Amri ya kutotoka nje usiku Tanzania yaondolewa
Amri hiyo ilikuwa imetolewa kufuatia vurugu za maandamano yaliyotokea siku ya uchaguzi.
Muhtasari
- Baraza la Katiba Ivory Coast lathibitisha ushindi wa Ouattara
- Usafiri wa Mwendokasi wasitishwa kwa muda Tanzania
- Dick Cheney afariki akiwa na umri wa miaka 84
- Yesu pekee ndiye aliyeokoa ulimwengu, sio Bikira Maria, Vatican inasema
- Tanzania yaondoa amri ya kuwa majumbani kuanzia saa 12 jioni
- 'Uhusiano wa Marekani na Tanzania unapaswa kutazamwa upya' - Kamati ya Seneti Marekani
- Kanali Mamadi Doumbouya atangaza kugombea urais Guinea licha ya ahadi ya kutowania
- Rais Samia Suluhu Hassan afanya uteuzi wa mwanasheria mkuu wa serikali mpya
- White House yatangaza msaada wa dharura wa chakula kwa Wamarekani katikati ya mkwamo wa matumizi ya serikali
- Wakili wa zamani wa jeshi la Israel akamatwa kwa kuvujisha video ya wafungwa wa Kipalestina wakinyanyaswa
Moja kwa moja
Na Mariam mjahid & Asha Juma
Baraza la Katiba Ivory Coast lathibitisha ushindi wa Ouattara

Chanzo cha picha, Reuters
Baraza la Katiba la Ivory Coast siku ya Jumanne limethibitisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi na kumhakikishia ushindi Rais Alassane Ouattara muhula wa nne, rais wa baraza hilo Chantal Nanaba Camara alitangaza.
Rais Alassane Ouattara alishinda kupata asilimia 89.77 ya kura zilizopigwa huku wapinzani wake wakuu wakizuiliwa.
Ouattara, 83, alishinda kura ya Oktoba 25 katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika huku wagombea wawili wakuu wa upinzani, rais wa zamani Laurent Gbagbo na aliyekuwa benki ya Credit Suisse Tidjane Thiam, wote wakizuiwa na mahakama kugombea.
"Bw Alassane Ouattara ametangazwa kuchaguliwa katika duru ya kwanza kama Rais wa Jamhuri ya Ivory Coast," Rais wa Baraza la Katiba, Chantal Nanaba Camara, alisema mjini Abidjan.
Akisema mahakama "haijapokea malalamishi yoyote", aliongeza kuwa "uchunguzi wa ripoti rasmi unaonyesha hakuna dosari zinazoweza kudhoofisha uadilifu wa uchaguzi au kuathiri matokeo".
Soma zaidi:
Usafiri wa Mwendokasi wasitishwa kwa muda Tanzania

Usafiri wa Mwendokasi hautaweza kuendelea kwa muda nchini Tanzania kutokana na athari za maandamano yaliyotokea wakati wa maandamani.
''Vituo vingi vya Mwendokasi vimeharibiwa na kwa mantiki hiyo tunaendelea kuusitisha usafiri huu kwa njia ya morogoro road na …Mbagala yaani BRT 2,'' amesema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.

Chalamila amesema kuwa sababu msingi iliyopelekea kuchukuliwa kwa hatua hiyo ni kutathmini uharibifu uliotokea.
''…Tunajua kwamba mfumo wa ukataji tiketi na mageti pia yameharibiwa, na kwa mantiki hiyo inatupasa tuwe na muda wa kuweza kurudisha hali kama ilivyo.'' Chalamila aliongeza.
Kutokana na hatua hiyo, Chalamila aliombaMamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kutoa vibali vya muda mfupi kwa mabasi ya kawaida ili yaweze kutoa huduma katika njia hizi.
Aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani afariki dunia

