Jinsi nchi za Magharibi zinavyokabiliana na tisho la ujasusi la China linaloongezeka

Na Gordon Corera ,

Mwandishi wa habari za usalama

f

Kwa miaka mingi, mashirika ya kijasusi ya Magharibi yamekuwa yakizungumzia juu ya hitaji la kuzingatia mabadiliko ya ujasusi wa China. Wiki hii, mkuu wa shirika la ujasusi la GCHQ la Uingereza aliuelezea kama "changamoto inayofafanua suala hili".

Hii inafuatia msururu wa kukamatwa kote Magharibi kwa watu wanaoshutumiwa kwa ujasusi na udukuzi wa China. Na siku ya Jumatatu, balozi wa China aliitwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, baada ya watu watatu kushutumiwa kusaidia idara za kijasusi za Hong Kong.

Hizi ni ishara za shindano la kawaida lililofichika la mamlaka na ushawishi kati ya Magharibi na Uchina linaloibuka wazi.

Mataifa ya Magharibi - Marekani na washirika wake - wamedhamiria kukabiliana nao.

Lakini maafisa wakuu wana wasiwasi kuwa nchi za Magharibi hazijazichukua changamoto za ujasusi kutoka China kwa uzito wa kutosha na zimerudi nyuma katika suala la kijasusi, na kuziacha nchi za Magharibi zikiwa hatarini zaidi kwa ujasusi wa Beijing, na pande zote mbili ziko katika hatari ya kufanya makosa yanayoweza kusababisha janga.

Kinachowatia wasiwasi maafisa wa nchi za Magharibi ni azma ya Rais wa China Xi Jinping kwamba Beijing itaunda utaratibu mpya wa kimataifa. "Mwishowe inatamani kuiondoa Marekani kama taifa lenye mamlaka makuu ," mkuu wa MI6, Sir Richard Moore, aliniambia katika mahojiano nadra ofisini kwake kwa ajili ya mfululizo mpya wa BBC kuhusu taarifa za China na Magharibi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini licha ya miaka kadhaa ya kutoa maonyo, idara za ujasusi za nchi za Magharibi zimejitahidi hadi hivi majuzi kuzingatia shughuli za Wachina.

Nigel Inkster, ambaye alikuwa na cheo cha pili katika shirika la ujasusi la Uingereza MI6 alipostaafu mwaka 2006, anasema kuibuka kwa China kama taifa kubwa duniani "kulitokea wakati ambapo kulikuwa na kazi nyingine nyingi za awali".

Wakati Beijing ilipopanda ngazi ya dunia katika miaka ya 2000, fikra za watunga sera na maafisa wa usalama wa nchi za Magharibi - na mwelekeo wa idara za kijasusi - zilitawaliwa na kile kinachoitwa vita dhidi ya ugaidi na uingiliaji kijeshi nchini Afghanistan na Iraq.

Kuinuka kwa Uchina ndio changamoto kuu ya nyakati zetu - ni umbali gani wa kushirikiana, kushindana au kukabiliana? Gordon Corera anauliza iwapo nchi za Magharibi yamezorota kuamka.

Kuibuka kwa hivi karibuni kwa Urusi na sasa vita vya Israel-Gaza vimeonekana kuwa changamoto za dharura zaidi, maafisa wa Marekani na Ulaya wameafiki.

Wakati huo huo, kumekuwa na shinikizo kutoka kwa serikali na wafanyabiashara wanaotaka kupata ufikiaji wa soko kubwa la Uchina, badala ya kukabili hatari ya usalama inayotokana na soko hilo.

Viongozi wa kisiasa mara kwa mara walipendelea wakuu wao wa kijasusi wasiitaje China kwa majina. Na wafanyabiashara pia walipendelea kutokubali kwamba siri zao zilikuwa zikilengwa.

Ujasusi wa China ulikuwa tayari ukijihusisha na ujasusi wa viwandani miaka ya 2000, anasema, lakini makampuni ya Magharibi kwa kawaida yalikaa kimya. "Hawakutaka kuripoti kwa hofu kwamba kufanya hivyo kungehatarisha nafasi yao katika masoko ya Uchina," anasema Nigel Inkster.

