Mwili wa Mtanzania aliyeuawa na Hamas wazikwa baada ya miaka miwili
Maziko yake yamefanyika Simanjiro, Manjara na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, dini, wananchi wa maeneo mbalimbali pamoja na mwakilishi wa ubalozi wa Israel kwa nchini Tanzania na Kenya.
Muhtasari
- Shule zafungwa katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria
- Ruto: "Lazima tuondokane na mawazo ya kuridhika na kawaida"
- Jeshi la Sudan lakaribisha juhudi za Marekani-Saudia kumaliza vita
- BBC yathibitisha taarifa zinazosambaa mtandaoni
- Trump atangaza kuwa Marekani itajitahidi kumaliza vita nchini Sudan
- Mashambulizi ya Israel Gaza yaua Wapalestina 25, wizara ya afya yasema
- Mwili wa Mwalimu Mkenya aliyeuawa Tanzania haujapatikana, huku wakenya wawili wakishikiliwa Tanzania
- Clement Mzize wa Yanga atangazwa mshindi wa goli bora la mwaka CAF 2025
- Marais wa Afrika Mashariki wapongezwa na CAF kwa mchango wao kwenye michezo
- Ufilipino yamhukumu 'meya jasusi wa China' kifungo cha maisha jela
- Maafisa wa jeshi la Marekani wako Ukraine kwa mazungumzo ya kumaliza vita
- Trump asaini muswada unaoamuru wizara ya sheria kutoa nyaraka za Epstein
Moja kwa moja
Na Lizzy Masinga
Shule nchini Nigeria zafungwa katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria

Chanzo cha picha, Reuters
Mamlaka nchini Nigeria imefunga shule katika sehemu za jimbo la kaskazini mwa Kwara baada ya shambulio la hivi karibuni la kanisa na watu wenye bunduki.
Nchi inaendelea kukabiliwa na changamoto za usalama huku kukiwa na madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba Wakristo wanateswa.
Kamishna wa Serikali ya Jimbo la Kwara, Lawal Olohungbebe, alisema kufunga shule ni hatua ya usalama ya kuzuia wateka nyara kutumia watoto wa shule kama ngao.
Alisema shule zimefungwa hadi mwongozo zaidi wa usalama utakapotolewa.
Watu wenye silaha, wanaojulikana kama majambazi huwa wanatekeleza utekaji nyara wa shule na kudai ruzuku kubwa nchini Nigeria.
Siku ya Jumatatu, wasichana wa shule 25 walitekwa nyara kutoka shule ya bweni kaskazini magharibi mwa Jimbo la Kebbi.
Shambulio la kanisa hilo siku ya Jumanne lilisababisha vifo vya waumini wawili huku wengine kadhaa wakitekwa nyara na watu wenye bunduki.
Ruto: "Lazima tuondokane na mawazo ya kuridhika na kawaida"

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais William Ruto leo amehutubia taifa na kusema kuwa Kenya imepata "maendeleo ya kupigiwa mfano" katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita lakini bado iko "chini ya uwezo wake," na kuitaka nchi hiyo kuachana na kile alichokiita utamaduni wa "mawazo madogo na matarajio ya kawaida."
Akitoa hotuba ya kitaifa Bungeni leo Alhamisi, Ruto alisema anaondokana na “maono ya kuuza” hadi “hadithi ya kusimulia,” akitafakari safari ya Kenya ya miaka 62 ya “mapambano, changamoto, ushindi na hatua muhimu,” ilizopiga.
Rais alitoa wito wa kuwa na mtazamo mpya wa kitaifa unaozingatia matamanio na ujasiri, akisema ni wakati wa kusonga mbele zaidi ya kawaida iliozoeleka.
"Lazima tuondokane na mawazo ya kuridhika na kawaida"," aliwaambia wabunge.
"Lazima tuondokane na tulichozoea na cha kawaida na kufikia kwa ujasiri, uwazi na usadiki wa kilicho bora zaidi."
Ruto alikiri misukosuko ya miaka mitatu iliyopita, iliyoghubikwa na mizozo ya kisiasa, maelewano, na kile alichotaja kuwa "dhoruba ambazo hakuna hata mmoja wetu aliyezitarajia." Alisema, pamoja na matatizo hayo, nchi imeweka misingi ya kujikwamua kiuchumi.
"Miaka mitatu iliyopita haikuwa rahisi," alisema.
Ruto alionyesha taswira ya uchumi aliorithi mnamo mwaka 2022, akisema Kenya ilikuwa "katika matatizo," na mfumko wa bei, shilingi dhaifu, na akiba ya fedha za kigeni ikiwa kiwango cha chini zaidi katika historia.
"Mwaka 2022, mfumuko wa bei uliongezeka. Shilingi ilikuwa inaanguka kuendelea na akiba ya fedha za kigeni ikipungua katika kiwango kilichoweka historia," alisema.
Rais aliongeza kuwa utawala wake ulichukua "maamuzi ya ujasiri na wakati mwingine magumu," ikiwa ni pamoja na kukomesha kile alichokiita ‘ruzuku isio na msingi’ na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Mwili wa Mtanzania aliyeuawa na Hamas wazikwa baada ya miaka miwili

