Kuitunza amani wakati wa mageuzi changamoto na funzo Tanzania

s

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Na Lameck Jaston
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025 ulioacha majeraha ya kisiasa na kijamii, Tanzania inakabiliwa na swali muhimu: inaweza vipi kudumisha amani yake ya muda mrefu huku ikiitikia wito wa mageuzi ya kisiasa na kijamii?

Kwa hakika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 umeiacha Tanzania katika mojawapo ya nyakati za tafakuri kubwa katika historia yake ya kisasa. Kwa miongo kadhaa, Tanzania imekuwa mfano wa amani na utulivu katika ukanda uliojaa migogoro. Lakini sasa taifa hili linapitia matukio ya machafuko na majonzi, likiwa katika kipindi kipya cha tafakuri, wakati wananchi, hususani vijana, wanapotoa wito wa mabadiliko makubwa katika utawala, uwajibikaji, haki na usawa wa kijamii.

Pamoja na wito huo, kwa Watanzania wengi, maandamano yaliyoenda na vurugu katika siku ya uchaguzi na zilizofuata baada ya uchaguzi hazikuwa tu vurugu bali zilikuwa jaribio la utambulisho wa taifa hilo kama moja ya mataifa yaliyodumu na amani kwa miongo mingi.

Amani na utulivu umekuwa uti wa mgongo wa Tanzania. Tangu siku za mwanzo za uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alitambua kuwa uhai wa taifa lenye makabila na dini nyingi unahitaji zaidi ya taasisi za kisiasa; unahitaji kiapo cha maadili cha kuvumiliana, kujadiliana, na kuwa na lengo la pamoja. Kiapo hicho ndicho kilichotuvusha miongo kadhaa ya misukosuko ya kikanda, hata pale mataifa mengine yakiporomoka kwa migogoro. Lakini nyakati hizi zinalazimisha kuibuka kwa maswali muhimu kuhusu Tanzania: Inawezaje kuhifadhi amani huku ikikabiliwa na wito wa ndani halali wa mageuzi? Na je, inawezaje kulinda umoja bila kukandamiza haja ya mabadiliko?

1. Changamoto za amani na mageuzi

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ibada na maombi kutoka dini na madhehebu mbalimbali zinaendelea kuombea amani na walioathirika na vurugu za uchaguzi Tanzania

Machafuko ya baada ya uchaguzi yalionyesha hali ya kuchoshwa siyo tu kutokana na matokeo ya kisiasa, bali pia na kasi ndogo ya mageuzi katika mifumo yetu ya kijamii na kiutawala. Wananchi wengi, hususan vijana, wanatamani kuona utawala wenye uwazi zaidi, taasisi zinazowajibika zaidi, na fursa sawa kwa wote. Matamanio haya siyo tishio kwa utulivu wa amani ya Tanzania; ni kilio cha kuimarisha msingi wake. Hatari ipo pale ambapo kilio hicho kinachanganywa na uasi, au pale ambapo imani inapotengana na mchakato wa kidemokrasia.

Vurugu, bila kujali zinatoka wapi, haziwezi kujenga taifa bora. Zinaharibu imani, zinagawa jamii, na zinabadilisha tofauti za kisiasa kuwa chuki ya kudumu. Mara jamii inapofikia hatua ya kuona wananchi wake kama maadui, kurejea katika hali ya kawaida huwa ni safari ndefu na yenye gharama kubwa. Tanzania haipaswi kuingia katika mzunguko huo. Amani yake siyo tu ukosefu wa vita, bali ni muundo wa heshima ya pamoja unaoliweka taifa hilo pamoja.

Historia inatupa funzo muhimu. Ethiopia, iliyokuwa moja ya nchi zenye matumaini makubwa barani Afrika kabla ya mwaka 1974, iliingia katika machafuko baada ya madai ya mageuzi kuzidi uwezo wa taasisi zake. Matokeo yake yalikuwa miongo ya misukosuko na kudorora kwa maendeleo. Vivyo hivyo, mapinduzi ya Tunisia mwaka 2011 yalichochea matumaini makubwa katika ulimwengu wa Kiarabu, lakini matarajio hayo yakapungua pale hamasa ilipozidi maandalizi ya taasisi. Matukio haya yanatufundisha kuwa mageuzi ya kweli lazima yatekelezwe kwa uangalifu, kwa ushirikiano, na kwa makubaliano, si kwa migongano.

