United Front: Silaha ya ajabu ya China na tuhuma za ujasusi wa kimataifa

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa kiongozi muasisi wa Chama cha Kikomunisti, Mao Zedong, na kiongozi wa sasa, Xi Jinping, China ina 'silaha ya ajabu'.
Silaha hii inaitwa United Front Work Department (UFWD) na mataifa ya magharibi yana wasiwasi mwingi juu yake.
Yang Tengbo, ambaye pia amehusishwa na mwanamfalme Andrew wa familia ya kifalme nchini Uingereza,ni raia wa China ambaye amepigwa marufuku kwa kujihusisha na UFWD.
Uwepo wa idara hii sio siri tena.Uwepo wao umethibitishwa katika nyaraka za chama cha kikomunisti cha China kwa miongo kadhaa,na idara hiyo ya China imekuwa jambo tata katika siku zilizopita.
Wachunguzi kutoka Marekani hadi Australia wametaja UFWD katika visa vingi vya ujasusi na pia wameishutumu China kwa kuingilia masuala ya nchi nyingine.
China imekanusha madai haya yote na kuyataja kuwa ya kipuuzi.
Bila shaka, watu watakuwa na maswali katika fikra zao: DFWD ni nini na inafanya nini?
Je, 'DFWD' ni idara ya kijasusi?
The United Front'ilimaanisha umoja wa kikomunisti na ulielezewa na Mao Zedong kama 'ufunguo wa ushindi' wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini China.
Vita nchini China vilipoisha mwaka 1949, shughuli za United Front zilipungua na vipaumbele vya China vilibadilika.
Lakini katika muongo mmoja uliopita, United Front ulianza maisha mapya chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping.
Kwa mujibu wa Dk. Marieke Olberg, mshirika mkuu katika taasisi ya Marshall ya Ujerumani, wazo la Rais Xi Jinping la United Front linaendana na ilivyokuwa hapo awali: "kuunda muungano na nguvu zote za kijamii ambazo bado zina tija hivi leo.
Kwa upande mwingine, UFWD sio idara ya siri, lakini ina tovuti na inachapisha taarifa za shughuli zake. Lakini kazi na ushawishi wake bado haueleweki.
Kwa mujibu wa Dk. Olberg, sehemu kubwa ya shughuli za UFWD zinajumuisha kazi za ndani ya nchi, hata hivyo, "lengo lililotajwa kwa United Front ni kufuatilia raia wa China nje ya nchi.

Chanzo cha picha, Getty Image
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hii leo,UFWD inalenga kushawishi mijadala ya umma na mada hizi ni pamoja na masuala yanayohusiana na Taiwan, Tibet, na Xinjiang.
Moja ya malengo ya UFWD ni kushawishi masimulizi kuhusu China katika vyombo vya habari vya kigeni, kuwalenga wakosoaji wa serikali ya China, na kushawishi raia wa China wenye ushawishi nje ya nchi.
"Jukumu la United Front linaweza kujumuisha ujasusi, lakini ni zaidi ya ujasusi," anasema Audrey Wong, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Southern California.
Aliongeza kuwa "pamoja na kupata taarifa nyeti kutoka kwa serikali ya kigeni, shughuli za United Front zinalenga kuhamasisha raia wa China nje ya nchi kwa kiwango kikubwa.
China daima imekuwa na lengo la kupata ushawishi, lakini katika miongo ya hivi karibuni imeshuhudia ongezeko la juhudi za China kufikia lengo hili.
Xi Jinping alikua rais wa China mwaka 2012 na amekuwa na nia ya kueneza ujumbe wa China duniani tangu wakati huo. Amewataka Wachina wa ng'ambo "kusimulia mazuri ya China.
UFWD inafanya kazi kupitia mashirika mbalimbali nje ya nchi ambayo hapo awali yalitetea Chama cha Kikomunisti.
Mashirika haya hayakupuuza tu sanaa ya Chama cha Kikomunisti kinachopinga China bali pia yalipinga shughuli za Dalai Lama, kiongozi wa kidini wa Tibet.
Katika siku za nyuma, jina la AWF pia lilihusishwa na vitisho vilivyopokelewa na watu wa makabila madogo ya Tibet na Uyghur nje ya nchi.
Lakini shughuli ya UFWD mara nyingi inakinzana na mashirika mengine ya Chama cha Kikomunisti, na waangalizi wanasema hii inaipa China fursa ya 'kukataa' shughuli zake.
Shughuli za UFWD hapa ni chanzo cha mashaka na wasiwasi katika ulimwengu wa Magharibi.
Wakati Yang Tengbo alipokata rufaa dhidi ya vikwazo alivyowekewa, majaji walinukuu ripoti ya Marekani iliyomtaja kuwa "tishio kwa usalama wa taifa" na kusema kwamba Yang Tengbo alikuwa ameficha uhusiano wake na UFWD.
Hata hivyo, Yang Tengbo anasema hajawahi kufanya chochote kinyume cha sheria na madai ya ujasusi dhidi yake "ni ya uongo kabisa."
Kesi zinazolingana na za Yang Tengbo sasa zinaibuka mara kwa mara.
Mnamo 2022, shirika la ujasusi la Uingereza 'MI Five' pia lilishutumu wakili wa Uingereza mzaliwa wa China Christine Lee kwa kufanya uhusiano na watu wenye ushawishi nchini Uingereza.
Mwaka huo huo, Liang Litang, ambaye aliendesha mgahawa wa Kichina katika jiji la Boston Marekani, alishtakiwa kwa kutoa taarifa juu ya wakosoaji wa Kichina kwa UFWD.
Baadae mnamo Septemba, Linda Sun, mfanyakazi wa zamani wa Ofisi ya Gavana wa New York, pia alishtakiwa kwa kufanyia kazi maslahi ya Wachina.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya serikali ya China, Linda alikutana na afisa mkuu wa UFWD mwaka wa 2017 ambaye alimwomba Linda kuchukua nafasi ya "balozi wa Sino-US."

Chanzo cha picha, Supplied
Ni jambo la kawaida kwa raia wa China wenye ushawishi nje ya nchi kuwa na uhusiano na Chama cha Kikomunisti, na takwimu hizi mara nyingi hutafuta ruhusa kutoka kwa maafisa wa chama hata katika masuala ya biashara.
Linapokuja suala la China, "tunaona mstari kati ya ujasusi na juhudi za kukusanya ushawishi ukizidi kuwa finyu," anasema Dk. Ho Fang-hung, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Hili lilifahamika zaidi wakati China iliidhinisha sheria mpya mwaka 2017 ambazo zilitaka raia na makampuni ya China kushirikiana na mashirika ya kijasusi na kutoa taarifa kwa serikali ya China.
Kulingana na Dk. Hung, sheria hii 'iligeuza kila mtu kuwa jasusi wa kisiasa.'
Kuhusiana na hilo, Wizara ya Usalama wa Nchi ya China pia ilitoa video za propaganda zinazoonya umma kwamba majasusi wa kigeni wameenea kila mahali.
Baadhi ya wanafunzi wa China wanaofanya safari maalum katika nchi nyingine pia waliagizwa na vyuo vikuu vya China kupunguza mawasiliano yao na raia wa kigeni na pia kuwasilisha ripoti za shughuli zao.
Lakini pamoja na hayo yote, Rais Xi Jinping anataka kukuza maslahi ya China duniani na amekabidhi jukumu hili kwa UFWD.
Masuala haya yote yanazidisha ugumu kwa mataifa ya Magharibi kuamua jinsi ya kufanya biashara na taifa hilo la pili kwa uchumi mkubwa duniani, licha ya wasiwasi wa kiusalama.
Juhudi za kuzuia kuingiliwa na China
Juhudi za kuzuia ushawishi unaoongezeka wa China katika nchi za Magharibi sasa zinaongezeka.
Nchi kama Australia zimeanzisha sheria za kuzuia kuingiliwa na mataifa ya kigeni kwa ajili ya kujilinda, ambapo wale wanaoingilia masuala ya ndani ya nchi wataadhibiwa kama wahalifu.
Mnamo 2020, Marekani ilipiga marufuku hati ya kusafiria kwa watu ambao walikuwa wakijihusisha na UFWD.
Hatua hizi pia ziliibua wasiwasi nchini China, ambapo ilisema kuwa vikwazo hivi vinazuia uhusiano wa pande mbili.

Chanzo cha picha, Getty
Dk. Hung anasema, "Serikali za Magharibi zinapaswa kuichukulia The United Front ya China sio tu kama tishio kubwa kwa usalama wa taifa lao, bali pia kama tishio kwa usalama na uhuru wa wakosoaji wa China."
Hata hivyo, pia anasema kuwa "serikali za Magharibi pia zinahitaji kufuatilia upendeleo dhidi ya China na kujenga imani na jumuiya ya China ili wafanye kazi pamoja kuzuia tishio hili."
Mwezi Disemba mwaka jana, Di Sinh Dong, kiongozi wa jumuiya ya China nchini Australia mzaliwa wa Vietnam, alitiwa hatiani kwa kujaribu kuingilia masuala ya ndani ya Australia kwa kuendeleza uhusiano na waziri wa Australia.
Waendesha mashtaka walisema Dong alikuwa "mgombea bora" wa U.F.W.D. kwa sababu pia alikuwa amegombea katika uchaguzi wa miaka ya 1990 na mara nyingi alitia chumvi uhusiano wake na maafisa wa China.
Kesi hii dhidi ya Dong ilivutia hisia za kimataifa baada ya kusema katika hafla ya kutoa misaada kuwa kuwepo kwa waziri wa Australia huko kutakuwa na manufaa kwa "raia wa China."
Swali liliibuka ikiwa Dong alikuwa akimaanisha jamii ya Wachina huko Australia au China moja kwa moja.
Wakati Dong akihukumiwa, wasiwasi pia uliibuka kwamba sheria za kupinga ujasusi zinaweza kutumika kama silaha dhidi ya raia wa China.
"Pia ni muhimu kukumbuka kuwa sio kila Mchina ni mfuasi wa Chama cha Kikomunisti, na sio kila shirika la Kichina linalofanya kazi nje ya nchi ni tiifu kwa China," anasema Dk. Hong.
'Sera za kichokozi zinazotegemea upendeleo wa lugha zitaimarisha propaganda za serikali ya China.'
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