Mtanzania Joshua Loitu Mollel ameagwa na kuzikwa leo katika Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, baada ya mabaki ya mwili wake kurejeshwa kutoka Israel kufuatia mauaji ya Oktoba 7, 2023.
Maziko hayo yalihudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wananchi wa maeneo mbalimbali pamoja na mwakilishi wa ubalozi wa Israel nchini. Familia yake, ndugu na jamaa walijitokeza kwa wingi kumuaga kijana huyo aliyekwenda Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo.
Mwili wa Joshua uliwasili nchini jana, Novemba 20, 2025, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambapo ulipokelewa na familia pamoja na maafisa wa serikali. Kabla ya kusafirishwa kutoka Israel, ubalozi wa Tanzania nchini humo uliandaa ibada maalum ya kumuaga katika mnara wa kumbukumbu wa Tel Aviv.
Joshua alikuwa nchini Israel kwa karibu wiki tatu tu kabla ya kushambuliwa na kuuawa katika kibbutz cha Nahal Oz, eneo la kusini mwa Israel. Alikuwa akifanya mafunzo kwa vitendo katika shamba la kijiji hicho aliposhambuliwa na wanamgambo wa Hamas tarehe 7 Oktoba 2023. Mwili wake ulitekwa na washambuliaji hao na kupelekwa Gaza.

Serikali ya Israel ilithibitisha kurejeshwa kwa mabaki ya mwili wake mnamo Novemba 19, 2025, chini ya makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyosimamiwa na Marekani. Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu katika kituo cha kitaifa cha uchunguzi wa vinasaba, familia iliithibitishiwa rasmi kuwa mabaki hayo ni ya Joshua.
Katika makubaliano hayo, Hamas ilirejesha miili ya mateka 19 wa Israel pamoja na miili ya raia watatu wa kigeni, raia mmoja wa Thailand, mmoja wa Nepal, na Joshua kutoka Tanzania, wakati Israel ikikabidhi miili ya Wapalestina 285. Hadi sasa, miili ya mateka sita, Waisraeli watano na raia mmoja wa Thailand inaendelea kushikiliwa Gaza.
Maziko ya Joshua Simanjiro yamehitimisha safari ndefu na yenye uchungu kwa familia yake, ambayo kwa miaka miwili imekuwa ikisubiri uthibitisho na hatimaye kurejeshwa kwa mabaki ya mpendwa wao.

Maelezo ya picha, Sehemu ya waombolezaji waliofika kumzika Joshua, Simanjiro Jeshi la Sudan lakaribisha juhudi za Marekani-Saudia kumaliza vita
Serikali inayoongozwa na jeshi la Sudan imesema iko tayari kwa juhudi mpya za Marekani na Saudi Arabia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Rais Trump aliahidi Jumatano kusaidia kutatua mzozo huo baada ya ombi kutoka kwa kiongozi wa Saudia, Mohammed bin Salman.
Uongozi wa kijeshi wa Sudan unasema inaunga mkono juhudi za kufikia "haki na amani" na iko tayari kutoa ushirikiano ili kusonga mbele.
Hapo awali ilitupilia mbali juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Marekani kwa sababu ya kuhusika kwa nchi ya Falme za Kiarabu - ambayo inaishutumu kwa kuwasaidia wapinzani wake, Rapid Support Forces.
Mabadiliko hayo yametokea saa kadhaa baada ya Rais Trump kutangaza mpango mpya wa Marekani juu ya Sudan baada ya kile alichosema ni takwa la moja kwa moja kutoka kwa kiongozi wa Saudia.
Akiandika kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema kuwa viongozi wa Kiarabu walimsihi kukomesha kile alichokiita "ukatili mkubwa" nchini humo.
Pia unaweza kusoma:
BBC yathibitisha taarifa zinazosambaa mtandaoni

Chanzo cha picha, Telegram
Tunachunguza ripoti kuwa kiwanda cha kusafisha mafuta kinawaka moto huko Ryazan, jiji lililo umbali wa maili 110 (km 180) kusini-mashariki mwa mji mkuu wa Urusi Moscow.
Ni mtambo huo ambao ulishambuliwa na Ukraine wikendi iliyopita na kulazimika kusimamisha shughuli zake. Gavana wa mkoa wa Ryazan ameripoti kuwa ndege zisizo na rubani zilidunguliwa usiku kucha, akisema vifusi vya ndege moja vilisababisha moto kuzuka katika biashara moja.
Picha zinazoonyesha moto katika kituo cha kemikali ya petroli nchini Venezuela Jumatano zinashirikishwa mtandaoni jambo ambalo tunathibitisha. Kwa mujibu wa Reuters, mlipuko ulisikika kabla ya moto huo. Inaarifiwa kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa na bado haijafahamika ni nini kilisababisha tukio hilo.
Na tumekuwa tukichunguza kwa nini Grok chatbot ya AI imekuwa akiwaambia watumiaji wa mtandao wa kijamii wa X kwamba Rais wa Marekani Donald Trump hakusema "nyamaza nguruwe" kwa ripota. Grok imekuwa ikisema uwongo kwamba Trump alisema "nyamaza, nguruwe" - lakini kuna sababu kwa nini huo si kweli.
Tutakuletea mengi zaidi kutoka kwa timu ya BBC fact-checkers, wataalamu wa uthibitishaji na wanahabari wanaotumia data.
Pia unaweza kusoma:
Mashambulizi ya Israel Gaza yaua Wapalestina 25, wizara ya afya yasema

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Takriban Wapalestina 25 wameuawa katika mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza siku ya Jumatano, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas imesema, katika siku ambayo ilikuwa mbaya zaidi tangu usitishaji mapigano uanze kutekelezwa wiki tano zilizopita.
Watu kumi waliuawa wakati jengo la wizara ya karama za kidini katika kitongoji cha Zeitoun mashariki mwa Gaza liliposhambuliwa, kulingana na waokoaji.
Jeshi la Israel limesema lilishambulia "maeneo lengwa ya kigaidi ya Hamas" baada ya watu wenye silaha kufyatua risasi kuelekea eneo ambalo wanajeshi wake walikuwa wakiendesha shughuli zao katika mji wa kusini wa Khan Younis kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hamas ilitilia shaka madai hayo na kushutumu kile ilichosema ni "ongezeko la hatari" ambalo linaweza kuhatarisha usitishaji mapigano.
Kuongezeka kwa ghasia hizo kumetokea baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio lililoidhinisha mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump wa Gaza kumaliza miaka miwili ya vita vikali.
Soma zaidi:
Trump atangaza kuwa Marekani itajitahidi kumaliza vita nchini Sudan

