Tanzania inahitaji maridhiano ya aina gani?

po

Chanzo cha picha, AFP

Muda wa kusoma: Dakika 6

“Bongozozo ataja mbizu za kuliponya taifa,” “Wito wa kukiri makosa, kusamehe na kuponya watolewa,” “Wadau: Maridhiano yataponya taifa,” “Utaifa kwanza,” “Watanzania hawajazoea mabavu, kutoana ngeu,” “Tunatokaje!”

Kwa takribani wiki moja sasa, kurasa za mbele za magazeti ya Tanzania zimepambwa na vichwa vya habari vya aina hiyo, vinavyo hoji kuhusu maridhaino baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 ambao ulikumbwa na vurugu zilizopelekea uharibifu na umwagaji damu.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema serikali itachukua hatua ya maridhiano.

"Ni dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaanzisha mazungumzo ya maridhiano ili kuhakikisha hata hao wachache wanapata nafasi ya kusikilizwa ili kuwa na taifa lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na dunia.”

Mjadala sasa utatuama juu ya aina gani ya maridhiano Tanzania inahitaji? Pia ni maeneo gani ambayo watu wanapaswa kuridhiana? Ongezea ni swali la serikali inapanga kuridhiana na nani? Haya yote ni muhimu.

Pia unaweza kusoma

Kuridhiana na nani?

Ili kujua unafanya maridhiano na nani, yakupasa kwanza kuelewa umekoseana na nani. Kuridhiana na Mama aliyepoteza mtoto wake baada ya kupigwa risasi? Ama kuridhiana na familia ambazo wapendwa wao hawajui ikiwa wako hai au wamefariki na kuzikwa wasikokujua? Au kuridhiana na ndugu ambao jamaa yao alitekwa na hakuonekana tena hadi leo?

Hao ni watu ambao maridhiano yanapaswa kuwafikia. Yaani watu ambao wamedhulumiwa, kwa kutekwa, au kuuawa au kupotezwa isivyo haki – iwe ni kabla ya maandamano, wakati wa maandamano au baada ya maadamano.

Maandamano yaliyopelekea ghasia kwa sehemu kubwa yalitokana na wito wa Chama cha Upinzani Chadema, kuzuia uchaguzi kwa sababu ya kutoridhishwa na mifumo ya kusimamia uchaguzi na kukosekana uhuru wa kisiasa. Ingawa wenyewe hawakueleza kama watafanya maandamano. Hili ni kundi jingine ambalo maridhiano nao yanapaswa kufanyika.

Ni muhimu kuliponya kundi la wale ambao wamepoteza wapendwa wao au mali zao. Ila ni makosa maridhiano yakiishia hapo, na yakaacha zile sababu za msingi hasa zilizowasukuma watu kuingia barabarani. Ni muhimu kuridhiana kwenye mzizi wa fitina.

Wanaharakati watakuwa sehemu yao maridhiano? vijana wanaojiita Gen Z? viongozi wa dini? wanasiasa na mashirika ya kutetea haki za binadamu? kwa mantiki ya kawaida, ni makundi muhimu kwa kuanzia.

Viongozi wa Chadema, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, John Heche baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa, wameachiwa huru Novemba 10, 2015, Je ni sehemu ya mchakato wa maridhiano?

Maridhiano kwenye nini?

X
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vyama vya upinzani vinataka mabadiliko kwenye tume ya uchaguzi – kuwepo na tume huru ambayo wataamini inaheshimu kweli kura za wananchi. Hoja hii ni ya msingi, kwa sababu kuna walakini mkubwa kwamba vyama vya upinzani vilishindwa kupata majimbo hata katika ngome zao katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Kuwepo na uhuru wa kisiasa, utakao ondosha kubughudhiwa wanapofanya mikutano yao, au viongozi wao kukamatwa ovyo na kubebeshwa msururu wa kesi. Na usisahau, kwa muda mrefu Tanzania kulikuwa na marufuku ya maandamano na mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Lakini hata iliporuhusiwa, bado ule utamaduni wa kukamatwa viongozi wa upinzani na kuvunja mikutano hiyo kwa nguvu uliendelea kuwepo. Wakati mwingine sababu zinazotumiwa na vyombo vya dola kufanya hayo, hazina mantiki wala mashiko.

Na jambo jingine ni uhuru wa kujieleza, mbali na uhuru kupitia majukwaa ya kisiasa, wapo wanaotaka uhuru zaidi katika mitandao ya kijamii, hawataki kuona watu wanapotea au kukamatwa kwa sababu tu ya maoni yao kwenye Twitter au Instagram.

Wanaotaka haya, wanaamini yote yanaweza kupatikana kupitia Katiba mpya, ambayo italinda kura wakati wa uchaguzi, italinda uhuru wa watu kutoa maoni, italinda uhuru wa kisiasa na vilevile kuondoa makundi ya watu ambao hupoteza wengine na wala hawajawahi kukamatwa.

Hakuna shaka kwamba maridhiano ni muhimu, lakini hayapaswi kuwa maridhiano nusu nusu. Ili kuzuia kisitokee kile kilichotokea Oktoba 29, ni muhimu yale yote yaliyoingiza Tanzania katika mtafaruku yakashughulikiwa kwa ukamilifu wake.

Aina za maridhiano na cha kujifunza

Ili Tanzania ipone kutokana na majeraha ya kisiasa na kijamii yaliyosababishwa na vurugu za uchaguzi na hata kabla ya uchaguzi, ni lazima ichague aina ya maridhiano yenye mizizi katika ukweli, uwajibikaji na matumaini ya pamoja. Dunia imeonyesha mifano mizuri ya aina mbalimbali za maridhiano ambayo Tanzania inaweza kujifunza.

Afrika Kusini kupitia Tume ya Ukweli na Maridhiano, ilipokuwa kwenye mkwamo wa aina hii ilitumia maridhiano ya ukweli na uwajibikaji. Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Afrika Kusini (TRC), ilikuwa chombo kilichoanzishwa baada ya ubaguzi wa rangi mwaka 1996 ili kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu uliotokea kati ya Machi 1, 1960 na Mei 10, 1994. Hapa, si tu kusamehe bali kusikiliza walioumia, kukiri makosa, na kuwawajibisha waliokiuka haki za binadamu. Hii ni njia ya kuponya kwa kusema ukweli, si kufunika majeraha ama kombe mwanaharamu apite.

Pili, yapo maridhiano ya kijamii, kama yaliyotekelezwa Rwanda baada ya mauaji ya kimbari miongo mitatu iliyopita. Japo yalichukua muda kufanikiwa lakini yamefanikiwa kwa kiwango cha kufurahisha. Maridhiano baada ya mauaji ya kimbari yalijikita katika kujenga upya uhusiano kati ya wananchi kupitia majadiliano ya kijamii. Maandamano yaliyofanyika Tanzania hayaonyeshi sana 'uchama' hivyo inaweza kutumia mfano huu kuunganisha tena vijana, wanaharakati, wanasiasa na wananchi wa kawaida waliotengana kwa misimamo ya kisiasa.

Ukiacha maridhiano ya watu wenye nguvu kama Raila Odinga na Uhuru Kenyatta au Odinga na Ruto nchini Kenya, pia inaweza kutumia maridhiano ya kitaasisi, kama yaliyofanywa Chile na Colombia ambayo yalihusisha mageuzi ya taasisi za dola, hasa vyombo vya usalama, tume za uchaguzi na mahakama, ili kuhakikisha maovu hayajirudii. Maridhiano ya aina hii yanaondoa hofu, yanaimarisha uwajibikaji, na kurejesha imani kwa mfumo wa utawala.

Ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Vurugu za kisiasa zilizotokea Zanzibar Januari 2001, za kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2000- zilisababisha vifo na majeruhi. Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch (HRW) iliyopewa jina, "Tanzania: Risasi zilinyesha kama mvua", inakisia watu 35 waliuwawa, wapatao mia sita walijeruhiwa na takribani 2000 walikimbilia nchi jirani.

Mauaji ya 2001 na mchafukoge wa kisiasa uliofuatia ulichangia kuwaleta pamoja Rais wa wakati huo Amani Abeid Karume wa Chama cha Mapinduzi CCM na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF kwa wakati huo hayatu Maalim Seif, katika meza ya mazungumzo yaliyopelekea kuasisiwa serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Tarehe 31/07/2010, Wazanzibari kupitia kura ya maoni walichagua kwa zaidi ya asilimia 60 kuongozwa kwa mfumo wa serikali hiyo ambayo kwa mara ya kwanza iliundwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010 na kuongozwa na Dkt. Ali Mohammed Shein huku Maalim Seif akiwa Makamu wa kwanza wa Rais.

Mchakato huo ukaleta mageuzi mengine pia ya kisiasa. Bado changamoto zipo, akini lengo kuu ni kupunguza mivutano ya kisiasa na umwagaji damu. .Bilashaka upande mwingne wa muungano, kwa maana ya Tanzania bara kuna mawili matatu wanaweza kuchukua katika mchakato wa maridhiano ya Zanzibar kwa kuunda maridhiano bora zaidi.