Utekaji nyara Nigeria: Hadithi ya mpatanishi wa malipo ya kukomboa mateka

FVC

Chanzo cha picha, REUTERS

    • Author, Priya Sippy
    • Nafasi, BBC

Mpatanishi mmoja ameiambia BBC kwamba kulipa fidia kunaweza kuwa kinyume cha sheria, lakini ndiyo njia pekee ya familia kuhakikisha jamaa waliotekwa nyara na magenge wanaachiliwa huru huko kaskazini mwa Nigeria.

Sulaiman, jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, anatoka jimbo la Kaduna, ambako watoto 280 walitekwa nyara hivi karibuni kutoka shule moja katika mji wa Kuriga.

Amekuwa akifanya kazi kwa njia isiyo rasmi - jukumu hili lenye utata na hatari kwa miaka kadhaa - ni baada ya jamaa zake kuchukuliwa mateka.

"Lazima tujadiliane. Huwezi kutumia nguvu kuwarejesha mateka," anaiambia BBC.

Pia unaweza kusoma

Namna anavyofanya kazi hiyo

FV

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mwanafunzi huyu, aliyetekwa nyara Julai 2021, aliachiliwa kabla ya malipo ya fidia kuwa haramu

Sulaiman alijihusisha kwa mara ya kwanza katika mazungumzo na wateka nyara, mwaka 2021 - mwaka mmoja kabla ya malipo ya fidia kuwa kinyume cha sheria nchini Nigeria.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita anasema amefanya mazungumzo ya kuachiliwa kwa mateka zaidi ya 200. Hiyo ni sehemu ndogo ya maelfu ya watu waliotekwa nyara katika muongo mmoja uliopita.

"Serikali inaamini nimekuwa nikiwasaidia majambazi," anasema, akizungumza kutoka eneo lisilojulikana.

"Majambazi wanadhani nimekuwa nikipata pesa kutoka kwa serikali, kwa hivyo mimi pia ni mlengwa wa utekaji nyara."

Mazungumzo yake ya kwanza ni pale alipokuwa akijaribu kutafuta fidia ya karibu dola za kimarekani 12,500, kwa jamaa zake wawili ambao walikuwa wametekwa nyara.

Mbinu yake ya subira, hatimaye ilifanya kazi na mwishowe jamaa zake waliachiliwa - ingawa ilimbidi kuuza shamba lake kijijini kwao ili kutoa fidia.

Habari zilipoenea kuhusu kuachiliwa kwa mafanikio, familia nyingine ambazo jamaa zao walitekwa nyara zilimjia ili kupata msaada. Muda si muda simu yake ilikuwa bize kila mara.

"Karibu kila mtu katika kijiji changu ametekwa nyara," anasema, akiongeza kuwa huwasaidia bila malipo.

Na licha ya kuharamishwa kwa malipo ya fidia, watu bado wanakuja kwake - wakihitaji msaada.

Sulaiman anakiri ni kazi ya kutisha kwake: "Serikali haipendi mazungumzo na majambazi, na inaweza kuwapeleka watu jela kwa kufanya hivyo."

Mzizi wa tatizo

FDV

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kumempa mpatanishi huyo kuelewa masuala yanayochochea utekaji nyara.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anafahamu sababu kuu za mgogoro wa utekaji nyara Nigeria, anasema unachochewa zaidi na umaskini na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira kwa vijana.

Migogoro ya ardhi na rasilimali kati ya wafugaji na wakulima pia imechangia tatizo hilo. Watekaji nyara huwa ni wafugaji wa zamani kutoka kabila la Fulani, ambao wanalenga vijiji ambako wakulima wengi wa Kihausa wanaishi.

Mazungumzo hufanyika kwa lugha ya Kihausa, lugha ya kaskazini kwenye Waislam wengi - ingawa wateka nyara wengi wanazungumza Kifulfulde, lugha inayozungumzwa na watu wa Wafulani.

Mara nyingi magenge hayo yanaundwa na watu wenye bunduki na hupanda pikipiki na kulenga maeneo au familia fulani kwa maelekezo ya mpasha habari anaelipwa. Ni operesheni kubwa na ya kutengeneza pesa.

Kuna takribani majambazi 30,000 katika zaidi ya vikundi 100 vya magenge – yanayofanya kazi kaskazini-magharibi mwa Nigeria, kulingana na Kituo cha Demokrasia na Maendeleo - chenye makao yake katika mji mkuu, Abuja.

Namna mazungumzo yanavyofanyika

FV

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Sulaiman anaamini mazungumzo yangefanya kazi vizuri zaidi kuliko mbinu za kijeshi kutatua mgogoro

Sulaiman anasema mafanikio ya mazungumzo yake yanategemea kiongozi wa watekaji nyara: "Baadhi ya majambazi ambao nimeshughulika nao bado wanashikilia mateka na wanataka pesa zaidi, hata baada ya kulipa fidia.

"Lakini baadhi yao huwaachilia mateka mara tu unapolipa. Mchakato unaweza kuwa mgumu, na kuchukua hadi siku 50 kumwachilia mateka mmoja na simu kati ya 20 na 30.’’

"Lazima utumie lugha laini, wanaweza kukuvunjia heshima na wakakutukana lakini lazima utulie," anasema.

Licha ya uhaba wa noti za benki nchini Nigeria, watekaji nyara wanadai kuwa fidia zilipwe kwa pesa taslimu kwani uhamisho kwa kutumia benki ni rahisi kufatiliwa.

Malipo kwa kawaida hutolewa na mzazi au jamaa wa mmoja wa waliotekwa nyara, Sulaiman anaeleza.

"Jambazi atawapigia simu na kuwapa maelekezo ya hatua kwa hatua jinsi ya kuwafuata porini. Wakifika huko, jambazi atahesabu pesa, noti kwa noti."

Wakati mwingine majambazi huomba pikipiki kama sehemu ya malipo ya fidia, pamoja na pombe na sigara.

Jamaa mwingine wa Sulaiman alipotekwa nyara kutoka chuo kikuu pamoja na wanafunzi wengine - anasema serikali ililipa karibu dola 2,370 kwa uhuru wa kila mwanafunzi - ingawa hakujawa na uthibitisho wowote rasmi wa hili.

"Serikali haitakubali kamwe katika rekodi kwa sababu kwao itakuwa ni kukiri kushindwa. Lakini kama watu wa ndani tunajua kilichotokea na hatukuwa na aina hiyo ya pesa," anasema.

Sulaiman alihusika katika mazungumzo hayo na anasema watekaji nyara walidai kwanza karibu dola 32,000 kwa kila mateka na hatimaye wakapunguza.

Siku hizi ni watu wachache wanaoweza kumudu kulipa fidia. Mara nyingi hupitisha mchango, ingawa hilo nalo ni gumu kwa sasa kutokana na jinsi ukosefu wa usalama ulivyoharibu uchumi.

Majambazi huua mateka au kuwaachilia waonapo hakuna matumaini ya malipo.

Sulaiman anadhani msururu wa utekaji nyara wa watu wengi katika shuleni, na tishio la kuwaua wanafunzi, inaweza kuwa njama ya kutaka mamlaka kuchukua hatua: "Wanadhani serikali italipa."

Kuna ripoti kwamba mamlaka imeendelea kulipa fidia mara kwa mara - ingawa mamlaka hukataa hilo kila wakati.

Na Rais Bola Ahmed Tinubu anasema hakuna senti italipwa. Kwa watoto wa shule waliotekwa nyara hivi karibuni, akiviagiza vikosi vya usalama kuhakikisha wanaachiliwa.

Kati ya Julai 2022 na Juni 2023, magenge yenye silaha yalidai zaidi ya milioni 6 katika malipo ya fidia, kulingana na ripoti ya SBM Intelligence, kampuni ya ushauri wa usalama.

Sulaiman anakubaliana na serikali kwamba kuendelea kulipa kutachochea biashara ya utekaji nyara kukuwa: "Malipo ya fidia yanachochea utekaji nyara. Majambazi wanatafuta pesa tu."

Lakini ana hakika kwamba mbinu za kijeshi sio jibu: "Ikiwa naweza kuishauri serikali, wanapaswa kukutana na watu hawa na kufanya mazungumzo nao."

Akiwa amedhamiria kuendelea kusaidia jamii yake, ana uhakika ataendelea kuitikia wito na kupokea simu.