'Afadhali kumuoza binti yangu kuliko majambazi wamuibe'

tt

Harusi kubwa iliyokuwa imepangwa katika jimbo la Niger, kaskazini mwa Nigeria ilipaswa kuwa na wachumba 100 kuozwa kwa wakati mmoja.

Ingawa mpango huo ulikosolewa vikali matukio kama haya kufanyika katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria ni jambo la kawaida. Kilichozua mjadala ni madai kwamba baadhi ya maharusi watarajiwa ni wasichana wenye umri mdogo.

Ndoa ya pamoja kwa wasichana hao ilisemekana kuwa mradi wa ‘jimbo’ unaofadhiliwa na Mohammed Abdulmalik Sarkin-Daji, Spika wa Bunge la Jimbo la Niger.

Madai ya kujumuishwa kwa wasichana wenye umri mdogo yalimfanya, Waziri wa Masuala ya Wanawake, Uju Kennedy–Ohanenye kwenda mahakamani kuizuia akiahidi uchunguzi wa ndoa hiyo ya pamoja, ambayo ilisitishwa. Wakati mwakilishi wa waziri alipotembelea jamii wiki hii, wasichana 100 waliwasilishwa katika ikulu ya mtawala wa jadi, na hakuna hata mmoja aliyepatikana kuwa na umri mdogo.

Soma pia:

Lakini baadhi ya wanajamii, walioomba kutotajwa majina yao, waliambia BBC kwamba kulikuwa na wasichana wapatao 38 wenye umri wa chini katika orodha ya awali.

Akizungumza na BBC Pidgin, Sarkin-Daji alikanusha madai ya kuwabadilisha wasichana wenye umri mdogo waliokuwa kwenye orodha ya awali, kufuatia malalamiko ya umma.

"Hakuna msichana aliyebadilishwa, na haiwezi kutokea chini ya uangalizi wangu," alisema.

Bi Asamau Abdullahi na binti yake
Maelezo ya picha, Bi Asamau Abdullahi na binti yake mwenye umri wa miaka 22 ambaye ni mmoja wa 'bibi harusi mtarajiwa'.

Wakati taarifa za kusitishwa kwa harusi hiyo zilipowafikia wazazi na walezi wa maharusi watarajiwa, waliiambia BBC Pidgin kuwa ni habari za kuhuzunisha kwao.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Ni afadhali kumuoza binti yangu kuliko majambazi wamuibe," alisema Asamau Shehu, mama wa mmoja wa maharusi watarajiwa. Bi Shehu ambaye anatoka katika jamii ya Gulbin Boka, alisema bintiye ana umri wa miaka 22 na aliunga mkono ndoa hiyo.

Kwake, hana budi ila kumuoza binti yake kutokana na masuala ya ukosefu wa usalama yanayohusiana na ujambazi na utekaji nyara. Afadhali kujua alipo binti yake kuliko majambazi wamchukue na kumpeleka kusikojulikana, ambako asingejua binti yake anaendeleaje.

Ndiyo sababu amewaoza binti zake wengine, lakini umaskini pia umechangia.

"Binti yangu ni pacha," alisema, akimuashiria bibi-harusi mtarajiwa, "tulimuoza dada yake pacha mwaka jana kwa sababu hatukuwa na chochote. Tulichukua mahari ya N80,000 sawa na dola 54.7.”

Wanawake kama Bi Shehu ni wengi katika eneo hilo, wajane ambao waume zao wameuawa na majambazi na watoto wao kutekwa nyara, ambao wengi wao wanasalia utumwani. Familia zilizosalia, anasema, hazina uwezo wa kusomesha watoto wao na wengine hata kuuza nyumba zao ili kujikimu.

Utekaji nyara na ujambazi si jambo geni katika jimbo la Niger, hasa katika jamii zilizo mbali na mji mkuu. Vyanzo vya jamii viliiambia BBC kuwa kwa kawaida kuna mashambulizi ya kikatili na utekaji nyara takriban mara tatu hadi tano kwa wiki, lakini imepungua katika miezi miwili iliyopita.

Abdulmalik Sarkin-Daji
Maelezo ya picha, Spika, wa jimbo la Niger, Mohammed Abdulmalik Sarkin-Daji

Abdulmalik Sarkin-Daji, Spika wa Bunge la Jimbo la Niger, Mohammad aliiambia BBC Pidgin kwamba mpango wa ndoa ya pamoja kwa wasichana hao 100 ulianza baada ya kukutana na mkuu wa kijiji. Mtu huyo alikuwa amempigia simu kuhusu mwanamke ambaye mumewe alitekwa nyara na majambazi na kudai fidia ya naira milioni mbili. Aliuza kila kitu ambacho familia ilikuwa nacho ikiwa ni pamoja na pikipiki ya mume wake ili kupata pesa hizo ndani ya siku nane, lakini watekaji nyara hao waliomba nyongeza ya naira milioni moja.

Kufikia wakati huu, hakuna chochote kilichobaki. Mwanamke huyo, ambaye alikuwa na binti wawili walioolewa katika muda wa miezi sita wakati huo, aliwaita wakwe zake watarajiwa kuleta mahari na kuwaoa mara moja. Naira milioni moja za ziada zilitolewa na wachumba hao wawili, lakini mwanamume huyo aliuawa baada ya watekaji nyara kugundua alikuw askari wa eneo hilo. Wachumba walihamaki wakiomba ndoa au kurudishiwa pesa.

Hii, Sarkin-Daji alisema, ilimsukuma kumuunga mkono mwanamke huyo na naira milioni mbili kwa ndoa hiyo. Akiwa na furaha tele, alimwambia mkuu wa kijiji na Imamu wa Jumaat kuhusu usaidizi aliopata, na baadaye wangeomba msaada kama huo kwa kaya 270 zenye masuala kama hayo.

"Niliambiwa kuna kaya 270 zinazohitaji msaada wa kuozesha binti zao. Kila moja ingegharimu kati ya N400,000 na N450,000 na ningeweza kumudu watu 100 tu," alisema. "Niliwasaidia kwa N50 milioni kwa nia njema bila kuwajua wao au familia zao.”

Ingawa aliiambia BBC Pidgin kwamba alihuzunishwa na mabishano yaliyotokana na tukio hilo, pia alisema alikuwa "na furaha kila kitu kimetatuliwa".

xx

Kama sehemu ya uchunguzi wa kubaini umri wa wasichana ambao wangeolewa na ikiwa waliridhia ndoa hiyo, waziri wa Masuala ya Wanawake alituma wawakilishi katika jimbo la Niger.

Siku moja kabla ya mpango huo, maofisa wa jimbo waliwaleta wasichana 100 kutoka vijijini kwao, kwa ajili ya kuwawasilisha hadharani kwa wawakilishi wa waziri.

Wakati wawakilishi waliyoandamana na BBC Pidgin walipofika katika jumba la Emir katika Eneo la Serikali ya Mtaa ya Kontagora, walikutana na umati wa watu ambao haukuwakaribisha.

Mvutano katika jimbo hilo ulipungua tu wakati mwakilishi wa waziri, Adaji Usman alipotangaza kwamba "hatukuja kukomesha ndoa, tulikuja (tu) kuona ikiwa kuna msichana mdogo kati yao na ikiwa wasichana walikubali". ilisema ikiwa msichana yeyote angetaka kwenda shule, atapata ufadhili wa masomo na wale wanaotaka kusoma watapewa nafasi ya kupata elimu.

Maelezo ya video, Mgogoro wa utekaji nyara Nigeria: ‘Tunawaangalia wezi wakiwachukua watoto wetu’

Umati ulipiga makofi na kushangilia wakati Bw Usman, akizungumza kwa Kihausa, alipotangaza "tutawatambulisha wasichana na kukusanya nambari zao za akaunti pia kwa ajili ya kuwawezesha".

Lakini baada ya wasichana hao kuorodheshwa na kushirikishwa kwa matakwa yao, hakuna aliyependa kwenda shule. Wote walipendelea kujifunza ujuzi fulani, wengine wakionyesha nia ya ushonaji ilhali walio wengi walitaka kulima.

Wawakilishi wa waziri baadaye wangesema ndoa hiyo ya watu wengi isifanywe hadi Serikali ya Shirikisho, kupitia wizara ya Masuala ya Wanawake itakapokamilisha mpango wa kuwawezesha wasichana hao, ili kuwawezesha kuishi kwa raha katika ndoa.

Lakini BBC Pidgin imeambiwa na baadhi ya vyanzo kwamba kinyume na matakwa ya Waziri wa Masuala ya Wanawake, harusi hizo zinaendelea kibinafsi katika maeneo mbalimbali ya serikali za mitaa lakini si kama harusi ya pamoja ambayo ilikusudiwa awali.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi