Wanaharakati wapinga mifumo ya akili bandia inayowapeleleza watu wa jamii ya Uyghur China

Kamera ya Hikvision

Chanzo cha picha, VCG

Mfumo wa kamera unaotumia akili bandia na utambuzi wa sura kwa ajili ya kubaini hisia umejaribiwa kwa watu wa jamii ya Uyghur mjini Xinjiang, BBC imeelezwa.

Mhandisi wa Programu amedai kuiweka mifumo hiyo kwenye vituo vya polisi vya jimbo.

Mwanaharakati wa masuala ya kibindamu aliyeoneshwa ushahidi ameeleza kama kitendo cha kushtusha.

Ubalozi wa China nchini Uingereza haujajibu shutuma zilizoelekezwa kwa China lakini umesema kuwa wanahakikisha kuzingatiwa kwa haki za kijamii na kisiasa kwa makundi ya jamii zote.

Xinjiang ni makazi ya jamii ya walio wachache wa Uyghur milioni 12, wengi wao Waislamu.

Raia katika mkoa huo hupelelezwa kila siku. Eneo hilo pia ni makazi ya "vituo vya mafunzo " vilivyosababisha utata, vinaitwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kama kambi za kizuizi na ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni moja wamewekwa katika kambi hizo.

Beijing daima imekuwa ikisema kuwa upelelezi ni muhimu katika eneo hilo kwa sababu inasema jamii hiyo inayotaka ambao kuanzisha jimbo lao wameua mamia ya watu katika mashambulio ya kigaidi.

Mhandisi wa programu hiyo alikubali kuzungumza na kipindi cha BBC cha Panorama bila kutajwa jina, kwa sababu anahofia usalama wake. Kampuni aliyoifanyia kazi pia haijawekwa wazi.

Lakini aliionesha Panorama picha tano za wafungwa wa Uyghur ambao alidai walipimwa kwa mfumo huo wa akili bandia.

"Serikali ya China hutumia watu wa Uyghurs kwa majaribio kama vile panya wanavyotumiwa kwenye maabara," alisema.

Na alielezea jukumu lake katika la kufunga kamera katika vituo vya polisi katika jimbo hilo: "Tuliweka kamera ya kugundua hisia umbali wa mita 3 aliposimama mtu. Ni sawa na kifaa cha kupeleleza kama mtu anasema uongo lakini teknolojia hii ni ya hali ya juu zaidi."

Alisema maafisa walitumia "viti vya kuzuia wafungwa" ambavyo vimewekwa sana katika vituo vya polisi kote China.

"Mikono yako imefungwa mahali na vizuizi vya chuma, na pia vifundo vya miguu."

Alitoa ushahidi wa jinsi mfumo wa akili bandia umefundishwa kugundua na kuchambua hata mabadiliko ya dakika katika sura na vishimo vya ngozi.

Kulingana na madai yake, programu hiyo inaunda chati ya pai, na sehemu nyekundu ikiwakilisha hali hasi ya akili au wasiwasi.

Alidai programu hiyo ilikusudiwa "kutoa majibu kabla ya uamuzi bila ushahidi wowote wa kuaminika".

Ubalozi wa China huko London haukujibu maswali kuhusu utumiaji wa programu ya kutambua mihemko katika jimbo hilo lakini ilisema: "Haki za kisiasa, kiuchumi, na kijamii na uhuru wa imani ya kidini katika makabila yote huko Xinjiang umehakikishiwa kikamilifu.

"Watu wanaishi kwa umoja bila kujali asili zao za kikabila na wanafurahia maisha thabiti na yenye amani bila kizuizi kwa uhuru binafsi."

Ushahidi huo ulioneshwa kwa Sophie Richardson, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu nchini China.

"Ni nyenzo ya kushangaza, ni watu ambao wako katika mazingira ya kulazimishwa sana, chini ya shinikizo kubwa, wanawatia wasiwasi na hiyo inachukuliwa kama dalili ya hatia, na nadhani, hili ni tatizo kubwa.''

Tabia zenye mashaka

Kwa mujibu wa Darren Byler, kutoka Chuo Kikuu cha Colorado, jamii ya Uyghur mara kwa mara hulazimika kutoa sampuli za vinasaba (DNA) kwa maafisa wa eneo hilo, ili kufanyiwa uchunguzi wa kidigitali na wengi wanapaswa kupakua programu ya simu ya serikali, ambayo inakusanya data pamoja na orodha za mawasiliano na ujumbe mfupi.

"Maisha ya Uyghur sasa ni kuhusu kutengeneza data," alisema.

"Kila mtu anajua kuwa smartphone ni kitu ambacho unapaswa kuwa nayo, na ikiwa hautakuwa nayo unaweza kushikiliwa na maafisa, wanajua kuwa unafuatiliwa. Na wanahisi kama hakuna namna ya kukwepa," alisema. .

Takwimu nyingi zinaingizwa kwenye mfumo wa kompyuta unaoitwa Jukwaa la operesheni la pamoja, ambalo Human Rights Watch inadai kuwa mtandao huo unabainisha tabia inayodhaniwa kuwa ya kutiliwa shaka.

"Mfumo huu unakusanya taarifa za aina tofauti za tabia halali kabisa ikiwa ni pamoja na vitu kama ikiwa watu walikuwa wakitoka kwa mlango wa nyuma badala ya mlango wa mbele, ikiwa walikuwa wakiweka gesi kwenye magari ambayo sio yao," alisema. Bi Richardson.

"Mamlaka sasa huweka nambari za QR nje ya milango ya nyumba za watu ili waweze kujua kwa urahisi ni nani anayepaswa kuwapo na nani hayuko."

Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kuhusu jinsi kampuni za teknolojia za Kichina zilivyo karibu na serikali. Kikundi cha utafiti chenye makao makuu yake Marekani , IPVM kinadai kuweka wazi ushahidi katika hati miliki zilizowasilishwa na kampuni hizo ambazo zinaonesha utambuzi wa uso zilibuniwa haswa kuwatambua watu wa jamii ya Uyghur.

Hati miliki iliyowasilishwa mnamo Julai 2018 na Huawei na Chuo cha Sayansi cha China inaelezea bidhaa inayotambulisha uso ambayo ina uwezo wa kutambua watu kwa misingi ya kabila lao.

Huawei alijibu kwamba "haikubaliani matumizi ya teknolojia kuwabagua au kuwakandamiza watu wa jamii yoyote" na kwamba ilikuwa "serikali huru " popote ilipofanya kazi.

Kikundi pia kimepata hati ambayo inaonekana kubainisha kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza teknolojia iitwayo Mtu Mmoja, Mfumo wa Jalada Moja.

"Kwa kila mtu serikali huhifadhi taarifa zao binafsi, shughuli zao za kisiasa, mahusiano ... chochote ambacho kinaweza kukupa ufahamu kuhusu tabia ya mtu huyo na kama anaweza kuwa tishio la namna gani '', alisema Conor Healey wa IPVM.

Lango kuu la kituo kinachofahamika kama'' kituo cha elimu ya ufundi'' mjini Xinjiang

Chanzo cha picha, Reuters

Huawei haikujibu maswali haswa kuhusu ushiriki wake katika kukuza teknolojia hiyo.

Ubalozi wa China huko London ulisema "hautambui" programu hizi.

IPVM pia ilidai kuwa imepata vifaa vinavyouzwa kutoka kampuni ya Kichina Hikvision ikitangaza kamera ya akili bandia inayotambua jamii ya Uyghur, na hati miliki ya programu iliyoundwa na Dahua, kampuni nyingine kubwa ya teknolojia, ambayo inaweza pia kutambua jamii ya Uyghur.

Dahua alisema hati miliki yake inahusu makabila yote 56 yaliyotambuliwa nchini China na hayakulenga kabila moja pekee.

Iliongeza kuwa ilitoa "bidhaa na huduma ambazo zinalenga kusaidia kuwaweka watu salama" na kutii "sheria na kanuni za kila soko" ambayo inafanya kazi, pamoja na Uingereza.

Hikvision ilisema maelezo kwenye wavuti yake hayakuwa sahihi na "yalipakiwa mkondoni bila uhakiki unaofaa", na kuongeza kuwa haikuuza au kuwa na bidhaa zake "kazi ya utambuzi wa wachache au teknolojia ya uchambuzi".

Upelelezi wa kila siku

Mwanaume akitembea kwenye mtaa wa Chongqing wenye kamera za upelelezi

China inakadiriwa kuwa na nusu ya kamera za upelelezi karibu milioni 800 duniani.

Pia ina idadi kubwa ya miji mizuri, kama Chongqing, ambapo kamera ya akili bandia imejengwa katika misingi ya mazingira ya mijini.

Hu Liu, mwandishi wa habari anayefanya uchunguzi huko Chongqing aliiambia Panorama kuhusu uzoefu wake mwenyewe: "Mara tu utakapoondoka nyumbani na kuingia kwenye lifti, unapigwa picha na kamera. Kuna kamera kila mahali."

"Ninapoondoka nyumbani kwenda mahali pengine, napiga simu teksi, kampuni ya teksi inapakia data kwa serikali. Basi naweza kwenda kwenye mgahawa kukutana na marafiki wachache na viongozi wa mamlaka wakajua eneo nilipo kupitia kamera kwenye kwenye mgahawa huo.

"Kumekuwa na hafla ambazo nilikutana na marafiki na mara tu mtu kutoka serikalini aliwasiliana nami. Walinionya," Usiambatane na mtu huyo, usifanye hivi na vile.

"Kwa progaramu hii ya akili ya bandia hatuna pa kujificha," alisema.