Kwa nini utekaji nyara wa watu wengi umerejea nchini Nigeria

Chanzo cha picha, AFP
Nigeria inakabiliwa tena na utekaji nyara mkubwa.
Mara mbili katika wiki moja, magenge ya watu wenye silaha wakiwa katika pikipiki, wanaoendesha shughuli zao kutoka kwenye misitu katika maeneo mawili tofauti kaskazini mwa nchi, wameteka nyara mamia ya watu.
Kwanza siku ya Jumatano tulipata habari kutoka mji wa mbali katika jimbo la Borno kaskazini-mashariki kwamba watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kiislamu wamewakamata wanawake na watoto kutoka kambi ya watu waliokimbia makazi yao waliokuwa wakitafuta kuni. Ilichukua siku kadhaa kwa habari hiyo kuibuka kwa sababu milingoti ya simu za rununu ilikuwa imeharibiwa.
Kisha siku iliyofuata, zaidi ya watoto 280, wenye umri wa kati ya miaka minane na 15, na baadhi ya walimu, walichukuliwa na watu wenye silaha kutoka shule iliyo umbali wa mamia ya maili katika jimbo la kaskazini-magharibi la Kaduna hadi kwenye msitu wa karibu.
Kuna ripoti za ndani kwamba shambulio hili lilitekelezwa na wanamgambo wa kundi la Ansaru lenye uhusiano na al-Qaeda.
Katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na utulivu katika aina hii ya utekaji nyara mkubwa ambao ulikuwa umeikumba Nigeria tangu utekaji nyara wa takriban wasichana 300 kutoka shule ya Chibok mwezi Aprili 2014 ambao uligonga vichwa vya habari vya kimataifa.
Lakini sasa, ni kama kumbukumbu ya miaka 10 ya mkasa huo inakaribia.
Utekaji nyara wa watu wengi huko Kaduna ndio mkubwa zaidi kutoka shuleni tangu 2021.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sasa kwa nini kuna kuzuka upya kwa utekaji nyara huu unaohatarisha maisha ya Wanigeria walio hatarini zaidi?
Ni vigumu kutofautisha muundo kutokana na muda wa yote matukio mawili ambayo inaonekana hayana uhusiano, lakini pia ni ukumbusho kwamba tishio halijaisha.
Ukweli kwamba yalitokea siku chache kabla ya mwezi wa mfungo wa Kiislamu wa Ramadhani inaweza kuwa muhimu.
Wale ambao wametekwa nyara na kuachiliwa siku za nyuma wamezungumza kuhusu kulazimishwa kufanya kazi za upishi na nyingine duni katika kambi za misitu.
Lakini kwa ujumla, utekaji nyara kwa ajili ya fidia nchini Nigeria ni biashara isiyo na hatari ndogo, yenye faida kubwa. Wale waliotekwa nyara huwa wanaachiliwa baada ya kukabidhiwa pesa, na wahusika ni mara chache sana hukamatwa
Hii ni pamoja na ukweli kwamba kulipa fidia ili kumkomboa mtu kumeharamishwa.
Kwa jumla, zaidi ya watu 4,700 wametekwa nyara tangu Rais Bola Tinubu aingie madarakani Mei mwaka jana, washauri wa masuala ya ujasusi wamesema.

Chanzo cha picha, AFP
Utekaji nyara umekuwa mradi wa faida kwa watu wanaoendeshwa na kukata tamaa kiuchumi ili kupata pesa.
Kando na fidia ya pesa, magenge yamekuwa yakidai siku za nyuma vyakula, pikipiki na hata petroli ili kuwaachilia mateka.
"Uchumi duni wa Nigeria unatengeneza mazingira ya utekaji nyara. Katika mwaka uliopita, serikali haijaweza kutatua tatizo lake la ubadilishanaji wa fedha za kigeni," William Linder, afisa mstaafu wa CIA na mkuu wa 14 North, mshauri wa masuala ya hatari kwa Afrika, aliiambia BBC.
"Bei ya vyakula imepanda sana, hasa katika kipindi cha miezi sita iliyopita. Mtazamo wa rushwa unaendelea."
Alex Vines, mkurugenzi wa programu ya Afrika katika jumba la Chatham House anakubaliana na hili.
Alisema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni yanaweza kuhusishwa na uchumi duni wa Nigeria na kutokuwa na uwezo wa vikosi kuvuruga shughuli za magenge ya utekaji nyara.
Kupanda kwa gharama za chakula kumezidishwa na wakulima kushindwa kufikia mashamba yao kulima chakula huku wakihofia kushambuliwa au kutekwa nyara.
"Katika maeneo makubwa eneo hili, magenge yenye silaha yamechukua nafasi ya serikali na watawala wa kitamaduni kama mamlaka kuu," Dk Vines alieleza.
Magenge mara nyingi huwapora watu pesa, lakini ukweli kwamba hawawezi kulima unamaanisha kuwa kuna fedha chache zinazopatikana, ambazo zinaweza kuelezea magenge hayo kugeukia utekaji nyara.
Kadhalika, kupungua kwa bonde la Ziwa Chad na kuenea kwa Jangwa la Sahara kuelekea kusini kumesababisha kutoweka kwa mashamba ya kilimo na uhaba wa maji.
"Shinikizo hizi huongeza tu masaibu ya wengi, haswa kaskazini. Hii inasukuma watu kutafuta njia mbadala za kujipatia mapato. Kwa bahati mbaya, utekaji nyara ili kulipwa fidia ni moja wapo," Bw Linder alisema.
Magenge hayo yanasaidiwa na ukweli kwamba mipaka ya Nigeria ina vinyweleo na ukosefu wa usalama. Ghasia za Kiislamu katika eneo pana zimeongeza ukosefu wa usalama.
Hifadhi kubwa za misitu katika mikoa ya mpakani zimegeuzwa kuwa vituo vya kufanya kazi kwa wahalifu.
"Nigeria inahitaji kufanya kazi na majirani zake," alisema Bulama Bukarti, mchambuzi mkuu wa migogoro katika Taasisi ya Tony Blair ya Mabadiliko ya Ulimwenguni.
"Bila ya ushirikiano wa kimataifa hasa na Niger, Cameroon, Chad, ikiwa ni pamoja na sehemu ya kaskazini-magharibi ya mpaka wa Nigeria, matukio haya yataendelea kujirudia."
Lakini hilo pekee halingesaidia Nigeria kuwashinda magenge hayo, Bw Bukarti aliongeza. Mamlaka pia zinatakiwa kuwa tayari kuwafikisha wahusika katika vyombo vya sheria.
"Hatujawahi kuona kiongozi wa genge akikamatwa na kufunguliwa mashitaka. Hii inamaana kuwa watu wengi zaidi watajiunga, na hali ya kutokujali itaongezeka," alisema.