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
Rais Donald Trump amesema Jumatano tarehe 19/11/2025, kwamba Marekani itaanza mara moja juhudi mpya za kumaliza mzozo nchini Sudan, akisema alikuwa akitekeleza matakwa ya Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman, ambaye alikutana naye katika Ikulu ya White House siku ya Jumanne.
"Mkuu angependa nifanye jambo kubwa sana kuhusiana na Sudan. Haikuwa kwenye ratiba zangu kuhusika katika hilo," Trump alisema wakati wa hotuba yake katika Jukwaa la Uwekezaji la Marekani na Saudia katika Kituo cha Kennedy ambapo MBS, kama anavyojulikana, alikuwepo.
Sudan imekuwa katika vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe tangu 2023. Vita hivyo vilizuka kati ya jeshi la taifa hilo, Jeshi la Sudan (SAF), na kundi lenye nguvu la kijeshi, Rapid Support Forces (RSF).
Kundi la mataifa, likiongozwa na Marekani, liliweka suluhu ambayo RSF ilikubali mapema mwezi Novemba. Karibu wakati huo, balozi wa Sudan nchini Marekani Mohamed Abdalla Idris, alisema kwamba "wanathamini mapendekezo ya Marekani, na serikali inayofuatilia."
Tangazo la Trump linaashiria kwamba utawala wake, na pengine hata rais binafsi, angefanya juhudi upya kumaliza mzozo huo.
Soma zaidi:
Mwili wa Mwalimu Mkenya aliyeuawa Tanzania haujapatikana, huku wakenya wawili wakishikiliwa Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkuu wa mawaziri wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema kuwa mwili wa Mwalimu John Ogutu, ambaye ripoti zinasema aliuawa wakati wa maandamano Tanzania alikokuwa akifanya kazi, bado haujapatikana.
Hata hivyo amebainisha kuwa ameandika barua mbili kwa mwenzake wa Tanzania.
Aliongeza kuwa jitihada za kutafuta mwili katika hospitali na makafani ya serikali nchini Tanzania hazijazaa matunda.
Akizungumza mbele ya Bunge la Kitaifa katika kikao cha Maswali na Majibu siku ya Jumatano ya Novemba 19,2025, Mudavadi amefichua kuwa Wakenya wawili bado wako mikononi mwa mamlaka za Tanzania kufuatia vurugu zilizoibuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Aliongeza kuwa serikali inaendelea kutoa msaada unaohitajika ili kuwezesha kuachiliwa kwa Wakenya hao wawili.
Vile vile, alithibitisha kuwa Wakenya wengine wote waliokamatwa tayari wameachiliwa baada ya uingiliaji wa serikali.
Aidha, alibainisha kuwa maandamano hayo hayakuwa na athari kubwa kwa biashara za Wakenya ndani ya Tanzania. “Hadi sasa, na kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa kutoka kwa ujumbe wa Kenya katika Arusha na Dar es Salaam, kifo kimoja cha raia wa Kenya kilithibitishwa kuhusiana na vurugu za Oktoba 29, 2025,” alisema Mudavadi.
'' Bw. John Ogutu, mwalimu wa Shule ya Sky wilayani Kinondoni, alipigwa risasi hadi kufa majira ya saa 1 jioni (7p.m.) tarehe 29 Oktoba 2025.” Aidha, Mkuu wa Mawaziri ambaye anashughulikia masuala ya mambo ya kigeni ya Kenya, Mudavadi alifichua kuwa rejista rasmi zinaonyesha kuwa Wakenya takribani 5,503 wanaishi Tanzania, jambo linaloashiria ukuaji wa wafanyakazi kati ya mataifa haya mawili.
Vurugu hizo zimemulikwa na wadau wa ndani na kimataifa kufuatia waangalizi wa uchaguzi kusema mchakato mzima ulikuwa na dosari na kutaka uchunguzi ufanyike kufuatia maandamano ya vurugu.
Kwamujibu wa rekodi za mahakama ya Tanzania, takribani vijana 400 walikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la uhaini wakati wa maandamano hayo.
Unaweza kusoma;
Clement Mzize wa Yanga atangazwa mshindi wa goli bora la mwaka CAF 2025

Chanzo cha picha, Yanga
Mshambuliaji wa Yanga SC, Clement Mzize, ameshinda tuzo ya Goli Bora la Mwaka (CAF Goal of the Season 2025) katika Tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) 2025.
Mzize alithibitisha ubora wake baada ya kufunga goli la shuti la mbali wakati wa mchezo dhidi ya TP Mazembe, katika hatua ya makundi ya Michuano ya Klabu Bingwa Afrika msimu uliopita.
Goli hilo limechaguliwa kuwa bora zaidi kutokana na ubora wa kiufundi, ufanisi na umuhimu wake katika michezo ya mashindano ya klabu bingwa barani Afrika, na limeipa Mzize heshima kubwa katika soka la kikanda.
Marais wa Afrika Mashariki wapongezwa na CAF kwa mchango wao kwenye michezo

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wametunukiwa Tuzo za Heshima na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya michezo barani Afrika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Samia, katika hafla ya utoaji tuzo za CAF iliyofanyika mjini Rabat, Morocco.
Pia, Rais wa Kenya, William Ruto, pamoja na Marais Samia na Museveni, walikabidhiwa tuzo maalumu za ufanisi na Rais wa CAF, kutokana na kuandaa kwa mafanikio Mashindano ya CHAN 2024, yaliyohusisha nchi zao kama wenyeji wenza.
Tuzo hizi ni ishara ya kutambua mchango wa viongozi hao wa Afrika Mashariki katika kuendeleza soka na michezo barani Afrika, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya michezo.
Ufilipino yamhukumu 'meya jasusi wa China' kifungo cha maisha jela