Chanzo cha picha, Reuters
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani Dick Cheney amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake.
Cheney alikuwa sehemu ya utawala wa Republican wa rais wa zamani George W Bush.
Alikuwa na jukumu muhimu katika uvamizi wa Iraq wa 2003 na Marekani na vikosi vya washirika.
Dick Cheney alikuwa makamu wa rais wa Rais wa Republican George W Bush kati ya 2001 na 2009.
Pia aliwahi kuwa waziri wa ulinzi chini ya George Bush Snr, kati ya 1989 na 1993.
Kabla ya hapo, Cheney aliwahi kuwa mkuu wa wafanyikazi wa Ikulu ya Gerald Ford katika miaka ya 1970, kabla ya kukaa muongo mmoja katika Bunge la Wawakilishi.
Cheney alijulikana sana katika "vita dhidi ya ugaidi" vya George W Bush kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001, na aliyeunga mkono uvamizi wa Iraq.
Hali ya kawaida yaanza kurejea Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia wa Tanzania leo wameanza kurejelea shughuli zao za kawaida, baada ya serikali kuondoa vikwazo vya usafiri na huduma za internet kurejeshwa vilivyokuwa vimewekwa tangu siku ya jumatano wiki iliyopita, baada ya maandamano kulipuka wakati wa shughuli ya kupiga kura katika maeneo kadhaa.
Maduka mengi yalifunguliwa hii leo katika maeneo mengi sawia na vituo vya mafuta ambavyo vilikuwa vimefungwa wakati wa maandamano hayo.
Katika vituo vya mafuta ya petroli, milolongo mirefu ilishuhudiwa hii leo huku bei nazo zikipandishwa.
Tume ya uchaguzi ilimtangaza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mshindi wa uchaguzi huo uliokumbwa na maandamano, baada ya vyama kadhaa vya upinzani kuzuiwa kushiriki.
Serikali ilitangaza amri ya kutotoka nje kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi siku ya jumatano wiki iliyopita lakini agizo hilo sasa limeondolewa rasmi kuanzia leo.
Huduma za internet pia zimeanza kurejeshwa ila katika baadhi ya maeneo bado inasuasua.
Katika mji mkuu wa Dar es Salaam, maduka mengi yalifunguliwa na usafiri wa umma pia umeanza kurejea licha ya kuwepo kwa magari machache.
Wakaazi wa mji huo ambao wamezungumza na BBC wanasema kuwa licha ya shughuli kurejea kwa mwendo wa kinyonga, hali ya sasa imeleta afueni kwa sababu sasa wanaweza kwenda madukani, sokoni au hata kwenda kazini bila uoga lakini wengine nao wamesema licha ya vikwazo kuondolewa watu wangali wanafanya shughuli zao kwa tahadhari.
Maafisa wa ulinzi wangali wanashika doria katika barabara za miji lakini idadi yao imepungua kuliko ilivyokuwa mwishoni mwa juma lililopita.
Katika miji ya Mbeya na Mwanza ambayo pia ilishuhudia maandamano, hali ya maisha pia imeanza kurejea ila kwa tahadhari. Idadi kubwa ya watu leo walifika mjini kwa shughuli mbali mbali na maduka mengi yalifunguliwa.
Licha ya onyo kutoka kwa idara ya polisi kwa raia wa nchi hiyo kutosambaza habari au picha zinazoweza kuzua taharuki, raia wa Tanzania wametumia fursa ya uwepo wa huduma za interneti kusambaza picha za matukio ya wakati wa maandamano kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo picha hizo hazingeweza kuthibitishwa ikiwa kweli matukio hayo yaliyotekea wakati huo au la.
Aidha kuna ripoti ya kutatanisha kuhusu idadi ya vifo na majeruhi. Serikali ya Tanzania haijatoa ripoti yoyote kuhusu idadi ya watu waliofariki lakini imekiri kutokea kwa vifo kadhaa.
Soma zaidi:
Yesu pekee ndiye aliyeokoa ulimwengu, sio Bikira Maria, Vatican inasema

Chanzo cha picha, Reuters
Huenda Yesu alisikia maneno ya hekima kutoka kwa mama yake Maria (Mamake Yesu), lakini hakumsaidia kuokoa ulimwengu kutokana na laana, Vatican ilisema Jumanne.
Katika agizo jipya lililoidhinishwa na Papa Leo, ofisi kuu ya mafundisho ya Vatican iliwaagiza Wakatoliki bilioni 1.4 duniani kutomtaja Maria (Mamake Yesu) kama "mkombozi mwenza" wa ulimwengu.
Yesu peke yake ndiye aliyeokoa ulimwengu, limesema agizo hilo jipya, na kuhitimisha mjadala wa ndani ambao ulikuwa umewavuruga viongozi wakuu wa Kanisa kwa miongo kadhaa, na hata kuzua kutoelewana ambako ni nadra kati ya mapapa wa hivi karibuni.
"Haitakuwa sahihi kutumia jina 'mkombozi mwenza," maandishi hayo yalisema. "Jina hili ... (linaweza) kuleta mkanganyiko na kutokuwa na usawa katika upatanifu wa ukweli wa imani ya Kikristo."
Wakatoliki wanaamini Yesu alikomboa ubinadamu kwa kusulubishwa na kifo chake. Wasomi wa kanisa wamejadiliana kwa karne nyingi ikiwa Mary, ambaye Wakatoliki na Wakristo wengi humwita Mama wa Mungu, alimsaidia Yesu kuokoa ulimwengu.
Marehemu Papa Francis alipinga vikali kumpa Maria cheo cha "mkombozi mwenza", wakati fulani akiliita wazo hilo "upumbavu".
"Hakutaka kuchukua chochote kutoka kwa mtoto wake," Papa Francis, ambaye alikufa mnamo Aprili, alisema mnamo 2019.
Mtangulizi wa Francis, Benedict XVI, pia alipinga cheo hicho. Mtangulizi wake, John Paul II, aliiunga mkono, lakini aliacha kutumia jina hilo hadharani katikati ya miaka ya 1990 baada ya ofisi ya mafundisho kuanza kuonyesha mashaka.
Maagizo mapya ya Vatican yaliangazia jukumu la Maria mama wa Yesu kama mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu. Kwa kumzaa Yesu, "alifungua milango ya Ukombozi ambayo wanadamu wote walikuwa wakingojea", ilisema.
Kulingana na Biblia, jibu la Maria kwa malaika aliyemwambia kwamba angepata mimba lilikuwa: “Na iwe.”
Soma zaidi:
Amri ya kutotoka nje usiku Tanzania yaondolewa

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Tanzania imeondoa amri ya kuwa majumbani kuanzia saa 12 jioni imeondolewa.
Taarifa hiyo imetolewa na Jeshi la Polisi kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia wakati wa hafla ya kuapishwa tarehe 3/11.2025.
Amri hiyo ilikuwa imetolewa kufuatia vurugu za maandamano yaliyotokea siku ya uchaguzi.
Hapo jana, serikali ilitoa taarifa ya wafanyakazi kurejea katika shughuli zao kama kawaida.
Soma zaidi:
Human Rights Watch yashutumu Tanzania kwa ukiukaji wa haki za binadamu baada ya uchaguzi mkuu

Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch (HRW), limeitaka serikali ya Tanzania kuheshimu na kulinda haki za msingi za wananchi, ikiwemo uhuru wa kujieleza, kukusanyika kwa amani na kuungana, kama inavyotakiwa na sheria za kimataifa za haki za binadamu na katiba ya nchi.
Akihutubia Watanzania punde tu baada ya kula kiapo cha kuongoza taifa hilo kwa muhula wa pili, Rais Samia Suluhu aliwataka Watanzania kuendeleza umoja, upendo, amani na kuheshimu sheria za nchi.
"Nawasihi Watanzania, tuchague hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemko, upendo badala ya chuki, uvumilivu badala ya vinyongo, umoja badala ya migawanyiko na amani badala ya vurugu," alisema Rais Samia.
Katika ripoti yake mpya, HRW imesisitiza kuwa vyombo vya usalama zinapaswa kutumia njia zisizo za vurugu na kutumia nguvu tu pale inapokuwa haiwezekani kuepuka, kwa lengo la kulinda maisha wakati wa maandamano.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa matumizi mabaya au kutumia nguvu kupita kiasi kwa vikosi vya usalama huchukuliwa kama makosa ya jinai chini ya sheria za taifa.
Upande wa Rais Samia Suluhu alikemea vikali matendo hayo alisema "kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzani akidai kuwa wengine waliokamatwa wakati wa vurugu hizo ni raia kutoka nje ya Tanzania.
Rais Samia pia ametoa onyo kwa wote waliofanya vurugu.
"Sasa tuchague lenye manufaa kwetu kwani usalama wa taifa lolote hulindwa kwa wote, kwa nguvu zote na kwa gharama zozote."
Wakati huo huo, HRW pia imekosoa hatua za serikali kuzima au kudhibiti huduma za intaneti kabla na baada ya uchaguzi, ikisema zinakiuka Ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, unaolinda haki ya kupata taarifa na uhuru wa maoni.
“Maandamano ya kupinga mwenendo wa uchaguzi hayapaswi kuwa kisingizio cha kukiuka haki za wananchi,” alisema Oryem Nyeko, mtafiti mwandamizi wa Afrika wa Human Rights Watch.
“Mamlaka zina wajibu wa kulinda na kuendeleza haki za uhuru wa kujieleza na mikutano ya amani, na kurejesha huduma za intaneti kikamilifu.”
Soma pia:
'Uhusiano wa Marekani na Tanzania unapaswa kutazamwa upya' - Kamati ya Seneti Marekani

Chanzo cha picha, Jeanne/X
Maelezo ya picha, Seneta wa Marekani Jeanne Shaheen Kamati ya Uhusiano waMasuala ya Kigeni ya Bunge la Seneti la Marekani imeeleza wasiwasi kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini Tanzania.
Kupitia mtandao wa X, Kamati hiyo aliandika: “Chama tawala cha Tanzania kimeweka hatarini usalama wa wananchi wake na watalii.''
Seneta wa Marekani Jeanne Shaheen ametoa wito wa uhusiano wa Marekani na Tanzania kutazamwa upya.
''Baada ya uchaguzi huu uliokumbwa na dosari, uhusiano wa Marekani na Tanzania unapaswa kutazamwa upya.” alisema Seneta Shaheen.
Haya yanajiri, siku moja baada ya Ubalozi wa Marekani kuongeza kiwango cha tahadhari ya usafiri kuelekea Tanzania kutoka kiwango cha 2 hadi kiwango cha 3, ikimaanisha kuwa inashauriwa kuepuka safari zisizo za lazima kwenda nchini humo.
Kwa upande wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan taifa lake halitakubali maagizo yaliotolewa na waangalizi katika uchaguzi uliokamilika na badala yake akasema kuwa taifa lake litazingatia ushauri wao.
Akiwashukuru punde tu baada ya kuapishwa , kiongozi huyo ameweka wazi kuwa sio kila jambo walilotaka linaweza kutekelezwa ila Tanzania yenyewe ndio yenye uwezo wa kuamua nini cha kufanya na kunukuu maneno ya Rais wa awamu ya Tatu Benjamin Mkapa wakati akiapishwa kuwa rais mwaka 2000.
"Nawashukuru watazamaji wetu wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika,walipotusifu tumepokea sifa hizo kwa nyenyekevu mkubwa. Tumesikia pia waliodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi wenyewe tumeyaona. Maagizo ya kutuelekeza nini cha kufanya tumeyakataa," mwisho wa nukuu ya Rais Benjamin Mkapa iliyosomwa na Rais Samia.
Rais Samia aliongeza kuwa hakuna aliyemkamilifu duniani.
Waangalizi waliokuwepo kutoka Afrika ni pamoja na Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya nchi za Mawiza Makuu (ICGLR), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na wengineo kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Waangalizi wa SADC wamesema kwamba uchaguzi wa Tanzania uligubikwa na dosari .
Soma pia:
Kanali Mamadi Doumbouya atangaza kugombea urais Guinea licha ya ahadi ya kutowania

Chanzo cha picha, GUINEA TV
Maelezo ya picha, Kanali Doumbouya, ambaye anasemekana alipata mafunzo ya kijeshi nchini Ufaransa Kanali Mamadi Doumbouya aliyenyakua madaraka Guinea kupitia mapinduzi ya kijeshi miaka minne iliyopita,atashiriki katika uchaguzi wa rais licha ya kuahidi hapo awali kuwa hatawania urais na atarejesha utawala wa kiraia.
Kanali Doumbouya aliwasili katika mahakama ya juu hapo jana Jumatatu akiwa amendamana na wanajeshi kuwasilisha rasmi azma yake ya kugombea urais.
Vyama viwili vikuu vya upinzani vimepigwa marufuku kushiriki katika uchaguzi huo unaotarajiwa mwezi ujao Desemba.
Waguinea walishangazwa na tangazo kuwa wagombea urais watahitajika kulipa ada ya dola laki moja kushiriki katika uchaguzi huo.
Mnamo Septemba mwaka 2021,mapinduzi ya kushtukiza ya kijeshi yalifanyika nchini Guinea nakumaliza hatamu yenye utata ya Rais Alpha Conde, chini ya mwaka mmoja baada ya kushinda muhula wa tatu uliogubikwa na maandamano mabaya na ukandamizaji mkali dhidi ya upinzani katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika.
Soma pia:
Rais Samia Suluhu Hassan afanya uteuzi wa mwanasheria mkuu wa serikali mpya

Chanzo cha picha, Hamza Johari/X
Maelezo ya picha, Picha ya atakayekuwa mwanasheria mkuu katika serikali mpya ya Tanzania Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika siku yake ya kwanza ya kuanza rasmi muhula wake wa pili wa uongozi baada ya kula kiapo cha kuiongoza Tanzania, amemteua Bw. Hamza Said Johari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kupitia mitandao ya kijamii na Msemaji wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, imeelezwa kuwa Bw. Hamza Said Johari ataapishwa siku ya Jumatano, tarehe 5 Novemba 2025, saa 4:00 asubuhi, katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Pia unaweza kusoma:
White House yatangaza msaada wa dharura wa chakula kwa Wamarekani katikati ya mkwamo wa matumizi ya serikali