Hata hivyo, historia pia ina mifano chanya ya mataifa yaliyopata uwiano kati ya mageuzi na utulivu na amani. Ghana katika miaka ya 1990 ilibadilika kutoka utawala wa kijeshi kwenda ule wa demokrasia, si kwa sababu haikuwa na migogoro, bali kwa sababu viongozi na wananchi walikubaliana kwamba mabadiliko lazima yafanyike kwa misingi ya sheria na mazungumzo. Afrika Kusini, baada ya nyakati mbaya za ubaguzi wa rangi, iliepuka kuporomoka kwa taifa kwa kutumia mazungumzo yaliyopangwa kwa misingi ya maadili ya maridhiano. Mifano hii inaonyesha wazi kwamba njia salama ya mageuzi si mapinduzi, bali ni kuaminiana na kusikilizana kati ya dola na jamii.

2. Urithi wa utamaduni wa mazungumzo na nidhamu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nguvu ya Tanzania imekuwa daima katika utamaduni wake wa mazungumzo badala ya migogoro. Mila za baraza la kijiji na mazungumzo ya kitaifa tangu enzi za Nyerere ndizo msingi wa mageuzi ya amani. Taifa halihitaji kuacha urithi huu ili kubadilika. Mageuzi yanayojengwa juu ya mazungumzo huwa na maisha marefu kuliko yale yanayolazimishwa kwa nguvu.

Rosa Parks, ambaye hatua yake ndogo ya kijasiri ilianzisha harakati kubwa za haki za kiraia nchini Marekani, aliwahi kusema kuwa angependa kukumbukwa kama mtu aliyekuwa na wasiwasi juu ya uhuru na usawa kwa wote. Ujasiri wake wa nidhamu si machafuko, ndio uliobadilisha jamii. Tanzania inaweza kufuata njia hiyo: thabiti katika dhamira, lakini tulivu katika mbinu.

Safari ya taifa hilo mbele lazima ianze kwa kujitafakari. Serikali na jamii lazima zijiulize si tu nini kibadilike, bali jinsi ya kubadilika. Wito wa mageuzi haupaswi kuonekana kama tishio kwa mamlaka; ni uthibitisho wa imani ya wananchi katika uwezo wa nchi yao. Mageuzi yanayojengwa juu ya amani ni alama ya ukomavu, si upinzani. Yanamaanisha kuboresha taasisi badala ya kuzivunja, kuimarisha uwajibikaji bila kuharibu imani, na kuhakikisha kila raia anasikilizwa ndani ya mipaka salama na halali.

Kwa upande wa dola, nyakati kama hizi zinahitaji uongozi wenye mizani ujasiri uliounganishwa na huruma. Hatua za kiusalama, ingawa ni muhimu kudumisha utulivu, lazima ziendeshwe kwa ustahimilivu na uhalali. Uhalali wa serikali hauimarishwi na nguvu inazoweza kutumia, bali na imani inayoijenga kwa wananchi. Viongozi wakubwa wa mageuzi duniani walielewa ukweli huu: mamlaka ya kimaadili hudumu zaidi kuliko mamlaka ya nguvu.

Kwa upande wa wananchi, amani si jukumu la serikali pekee. Ni nidhamu ya pamoja, maadili ya uraia. Amani inahitaji subira, mazungumzo, na uwajibikaji wa kiraia hasa katika nyakati za maumivu. Ushiriki wa kujenga katika maisha ya umma, si uharibifu au kujiondoa, ndiyo njia ya maendeleo ya jamii. Ujasiri wa kusema ukweli lazima uambatane na hekima ya kulinda yanayotuweka pamoja.

3. Mageuzi jumuishi na mustakabali wa Tanzania

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha za waathirika wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 huko Rwanda.

Mageuzi nchini Tanzania lazima pia yawe jumuishi. Hayapaswi kuishia kwenye siasa pekee. Tofauti za kiuchumi na kijamii mara nyingi huchochea migogoro ya kisiasa. Kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, kuhakikisha fursa sawa, na kuimarisha uwajibikaji katika serikali za mitaa ni msingi wa kurejesha imani. Mfumo unaoonekana kuwa wa haki na unaojibu mahitaji ya watu hauwi chanzo cha hasira.

Tukiangalia nyuma, historia inatoa mwanga. Msisitizo wa Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa taifa hilo, juu ya uongozi wa kimaadili kwamba siasa lazima iwe "mtumishi wa watu" unabaki kuwa kanuni ya kudumu.

Hakuwa akipinga upinzani, bali alihimiza ustaarabu. Kauli yake kuwa "bila umoja, Afrika haina mustakabali" bado ina uzito leo kama ilivyokuwa miaka sitini iliyopita. Umoja huo, hata hivyo, lazima uwe hai ukihusisha mitazamo tofauti, maslahi ya maeneo na vizazi, huku ukidumisha mshikamano wa kitaifa.

Mataifa mengine yameonyesha kuwa amani na mageuzi vinaweza kuimarishana yakifanywa kwa maono. Mageuzi ya Rwanda baada ya mauaji ya kimbari, ingawa mazingira yake ni tofauti, yanaonyesha jinsi utulivu uliojengwa juu ya mazungumzo na taasisi imara unavyoweza kuleta urejesho mkubwa wa kijamii.

Mabadiliko ya Ghana kupitia chaguzi za amani yanaonyesha jinsi demokrasia inavyokua pale taasisi zinapokuwa na nguvu kuliko watu binafsi. Mageuzi ya Singapore kutoka taifa dogo lenye changamoto hadi nchi yenye mafanikio makubwa yanaonyesha kuwa utawala wa nidhamu na mipango ya muda mrefu unaweza kubadilisha utulivu kuwa ustawi. Njia zao hazikuwa kamilifu, lakini zote zilikuwa za amani.

Kinachowaunganisha si itikadi, bali mbinu: heshima kwa mchakato, na imani kuwa mageuzi hupatikana kwa ushawishi, si kwa kulazimisha. Ndivyo inavyopaswa kuiongoza Tanzania. Sisi si taifa linalohitaji mapinduzi makubwa; tunahitaji upya, ukarabati wa taratibu za kijamii, uboreshaji wa mifumo ya utawala, na urejeleo wa dira ya maadili ya pamoja.

Amani, kwa maana hii, si kinyume cha mageuzi bali ni sharti lake. Bila amani, mageuzi hayadumu; bila mageuzi, amani hudhoofika. Jukumu la Watanzania ni kushikilia mambo haya mawili kwa Pamoja, kujenga mfumo ambao wananchi wanaweza kudai maendeleo bila hofu, na viongozi wanaweza kutawala kwa kujiamini bila mashaka.

Uchaguzi wa 2025 kimalizika, taifa hilo linapitia majaribu ya kurudi katika hali ya kawaida, ya kuchoka na tafakuri. Hilo linaweza kuwa kosa. Wakati huu uwe mwanzo mpya nafasi ya kuimarisha mazungumzo ya kitaifa, kujenga taasisi imara, na kuinua utamaduni wa uraia wa kujenga.

Ikitumia kipindi hiki vizuri, Tanzania haitalinda tu amani yake, bali itaipa maana mpya vizazi vijavyo.

Kofi Annan, mmoja wa viongozi wakubwa wa Afrika, aliwahi kusema: "Huwezi kufanya chochote bila amani, na unaweza kufanya machache sana ukiwa na amani isiyo na haki." Tanzania tayari ina msingi wa kimaadili wa utulivu na amani; kinachohitajika sasa ni mfumo wa haki unaoipa amani maana.

Matukio ya Oktoba 2025 yatakumbukwa ama kama wakati Tanzania iliteleza, au kama wakati ilipojijenga kimaadili. Mustakabali wake utategemea jinsi inavyoshughulikia kipindi hiki nyeti. Ikiijifunza kutokana na historia, kuaminiana sasa, na ikitekeleza mageuzi yanayoinua kila raia, amani iliyowahi kuigwa barani Afrika haitadumu tu, bali itastawi zaidi.

Historia ya Tanzania haijawahi kuwa ya mapinduzi ya ghafla, bali ya maendeleo ya taratibu. Dunia itatazama kuona kama inaweza tena kugeuza uvumilivu kuwa nguvu, mazungumzo kuwa mageuzi, na amani kuwa ustawi. Jibu halipo mitaani au serikalini pekee, bali katika dhamira tulivu ya taifa lililoamua kubaki moja.

Lameck Kumbuka Jaston ni mtaalamu wa diplomasia ya uchumi kutoka Tanzania.