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Meya wa zamani wa Ufilipino ambaye alishtakiwa kwa kuipeleleza China amepatikana na hatia ya biashara haramu ya binadamu kwa jukumu lake katika kuendesha kituo cha utapeli.
Siku ya Alhamisi, yeye na wengine watatu walihukumiwa kifungo cha maisha jela na faini ya peso milioni 2 ($33,832).
Kesi ya Alice Guo imeikumba Ufilipino kwa miaka mingi, baada ya mamlaka kugundua moja ya vituo vikubwa vya utapeli nchini humo katika mji wake mdogo wa Bamban.
Wafilipino na wageni wapatao 800 baadaye waliokolewa kutoka kwenye kituo cha utapeli baada ya uvamizi, huku wengi wao wakisema walilazimishwa kuendesha utapeli wa "uchinjaji wa nguruwe".
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 35, ambaye alikamatwa mwaka jana baada ya kutoroka kwa wiki kadhaa, amekanusha madai yote dhidi yake.
Bado haijabainika kama anaweza kukata rufaa. Bado kuna kesi tano zinazoendelea dhidi ya Guo, ikiwemo moja ambapo ameshtakiwa kwa utakatishaji fedha.
Unaweza kusoma;
Maafisa wa jeshi la Marekani wako Ukraine kwa mazungumzo ya kumaliza vita

Chanzo cha picha, Reuters
Maafisa wakuu wa Pentagon wamewasili Ukraine "kujadili juhudi za kukomesha vita" na Urusi, jeshi la Marekani limesema.
Timu hiyo, ikiongozwa na Waziri wa Jeshi la Marekani Dan Driscoll, inatarajiwa kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky huko Kyiv siku ya Alhamisi atakaporejea kutoka ziarani Uturuki.
Ripoti zilianza kujitokeza Jumatano kwamba Marekani na Urusi zilikuwa zimeandaa mpango mpya wa amani, wenye makubaliano makubwa kutoka Ukraine.
Si Washington wala Moscow waliothibitisha rasmi mpango huo.
Mapema siku hiyo, takribani watu 26 waliuawa katika shambulio la kombora la Urusi na ndege zisizo na rubani katika mji wa Ternopil magharibi mwa Ukraine, maafisa walisema.
Urusi ilianzisha uvamizi dhidi ya Ukraine mwaka wa 2022.
''Driscoll na timu walifika Kyiv asubuhi ya leo kwa niaba ya serikali katika ziara ya kukusanya taarifa ili kukutana na maafisa wa Ukraine na kujadili juhudi za kumaliza vita,” msemaji wa Jeshi Kanali David Butler alisema katika taarifa.
Driscoll ameandamana na Mkuu wa Majeshi ya Marekani Jenerali Randy George, kamanda mkuu wa jeshi la Marekani barani Ulaya Jenerali Chris Donahue, na Sajenti Mkuu wa Jeshi Michael Weimer.
Driscoll na Jenerali George ndio maafisa wa juu zaidi wa kijeshi wa Marekani kufanya mazungumzo katika mji mkuu wa Ukraine tangu Rais Donald Trump aingie madarakani Januari.
Picha iliyotolewa Jumatano ilionysha Driscoll akikutana na kushikana mkono na Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Denys Shmyhal.
Trump asaini muswada unaoamuru wizara ya sheria kutoa nyaraka za Epstein

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza Jumatano kwamba alisaini muswada unaoagiza kutolewa kwa nyaraka zote zinazomhusu marehemu Jeffrey Epstein.
Muswada huo unaitaka wizara ya sheria kutoa taarifa zote kutoka kwa uchunguzi dhidi ya Epstein "katika muundo unaoweza kutafutwa na kupakuliwa" ndani ya siku 30.
Hapo awali Trump alipinga kutolewa kwa nyaraka hizo, lakini alibadilisha msimamo wiki iliyopita baada ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa waathirika wa na wanachama wa Chama chake cha Republican.
Katika chapisho kwenye Truth Social siku ya Jumatano, rais aliwashutumu Wademocrat kwa kutetea suala hilo ili kuvuruga umakini kwa mafanikio ya utawala wake.
"Labda ukweli kuhusu Wademocrat hawa, na uhusiano wao na Jeffrey Epstein, utafichuliwa hivi karibuni, kwa sababu NIMESAINI MUSWADA WA KUTOA NYARAKA ZA EPSTEIN!" aliandika.
Wabunge katika Baraza la Wawakilishi walipitisha muswada kwa kura 427-1.
Seneti ilitoa idhini ya kauli moja kuipitisha itakapofika. Takribani kurasa 20,000 za nyaraka kutoka kwa mali ya Epstein, ikiwa ni pamoja na baadhi zinazomtaja Trump moja kwa moja, zilitolewa wiki iliyopita.
Zinajumuisha jumbe za 2018 kutoka kwa Epstein ambapo alisema kuhusu Trump: "Mimi ndiye ninayeweza kumng'oa madarakani" na "Ninajua jinsi Donald alivyo mchafu".
Unaweza kusoma;
Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu
