wake kuhusu kesi ya ufisadi wa ksh. 200m ambayo ilikuwa ikimkabili Gachagua kabla ya kampoeni za uchaguzi wa 2022.
Katika Uamuzi wake Jaji aliamua kwamba Gachagua alipaswa kuziachia serikali fedha hizo ambazo alidaiwa kuzipata kwa njia ya ufisadi .
Na alipokuwa akihutubia umma Naibu Rais alisema atawasilisha ombi lake binafsi mbele ya Jaji Mkuu Bi Martha Koome kumpinga Jaji huyo ili aondolewa katika idara hiyo ya mahakama kwa utovu wa nidhamu na ufisadi.
Kesi hiyo iliokuwa inamkabili Gachagua ilikuwa miongoni mwa kesi zilizoondolewa na Rais punde tu baada ya Viongozi hao wawili kuchukua mamlaka.
Uhalifu katika uwiano na uadilifu wa kitaifa
Pia kulikuwa na imani kwamba aliyekuwa naibu wa Rais Rigathi Gachagua alitekeleza uhalifu dhidi ya sheria ya uwiano na uadilifu wa kitaifa.
Sheria hiyo inasema kwamba ni kinyume na sheria kwa mtu yeyote kutumia matamshi ya vitisho na ya unyanyasaji au kuonesha tabia kama hiyo kutamka maneno ya kutaka kuzua hofu miongoni mwa makabila, kusababisha uadui au ubaguzi.
Matamshi ya mara kwa mara yenye chuki ya kiongozi huyo hadharani katika kipindi cha miaka miwili iliopita yalimfanya aonekane kufanya uhalifu chini ya sheria hiyo.
Kwenda kinyume na kiapo cha utiifu alichokula
Naibu Rais alidaiwa kukiuka kiapo chake alichokula na uaminifu kwa sababu ya matamshi yake ya umma na hatua zake.
''Kiapo cha afisi ya naibu rais kinamkataza kiongozi huyo kufichua mambo hasa yanayohusu usalama wa taifa. Ni ukiukaji wa kiapo chake cha ofisi na katiba kujadili mambo ya aina hiyo hadharani", alisema wakili wa bunge la kitaifa, Muthomi Thiankolu.
Kulingana na na shataka hilo hatua ya kiongozi huyo kushtumu shirika la Ujasusi nchini ni kinyume na kiapo alichokula wakati akiapishwa kua naibu wa rais.
Wakili Thainkolu anasema kwamba kiongozi huyo 'alimwaga mtama mbele ya kuku wengi' jambo ambalo ni kinyume na kiapo hicho.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukiukaji wa masharti ya katiba
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tuhuma hizo zinatokana na madai ya ukiukwaji mkubwa wa vifungu vya Katiba, vya Ibara ya 10, 27, 73, 75, 129, 147, na 152 vinavyotoa masharti ya Uongozi wa Taifa na vifungu vinavyosimamia uadilifu wa uongozi.
Naibu Rais anashutumiwa kwa kuhujumu mamlaka ya Rais na Baraza la Mawaziri na kuvuruga serikali ya kitaifa kutekeleza majukumu yake. Zaidi ya hayo, Hoja hiyo inadai kuwa Gachagua alikiuka Kifungu cha 147, ambacho kinaainisha majukumu na wajibu wa Naibu Rais kwa kujihusisha na shughuli zilizotatiza utendakazi wa Baraza la Mawaziri na shughuli za serikali.
Gachagua anashtakiwa zaidi kwa kuhujumu ugatuzi, nguzo kuu ya muundo wa utawala wa Kenya, kwa kukiuka Vifungu 6, 10, 174, 186, na 189 vya Katiba vinavyoelezea uhusiano kati ya Serikali ya Kitaifa na Serikali za Kaunti. Gachagua anadaiwa kuvuka mamlaka yake kwa kuingilia maswala ya Serikali za Kaunti, haswa Nairobi, ambapo kuhusika kwake katika uhamishaji wa soko na ukosoaji wa sera za udhibiti wa pombe ilizua mvutano.