Changamoto nyingine kubwa imekuwa ni kwamba China inafanya ujasusi tofauti na nchi za Magharibi. Hiyo imefanya shughuli zake za ujasusi kuwa ngumu kuzitambua na kukabiliana nazo.

Jasusi wa zamani wa nchi za Magharibi anasema aliwahi kumwambia mwenzake wa China kwamba China ilifanya "aina mbaya" ya ujasusi.

Alichomaanisha ni kwamba mataifa ya Magharibi yanapendelea kujikita katika kukusanya aina ya ujasusi inayowasaidia kuwaelewa wapinzani wao.

Lakini wapelelezi wa China wana vipaumbele tofauti.

Kulinda nafasi ya Chama cha Kikomunisti ni muhimu. "Utulivu wa serikali ndio lengo lao kuu," Roman Rozhavsky, afisa wa ujasusi wa FBI, anaelezea.

Hilo linahitaji kuleta ukuaji wa uchumi. Na kwa hivyo majasusi wa China wanaona kupata teknolojia ya Magharibi kama hitaji la juu la usalama wa kitaifa.

Majasusi wa Magharibi wanasema wenzao wa Beijing wanashiriki taarifa walizokusanya na makampuni ya serikali ya China, kwa njia ambayo mashirika ya kijasusi ya Magharibi hayafanyi na makampuni yao ya ndani.

'Kushughulikiwa kwa njia maalumu'

"Shirika langu lina shughuli nyingi zaidi kuliko tulivyowahi kuwa nazo katika miaka 74 ya historia," Mike Burgess, mkuu wa Shirika la Usalama na Ujasusi la Australia (Asio) alinieleza.

"Siziita nchi mara chache kwa sababu linapokuja suala la ujasusi moja kwa moja, tunaufanya hivyo kwao," Burgess aliniambia. "Ujasusi wa kibiashara ni jambo tofauti kabisa, na ndiyo maana China inashughulikowa kwa njia maalumu kwa hili."

Alikiri kwamba washirika wa Magharibi wamechelewa kuelewa tisho hili. "Nadhani imekuwa likiendelea kwa muda mrefu na kwa pamoja tumekosa," anakiri.

Tulikuwa tukizungumza naye mwezi Oktoba mwaka jana huko California, ambapo alikuwa akishiriki katika kikao cha kwanza kabisa ambapo - wakuu wa usalama walionekana wazi katika kile kinachojulikana kama Five Eyes (Macho Matano) - muungano wa ushirikiano wa kijasusi unaoundwa na Marekani, Uingereza, Australia, Canada na New Zealand.

g
Maelezo ya picha, Katika hali isiyo ya kawaida, wakuu wa usalama wa "Five Ayes" walionekana pamoja Oktoba 2023 wakionya kuhusu China kupata siri za kibiashara.

Kusanyiko hilo ambali halijawahi kushuhudiwa lilikuwa ni jaribio la makusudi la kuongeza idadi ya maonyo kuhusu China kwa sababu ya hofu kwamba makampuni na mashirika mengi yalikuwa bado hayasikii.

Eneo la mkutano lililopo katika Silicon Valley pia lilichaguliwa kwa uangalifu – kama mahala palipocha majaribio ya Uchina ya kuiba teknolojia, wakati mwingine kupitia ujasusi wa mtandao na wakati mwingine kupitia kuajiri watu wa ndani.

Rasilimali za China kwa hili ziko kwa kiwango tofauti. Afisa wa kijasusi wa nchi za Magharibi anakadiria kuwa China ina takriban watu 600,000 wanaofanya kazi katika masuala ya kijasusi na usalama, zaidi ya nchi nyingine yoyote duniani.

Huduma za usalama za Magharibi haziwezi kuchunguza kila kisa. Kulingana na shirika la ujasusi la Uingereza MI5, zaidi ya watu 20,000 nchini Uingereza pekee wamefikishwa kwenye tovuti za kitaalamu za mitandao kama vile LinkedIn na majasusi wa China ili kukuza uhusiano.

"Watu wanaweza kuwa hawajui kwamba kwa kweli wanawasiliana na afisa wa upelelezi kutoka taifa lingine - lakini hatimaye wanajikuta wakitoa taarifa zinazoharibu mustakabali wa kampuni yao," mkuu wa MI5, Ken McCallum aliniambia kwenye mkusanyiko wa California.

