Nini mustakabali wa Tanzania baada ya maandamano?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ule uchaguzi uliotarajiwa ufanyike bila vifo na majeruhi, uligubikwa na vurugu, milio ya risasi na misiba iliyofuata baadaye - katika nchi ambayo kwa muda mrefu imepewa lakabu ya 'kisiwa cha amani' barani Afrika.
Huo ndio ufupisho wa kile kilichotokea Tanzania kuanzia Oktoba 29, 2025. Siku ambayo Watanzania waliingia vituoni kupiga kura, wakati huo huo wengine wakaingia barabarani kufanya maandamano ambayo yaligeuka kuwa vurugu mbaya kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni.
Maisha yanaendelea kurudi polepole, ingawa yanarudi huku kukiwa na ulinzi mkali wa vikosi vya usalama katika miji, wananchi wakizika wapendwa wao waliofariki na wakitafuta wengine walio katika hospitali na wale wasiojuulikana walipo.
Katika mjumuiko wa hayo yote, maswali makubwa yanaibuka: Huku tumefikaje? Je, maandamano yamefanikiwa? Kipi kifuatacho kwa raia na serikali baada vurugu mbaya za usiku na mchana, zilizoondoka na vijana wengi na uharibifu mkubwa wa mali za watu?
Hapa tumefikaje?

Harufu ya uwepo wa maandamano Oktoba 29, ilianza baada ya chama cha upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza hakitashiriki uchaguzi ikiwa hakuna mageuzi ya kupata katiba mpya na hasa tume huru ya uchaguzi. Badala yake wakatangaza tarehe hiyo wataitumia kuingia barabarani kuzuia uchaguzi usifanyike.
Lakini mwandishi wa habari na mchambuzi wa masula ya siasa kutoka Tanzania, Khalifa Said, anasema ni makosa kuyatazama maamdano ya Oktoba 29 kuwa yalikuja kama mwitikio wa wito wa Chadema pekee.
Anafafanua, ''ingawa wapo walioshiriki ili kuzuia uchaguzi, pia wapo walioandamana kupaza sauti zao, kwa sababu ya kutoridhishwa na mambo yanayoendelea nchini na namna serikali inavyoyashughulikia, matukio kama watu kutekwa na kupotea katika mazingira yasiyoeleweka.''
Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRD), anasema kutosikilizana kwa pande mbili zilizokuwa na mawazo tofauti ni sababu kubwa ya Tanzania kufika ilipofika sasa.
"Suala la msingi ambalo limetufikisha hapa tulipo ni suala la taifa kugawanyika, manung'uniko, malalamiko mengi ya wananchi, taasisi mbalimbali vikiwemo vyama vya upinzani", anasema Olengurumwa na kuongeza kuwa kukutana kama taifa na kuweka mjadala wa kitaifa kungezuia madhara yaliyoletwa na maandamano.
Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu, likiwemo la Amesty International wanasema mamia ya watu wameuawa katika maandamano hayo. Huku wakivutuhumu vyombo vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi katika kupambana na waandamanaji.
Serikali ya Tanzania imekana vyombo vyake vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi, na licha ya kukiri kutokea kwa vurugu, vifo na uharibifu wa mali, bado haijatoa idadi ya waliouwawa hadi wakati makala hii inachapishwa.
Maandamano yamefanikiwa?

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufanikiwa kwa maandamano kutategemea kwa sehemu kubwa na lengo la maandamano yenyewe na yale yatakayo fuata baaye. Bila shaka watu walifanikiwa kuingia babarani, licha ya ukweli kwamba gharama kubwa ya uhai imelipwa.
Pengine serikali itajitapa kwamba waliongia barabarani wameshughulikiwa na kila kitu kinaanza kurudi kama kilivyokuwa. Na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan tayari ameapishwa kwa ushindi wa zaidi ya asilimia 90.
Ikiwa nitakuwa na dhana njema, naamini serikali inajindaa kujibu maswali juu ya kile kilichotokea, haitokuwa uungwana kukaa kimya mileleni bila kujibu maswali juu majeruhi na vifo ambavyo vimerikodiwa katika maeneo mbali mbali ya Tanzania.
Bila shaka swali lililobaki kwa wachambuzi wa siasa: Je, maandamano yamefanikiwa au damu ilimwagika bure?
''Yamefanikiwa,'' anasema Said, ''kwa sabab si jambo ambalo limezoeleka kwa watanzania. Vile tu kwamba maandamano yamefanyika na kwa kiwango kikubwa, ni mafanikio makubwa. Yameandika historia mpya katika siasa za Tanzania na yatatoa mwelekeo jinsi siasa zetu zitakavyo fanyika huko mbeleni, kuanzia sasa. Na Serikali haiwezi kuliacha jambo hili lipite, bila kuchota mafunzo na kuchukua hatua za kuboresha mahusaino kati yake na wananchi.''
Kifuatacho ni nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika nchi yenye zaidi ya raia milioni 60, wakiunganishwa na lugha moja ya kiswahili, na tofauti zao za asili, rangi na dini – kwa hakika Oktoba 29 itabaki katika historia ya vurugu mbaya za kisiasa nchini humo.
Turudi nyuma kidogo. Kabla ya Kenya kuwa na katiba mpya mwaka 2010 ambayo imeisukuma mbele kwenye uwanda mpana zaidi wa uhuru wa kisiasa, kwanza nchi hiyo iliingia kwenye machafuko mwaka 2007/8.
Kwa mujibu wa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC), vurugu hizo zilisababisha zaidi ya watu 1, 100 kuuawa, 3,500 kujeruhiwa na 600,000 kulazimika kuyahama makazi yao. Katika siku 60 za ghasia, kulikuwa na mamia ya ubakaji, na zaidi ya mali 100,000 ziliharibiwa.
Katiba mpya ilikuwa jibu la moja kwa moja kwa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007-2008 na iliundwa kushughulikia masuala ya msingi yaliyochochea ghasia hizo.
Tukirudi nchini Tanzania: Wapo watakaojenga hoja kwamba kama matakwa ya upinzani yangesikilizwa, pengine tusingefika hapa tulipofika. Wengine watasema, kama watu wasingekuwa wanapotea na kutekwa, labda vijana wasingeingia barabarani, na wapo watakao fika mbali zaidi na kusema, ikiwa silaha za moto zisingetumika, yumkini waliofariki wengi wangekuwa bado wako hai.
Wakati Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Nchini Tanzania (THBUB) ikijiandaa kuchunguza yaliyotokea wakati wa maandamano, swali ni kwamba kipi kifuatacho kwa raia na serikali baada ya vurugu hizi mbaya?
Elizabeth Adundo, aliyekuwa mwangalizi wa uchaguzi Tanzania chini ya mwanvuli wa Africa Liberal Network, anasema, ''kwanza wafungwa wote wa kisiasa akiwemo Tundu Lissu, lazima waachiwe huru, huwezi kujenga maridhiano wakati bado watu wako ndani, pia lazima kuwe na mageuzi kwani katiba iliopo sasa ni ya zamani sana, ni lazima kutumike katiba inayoendana na matakwa ya watu.''
Naye Wakili Olengurumwa kutoka THRD, anasema ''kwanza tukiri makosa yaliyofanyika na kuomba radhi watanzania waliopoteza wapendwa wao, hatuwezi kwenda kwenye muafaka kabla ya kutibu majeraha. Na kwa sasa Watanzania wanataka taifa linalotenda haki, wasikilizwe na matakwa yao yatekelezwe.''
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Emmanuel John Nchimbi alisema kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua madhubuti za kulinda umoja wa kitaifa na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa utawala wa sheria.
"Ni dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba tunaanzisha mazungumzo ya maridhiano ili kuhakikisha hata hao wachache wanapata nafasi ya kusikilizwa ili kuwa na taifa lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na dunia" alisema, Dkt. Nchimbi.















