'Jeshi liko hapa, lakini sihisi kuwa niko salama tena'

Chanzo cha picha, Boko Haram
- Author, Aisha Babangida
- Nafasi, Broadcast Journalist
- Akiripoti kutoka, BBC News, Abuja
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Septemba mwaka jana, baada ya wanamgambo wa Boko Haram kushambulia mji wa Mafa huko Yobe, kaskazini mashariki mwa Nigeria, ilirudisha hofu ya enzi ambayo wakazi walidhani imepita. Vumbi lilipotulia, washambuliaji walikuwa wameua zaidi ya watu 100.
Boko Haram inakuza Uislamu ambao unafanya haram kwa waislamu kushiriki katika shughuli zozote za kisiasa au kijamii zinazohusiana na jamii ya Magharibi. Boko Haram inalichukulia jimbo la Nigeria kuwa linaendeshwa na watu wasio waumini, bila kujali kama rais ni Muislamu au la, kulingana na ripoti ya awali ya BBC.
Huku ikidhaniwa kuwa imedhoofishwa kwa miaka mingi na jeshi la Nigeria na operesheni za pamoja na nchi jirani, mashambulizi ya Boko Haram nchini Nigeria yamekuwa ya mara kwa mara katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Mashambulizi yanayohusishwa na kundi hilo yameongezeka taratibu katika miaka mitatu iliyopita, kutoka mashambulizi 105 mwaka 2022, hadi 147 mwaka 2023 na 191 mwaka 2024, kulingana na uchambuzi wa BBC wa data kutoka kwa shirika la kijasusi la SBM, kampuni ya kukusanya taarifa za usalama inayolenga Afrika.
Mnamo 2025, shambulio la kwanza lililorekodiwa lilikuwa Januari 4, wakati kundi hilo liliwavamia wanajeshi wa Nigeria katika kijiji cha Sabon Gari, na kuwaua sita. Siku tisa tu baadaye, Januari 13, Boko Haram walishambulia kijiji cha Dumba karibu na Baga, na kuua wakulima na wavuvi 40.
Mashambulizi mengine yamefuata kila mwezi mwaka huu, huku kukiongezeka mara kwa mara na kuashiria hali ya kutatanisha ya ghasia mpya, ambazo hadi sasa zinalenga jamii za vijijini na zile za viunga vya mijini.
Dalili za kufufuka tena?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo Aprili 8, 2025, Gavana wa jimbo la Borno, Babagana Umara Zulum alitoa tahadhari kuhusu mashambulizi mapya ya Boko Haram na ongezeko la utekaji nyara. Alisema kundi hilo linajipanga kurejea, likilenga vituo vya kijeshi na kuua raia.
"Mauaji ya raia wasio na hatia na maafisa wa usalama ni ya kutisha na yanaashiria kurudi nyuma kwa Jimbo la Borno na eneo la kaskazini mashariki," alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ripoti za kuongezeka kwa ghasia katika majimbo ya Borno na Yobe kaskazini mashariki mwa Nigeria zinaonesha kuwa kundi hilo bado halijashindwa kama inavyofikiriwa.
"Tulichoshuhudia sio tu kitendo kidogo cha vurugu; ni ishara kwamba tunapoteza matumaini na ujasiri. Kila mtu ana hofu, akili zimekumbwa na hofu, na watu wanajitahidi kuwa sawa," Aliyu Harande, mkazi wa Mafa aliiambia BBC kufuatia shambulio la mwaka jana.
"Kwa wale tuliodhani shughuli zao zimetulia, tukio hili limetufanya tutambue wanajipanga upya."
Zanna Umara, afisa wa baraza la serikali ya mtaa wa Tarmuwa pia aliiambia BBC "Hatuwaombei warejee tena, lakini kwa kuzingatia ukubwa wa shambulio la Mafa, inaonekana kama wanalenga kurejea."
Kuongezeka kwa mashambulizi ya hivi karibuni kunaweza kufuatiliwa kwa sababu fulani, kulingana na Dk. Kabir Adamu, Mkurugenzi Mkuu wa Beacon Security and Intelligence Limited. La kwanza, alisema ni kutolewa kwa Islamic State "maelekezo ya kimataifa yanayotaka washirika wake kuongeza mashambulizi, na tumeona makundi mbalimbali yakiitikia wito huo."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pili, Dk Adamu alitaja mifumo ya msimu. "Kabla tu ya msimu wa mvua, vikundi hivi kwa kawaida vinaongeza shughuli zao, wakijua kwamba operesheni za kijeshi huwa zinapungua katika kipindi hicho kutokana na mazingira magumu na kutoonekana vizuri."
Pia aliangazia ukosefu wa utulivu wa kikanda kama kichocheo kikuu: "Migogoro katika Sahel, hasa katika nchi kama Chad, Niger, na Burkina Faso, imedhoofisha usalama wa mpaka, na kuruhusu makundi haya kuhama, kuajiri, na kupokea msaada kwa uhuru zaidi," alisema.
Pia alisema mabadiliko ya ndani katika muundo wa kijeshi wa Nigeria yamekuwa na jukumu, haswa usafirishaji wa zana na wafanyakazi kutoka kaskazini mashariki kusaidia operesheni mpya kaskazini magharibi.
Lakini serikali ya Nigeria inasema kuongezeka kwa mashambulizi ya Boko Haram ni kwa sababu ya kuongezeka kwa shughuli za waasi katika nchi jirani.
"Kuongezeka kwa mashambulizi hakupaswi kuchukuliwa juu juu," Mohammed Badaru Abubakar, waziri wa ulinzi wa Nigeria aliiambia BBC. "Kinachotokea katika nchi zetu jirani ni muhimu. Waasi wameongeza shughuli zao katika eneo lote, na athari hiyo ya kuenea kwa sasa ni sehemu ya kile tunachokabiliana nacho hapa Nigeria."
Kulingana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), zaidi ya watu 35,000 wanakadiriwa kuuawa kutokana na mashambulizi ya moja kwa moja ya Boko Haram kati ya 2009 na 2024 na takribani mashambulizi 7 makubwa mwaka 2024 pekee ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya 200 na zaidi ya majeruhi 300 ambayo yaliongezeka ikilinganishwa na mashambulizi ya miaka iliyopita.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashambulizi haya kwa mujibu wa UNDP yamejikita kaskazini-mashariki mwa Nigeria, hasa katika Jimbo la Borno, ambako Boko Haram na kundi lililogawanyika, ISWAP, wanaendelea kuwalenga raia na wanajeshi.
Huku Nigeria ikikabiliwa na matatizo mawili ya kupanda kwa gharama za maisha na kuongezeka kwa ghasia za waasi, ustahimilivu wa watu walioathiriwa moja kwa moja unajaribiwa.
"Tunapaswa kushughulikia nini kwanza, shida ya gharama ya maisha au ukosefu wa usalama wa mara kwa mara na hofu kwa maisha yetu?" Alisema Harande.
Wakati wakazi wa vijijini, waathiriwa wa kawaida wa raia wa mashambulizi ya waasi, wakiomboleza hasara zao na kujenga upya maisha yao, wanafanya hivyo kwa hofu na kutokuwa na uhakika wa ni lini shambulio lijalo litakuja.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Watoto wangu wana hofu kubwa, na hatuna uhakika kama ni salama kurejea. Jeshi liko hapa, lakini sijisikii salama tena," Hajara Idris (si jina lake halisi), aliambia BBC baada ya shambulio hilo huko Mafa.
Hayuko peke yake. Fatima Bukar (si jina lake halisi) pia ana hofu hiyo, akisema "Shambulio hilo limetuacha tukiwa na kiwewe. Tumeona mambo ambayo hatukuwahi kufikiria, na ninahisi kama hakuna mahali salama kwetu tena. Hata nikiwa na jeshi hapa, nina hofu kila usiku kwamba Boko Haram wanaweza kurudi."
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