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Wakosoaji wanasema Donald Trump anatumia ushuru kama silaha Ikulu ya Rais ya White House imesema itatumia fedha kutoka kwa mfuko wa dharura kutoa misaada ya chakula kwa zaidi ya Wamarekani milioni arobaini ambao hutegemea malipo kwa ajili ya chakula kutoka kwa serikali kuu.
Hata hivyo serikali,imesema watapokea tu nusu ya fedha za kukidhia mahitaji yao ya chakula.
Mpango huo wa kufadhili familia zisizojiweza kupata chakula ujulikanao SNAP huigharimu serikali takriban dola bilioni nane kila mwezi.
Hayo yanajiri huku mkwamo wa matumizi ya serikali kuu ukiingia mwezi wa pili kukiwa hakuna dalili za kuwepo muafaka.
Majaji wawili walitoa uamuzi kuwa utawala wa Rais Donald Trump hauruhusiwi kusitisha malipo kwa familia zinazohitaji msaada wa chakula.
Soma pia:
Wakili wa zamani wa jeshi la Israel akamatwa kwa kuvujisha video ya wafungwa wa Kipalestina wakinyanyaswa

Chanzo cha picha, IDF
Maelezo ya picha, Meja Jenerali Yifat Tomer-Yerushalmi alijiuzulu siku ya Ijumaa, akikiri jukumu lake katika kuvujisha video hiyo. Wakili wa zamani katika jeshi la Israel amekamatwa, huku mzozo wa kisiasa ukizidi kufuatia kuvuja kwa video inayodaiwa kuonyesha unyanyasaji mkali wa mfungwa wa Kipalestina na wanajeshi wa Israel.
Meja Jenerali Yifat Tomer-Yerushalmi alijiuzulu kama Wakili Mkuu wa Kijeshi wa Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) wiki iliyopita, akisema kwamba alichukua jukumu kamili la uvujaji huo.
Siku ya Jumapili, tukio hilo lilichukua mkondo wa kutamausha zaidi aliporipotiwa kutoweka, huku polisi wakiweka msako wa saa moja kumtafuta kwenye ufuo wa bahari kaskazini mwa Tel Aviv.
Baadaye alipatikana akiwa hai na mzima, polisi walisema, lakini aliwekwa chini ya ulinzi.
Hisia mseto kutokana na video iliyovuja zinaongezeka kila siku.
Ilitangazwa mnamo Agosti 2024 kwenye kituo cha habari cha Israeli, picha zinaonyesha askari wa akiba katika kituo cha kijeshi cha Sde Teiman kusini mwa Israeli wakimchukua mfungwa, kisha kumzunguka kwa ngao za kutuliza ghasia ili kuzuia kuonekana huku akidaiwa kupigwa na kudungwa na kitu chenye ncha kali kwenye rektamu.
Mfungwa huyo alitibiwa majeraha mabaya.
Askari watano wa akiba walishtakiwa kwa unyanyasaji wa hali ya juu na kusababisha madhara makubwa ya mwili kwa mfungwa huyo.
Hata hivyo, wamekana mashtaka na hawajatajwa majina.
Siku ya Jumapili, wanne kati ya askari wa akiba walivalia vazi jeusi kuficha nyuso zao walipokuwa kwenye mkutano na wanahabari nje ya Mahakama ya Juu mjini Jerusalem pamoja na mawakili wao, waliotaka kesi yao itupiliwe mbali.
Adi Keidar, wakili kutoka shirika la usaidizi wa kisheria la mrengo wa kulia Honenu, alidai wateja wake walikuwa chini ya "mchakato wa kisheria mbovu, wenye upendeleo na uliopikwa kabisa".
Video hiyo inachukuliwa na upande wa kushoto kama ushahidi thabiti unaounga mkono ripoti nyingi za unyanyasaji wa wafungwa wa Kipalestina tangu shambulio la Hamas lililoongozwa na 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israeli.
Oktoba iliyopita, ripoti ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilidai kuwa maelfu ya watoto na wafungwa watu wazima kutoka Gaza "wamekabiliwa na unyanyasaji mkubwa na wa utaratibu, unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia, na unyanyasaji wa kijinsia sawa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu wa mateso na uhalifu wa kivita wa ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia".
Serikali ya Israel ilikanusha shutuma za kuenea kwa unyanyasaji na mateso kwa wafungwa, na kusisitiza kuwa "imejitolea kikamilifu kwa viwango vya kisheria vya kimataifa".
Pia ilisema imefanya uchunguzi wa kina katika kila malalamiko.
Soma pia:
Hujambo na karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya leo siku ya Jumanne tarehe 04/11/2025.Tutaangazia yanayojiri nchini Tanzania baada ya uchaguzi kukamilika na pia habari za kimataifa.