Hizi ni kampeni za "epic", Ken McCallum anasema, ambazo zinaweza kuwa na athari kubwa za usalama wa kitaifa, pamoja na athari za kiuchumi.

Wakati sehemu kubwa ya vifaa vikubwa vya Uchina vinalenga uchunguzi wa ndani, pia hutumia majasusi wake kupunguza ukosoaji wa vitendo vyake nje ya nchi.

Hivi majuzi, kumekuwa na ripoti za majasusi wa China wanaolenga siasa za Magharibi, na wamekamatwa nchini Uingereza, Ubelgiji na Ujerumani na uchunguzi unaoendelea nchini Canada.

Kumekuwa na ripoti za "vituo vya polisi vya ng'ambo" vya Uchina huko Ulaya na Amerika. Linapokuja suala la kuwafuata wapinzani wa China katika nchi za Magharibi, maafisa wa usalama wanasema maafisa wa ujasusi wa Beijing huwa wanafanya kazi kwa mbali badala ya kuwatumia majasusi mashinani -kwa kuwaajiri wachunguzi wa kibinafsi au kupiga simu za vitisho.

g
Maelezo ya picha, Wanaume wawili walikamatwa Aprili 2023, wakituhumiwa kusaidia kuanzisha kituo cha polisi cha siri huko New York

Kwa hakika, matukio ya kwanza ya mtandao yaliyolenga mifumo ya serikali ya Uingereza mwanzoni mwa miaka ya 2000 hayakutoka Urusi bali Uchina na yalilenga kukusanya taarifa kuhusu wapinzani wa ng'ambo kama vile vikundi vya Tibet na Uighur.

Australia imekuwa ikiongoza kwa wasiwasi wa kuingiliwa kisiasa. Shirika la ujasusi la Australia -Asio, linasema lilianza kugundua shughuli za ujasusi wa China kuanzia karibu 2016, mkiwemo kuwanadi wagombea katika uchaguzi. "Wanajaribu kusukuma ajenda zao, ambazo wana haki ya kufanya. Hatutaki waisukume kwa njia za siri," Mike Burgess aliiambia BBC. Australia ilipitisha sheria mbili mpya sheria zinazolenga kukabiliana na changamoto hii mnamo 2018.

Mnamo Januari 2022, MI5 nchini Uingereza ilitoa tahadhari ya uingiliaji kati usio wa kawaida ikidai wakili wa Uingereza Christine Lee amekuwa akitoa michango kwa vyama vingi vya kisiasa vya Uingereza kama sehemu ya kampeni ya kuendeleza ajenda ya Beijing.

Kwa sasa anafuatilia kesi ya kisheria dhidi ya MI5 kuhusu madai hayo. Ilikuwa ni mwaka wa 2023 tu ambapo Uingereza ilipitisha Sheria mpya ya Usalama wa Taifa ambayo ilitoa mamlaka mapya ya kukabiliana na kuingiliwa na shughuli nyingine za mataifa ya kigeni. Wakosoaji wanasema mamlaka hayo yamechelewa kutolewa.

Nchi za Magharibi, bila shaka, zinaipeleleza China, kama vile China inavyopeleleza nchi za Magharibi.

Lakini kukusanya taarifa za kijasusi kwa China ni changamoto ya kipekee kwa huduma za kijasusi za Magharibi kama vile MI6 na CIA.

Hali iliyoenea ya ufuatiliaji ndani ya nchi, kutokana na utambuzi wa uso na ufuatiliaji wa kidijitali, hufanya mtindo wa kitamaduni wa akili ya binadamu - mawakala wa kukutana ana kwa ana - karibu kutowezekana.

China ilifagia mtandao mkubwa wa mawakala wa CIA miaka kumi iliyopita. Na pia ni lengo gumu kitaalam kwa GCHQ na Shirika la Usalama la Kitaifa la Marekani (NSA), ambalo hukatiza mawasiliano na kukusanya taarifa za kiintelijensia za kidijitali, kwa kiasi fulani kwa sababu inatumia teknolojia yake - badala ya Magharibi.

"Kwa kweli hatujui jinsi kamati kisiasa sera (ya Kichina) inavyofikiri," afisa mmoja wa Magharibi anakiri.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi