Jinsi mvulana wa shule alivyowatoroka watekaji nyara Nigeria

- Author, Chris Ewokor
- Nafasi, BBC News, Kuriga
Musa Garba, 17, alilazimika kutambaa chini kama nyoka ili asigunduliwe na watekaji nyara wake alipokuwa akitoroka kupitia msitu wa kaskazini mwa Nigeria.
Hapo awali, akiwa amefichwa na sare yake ya shule, kijana huyo alifanikiwa kujificha kwenye rundo la nyasi zilizokatwa huku kundi la watoto wa shule waliotekwa nyara wakipumzika kutoka kwa safari yao ya kulazimishwa.
Zaidi ya 280 kati yao walitekwa wiki iliyopita mjini Kuriga, katika jimbo la Kaduna, katika hali iliyozua hofu katika jamii.
"Tuliona pikipiki barabarani. Tulifikiri walikuwa wanajeshi, kabla hatujagundua kuwa walikuwa wamevamia eneo la shule na kuanza kufyatua risasi," Musa alimbia BBC alipokuwa akikumbuka matukio ya kutisha ya Alhamisi asubuhi. Tumebadilisha jina lake kwa ajili ya usalama wake, pamoja na la mvulana mwingine aliyetekwa nyara aliyetajwa katika makala hiyo.
"Tulijaribu kukimbia, lakini walitukimbiza na kutukamata. Walitukusanya pamoja kama ng'ombe msituni."
Watu hawa wenye silaha wakiwa kwenye pikipiki - wanajulikana kama majambazi - walikuwa wakiitishia jamii kwa muda, huku vikosi vya usalama vikishindwa kukabiliana na tishio hilo. Kuriga imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na magenge yanayotaka kuwateka nyara watu na kupata pesa kutokana na malipo ya kikombozi.
Kiwango cha utekaji nyara huu wa hivi punde na ambao ulihusisha watoto wa umri wa miaka saba kimewagusa wengi hapa.
"Tuliwatazama wakiwabeba watoto wetu hapa na hatukuwa na uwezo wa kufanya lolote. Hatuna wanajeshi, hatuna polisi katika jamii," Hajiya Hauwa aliyefadhaika anasema, huku akitokwa na machozi.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Musa alikuwa mmoja wa waliochukuliwa.
“Wakati tunaelekea porini wakati fulani sote tulikuwa na kiu lakini hatukuwa maji, wasichana na wavulana walikuwa wanaanguka tu huku tukiendelea na mwendo kwa sababu wote walikuwa wamechoka,” anasema.
"Majambazi walilazimika kubeba baadhi yao kwenye baiskeli."
Wakati fulani wakiwa ndani kabisa ya msitu huo, waliweza kukata kiu yao kwenye mto ambao ulikuja kuwa ahueni kubwa kwa watoto ambao hawakupata kifungua kinywa na kulazimika kutembea kwa saa kadhaa chini ya jua kali.
Musa aliendelea kutafuta njia za kutoroka na kujaribu kuwahimiza wengine wajiunge naye lakini waliogopa sana.
Alipata nafasi yake wakati jua linazama. Akiwa anatazama huku na kule kuhakikisha hafuatiliwi, alijificha kwenye lundo moja la nyasi na kujilaza.
"Baada ya yote kuwa kimya, [ili kuepuka kugunduliwa] nilianza kujikokota kama nyoka chini." Mara giza lilipoingia, aliinuka na kwenda zake mpaka alipofika kijijini ambako alipata msaada.
Alichukua hatari kubwa ambayo ingeweza kumfanya auawe kwa kosa dogo, lakini wengine wanasema kwamba Mungu alimlinda.
Siku iliyofuata alipotokea Kuriga, wazazi wake walikuwa na furaha, lakini alikuja na hadithi za kuhuzunisha za watoto waliosalia mikononi mwa majambazi.
Wazazi wa Sadiq Usman Abdullahi mwenye umri wa miaka 10 bado wanasubiri taarifa kumhusu.
Mara ya mwisho familia hiyo ilipomwona mvulana huyo aliyekuwa mcheshi na anayependwa sana na watu ilikuwa wakati alipokimbia kurudi nyumbani Alhamisi asubuhi akisema kuwa amesahau penseli yake ya shule - muda mfupi kabla ya watekaji nyara kuingia mjini.
"Alikuja kuniuliza: 'Hassan una penseli?'" kaka yake mwenye umri wa miaka 21 anasema.
"Nilimwambia akague begi langu. Sadiq alikuwa anakimbia, akatawanya vitu vyangu, akapata penseli, nikamwambia aandae begi langu. Kisha akachukua soksi zake na kukimbia."

Mama yake, Rahmatu Usman Abdullahi, anasema hajaweza kulala tangu siku hiyo.
"Siku zote huwa nafikiria juu yake, siwezi kulala. Nitawezaje kupata usingizi? Angalia macho yangu! Nitoe wapi usingizi? Mungu atusaidie tu," anasema, akitazama juu kama ishara ya kuomba huruma ya Mungu.
Lakini Musa na Sadiq ni wawili tu kati ya zaidi ya watu 4,000 ambao wametekwa nyara nchini Nigeria katika muda wa miezi minane iliyopita, kulingana na mojawapo wa makadirio.
Katika muongo mmoja na nusu uliopita, watu kaskazini mwa Nigeria wameshambuliwa vikali na makundi ya wapiganaji wenye silaha.
Mara ya kwanza, hii ilitokea hasa katika majimbo ya kaskazini-mashariki ya Borno, Adamawa na Yobe, ambapo kundi la wanamgambo, linalojulikana kama Boko Haram (maana yake "elimu ya Magharibi imekatazwa") ni hai.
Kikosi cha pili, chenye uhusiano na kundi la Islamic State, pia kimeibuka.
Makundi yote mawili ya makundi ya wanajihadi yalihusika katika utekaji nyara, kulenga wakulima, wasafiri na hata kuharibu vijiji chini.
Shule, zinazoonekana kama mfumo wa kuendeleza ajenda za mataifa ya Magharibi, ndio maana zinalengwa. Shambulio baya zaidi dhidi ya shule ni lile lililofanyika katika shule ya wasichana huko Chibok miaka 10 iliyopita.
"Kumekuwa na ongezeko la mashambulizi dhidi ya shule kaskazini mwa Nigeria. Shule za msingi, shule za upili na vyuo vikuu vimeshambuliwa," anasema Shehu Sani, seneta wa zamani wa jimbo la Kaduna. Anasema kuwa lengo ni kuwakatisha tamaa wazazi kuwapeleka watoto wao shule.
"Wakati huo huo, wanaposhambulia na kuteka nyara, wanafanya hivyo kwa nia ya kutafuta fedha - kununua silaha zaidi na pia kuendeleza shughuli zao za uhalifu."
Lakini mbinu zao zimeenea kote kaskazini huku magenge ya wahalifu yanayojulikana kama majambazi yakitumia mbinu hiyo hiyo, kwani wameona kuwa utekaji nyara wa watoto wa shule mara nyingi huvutia hisia, kwa hivyo ni rajisi kwao kulipiwa fidia.
"Wanahamasishwa na pesa. Wanateka nyara watu tu, na mara tu wanapolipwa fidia, wanawaachilia mateka wao. Hawana ajenda ya kisiasa na hawana uongozi wa wazi," Bw Sani anasema.














